UTOROSHWAJI WA MADINI, NINI KIFANYIKE? Wakati Serikali yetu inalalamika kwamba haina fedha za kutosha kuongeza mishahara ya madaktari na walimu; haina fedha za kutosha kujeng barabara zote kwa kiwango cha lami; haina fedha za kutosha kusambaza umeme nchi nzima; haina fedha za kutosha kusambaza maji nchi nzima; haina fedha za kutosha kununua dawa na kutoa huduma nyingine muhimu kwenye hospitali zetu; haina fedha za kutosha kutengeneza madawati, kujenga vyoo na kujenga nyumba za walimu, madini yetu yanatoroshwa mchana kweupe! Na la kushangaza zaidi, hakuna linalofanyika kuhakikisha madini haya hayatoroshwi tena na mbaya zaidi hakuna hatua zinalizochukuliwa hadi sasa kwa wale wanaoruhusu madini yetu kutoroshwa. Tunachoendelea kusikia, wimbo unachosha masikio ya wazalendo ni kwamba watanzania ni wapole, watanzania wanapenda amani na utulivu. Hata ukiwanyanyasa ,watasamehe na kusahau; hata ukiwaibia, wakakukamata watakusamehe na kusahau; hata ukiwapiga marisasi na kuwaua, wanaobaki watakusamehe na kusahau kabisa tukiko hilo la mauaji. Yametokea matukio mengi ya wizi wa fedha za umma, lakini wezi wa fedha hizo wamesamehewa na matukio hayo sasa ni historia. La kushangaza, watanzania hao hao, mtu akiiba kuku au kukwapua simu anapigwa hadi kufa. Watanzania hao hao mtu akichomoa elfu moja anavikwa tairi shingoni na kuchomwa moto. Ni utamaduni wa kushangaza kidogo au ni aina ya ujinga Fulani vile? Labda kuna wachambuzi wazuri wanaoweza kutegua hiki kitendawili? Vinginevyo ni ngumu uelewa. Wezi wakubwa hawaguswi, wezi wadogo wanachomwa moto! Maana yake ni nini? Juma lililopita kwenye kipindi cha Kipima Joto, kinachorushwa na ITV, kulikuwa na mjadala juu ya Utoroshwaji Madini. Kama sikosei Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Steven Maselle, alikuwa kwenye mjadala huo? Kama nimekosea, waliokiangalia kipindi hicho watanisahihisha. Mbali na Naibu waziri kukiri wazi kwamba madini yetu yanatoroshwa, alielezea tukio la kushangaza, kusikitisha au kwa manenno makali kidogo la “Kijinga”: Ni kwamba “Mwekezaji” mmoja alikuwa akitorosha madini yetu kwa nyaraka bandia. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar-es-salaam, wakatilia mashaka nyaraka hizo na kuwajulisha Wizara ya Nishati na Madini. Na kweli Wizara, iligundua kwamba nyaraka hizo ni bandia na kutoa maelekezo kwamba mtu huyo “Mwekezaji” asiruhusiwe kutoka nje ya nchi. La kushangaza, ni kwamba baada ya siku mbili, “Mwekezaji” huyo alisafiri na mzigo wake! Inawezekana namkosea haki Naibu Waziri, lakini kwa maoni yangu alielezea tukio hilo kana kwamba ni kitu kidogo. Hakuonyesha kuelezea tukio hilo kwa uchungu mkubwa;hakuonyesha kuongea kama Serikali, Naibu Waziri ni sehemu serikali; hakuonyesha kuguswa na kukerwa na tukio hilo au ni kwa vile ni tukio la “Kijinga” na la kutowajibika? Serikali, inasema “Mwekezaji” asisafiri. Ni mtu gani tena huyo mwenye madaraka ya kumruhusu kusafiri? Au serikali inajihujumu yenyewe? Na serikali ikianza tabia ya kujihujumu yenyewe, hiyo si tena serikali ya wananchi. Kwenye mjadala huo wa Kipima Joto, Naibu, waziri alikuwa akilaumu “Ukosefu wa ushirikiano”. Kwa maneno mengine ni kwamba bila ushirikiano wa idara zote: Uhamiaji, Usalama wa taifa, Wizara ya Nishati na Madini, Uongozi wa Uwanja wa ndege, madini yetu yataendelea kutoroshwa. Na je, huu si ujumbe tosha kwamba madini yetu yametoroshwa miaka mingi kwa mfumo kama huu wa kutumia nyaraka bandia; maana hata kama baadaya kukamatwa kwa nyaraka bandia, bado mzigo unapita na mtu anasafiri ni ujumbe mkubwa kwa watanzania wote. Ni ujumbe kwamba kuna kitu hakiko sawa katika serikali yetu. Nilijitahidi kupiga simu, ili nishiriki kipidi hiki na kuuliza maswali, lakini sikuweza kufanikiwa; Hivyo makala hii ni mchango wangu kwenye kipingi hicho cha Kipima Joto: Utotoshwaji wa Madini! Swali langu la kwanza ni: Nini kifanyike? Hili ni swali letu sote; viongozi na wananchi. Ni wazi ni lazima kuzuia utoroshwaji wa madini yetu; ni lazima kuwawajibisha wale wote waliokuwa wakiruhusu madini yetu kutoroshwa na endapo itagundulika kwamba kwa kufanya hivyo watu hawa wana utajiri mkubwa kupindukia, basi mali zao zifilisiwe. Serikali iunde mfumo mzuri wa kudhibiti madini yetu. Lakini pia ningependa kupata ufafanuzi kutoka kwa Naibu Waziri juu ya tukio nililolieleza hapo juu la “Mwekezaji” kutorosha madini wakati amekwishatiliwa shaka na maelekezo ya Wizara ya Nishati na madini kwamba mtu huyo asisafiri. Kama sikusikia vibaya, madini aliyoyatorosha yaikuwa na thamani ya milioni 800? Labda nilisikia vibaya. Vyovyote vile ni kwamba alitorosha madini yenye thamani kubwa: Je huyu ni Mwekezaji Mtanzania au wa Kigeni? Je, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutorosha madini? Je ana kampuni hapa Tanzania? Na je baada ya kutorosha madini hayo, alirudi Tanzania au amebaki huko huko? Maana yote haya hayakuelezwa kwenye mjadala. Jina la mtu huyu halikutajwa! Labda keshi iko mahakamani, maana sisi Watanzania kama keshi iko mahakamni haturuhusiwi kujadili kitu hata kwenye suala kama hili la mwizi wa rasilimali zetu. Ni aina ya ujinga Fulani vile? Ufafanuzi mwingine ambao ningependa watanzania waupate ni je kwa nini baada ya mzigo ule kutiliwa mashaka, na Wizara kudhibitisha kwamba nyaraka za mzigo huo ni bandia, “Mwekezazji” aliendelea kukaa na mzigo ule? Kwa nini mzigo huo haukutunzwa na Uongozi wa Uwanja wa ndege ua mamlaka nyingine inayohusika na masuala kama hayo? Kuacha kuhoji haya na kuendelea “Kucheka cheka” ni kutolitakia mema taifa letu. Na je, wahusika wote walioshirikiana kuruhusu “Mwekezaji” huyo na mzigo wake kuondoka, wamechukuliwa hatua gani? Kufaatana na maelezo ya Naibu Waziri kwenye mjadala wa Kipima Joto, ni kwamba Uhamiaji walielekezwa mtu huyo asisafiri. Sasa alisafiri kupitia wapi na kwa ruhusa ipi? Kwa nini Mkuu wa idara ya Uhamiaji asihojiwe au kujiuzulu kwa kashfa hii kubwa? Kama “Mwekazaji” huyu ana kampuni hapa Tanzania, ni hatua gani zimechukuliwa hadi sasa hivi? Kwa vile ametuibia na inawezekana amekuwa akituibia, siku zote, kwa nini mali zake zilizo hapa Tanzania zisifilisiwe? Inawezekana serikali imechukua hatua Fulani juu ya suala hili, lakini kwa vile Naibu Waziri, hakuelezea chochote juu ya hatua zilichokuliwa, hivyo sisi tunafikiri bado! Au ni siri? Sisi wananchi hatuna umuhimu wa kufahamu juu ya mwizi wetu? Maana katika taifa letu, siri ni muhimu kuliko hata uhai wa mtu. Mtu anatuibia mchana kweupe, bado tunaona fahari kutunza siri za mwizi wetu! Kwa vile tunayahitaji madini yetu na rasilimali nyingine kuendeleza taifa letu na kwa lengo la kufikia maisha bora kwa kila mtanzania, kuna ulazima wa kutengeneza mifumo ya uwazi ya kudhibiti utoroshwaji wa madini. Jambo hili linawezekana, tukijenga utamaduni wa kuwajibishana. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment