JE! SASA NA HILI LIMEPITA? Niungame wazi kwamba nilipoandika makala yangu ya wiki iliyopita yenye kichwa cha habari “MTAMBO WA KUINGILIA MAWASILIANO YA SIMU: CHADEMA WANGEFANYA SUBIRA!”, sikujadiliana na mtu yeyote na nilikuwa sijapata habari zaidi juu ya suala hili zaidi ya yale niliyoyaona na kuyasikia kwenye taarifa ya habari. Hivyo na mimi sikuwa na subira nikafanya haraka kuwanyonyeshea CHADEMA kidole lakini kwa nia njema. Hoja yangu ya msingi ilikuwa ni kumkamata mtu huyo kwanza ndipo atangazwe. Nilikuwa naona ugumu wa kumwajibisha mtu huyo bila kuwa na ushahidi wa kutosha na hasa kumkatamata akiwa kazini. Pia nilihofu uwezekano wa mtu huyu kuficha mitambo yake mara baada ya kutambua kwamba njama zake zimegundulika. Kwa mtazamo wangu, nilifikiri mtu wa aina hii ni lazima ashughulikiwe na kujua malengo lake na kujua anatumwa na nani? Anatumwa na baba yake? Anatumwa na kikundi cha matajiri Fulani au anafanya kazi peke yake kwa manufaa yake mwenyewe? Je mtambo huo wa kuingilia mawasiliano ya watu ni kati ya mbinu za kugombea madaraka 2015? Nilifikiri maswali kama haya, ambayo ni muhimu kwa kila mtanzania yangejibiwa baada ya kumkamata “Jasusi” huyu. Leo, ninapoandika makala hii, tayari nimeongea na watu mbali mbali na kupata undani wa suala hili kwa mapana na marefu yake. Kumbe CHADEMA walichokifanya ni sahihi kabisa. Wangechelewa kufichua njama hizi za kijasusi, hali ingekuwa mbaya na baadhi ya wanachama wa CHADEMA wangefikishwa mahakamani na labda kufungwa kwa kosa la kutishia maisha ya mtu kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno. Kwenye utamaduni wetu uliojengeka wa kuitumia Mahakama kama kufunika maovu yote na kuwanyamazisha watu; kama wabunge wa Chadema wangekamatwa na kufikishwa mahakamani, mpango mzima wa kijasusi ungefanikiwa. Kesi ingeendelea miaka; Bungeni hakuna mtu angeruhusiwa kujadili; kwenye vyombo vya habari tungefungwa midomo maana kesi ingekuwa mahakamani; kuandika juu yake ni kuingilia uhuru wa mahakama. Pia tumesikia Bungeni ikitajwa wazi na kambi ya upinzani kwamba kuna mtambo wa kuingilia mawasiliano ya simu na hasa ujumbe mfupi wa maneno.Hadi leo hatujasikia serikali ikikanusha jambo hili, hivyo inawezekana kuna ukweli? CHADEMA, waliitisha vyombo vya habari na kusema wazi wazi kwamba kuna mtoto wa Kigogo, ameingiza mtambo kutoka Israeli, na kwamba mtambo huo ndo ulizalisha ujumbe mfupi wa vitisho aliotumiwa Kada wa CCM. Hadi leo hii hatujsikia serikali ama CCM wakikanusha jambo hili la mtambo wa kuingilia mawasiliano. Tunawafahamu CCM na serikali ya CCM walivyo wepesi wa kukanusha; kwa hili wamekaa kimya. Siwezi kusema wamedharau, maana huo si utamaduni wao. Ingawa kwa tukio la sasa mtambo huu umewalenga CHADEMA, inawezekana kesho na keshokutwa ukawalenga CCM wenyewe. Sasa hivi ndani ya CCM kuna kambi mbili kubwa. Kuna kambi ya Lowassa na kambi ya Membe. Kama mtoto huyu wa kigogo anayesemekana kuingiza mtambo huo yuko kambi ya Membe, basi na kambi ya Lowassa, haitakuwa salama. Na kama mtoto huyo wa kigogo yuko upande wa Lowassa, basi kambi ya Membe, haitakuwa salama. Vyovyote vile mtambo huu na mtoto huyu wa kigogo ni adui wa Umma. Huyu ataivuruga Tanzania, sitaki kuamini kwamba mtu huyu ana nguvu kuliko watanzania wote. Inawezekana ana nguvu ya fedha, lakini hawezi kuwa na nguvu ya umma. Swali ninalojiuliza kwenye makala hili ni Je, sasa na hili limepita? Hakuna wa kuwajibishwa? Hakuna wa kuhojiwa? Hakuna wa kushitakiwa? Tunaanzazisha utamaduni wa kuwa na Miungu watu? Watu wanaoweza kufanya lolote, wakati wowote na wasiguswe wala kuwajibishwa kwa vile ni watoto wa vigogo au ni vigogo wenyewe?Tunaendelea kulea azembe na kuendekeza matukio yasiyokuwa na tija kwa taifa letu? Hapa Tanzania tuna mambo mengi yanayoibuka na kuzimika bila jibu lolote na bila mbinu na mikakati ya kuhakisha mambo hayo “Mabaya” hayaibuki tena. MV Bukoba ilizama na kupoteza maisha ya watu, likapita na kana kwamba tukio hilo halijawahi kutokea, yakatokea matukio mengine kama hilo na kupita! Mabomu yakalipuka na kupoteza maisha ya watu, nalo likapita; yakaliputa tena mara ya pili, nalo hilo likapita! Lilipoibuka suala la Richmond, tulitegemea jambo hili lingefika mwisho wake na kuwekewa mikakati ili jambo hili lisitokee tena; la kushangaza ni kwamba la Richmond, lilipita na maisha yakaendelea kama kawaida na kesho na kesho kutwa kuna hatari ya kutokea Richmond nyingine. Likaibuka la EPA, nalo likapita! Likaja la Dowans, nalo kikapita! Balali, akafa na kuzikwa kule Amerika, nalo likapita! Likaja la Jairo, nalo likapita! Ulimboka akatekwa, akapigwa na kuumizwa vi baya sana; mshukiwa akakamatwa, hata bila kutuonyesha sura yake, tukaambiwa kesi iko mahakamani, hilo nalo limepita. Sasa na hili la mtambo huu wa kijasusi wa kuingilia mawasiliano ya watu unaomhusisha mtoto wa “Kigogo” nalo limepita? Katiba ya Tanzania, inazuia mtu kuingiliwa kwa mambo yake ya faragha. Kuingilia mawasiliano ni kuingilia mambo ya faragha na kuivunja katiba. Kwa maoni yangu, suala hili si la CHADEMA peke yao, hili ni la watanzania wote. Na hasa hili linawahusu zaidi Makampuni ya simu. Kama makampuni haya bado yanataka kuendelea kufanya biashara hapa Tanzania, ni lazima yafanye kazi ya ziada kurudisha imani ya watanzania. Maana kama mawasiliano ya wateja yanaingiliwa kwa makusudi mazima; ni wazi wateja wao wataanza kususia mitandao yao. Ni lazima kuwahakikishia wateja wao kwamba suala kama hili halitajirudia tena na punde likitoea, wao watakuwa watu wa kwanza kulitangaza na kumkamata mhusika badala ya jambo hili kugunduliwa na wateja wenyewe. Jambo la uhakika kufuatana na maendeleo ya teknolojia, makampuni ya simu ni lazima yanafahamu uingizwaji wa mtambo huu wa kuingilia mawasiliano. Kama ujumbe wa vitisho ulitoka CHADEMA, ni lazima makampuni haya ya simu yafahamu. Na kama haukutoka huko ni lazima wafahamu. Hivyo kwa suala hili ambalo linaelekea kuleta vurugu katika taifa letu, makampuni haya ni lazima yawe ya msaada mkubwa. Kwa vifaa vya kisasa kama GPS, ni rahisi kugundua mtu mwenye mtambo kama huo na sehemu aliyopo. Na hasa kama mtu huyu anaingilia mitambo ya makampni haya ya simu, ni kazi rahisi makampuni haya kumnasa mtu huyu na kumtangaza hata kama mtu huyu ni mtoto wa “Kigogo”. Ni dhambi kubwa kuliacha na ihili likapita. Mtu huyu ambaye ameanza mbinu chavu za kuingilia mawasiliano na kutengeneza ujumbe wa vitisho vya kutoa uhai anaweza kufanya mengine zaidi; anaweza kuanzisha vikundi vya kuteka watu na kuwatesa na wakati mwingine kutoa kabisa uahi wao; anaweza kutengeneza mitambo ya kuiba kura au kutengeneza mitambo ya kuiba fedha kwa kutumia mtandao. Vyovyote vile nia ya mtu huyu si njema na ni lazima watanzania tukawa macho na kuanza kuchukua hatua kwa watu wabaya na wenye nia mbaya na taifa letu la Tanzania. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 6331 22. www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment