KWANINI MADAKTARI WASIPATE MSHAHARA WA MILIONI 3? Nimezoea kuzisikiliza hotuba za Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, anazozitoa kila mwisho wa mwezi.Ni utamaduni mzuri ambao unaweza kuboreshwa kwa kuruhusu maswali ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Rais. Maana Rais, ni kiongozi wa nchi, fursa hii ya kuongea na kujadiliana na wananchi inaweza kuchangia ufanisi wa uongozi wake. Mfumo wa sasa wa kutoa hotuba bila maswali kutoka kwa wananchi, unaibua mambo mengi ambayo wakati mwingine Mheshimiwa Rais anakuwa amepotoshwa; kama maswali yangeruhusiwa, labda ufafanuzi zaidi ungefanyika kwa faida ya pande zote mbili. Hotuba yake ya mwisho wa mwezi wa Juni mwaka huu, ilijikita kwa kiwango kikubwa juu ya sakata la madaktari. Rais, alisisitiza kwamba serikali haina uwezo wa kuwalipa madaktari mshahara wa milioni tatu wanapoanza kazi. Sina lengo la kubishana na Mheshimiwa Rais, bali ni kuuliza ili kufahamu, pia ni kutaka kuonyesha kwamba kama tungekuwa tunauliza maswali,utata wa mambo mengi ungekuwa unapungua. Swali langu ni: Kwanini madaktari wasipate mshahara wa milimioni 3? Ina maana milioni 3, ni nyingi ukilinganisha na kazi wazifanyazo madaktari? Wanakesha wakihudumia wagonjwa, daktari mmoja anahudumia wagonjwa wengi ukilinganisha na nchi nyingine; hawafanyi kazi kwa kufuata saa, kila wakati wako kazini. Ina maana hakuna watanzania wengine wanaopata mshahara wa milioni 3? Ina maana serikali haina fedha za kulipa mshahara huo? Ina maana serikali yetu inaishi na kutenda kwa kuonyesha dunia nzima kwamba haina uwezo wa kulipa mshahara wa milioni 3? Kama serikali ina uwezo wa kununua magari ya milioni 300, na si gari moja – magari mengi! Itaweza kushindwa kulipa mshahara wa milioni 3? Serikali ina uwezo wa kununua ndege ya rais na kuitunza, itashindwa kulipa mshahara wa milioni 3? Serikali inaweza kufanya sherehe za Uhuru (Miaka50) kwa kutumia mabilioni ya fedha; na kusimama kusema haina uwezo wa kulipa mshahara wa milioni 3? Kuna mambo ambayo watu wa nchi za nje wakiyasikia watatushangaa. Wanakuja hapa tunawapokea kwa mabenzi ya gharama kubwa, alafu wasikie tunasema hatuna uwezo wa kulipa mishahara? Wanashuhudia tunavyowapeleka viongozi wetu kutibiwa nchi za nje na kulipia matibabu hayo kwa fedha nyingi. Nimeona fedha iliyotengwa kwa matibu ya Marais wetu wastaafu, bajeti hiyo si ya nchi masikini kama tunavyotaka watu waamini, haionyeshi unyonge wetu wa kushindwa kumlipa daktari mshahara wa milioni 3. Sitaki kugusia dhahabu, Almasi, Utalii na utajiri mwingine mkubwa unaojionyesha wazi kwa matumizi ya viongozi wetu. Viongozi wetu wanasafiri daraja la kwanza kwenye ndege na kulala kwenye hoteli za daraja la kwanza wanapokwenda nje ya nchi. Dunia nzima inajua na pia sisi tunajua kwamba Tanzania si nchi masikini, viongozi wetu hawaonyeshi umasikini huo.Tukisikika tunaongea lugha ya kinyonge na kimasikini wanatushangaa na kuhoji uadilifu wetu wa mawazo na kujieleza. Hoja yangu ni kwamba, mtu anayetoa hoja ya kinyonge, hoja ya umasikini ni lazima awe mnyonge pia, ni lazima naye awe anaishi maisha hayo ya umasikini. Kinyume na hapo ni kujichanganya na kuwachanganya wengine kiasi cha kujiuliza kama tuna fikra pevu au tunaishi kwa vile tumeumbwa na kujikuta duniani? Naogopa kutumia maneno makali ya kutukana. Hatupendi kuambiwa ukweli kwa kisingizio cha kutukanwa. Naogopa yasinikute ya John Mnyika ya kutolewa nje ya Bunge. Kabla ya kutoa hoja yangu, niweke mambo sawa: Si kweli kwamba madaktari waligoma kushinikiza kulipwa mshahara; hili ni kati ya mambo mengine mengi kama vile kuboresha huduma za afya na kupata vifaa bora na vya kisasa. Kutanguliza na kusisitiza hoja moja ya mshahara ni kutaka kuwachonganisha madaktari na wananchi, na hili ni kuwakosea haki. Lakini kwa vile Mheshimiwa Rais wetu amelisisitiza hili la mshahara na kusema kwamba daktari ambaye ataona bila kulipwa milioni tatu hawezi kufanya kazi, basi ajiondoe; kuna haja kulijadili hili. Hawa madaktari wanaandaliwa kwa miaka mingi na kwa fedha nyingi, fedha zinazotokana na jasho la wananchi. Kusema kirahisi kwamba wasipotaka mshahara wa kimasikini waondoke, ni kuwakosea haki wananchi na kuendelea kuwabebesha mzigo wa kuwaandaa madaktari wengine ambao labda nao kesho na keshokutwa watalazimishwa kuondoka. Naanza mjadala huu kwa swali: Kwanini madaktari wasipate mshahara wa milioni 3? Serikali yenye uwezo wa kuanzisha wilaya na mikoa mipya, inaweza kutoa hoja ya kutokuwa na uwezo wa kuwalipa madaktari milioni 3? Zinapoanzishwa Wilaya na mikoa mipya, mbali na fedha nyingi zinazohitajika kuandaa miundombinu; serikali inawaajiri wakuu wa wilaya wapya, wakuuu wa mikoa wapya: Hao ni pamoja na wakurugenzi, Katibu tawala, OCD, Mganga mkuu na wafanyakazi wote wa wilaya na mkoa. Hao wote wanahitaji magari, wanahitai nyumba za kuishi na fedha za kuendesha ofisi. Kama fedha hizo zinapatikana kwa nini mshahara wa madaktari usipatikane? Labda hapa suala ni vipaumbele. Tunaweza kujiuliza serikali yetu ina vipaumbele vipi? Kuanzisha wilaya na mikoa, au kuwalipa madaktari mshahara mzuri ili waweze kufanya kazi ya kuhudumia afya ya watanzania na kuokoa uhai? Tunahitaji watanzania wenye afya na nguvu za kufanya kazi, au tunahitaji wilaya nyingi na mikoa mingi? Kuanzisha wilaya na mikoa, bila kuwa na uhakika wa afya na uhai wa watanzania ni kupoteza tu fedha za wananchi. Serikali yenye uwezo wa kuliendesha baraza kubwa la mawaziri, haiwezi kutoa hoja ya kushindwa kuwalipa madaktari milioni 3. Sipendi kujua mawaziri hawa na manaibu wao wanapata mshahara kiasi gani; swali langu ni je wanafanya kazi? Maana kuna wizara ambazo mbali na kujibu maswali Bungeni, kazi za manaibu waziri hazijulikani! Manaibu waziri nao ni wengi, wana mishahara, wana magari, wanapewa nyumba za kuishi na posho nyinginezo. Serikali ambayo ina uwezo wa kuliendesha Bunge lenye wabunge zaidi ya miatatu, haiwezi kuleta hoja kwamba haina uwezo wa kuwalipa madaktari milioni tatu. Mishahara na posho za wabunge ni nyingi kulinganisha na kazi wanayoifanya.Tunashuhudima mara nyingi viti vikiwa wazi Bungeni; hata wale wanaokuwa waaminifu wa kubaki ukumbini wengine wanasinzia, wengine wanapiga michapo, wengine kazi yao ni kutupiana matusi. Wabunge wasiozidi ishirini ndo wanafanya kazi ipasavyo. Kwa maana hiyo, tunaweza kuwa na Bunge la wabunge ishirini na mabo yakaendelea. Kwa mfano tukiwa na mbunge mmoja kila mkoa, tunaweza kupunguza ukubwa wa Bunge na kuweza kuokoa fedha za kufanya mambo mengine kama vile kuongeza mshahara wa madaktari wetu. Kushughulikia huduma ya maji na kuboresha huma ya afya kwenye hospitali zetu. Serikali inayowaruhusu watu kuingia Benki kuu na kujichotea fedha na kuondoka bila kuwawajibishwa, haiwezi kuleta hoja kwamba haina uwezo wa kuwalipa madaktari milioni tatu. Serikali inayoshindwa kuwadhibiti wawekezaji, wanakuja, wanachota fedha na kuondoka, haiwezi kule hoja kwamba haina uwezo wa kuwalipa madaktari mshahara wa shilingi milioni 3. Serikali inayoruhusu kuwepo na Mishahara hewa. Tunasikia mabilioni yamepotea kupitia mishahara hewa, na hakuna aliyekamatwa na kuwajibishwa; haiwezi kuleta hoja ya kushindwa kuwalipa madaktari milioni 3. Madaktari wanaishi Tanzania, wanashuhudia yote hayo. Hivyo wanapodai mshahara wa milioni 3, wanajua inawezekana. Wanawafahamu watu waliosoma nao, wanaofanya kazi kwenye maeneo mengine, wana mishahara mikubwa kuzidi hiyo ya milionni 3. Mfano mtu ambaye anakuwa kwenye msafara wa Mheshimiwa rais, ukizingatia safari nyingi za Rais wetu za kuomba misaada huku na kule, anakuwa na mshahara (posho) kiasi gani? Au mtu anayefanya kazi TRA, ana mshahara kiasi gani? Kama hawa wengine, ambao baadhi yao wanafanya kazi nusu nusu, wanalipwa vizuri, kwanini madaktari wetu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu na kuyaweka maisha yao hatarini wasilipwe milioni 3? Tukumbuke, daktari anashughulikia maisha ya watu. Hivyo ni lazima mawazo yake yawe yametulia wakati anafanya kazi na hasa kama anafanya upasuaji; kama kichwani mwake kuna mawazo ya ugumu wa maisha; kama anafikiri juu ya karo ya watoto, kama anafikiri juu ya pango la nyumba, kama anafikiri jinsi ya kupambana na abiria wengine kwenye dalala, kama anafikiria michango ya kijamii ambayo mtu huwezi kuikwepa labda kama unaishi peke yako mwezini, hawezi kuwa na utulivu unaohitajika kutekeleza kazi zake. Mshahara mzuri kama wanaoushikiniza kuupata, unaweza kusaidia kuwapunguzia madaktari wetu msongo wa mawazo na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kulinda uhai wetu. Mwanzo wa makala hii nilisema ni kuwakosea haki Madaktari, kwa kutuaminisha kwamba tatizo lao ni kulalamikia mshahara tu. Tumewasikia wakipiga kelele kwamba hospitali zetu hazina vifaa. Tumesikia serikali ikisema kwamba madaktari wakiendeleza mgomo, itawatafuta madaktari kutoka nje ya nchi na kuwaomba madaktari wastaafu kurudi kazini. Na hapo ndo tunajiuliza swali: Je hao madaktari kutoka nje ya nchi, watakuja kutalii ama kufanya kazi? Kama hospitali hazina vifaa bora na vya kisasa, madaktari hao wageni watakuja kufanya kazi vipi au watakuwa ni madaktari wa miujiza kama ule wa Loliondo? Au kwa vile watakuja madaktari wa kigeni, basi vifaa vitapatakana? Madaktari wetu wanalalamikia viongozi wa serikali kwenda kutibiwa nchi za nje. Hoja yao ni kwamba fedha zinazolipia matibabu yao kule nje, zingeweza kununulia vifaa bora na vya kisasa na watu wengi wangenufaika kwa kutumia vifaa hivyo. Hii ni hoja ya msingi; kuendelea kuwabeza madaktari wetu kwamba wanataka mshahara mkubwa na kuyatelekeza maisha ya watanzania ni kuwakosea haki. Wengine wanapendekeza kwamba madaktari washitakiwe kwa kusababisha vifo vivyolivyotokea wakati wa Mgomo. Hatuwezi kufanya hivyo kablda ya kuiomba serikali iliyo madarakani kuwajibika kwanza kwa uzembe mkubwa wa kulishughulikia suala zima la mgomo wa madaktari. Pendekezo langu ni kwamba serikali yetu ipange vipaumbele vyake kulingana umuhimu wa mambo na kuutanguliza Uhai. Hakuna taifa linawoze kuendelea bila kuwa na raia wenye afya bora. Hivyo badala ya kuanzisha Wilaya na Mikoa, serikali iboreshe kwanza Wilaya na mikoa iliyopo; wananchi wapate maji bora na salama, wananchi wapate barabara nzuri, shule nzuri na hospitali nzuri. Serikali ihakikishe wahudumu wake, wanafanya kazi kwenye mazingira mazuri na salama. Madaktari wanaoshughulikia afya zetu, wapate mshahara mzuri na kuishi maisha bora na salama. Mwalimu, alitufundisha kwamba Kupanga ni kuchagu. Tukipanga vizuri; na kuainisha vipaumbele vyetu, Madaktari wetu watapata mshahara wa milioni 3 na kuzidi. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 633122 pkarugendo@yahoo.com www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment