WAHIMA WARUDI KWAO WAPI? Nilitaka kuandika barua ya wazi kwa waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Dk Nchimbi; kuhusu mgogoro wa Wahima(wafugaji) “Wahamiaji haramu” mkoani Kagera na hasa wilaya ya Karagwe; kwa vile siku hizi mambo mengi yanakatazwa kwa visingizio vingi kama “kesi iko mahakamani”, “Kuvunja amani” “Kutokuandika mambo ya kuchafuana” na mambo mengine mengi kama vile zuio la kuwazomea viongozi wetu maana wao ni waheshimiwa, hata wakikosea tushangilie! Nimechelea kuandika barua ya wazi kwa mheshimiwa waziri. Nimechagua kuandika makala! Mwaka jana, wanyambo walikuwa na Tamasha lao kwenye kijiji cha Makumbusho jijini Dar-es-salaam. Mheshimiwa Waziri Nchimbi, wakati huo akiwa Naibu waziri wa Utamaduni na michezo? kwa niaba ya Makamu wa Rais, alilifungua tamasha hilo. Katika risala yao waliyoisoma mbele ya Waziri Nchimbi, wanyambo walikuwa na mambo makuu mawili ya kusisitiza. La kwanza ni kwamba wao si Warundi, Wanyarwanda wala waganda. Wao ni watanzania. Walitegemea tamasha hilo la wanyambo lingesaidia kuondoa utata unajitokeza mara nyingi juu ya kabila la wanyambo. Kwa vile wanapakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi, wamekuwa wakisumbuliwa mara nyingi kwa kuzaniwa kwamba wao ni wahamiaji haramu. Pamoja na ukweli kwamba Tanzania ina wilaya nyingi zinazopakana na nchi jirani kama vile Zambia, Kenya, Malawi na DRC, lakini wenyeji wa huko hawasumbuliwi kama wanyambo. Pia walifafanua vizuri na kuonyesha kwamba wao si wahaya kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakifiria. Na wala Karagwe haukuwa utemi mdogo wa wahaya: Karagwe sio utemi mdogo wa kabila la Wahaya kama ambavyo walio wengi wamekuwa wakiamini. Karagwe Kwa asili ni wilaya ya kabila la Wanyambo(Ab'hanyambo) na lugha yao ni Orunyambo. Kuwaita Wahaya ni kuwanyang'anya haki yao ya msingi ya kuwa kabila kubwa na huru linalojitegemea. Kuna Wahaya wachache waliohamia Karagwe katika harakati za kutafuta makazi na udongo wenye rutuba, nao wamejikita sana maeneo ya Keiso(Kaisho) na Mab'hira(Mabira) Upo ushahidi wa kutosha wa maandishi unaoelezea kabila la Wanyambo na jinsi mwingiliano wao na makabila mengine ulivyokuwa. Wahima wafugaji waliingia Karagwe miaka mingi iliyopita; hivyo kuna wahima-wanyambo wanaoishi Karagwe; hawa wamekuwa wakisumbuliwa na watu wasioijua historia ya Tanzania, kwamba wahima ni Wanyarwanda na baadhi yao walirudishwa kwa nguvu Rwanda wakati wa harati za kurudisha wahamiaji haramu. Jamii ya wahima ni wafugaji; kama walivyo Wamasai, hawa hawana habari ya mipaka; hivyo kuna wahima Rwanda, Burundi, Uganda na Tanzania. Wanahama kutafuta malisho ya mifugo yao. Kwa vile ardhi ya Karagwe ina rutuba na ukubwa wa kutosha, wahima walioingia Karagwe, walifanya makao. Kuna Wanyarwanda waliokimbilia Karagwe, na sasa hivi wanaishi Karagwe kama sehemu ya wanyambo wa Karagwe. Pia kuna warundi waliokuja Karagwe kwa lengo la kufanya kazi ya vibarua na wamebaki; wameoleana na wanyambo, nao sasa ni sehemu ya wanyambo wa Karagwe. Makabila ya Wakiga na wanyakonle wa Uganda, nao walihamia Karagwe na kuwa wanyambo wa Karagwe. Jambo la pili walilolisisitiza kwenye risala yao ni juu ya wilaya yao ambao hivi sasa imetengwa na kuwa wilaya mbili za Karagwe na Kyerwa. Huko nyumba walikuwa na majimbo mawili ya uchaguzi kwa majina hayo hayo ya Karagwe na Kyerwa. Lakini sasa kwa sababu ya kutotaka kupoteza historia ya wanyambo wa Karagwe, wanapendekeza wilaya zao hizo mbili ziitwe Karagwe Kaskazini na Karagwe kusini. Wanataka wilaya zoa hizo mbili ziwe na neno Karagwe! Ni imani yangu kwamba Mheshimiwa Waziri Dkt Nchimbi, bado anaikumbuka risala hiyo. Leo hii kwa vile yeye ni waziri wa Mambo ya Ndani, risala hii ni muhimu kwake zaidi kuliko mwaka jana. Mwezi wa nane, Waziri Nchimbi alifanya ziara wilaya ya Karagwe na kuongea na wananchi juu ya mgogoro wa wafugaji na hasa wahima waliobatizwa jina wahamiaji haramu. Habari zinazotoka Karagwe ni kwamba serikali ina mpango wa kuendesha zoezi la kuwarudisha kwao kwa nguvu wahamiaji haramu ambao kwa wingi ni Wahima. Swali la kujiuliza ni je wahima hawa wanarudishwa kwao wapi? Kwa kufuatana na historia ambayo wanyambo waliyomweleza Waziri Nchimbi mwaka jana kwenye tamasha la wanyambo, wahima wa Karagwe, si wanyarwanda! Hivyo kusema watarudishwa kwao Rwanda, ni kinyume cha haki zote za binadamu tunazozijua na kuziheshimu. Pia, nina imani Rwanda, hawawezi kuwapokea wahima wa Karagwe, maana hawa si wanyarwanda! Hata kama baadhi ya wahima wanazungumza vizuri kinyarwanda hii haina maana kwamba wao ni wanyarwanda. Mimi naongea kinyarwanda, lakini mimi si mnyarwanda, naongea kinyankole lakini mimi si mnyankole, naongea kiingereza lakini mimi si mwingereza, naogea kijerumani lakini mimi si mjerumani. Najua kuna wanaopinga msimamo kama wangu, lakini ni muhimu tuyaandike, maana kilichoandikwa kimeandikwa. Historia itahukumu, na wakati huo ukifika, watakaokuwepo watambue jitihadi zilizokuwepo za kujaribu kulielezea jambo hili. Ikitokea nguvu zikatumika kuwaondoa wahima na kuwapeleka popote ambako serikali inafikiria, hatuwezi kukwepa hukumu ya historia. Leo hii jambo hili litafanyika kiushabiki, kulinda maslahi binafsi, kulinda maslahi ya vyama vya siasa; lakini ikumbukwe kwamba ni dhambi kuwabagua watu na kuwafanyia ukatili kwa kisingizio cha nchi zao za asili. Lakini pia nina imani kubwa kwamba kuna watu wanaounga mkono msimamo wangu; tatizo ni woga kujitokeza kupigania haki za watu hawa wahima wasiokuwa na hatia; wanaogopa kulaumiwa na labda kupotesa nafasi zao za kazi. Hivyo suala la wahima wa Karagwe, ni lazima lishughulikiwe kwa busara na hekima vinginevyo ni kujiingiza kwenye mgogoro usiokuwa wa lazima. Likishughulikiwa kwa lengo la kulinda maslahi binafsi, litatutesa wote. Wahima, ni kabila ambalo limeishi miaka mingi katika maeneo ya maziwa makuu. Wamekuwa wakihama kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta malisho ya mifugo yao. Mipaka ya wakoloni ndo iliwatenganisha Wahima wa Burundi, Wahima wa Rwanda, Wahima wa Uganda na Wahima wa Tanzania. Hata hivyo Wahima hawa wamekuwa wakivuka mipaka ya nchi hizi bila kujali vitambulisho wakiwa katika harakati zao za kutafuta malisho. Kwa maana hii basi, Wahima wamekuwa wakitoka Uganda, Rwanda na Burundi na kuja Tanzania kutafuta malisho ya mifugo yao. Lakini kuna wahima ambao wamekuwa wakiishi Tanzania miaka yote. Wanazunguka wilaya za Mkoa wa Kagera, bila kuvuka mipaka ya nchi. Mkoa wa Kagera unazalisha maziwa mengi na nyama kutokana na wafugaji hawa wahima. Kwa sura wahima wanafanana na Watutsi. Bila vitambulisho na mpango wa kudumu juu ya wahamiaji haramu, wahima wote watachukuliwa kuwa ni wahamiaji haramu. Wilaya ya Karagwe, ambayo ina wahima wengi, imekuwa ikitajwa kuongoza kwa kuwa na “Wahamiaji haramu”. Ukweli ni kwamba baadhi ya “Wahamiaji haramu” hawa ni wahima na kufuatana na mipaka ya kikoloni ya 1884? Hawa ni watanzania! Hawa wahima wa Karagwe, wamesumbuliwa sana. Baadhi yao wamefungwa mara nyingi na kutozwa “hongo” ya ng’ombe. Kwa kutotaka usumbufu, wahima hawa wamekuwa wakitoa ng’ombe na fedha kwa viongozi wa serikali na wafanyakazi wa Uhamiaji ili wasikamatwe na kupelekwa Rwanda. Hata hivyo kuna baadhi waliokumbwa na zoezi hili la kupelekwa Rwanda. Walinyang’anywa mifugo yao, kwa maneno mengine walinyang’anywa maisha yao na kupelekwa ugenini Rwanda. Kuna haja kubwa ya kuwa na mpango wa kudumu juu ya jamii hii ya Wahima. Kama ilivyo muhimu pia kuwa na mpango wa kudumu juu ya Wamasai wa Kenya na Tanzania na wasukuma wanaohama kutoka mkoa moja hadi mwingine wakitafuta malisho ya mifugo yao kiasi cha kuvuka hata mipaka ya nchi. Kule Sumbawanga, kuna habari kwamba wasukuma wameanza kuvuka na kuingia nchi jirani. Tunahitaji kuwatambua wahamiaji haramu na kuwatungia sheria na mpangilio wa kuendelea kuishi hapa Tanzania. Busara si kuwafukuza, maana kuna wahamiaji haramu wanaoweza kuishi hapa Tanzania kama wawekezaji; wanaweza kutoa kodi na kuchangia pato la taifa. Inawezekana kabisa kukaa kwao ndani ya nchi bila kibali, ni makosa yetu kama taifa kutokuwa na mpango wa kudumu kuhusu suala zima la wahamiaji haramu. Hivyo badala ya kelele za wabunge juu ya wahamiaji haramu, tunataka kusikia wakijadili mchakato wa kuanzisha mpango wa kudumu juu ya wahamiaji haramu na sheria ya kusimamia mpango huu. Hayo ndiyo mambo ya kujadiliwa na wabunge makini, si kulalamika bali ni kutafuta majibu na kupanga mipango ya kusonga mbele. Wahima, maisha yao yanategemea mifugo ni kama walivyo wamasai. Wanaishughulikia mifugo yao, wanafanya kazi kwa nguvu na wana mifugo mingi. Na kusema kweli wahima ni matajiri, wanauza mifugo yao, wanapata fedha. Hali hii ya kuwa na fedha na mifugo mingi inaleta aina ya wivu miongoni mwa jamii inayowazunguka wahima. Ni vita ile ile tunayoisikia sehemu mbali mbali za Tanzania ya wakulima na wafugaji. Lakini tatizo la Karagwe ni tofauti kidogo, mbali na malalamiko ya wakulima ya mifugo kuingia kwenye mashamba yao na wafugaji kumiliki ardhi kubwa, kuna tatizo sugu la baadhi ya wakulima wanaotaka nao kuwa wafugaji. Wakulima hawa nao wameanza kumiliki ardhi kubwa na wana mifugo mingi; baadhi ya hawa wako kwenye vyombo vya maamuzi na wengine ni wafanyakazi serikalini. Hawa kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakichochea mgogoro huu wa wahima, ili wahima wakiondoka wamiliki ardhi yao na kununu mifugo yao wa bei ya kutupwa. Wale wanaopiga kelele kwa nguvu kwamba wahima warudi kwao, ni wale waliojiingiza kwenye ufugaji na sasa wako kwenye harakati za kumiliki ardhi kubwa. Ukilitazama suala hili kwa umakini ,mgogoro huu unazalishwa na wafugaji ambao si wahima. Ni wivu na wala si mgogoro wenye msingi wowote. Wilaya ya Karagwe ina matatizo sugu yanayohitaji majibu ya haraka. Mfano tatizo la maji, tatizo la barabara, tatizo la kuuza kahawa kwa magendo, “Butura” na “Ebyenju” na matatizo mengine kama shule, hospitali na kutokuwa na masoko bora ya mazao. Nguvu kubwa zinaoelekezwa kuwashughulikia wahima, zingeelekezwa kutanzua matatizo hayo niliyoyataka hapo juu, taifa letu lingepiga hatua kubwa ya maendeleo. Tusipoteze muda mwingi kuwafukuza wahima, maana hawana mahali pengine pa kwenda zaidi ya kuishi hapa nyumbani Tanzania. Na, Padri Privatus Karugendo, +255 754 6331 22 www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment