TUNAWASHUKURU SANA WALIOTUTUNZIA FEDHA ZETU BENKI ZA NJE! Watanzania tunalalamika! Mimi pia nimeambiwa mara nyingi kwamba ninaandika makala za kulalamika. Kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja aliyeniambia kwamba aliacha kusoma makala zangu kwa sababu kila nikiandika ni kulalamika. Aliniomba nitafute namna nyingine ya kuandika bila kulalamika. Ndo maana nilisita kuandika makala hii. Nilikuwa nikitafakari namna ya kuufikisha ujumbe huu;Tunawashukuru sana waliotutunzia fedha zetu benki za nje, sasa wakati umewadia rudisheni fedha zetu; nilijua nikiandika, yatakuwa ni yale yale ya “Watanzania wanalalamika”. Ikichukuliwa kwamba kulalamika ni kukata tama au ni kutokuwa na fikra pevu na ushupavu wa kupambana na hali halisi. Kulalamika bila matendo ni ishara ya kutowajibika! Kulalamika ni kutojiamini na kwa njia moja ama nyingine ni kutangaza udhaifu wa mtu mmoja mmoja! Nimewasikia wanasiasa wakikemea utamaduni wa kulalamika! Ingawa kwa kukemea kulalamika, wanafanya kitu kilele; ni kulalamika! Wabunge wana kazi ya kutunga sheria na kuisimamia serikali, lakini wakianza kuchangia ni kulalamika tangia mwanzo hadi mwisho, na bahati mbaya ni kwamba pamoja na kulalamika kwao, bado wanapitisha kila kitu asilimia zote. Waandishi wa habari wanalalamika, wasomi wanalalamika, viongozi wa dini wanalalamika, watoto wanalalamika, wazazi wanalalamika, wanasiasa wanalalamika, wafanyakazi wanalalamika, viongozi wa serikali wanalalamika hadi Rais wa nchi analalamika! Nina mashaka kama kuna mtu ambaye hadi leo hii ameweza kupambanua, kuchambua na kueleza kwa ufasaha maana nzima ya neno “Kulalamika”. Inawezekana tunachanganya Kulalamika na kuomboleza? Inawezekana tunachanganya kulalamika na kuonya, kusahihisha, kutoa maoni, kurekebisha? Kulalamika ni chanya au ni hasi? Yesu Kristu, alipomlilia Mungu wake pale msalabani alikuwa analalamika? “Mungu wangu.. mbona umeniacha”. Orodha ya yale yanayolalamikiwa ni kubwa. Tukisema watanzania ni wazembe ni kulalamika, tukisema rushwa ni kansa ya taifa letu, ni kulalamika, tukisema wanaouza madawa ya kulevya ni watu wa hatari na hawana upendo na taifa lao, ni kulalamika. Rais wa nchi alitangaza wazi kwamba anawafahamu watu hawa kwa majina, lakini hadi kesho hakuna hatua zilichokuliwa. Yesu, alikuwa analalamika, au alikuwa akipiga kelele kwa Mungu wake? Pamoja na kilio chake, kwa kuukubali msalaba, akatukuzwa na kuwa njia ya kupitia kuelekea maisha mapya; maisha ya kiumbe kipya; maisha ya kuishi na kumtumaini Mungu muumba mbingu na nchi; Mungu wa haki, wema na Huruma? Yawezekana na watanzania tunapiga kelele kwa Muumba wetu? Yawezekana tunaomboleza? Tukijua wazi kwamba hata tukikaa kimya kwa kuogopa kupachikwa jina la sifa za “ Kulalamika” hata mawe yatasimama na kuimba sifa za Mungu, aliyeumba Mbingu na Dunia. Tunajua wazi kwaba tukikaa kimya tutahukumiwa na historia! Tumesikia habari kwamba kuna watanzania wameficha fedha nyingi kwenye mabenki ya nje na hasa Uswisi. Na habari hizi si mpya, maana kuna wakati tulisikia kwamba kuna mtanzania ameficha fedha nyingi kwenye benki ya Afrika ya Kusini. Habari zote hizi ni mwendelezo wa wimbo ule ule wa kulalamika bila kupendekeza hatua za kuchukuliwa. Ndo maana nimeamua kuandika kwa mfumo mwingine wa kuwashukuru wale wote waliotusaidia kutuwekea fedha zetu kwenye benki za nje, tuna imani kwamba fedha hizo sasa hivi zimezaa kiasi cha kutosha, wakati umefika fedha hizo wazirudishe nyumbai ili tujenge taifa letu changa. Ninapoandika makala hii sijasikia tamko la Mheshimiwa Rais wetu kuhusiana na sakata hili la baadhi ya watanzania kuweka au kuficha fedha nyingi kwenye benki za Ulaya. Nina imani ana masikio ya kusikia; yamesemwa mengi juu ya upole wake, yamesemwa mengi juu ya Ombwe, yamesemwa mengi juu ya “Udhaifu”. Nimeanza makala hii kwa kutaja “kulalamika” kwa watanzania hadi Rais mwenyewe. Hivyo hakuna anayetegemea na kwa hili Rais, akubali kuendelea kuwapandisha chati wale wanaomkandia kila siku ya Mungu. Asilalamike, bali achukue hatua. Akisema fedha zinarudi, hata kesho zitakuwa zimefika hapa. Kwa neno lake moja tu, yatakuwa! Mungu, alivyo mwema daima, amemjalia Rais wetu kitu cha kumsaidia kuacha kumbukumbu chanya nyuma yake. 2015 si mbali, akiondoka madarakani tumkumbuke kwa kurudisha fedha zetu zilizokuwa zimewekwa nje ya nchi. Ingawa hakuna mwenye kujua fedha hizo ni kiasi gani; hapana shaka kwamba fedha hizo zinaweza kusaidia kulipa mishahara ya walimu, kulipia elimu ya juu, kununua vifaa vya kisasa kweye hospitali zetu, kulipa mishahara ya madaktari na kusaidia kiasi Fulani kuendesha bajeti ya serikali yetu. Sote tunajua kwamba kuna asilimia inayotoka nje kusaidia serikali kuendesha bajeti ya kila mwaka. Inawezekana kabisa kwamba fedha hizo zinazotoka nje ni pamoja na faida inayotengenezwa kutokana na afedha zetu zilizofichwa kwenye benki za nje. Wakati sisi tunaamini “wahisani” wana roho nzuri ya kutusaidia, kumbe ni wajinga ndio waliwao; wanatuletea mafungu kutokana na fedha zetu wenyewe. Ni lazima kuikataa hali hii na kuhakikisha hali hii haijirudii tena! Wazungu hawa wanashinikiza demokrasia na utawala bora; wanasisitiza uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma, Wazungu wamependekeza mipango mingi ambayo inaweza kuisaidia Tanzania kupiga hatua kubwa ya manedeleo. Itakuwaje wazungu hawa hawa wakae kimya wakiona fedha nyingi zinachotwa Afrika na kuwekezwa kwenye mabenki ya Nje? Ina maana wazungu hawa wanaamini kwamba wale wanaoweka fedha kwenye benki zao wanakuwa wamezitafuta fedha hizo kwa jasho lao? Inawezekana wana kaa kimya kulinda uchumi wa nchi zao? Inawezekana ni wao wanawashawishi watu wetu kuficha fedha hizo kwenye benki zao? Rais wetu akiweka pembeni upole wake, akiweka pembeni roho yake ya huruma ya kuogopa kuwaonea watu, ati kuchukua hatua ni lazima ahakikishe kwamba haki inatendeka – hata kwa wezi ambao aliwaomba warudishe fedha walizozichota benki kuu na kuwasamehe kwa kosa hilo, Rais wetu akiweka mbali urafiki na kufumba macho hata kwa wale ambao anajua fika walimsaidia kuingia Ikulu, fedha hizi zilizofichwa nje ya nchi zitarudi na zitachangia kwa kiasi kikubwa kuharakisha kasi ya maendeleo katika taifa letu. Kama walioficha fedha hizi ni wafanyabiashara, ambao wanajulikana kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha ziada, wafanyabiashara ambao wanalipa ushuru wao kwa uaminifu, ni lazima Rais wetu awe na kigugumizi cha kuchukua hatua dhidi ya watu hawa walioficha fedha kwenye benki za nje. Lakini kama wenye fedha hizi ni waajiriwa wa serikali ambao kipato chao kinategemea mshahara na posho, kwa nini Rais wetu awe na kigugumizi? Mfanyakazi wa umma atapata wapi fedha nyingi hivyo? Haiwezekani ukawa ni mshahara wake. Kutaka mtu huyu apate haki yake kwa njia zozote zile ni kukubaliana na wale wanaofikiri Rais wetu ni dhaifu. Mtu mwenye kipato kikubwa ambacho hakina maelezo ni mwizi. Haki za mwizi ni hukumu! Na hukumu ya wezi hawa ni kuwashukuru kwa kututunzia fedha zetu kwa miaka yote hiyo na sasa wakati umefika wa wao kuturudishia fedha zetu. Kuwataja kwa majina si dhambi pia, ingawa kuwanyonga ni kukiuka Haki za binadamu. Ili kumsaidia Rais wetu abaki kwenye mstari wa kuhakikisha haki inatendeka, mstari wa kuhakikisha hakuna anayeonewa, wale watakaoweza kuhakikisha njia walizozitumia kujipatia kuyapata mamilioni hayo, basi waachiwe asilimia kidogo ya fedha hizo ili waweze kuendesha maisha yao na kufurahia matunda ya kazi zao. Lakini kama fedha hizi wamezipata Serikalini, zichukuliwe zote bila ya huruma yoyote ile. Washitakiwe kama wahujumu uchumi na sheria ifuate mkondo wake. Bajeti ya mwaka huu, tumesikia kwamba Barabara ya kutoka Kyaka hadi Bugene, kule Karagwe imepangiwa Bilioni nne. Wanaofuatilia kwa karibu takwimu za Bunge, wanasema haijawahi kutokea fedha zilizotengewa kitu Fulani kwenye bajeti zikapelekwa zote zehemu husika. Kama hilo ni kweli, fedha hizi zilizotengwa kwa ujenzi wa barabara ya Kyaka – Bugene, zitafikishwa Bilioni mbili tu. Barabara hii ambayo inatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili inahitaji bilioni 60 kukamilika. Bila miujiza kama ule wa kurudisha fedha zilizofichwa Ulaya, barabara hii itakamilika mwaka gani? Si chini ya miaka 10 kuanzia sasa. Nimetoa mfano wa barababa ya Kyaka – Bugene, lakini ukweli ni kwamba Wizara zote zinalalamika kutengewa fedha kidogo za miradi ya maendeleo. Na bila kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo, bila kuwekeza kwenye utafiti, bila kuwekeza kwenye elimu, bila kuwekeza kwenye afya ili kuhakikisha watanzania wanabaki na afya nzuri na nguvu za kuzalisha hatuwezi kufika mbali kama taifa! Naandika makala hii kupiga kelele juu mbinguni! Naandika makala hii kukukaribisha wewe msomaji wangu kuniunga mkono tukashirikiana kupiga kelele. Tushirikiane kupiga kelele na kushinikiza hadi fedha zetu hizi zilizowekwa kwenye mabenki ya Ulaya, zirudishwe haraka iwezekananvvyo. Tuandike makala, tutangaze kwenye vyombo vyote vya habari, tufanye maandamano ya amani hadi Serikali itoke usingizini. Siandiki kuchochea, yule atakayefikiri ninaanzisha uchochezi atakuwa na lake jambo. Nina imani kwamba ni muhimu wachache wakajitoa muhanga ili kuokoa maisha ya watanzania wengi. Wakati wa maneno maneno umekwisha, enzi hizi ni za kuchukua hatua, ni enzi za kufanya maamuzi magumu. Wakati wa siasa za kuchafuana umepita; wakati wa siasa za kugombania kuingia Ikulu kwa gharama yoyote ile unaelekea mwisho na wala hauna faida yoyote ile kwa maendeleo ya watanzania. Ni enzi za kutanguliza taifa letu badala ya kutanguliza matumbo yetu. Ni enzi za kulitanguliza Taifa letu badala ya kuvitanguliza vyama vyetu vya siasa, si wakati tena wa kujenga na kutafuta sifa za mtu mmoja mmoja, ni wakati wa kujenga jina la taifa letu la Tanzania. Ni enzi za kulitanguliza taifa letu badala ya kutanguliza mambo mengine yasiyokuwa ya msingi. Ingawa fedha hizi zilizofichwa nje ya nchi haziwezi kumaliza matatizo yetu yote; Hatua itakuwa imepigwa uongo na ukweli vitakuwa vimejitenga! Waliokuwa wanalalamikia serikali yetu kutokuwa na fedha, watagundua ukweli ambao siku zote tuliusimamia kwamba nchi yetu si maskini. Rais wetu akifanikisha zoezi hili la kurudisha fedha zetu zilizowekwa nje ya nchi kwa kutumia madaraka yote aliyonayo, atakumbukwa milele! Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 6331 22. www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment