UHAKIKI WA KITABU: MIAKA 53 YA UTUMISHI KATIKA POSTA NA SIMU AFRIKA 1941- 1993.
1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA
Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Miaka 53 ya utumishi katika Posta na Simu Afrika 1941 – 1993 na kimetungwa na Mzee Rajabu M. Yusuf. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Tanzania Publishing House Limited na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 9976 1 0212 3 kimechapishwa mwaka 2008 kikiwa na kurasa 132. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. UTANGULIZI.
Kitabu hiki ambacho bado hakijazinduliwa, kimeandikwa na Mzee Rajabu M.Yusuf. Kinaelezea kwa kifupi historia ya Posta na Simu katika Afrika kwa kadiri ya mtazamo wa mwandishi kwa kuhusisha uzoefu na mang’amuzi katika utumishi wa mwandishi. Kwa kifupi kitabu hiki kina ujumbe wa aina mbili: Maisha ya Mzee Rajabu M. Yusuf na Maisha Posta na Simu Afrika (1941- 1993).
Ni watu wa chache katika taifa letu waliofanikiwa kuifanya kazi kama alivyoifanya Mzee Rajabu M.Yusuf. Kama anavyosema Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, katika dibaji ya kitabu hiki “ Kihifadhiwacho kifuani hupotea, kiandikwacho karatasini hubakia...” Kitabu hiki kitatuelimisha wengi, maana kilichoandikwa kimeandikwa! Bahati mbaya watanzania walio wengi hatujakubaliana na msemo huu na kukubali kuandika chini yale tunayofahamu, yale tunayoyaishi na yale tunayoyashuhudia siku hadi siku. Mengi yanapotea na kusahaulika!
Kitabu kinazo sura 19, Kiambatisho na marejeo, ramani ya Afrika, ramani ya Afrika mashariki na picha zinazoonyesha matukio mbalimbali ya Historia ya Posta na Simu Afrika, paia na picha za mwandishi akiwa kwenye matukio mbali mbali na kwenye mikutano mbali mbali ya kimataifa. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.
III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.
Baada ya awamu nne za Uongozi wa taifa letu, kizazi kilichoshuhudia awamu zote hizi kinaanza kutoweka. Bila kuandika ushuhuda wa kizazi hiki, tutabaki bila historia. Bahati nzuri kuna maandishi ya historia ya Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere, pia kuna maandishi ya historia ya Marehemu Abed Amani Karume na wengine wachache kama vile Wanawake wa Tanu wakiongozwa na Bibi Titi. Wengine wanaondoka bila kuandika na hakuna kinachoandikwa juu yao.
Mzee Rajabu M. Yusuf, ameamua kutufanyia kazi hii. Ametuandika historia ya maisha yake na hasa historia ya kazi aliyoifanya kwa kipindi cha miaka 53! Kwa kusoma kitabu chake tunapata historia ya Posta na Simu. Kwa mfano tunatambua kwamba:
Kwa upande wa Tanganyika, koloni la Wajerumani la Afrika Mashariki lililojumuisha nchi za Tanganyika, Rwanda na Burundi, huduma ya Posta pamoja na ile ya telegrafu zilianzishwa mnamo mwaka wa 1893. Baada ya Vita vya kwanza vya dunia, huduma za Posta na Simu zilitolewa chini ya Idara ya Posta na Simu ya serikali ya kikoloni ya Kiingereza nchini Tanganyika. Wakati huo, nchi za Rwanda na Burundi ziliwekwa chini ya Serikali ya ukoloni wa Ubelgiji. Pia kwamba Benki ya Posta iliuundwa 1927 na kuwekwa chini ya uendeshaji wa Mkurugenzi wa Posta na Simu kwa niaba ya Hazina ya Serikali Kuu.
Kwamba kwa upande wa Kenya, huduma za Posta na simu zilianzishwa mnamo mwaka 1890 na Uganda huduma hii ilianzishwa mnamo mwaka wa 1895.
Ilipofika 1933 Idara za Posta na Simu za nchi tatu (Kenya, Uganda na Tanganyika) ziliungana na kuwa idara moja chini ya mamlaka ya Postamasta Mkuu. Makao Makuu yalikuwa Nairobi, Kenya. Wakati huohuo, kila nchi ilikuwa na Mkurugenzi wake aliyewajibika kwa Postamasta Mkuu, kupitia kwa Katibu Mkuu (Chief Secretary) wa nchi husika.
Kwamba mnamo mwaka wa 1948 iliundwa East African Posts & Telecommunications Administration. Tanganyika, ilipopata uhuru kulikuwa na mabadiliko na huduma hii ya Posta na simu ilijulikana kama East African Common Services Organisation (EACSO). Nchi tatu za Tanganyika, Uganda na Kenya zilipopata uhuru na kuunda Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, huduma ya Posta na Simu, ilibadilika na kuwa East African Posts & Telecommunication Corporation. Makao yake yakahamia Kampala Uganda.
Mwaka 1977 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilisambaratika, wakati huo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Posta na Simu wa Jumuiya hiyo, alikuwa ni mwandishi wa kitabu hiki, Mzee Rajabu Mabula Yusuf, mkataba wake ulimalizika Aprili 1978.
Tarehe 27.10.1977 Shirika la Posta na Simu Tanzania (TPTC) liliundwa ili kuchukua nafasi ya East African posts&Telecommunications Corporation. Na kuanzia 1Jaunari 1994 TPTC iligawanyika na kuunda Shirika la Posta Tanzania (TPC), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Hii ndiyo historia nzuri ya Posta na Simu, anayotuletea mwandishi katika kitabu chake. Labda bila historia hii mwandishi asingesukumwa na lolote kutuletea historia yake! Karibia maisha yake yote yamekuwa ni ya Posta na Simu:
Rajabu Mabula Yusuf, alizaliwa tarehe 8 Agosti 1924. Alipata elimu ya msingi Handeni Chanika mwaka 1931-1934, na shule ya kati mjini Tanga 1935 – 1938 na hatimaye elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Tanga mwaka 1939-1940. Kati ya 1941 na 1942 alipata mafunzo ya mawasiliano ya posta na simu, Dar-es-Salaam. Kadhalika, alipata mafunzo nchi za nje, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Marekani na Japani.
Amefanya kazi katika asasi za posta na simu kwa takriban miaka hamsini na mitatu, huku akishika nyadhifa mbalimbali. Mathalani, alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mkurugenzi Mkuu wa Posta na simu Afrika Mashariki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Simu Barani Afrika. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.
IV. MUHTASARI WA KITABU.
Sura ya kwanza inaelezea Historia ya Mawasiliano Duniani na mchango wa Posta katika Maendeleo. Hapa tunaelezwa mengi juu ya aliyeanzisha huduma ya mawasiliano na hatua za huduma hii kuanzia mfumo wa mawasiliano ulioendeshwa kwa njia ya maneno ya kinywa au kwa maandishi kwa kutumia matarishi wapanda farasi au waenda kwa miguu, mashirika ya dini yalianzisha kusafirisha barua hadi teknolojia mpya za “Analogue” na “digital”. Mawasiliano yameharakisha maendeleo na kuwasogeza watu karibu.
Sura ya Pili, mwandishi anaelezea historia ya Mawasiliano katika Afrika ya Mashariki. Hapa tunaelezwa jinsi hali ya mawasiliano ilivyokuwa katika Koloni la Wajerumani Afrika Mashariki, yaani Tanganyika, Rwanda na Burundi. Baadaye jinsi mawasiliano yalivyokuwa Tanganyika ilipokuwa chini ya utawala wa Waingereza. Pia tunaelezwa huduma ya Posta na Simu ilivyokuwa kule Uganda na Kenya na baadaye nchi hizi tatu zilivyounda umoja wa huduma hii baada ya Uhuru.
Katika sura hii ya pili, ndipo Mwandishi anaelezea maisha yake ya utoto, shule na wazazi wake. Yeye mtu wa Tabora, lakini wazazi waliishi Tanga na baadaye walirudi kwao Tabora.
Katika Sura ya Tatu, mwandishi anatuelezea jinsi alivyopata ajira katika idara ya Posta na Simu. Na jambo muhimu katika sura hii ni kujifunza kutoka kwake pale anaposema hivi:
“Maskini, baadaye nilikuja kugundua kwamba kumbe ningefanya makosa kutokana na uelewa wangu mdogo kuipuuza sekta hii. Kwa yamkini, mawasiliano ya Posta na Simu yana mchango mkubwa sana katika kuchochea maendeleo ya watu katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na sekta ya afya kitaifa na kimataifa. Maendeleo ya maana hayawezi kupatikana bila mawasiliano safi na ya kutosha. Niligundua pia kwamba Posta na Simu ndio ushirikiano mkongwe zaidi duniani ulio na manufaa kwa wanadamu wote. Kama nilivyoeleza chini ya Historia ya Mawasiliano Duniani kwa upande wa simu, ushirikiano huo ulianzishwa mwaka 1865 wakati ulipoundwa Umoja wa Simu Duniani (ITU) na kwa upande wa Posta wakati ulipoundwa Umoja wa Posta Duniani (UPU) mwaka 1874. Ni utaratibu wa ushirikiano wa kimataifa mkogwe zaidi kuliko hata Umoja wa Mataifa....” (Uk wa 15).
Hapa kuna funzo na kutusaidia kutambua kwamba ushirikiano wa Posta na Simu ni mkongwe. Hivyo mawasiliano ni chombo cha umoja kuliko mengine yote!
Sura ya nne, mwandishi anasimulia juu ya kipindi chake cha Mafunzo ya posta. Hapa la kujifunza ni huduma ya posta iliyokuwa ikitolewa kwenye vituo vya treni. Huduma hii iliyokuwa nzuri ilisitishwa miaka 1950 kwa sababu ya kukosa tija.
Sura ya tano na sita mwandishi anaelezea maisha katika vituo vyake vya kazi: Mbeya, Tukuyu, Dodoma, Tanga, Arusha, Bukene, Urambo, Tabora. La kujifunza ni uzalendo wa kukubali kufanya kazi sehemu yoyote ya Tanganyika na jinsi utendaji ulivyokuwa wakati wa mkoloni. Uwajibikaji ulikuwa mkubwa kuliko leo hii!
Sura ya saba, mwandishi anaelezea maisha yake katika nchi ya Kenya, alikokwenda kufundisha kwenye chuo cha Posta na Simu. Huko anatuelezea ubaguzi wa rangi kati ya Wazungu na Waafrika na kati ya Wahindi na Waafrika. Pia tunaelezwa vita vya Mau Mau na habari za ndoa ya kwanza ya mwandishi. Ndoa hii iliyofungwa 1951, ilidumu miaka 20 na kuvunjika 1971.
Sura ya nane, ni maelezo mengine juu ya vituo vya kazi alikoishi na kufanya kazi mwandishi: Tabora, Mpanda, Mwanza, Geita na Kigoma. Hapa tunasikia vuguvugu la Waafrika kutaka usawa katika kazi: “ Pale Mwanza chama chetu hakikuchoka kuwakumbusha viongozi wa Posta, Wazungu na Wahindi kwamba tulichokuwa tukidai kama wazalendo haukuwa upendeleo maalumu bali fursa sawa kwa wote. Utaratibu wa enzi hizo ulimweka Mzungu juu, Mwasia kati na mzalendo chini na kwa hiyo hata mishahara nayo ilichukua sura hiyohiyo hata kama Mwafrika alikuwa na elimu sawa au ya juu na uzoefu mkubwa kazini.” (Uk wa 43).
Sura ya tisa tunasimuliwa “Naizesheni” (Africanisation”. Kipindi cha Uhuru. Mwandishi anatumwa Uingereza kusoma zaidi juu ya Posta na simu na anafunga ndoa yake ya Pili mwaka 1962 na kwa bahati mbaya nayo inavunjika mwaka 1971.
Sura ya kumi na ya kumi na moja mwandishi anasimulia mkutano Mkuu wa 15 wa Umoja wa Posta Duniani, uliofanyikia Vienna na safari za mafunzo Amerika na Japani.
Sura ya kumi na mbili na simulizi juu ya kuundwa kwa jumuiya ya Afrika Mashariki na ndoa ya tatu ya mwandishi. Alifunga ndoa tena mnamo mwaka wa 1972.
Sura ya kumi na tatu ni simulizi juu ya Mikutano ya Kimataifa ambayo mwandishi alihudhuria: Mkutano wa 16 wa Umoja wa Posta Duniani, uliofanyikia Tokyo Japan 1969 na Mikutano mingine ya Kimataifa iliyofanyika 1971 na 1977.
Sura ya kumi na nne, ni simulizi juu ya Mwandishi kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Posta na Simu Afrika Mashariki. Utumishi wake hadi Jumuiya inakufa na Shirika la Posta na Simu Tanzania linazaliwa.
Sura ya kumi na tano, ni kuundwa kwa Umoja wa Simu Afrika, na Mwandishi akahamia Kinshasa kufanya kazi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Simu Barani Afrika.
Sura ya kumi n asita inaelezea Miradi mikubwa miwili ya kuunganisha nchi za Afrika kimawasiliano. Miradi hii ni PANAFTEL NA RASCOM. Sura ya kumi na saba na kumi na nane zinaelezea utumishi wa mwandishi ndani ya Shirika na Posta na Simu Tanzania. Yeye kama mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, matatizo na mafanikio ya Shirika hili.
Sura ya Kumi na tisa inaelezea matukio muhimu katika Historia ya Huduma za Posta na Simu Afrika mashariki.
V. TATHMINI YA KITABU.
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Mzee Rajabu M. Yusuf, mzee wa Posta na Simu!
Awali ya yote lazima niseme kwamba kwa kuangalia hadhira anayoikusudia mwandishi, kitabu hiki kinasisimua sana, ukikianza hutaki kukiacha. Masimulizi hayachoshi na kwa vile yanaelezea matukio ya kihistoria yanayovutia sana kuyasoma.
Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kuandika historia ya maisha yake na historia ya Posta na Simu. Au kwa maneno mengine Rajabu Yusuf ni Posta na Simu, na Posta na Simu ni Rajabu Yusuf. Kwa simulizi lake, yeye na Posta na Simu ni kitu kimoja.
Tatu. Mwandishi amefanya kazi nzuri ya kutufundisha juu ya historia ya mawasiliano. Ametufumbua macho pale anapoelezea kwamba Umoja wa Posta na Simu, ni mkongwe hata kuliko Umoja wa Mataifa. Hii ni elimu nzuri na kumbukumbu nzuri katika historia ya Taifa letu.
Nnne, Pamoja na umoja wa Posta wa dunia, tunapata somo hapa kwamba hata Umoja wa Afrika Mashariki, ulianza zamani hata kabla nchi hizi kuwa huru. Mwaka 1933, nchi hizi ziliendesha huduma ya mawasiliano kwa pamoja. Hivyo tunapoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, hatufanyi kitu kipya. Ikumbukwe pia kwamba Rwanda na Burundi zilikuwa zikishiriki huduma ya mawasiliano na Tanganyika kabla ya kuwa chini ya utawala Wabelgiji.
Tano, mwandishi amefanikiwa kutushawishi kutambua kwamba utumishi katika sekta ya mawasiliano ni utumishi unaogusa jamii zote za binadamu kwa ujumla kwa vile mawasiliano ni kiungo muhimu kati ya watu takriban katika nyanja zote za maisha yao kitaifa na kimataifa katika mahusiano yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na kisiasa, kiutawala, kiutamaduni, kibiashara na kiuchumi.
Sita, mwandishi ameonyesha jinsi alivyofanya kazi kwa uzalendo na uadilifu mkubwa. Pia anawashauri watanzania kuiga mfano wake. Lakini pia anahimiza serikali kuwalipa vizuri wataalamu wetu ili wasikimbie nchi yao kutafuta kazi nje ya nchi.
Saba, mwandishi anaonyesha wazi undugu wa watanzania, kwamba mtu anaweza kuishi na kupokelewa sehemu yoyote ile bila kujali kabila lake. Amekulia nakusomea Tanga, lakini nyumbani kwao ni Tabora – familia yao ilipokelewa vizuri Tanga, kama inavyopokelewa na kukubalika nyumbani kwao Tabora.
IV. HITIMISHO.
Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania wakitafute kitabu hiki na kukisoma. Kitabu hiki kinapatikana kwenye duka la vitabu la TPH Bookshop, mtaa wa Samora, ili wapate elimu juu ya historia ya mawasiliano Tanzania na historia ya mambo mengine mengi ya taifa letu, Afrika Mashariki, Afrika na dunia nzima ambayo mwandishi anayataja katika kitabu chake.
Lakini kwa upande mwingine, napendekeza Shiriki la Posta Tanzania, Kampuni ya Simu Tanzania na Tume ya Mawasiliano Tanzania, wampatie Mzee Rajabu M.Yusuf, tuzo ya pekee kwa kazi aliyoifanya ya kuandika historia ya taasisi zao;
Na pia kwa vile Mzee huyu anaonekana kufanya kazi kwa muda mrefu katika Mawasiliano, ni bora akipata kumbukumbu ya aina yoyote ile katika mashirika haya: Mfano mojawapo ya majengo au vyuo vyao kupewa jina la Rajabu Yusuf, kama njia mojawapo ya kumkumbuka na kutambua mchango wake. Huyu ni miongoni mwa watanzania wachache waliofanya kazi za umma ndani na nje ya nchi kwa uaminifu mkubwa, kuna haja ya kumtuza. Tumejenga utamaduni wa kuwakumbuka wanasiasa na kuwasahau kabisa wale wanaofanya kazi za Utumishi wa Umma.
Pendekezo jingine ni kitabu hiki kutumika kwenye shule na vyuo katika somo la historia. Lakini pia vyuo vya mawasiliano vinaweza kukitumia kitabu hiki kwa kumbukumbu za huduma ya mawasiliano katika Taifa letu na bara letu la Afrika kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment