AJALI NYINGI TANZANIA NI UZEMBE WETU ! Ni masikitiko makubwa kuwapoteza watanzania zaidi ya miamoja kwa siku moja. Ajali ya Mv Skagit, Imetuletea majonzi makubwa. Miezi tisa baada ya meli nyingine kuzama kule Zanzibar na kupoteza maisha ya watu wengi, Mv Skagit nayo inaendeleza majonzi haya ya kuwapoteza watu wengi kwa siku moja. Ingawa sasa hivi si wakati muafaka wa kuonyesheana kidole na kumtafuta mchawi wa ajali hizi, itoshe tu kusema kwamba ajali nyingi hapa kwetu Tanzania zinatokana na uzembe wetu sote na hasa uzembe wa serikali yetu. Ajali za barabarani, ajali za majini na wakati mwingine ajali za moto ni uzembe wa serikali. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba Mv Bukoba wakati inazama kule ziwa Victoria na kuyapoteza maisha ya watu zaidi ya elfu moja, haikuwa na sifa kabisa za kusafirisha abiria. Ilikuwa na kasoro kubwa ambazo ilikuwa nazo tangia kutengenzwa kwake. Siku inazama ilipakia watu wengi na mzigo kuliko kiwango chake; serikali ikitizama tu! Hata baada ya tukio hilo la kizembe, serikali haikuwajibika wala kuwajibishwa. Baada ya ajali ya Mv Bukoba zimetokea ajali nyingine nyingi kwenye ziwa Victoria na hatujasikia mtu kuwajibika wala kuwajibishwa. Kibali cha vyombo kusafiri ndani ya ziwa kinatolewa na Serikali. Inakuwa je serikali kutoa vibali kwa vyombo chakavu na vyenye hitilafu kuendela kusafirisha abiria? Ajali za barabarani ambazo zinatokea kila kukicha nazo ni uzembe wa serikali. Chanzo cha ajali hizi ni magari chakavu, matairi yasiyokuwa na viwango na yamekuwa yakipasuka ovyo na kusababisha ajali, mwendo kasi, magari kujaza kupindukia na wakati mwingine madreva wasiokuwa na viwango. Yote hayo yako chini ya udhibiti wa serikali. Na wala hili halina ubishi au itikadi. Serikali ikizembea kusimamia ubora wa vyombo vya usafiri na ajali ikatokea, ni lazima serikali iwajibike au iwawajibishe wahusika wakuu. Kuna matuko mengi ya moto na mara nyingi tunasikia ni hitilafu ya umeme. Ukweli ni kwamba vifaa vingi vya umeme havina ubora unaohitajika kuunganisha umeme majumbani na kwa matumizi ya kila siku ya umeme. Usimamizi wa ubora wa vifaa vya umeme na bidhaa nyinginezo zinazoingizwa nchini ni wa serikali. Kama soko letu lina bidhaa bandia, si kosa la mtu mwingine bali ni kosa la serikali. Hivyo hitilafu ya umeme ikitokea, moto ukateketeza mali na kupoteza maisha ya watu ni lazima serikali iwajibike. Kuna ajali nyingine kubwa ambayo kama haijatokea leo, basi itatokea kesho. Kwa kuingiza bidhaa bandia na hasa vyakula na dawa kuna kipindi watu watakufa kwa magonjwa yanayotokana na vyakula hivi na dawa hizi bandia. Mafuta ya kupikia yanachakachuliwa na kuingizwa vitu vya hatari kwa afya ya binadamu; tunasikia watu wanachanganya mafuta ya kupikia na mafuta ya transfoma ili kukaangia viazi; tunasikia kwamba dawa za binadamu zinachakachuliwa; mafuta ya kujipaka na mafuta ya kutengeneza nywele yanatengenzwa kwa kemikali kali na hatari. Ajali hii ya kutokana na vyakula na dawa bandia ikitokea ni wazi utakuwa ni uzembe wetu na uzembe wa serikali yetu. Hoja hii kwamba ajali nyingi msingi wake ni uzembe wa serikai yetu haifuati itikadi; na wala hapa tusiingize suala la dini. Kuna watu wanakuwa na mawazo kwamba tunaisahihisha serikali kwa vile Rais ni Mwislamu. Mawazo haya ni ya kupuuzwa. Ilipozama Mv Bukoba,Rais alikuwa mkristu, napo tulisimama kidete kukosoa uzembe wa serikali iliyokuwa madarakani wakati ule. Si lazima kuwa Mkristu au mwislamu kuutambua au kutoutambua ukweli wa uzembee huu wa serikali yetu, si lazima mtu awe CCM kuutambua au kutoutambu ukweli huu wa uzembe wa serikali yetu, si lazima mtu awe CHADEMA kuutambua au kutoutambua ukweli huu wa uzembe wa serikali yetu. Mtu yeyote mwenye akili timamu ni lazima auone ukweli huu. Tumejenga utamaduni kwamba mtu yeyote anayeisahihisha serikali ni mpinzani na hasa mpinzani wa CHADEMA. Hata kama hoja ni muhimu na inaweza kusaidia kujenga na kuliendeleza taifa, kama ina harufu ya kusahihisha, basi ni upinzani na ni CHADEMA. Pia tunataka kuficha udhaifu wetu nyuma ya udini. Tuache kusema ukweli, tuache kukosoa kwa kuogoa kunyonyeshewa kidole na CCM au na waislamu? Tanzania ni nchi yetu sote, waislamu, wakristu, wanaoamini dini za jadi na vyama vyote vya siasa. Hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine. Ingawa si haki kuibebesha serikali lawama za ajali zote zinazotokea; Kimsingi serikali ndiyo ya kwanza kuwajibika yanapotokea majanga ambayo serikali ina uwezo mkubwa wa kuyakinga, lakini pia na sisi wananchi tuna mchango mkubwa kwa ajali hizi, na chanzo ni uzembe wetu. Kukubali kutumia vyombo vichakavu bila kuhoji ni uzembe wa hali ya juu. Kukubali kupanda meli au gari la abirira lililozaja kupindukia, ni uzembe mkubwa. Wananchi kukubali kuyapokea majanga yote yanayotokea kwa uzembe wa serikali bila kuhoji na bila hatua zozote za kuiwajibisha serikali ni uzembe wa hari ya juu. Kasumba tuliyolishwa na tunayoendelea kulishwa na wajanja wachache ni kwamba ajali ni mpango wa Mungu na kwamba ajali haina kinga! Eti mpango wa Mungu hauna makosa! Tununue vyombo vya usafiri vichakavu, tununue matairi bandia, tununue vifaa vya umeme bandia, ajali itokee tuseme ni Mpango wa Mungu? Ni kutumia vichwa kufikiri au kutumia vichwa kufuga nywele? Ni Mungu gani huyu mwenye mpango hasi wa kuwatesa viumbe vyake?Huyu ni Mungu wa Tanzania peke yake au ni Mungu yule yule anayeruhusu maendeleo ya sayansi na teknolojia yenye uwezo mkubwa wa kuzuia majanga na ajali zisizokuwa za lazima katika nchi nyingine? Nchi nyingine zikitokea ajali kama hii ya Mv Skagit, watu wanaokolewa kwa muda mfupi, sisi inatuchukua siku nzima hadi mbili kuelekea kwenye eneo la tukio. Je na huo ni mpango wa Mungu? Huo ndo mpango wa Mungu usiokuwa na makosa?Tunaandaa bajeti yenye fedha nyingi za posho na vitafunio, tunasahau kuandaa bajeti yenye fedha nyingi za kushughulikia maafa. Tunaandaa bajeti yenye fedha nyingi za kununulia magari na kushindwa kuandaa bajeti yenye fedha yingi za kutetea na kulinda uhai wa watanzania. Tumeambiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwamba kazi ya kichwa si kufuga nywele bali ni kufikiri. Ni kweli kazi ya kichwa ni kufikiri. Kupinga ukweli huu ni ushahidi wa wazi kwamba kichwa kinafuga nywele bila kufanya kazi yake ya mzingi ya kufikiri. Mtu asiyeweza kufikiri na si kufikiri tu bali kufikiri na kutafakari, kufikiri na kuchukua hatua, kufikiri na kuvumbua na kufikiri na kupambana na changamoto za maisha anakuwa si mtu na hana haki ya kuishi! Swali na kujiuliza ni je Utamaduni unaojengeka kwamba kila anayejaribu kuikosoa na kuisimamia serikali (Bunge) ni mpinzani au ni CHADEMA, ni utamaduni wa kichwa kufuga nywele au kufikiri? Kuzima hoja ya kujadili tukio la Mv Skagit Bungeni, ni kichwa kufuga nywele au kichwa kufikiri? Au kukataa ukweli kwamba kumwambia mtu anatumia kichwa kufuga nywele badala ya kutumia kichwa kufikiri ni tusi, ni kutumia kichwa kufikiri au kufuga nywele? Tanzania ni nchi tajiri na ndiyo maana mataifa makubwa yanataka kuja na kuwekeza. Utajiri wa Tanzania unajulikana dunia nzima. Mfano kuzungukwa na nchi zaidi ya tano zisizokuwa na bandari ni utajiri wa kupindukia. Uchumi wa Tanzania unaweza kuendeshwa na bandari tu kama tungekuwa na mipango mizuri. Kuwa na ardhi kubwa yenye rutuba ni utajiri mkubwa, uchumi wa Tanzania unaweza kuendeshwa na kilimo peke yake kama tungekuwa na mipango mizuri. Kuwa na mbuga za wanyama ni utajiri kupita kiasi, maana kuna nchi duniani zinaendesha uchumi kwa utalii peke yake. Kuwa na madini mengi na kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini ni utajiri wa kutosha. Kusimama na kuitangazia dunia nzima kwamba Tanzania ni nchi masikini ni kutumia vichwa vyetu kufikiri au kutumia vichwa vyetu kufuga nywele? Bahati mabaya au nzuri msemo huu umeanzishwa na kiongozi serikalini; lengo lake likiwa kuwatusi na kuwakejeli wapinzani kumbe ni kinyume chake! Pamoja na ukweli kwamba MV Skagit, ilikuwa na mapungufu makubwa ya kuilazimisha kutoendelea kusafirisha abiria na wale walioiuza meli hiyo walibainisha mapungu hayo wazi bila kificho kuna mambo mengine juu ya meli hii yanayotia mashaka kama kweli tunatumia vichwa vyetu kufikiri au tunavitumia kufuga nywele: Mv Skagit, ilitengenezwa kubeba watu 250 bila mizigo, sisi tulikuwa tunaibebesha watu zaidi ya hao ni mzigo juu yake. Mv Skagit ilitengenezwa kusafiri kwenye mto, sisi tukainunua na kuilazimisha kusafiri baharini! Meli haikutengenezwa kupambana na mawimbi ya baharini. Hivyo aliyekwenda kuinunua meli hii ni lazima angeyajua yote haya na kuacha utamaduni wetu wa kushabikia vitu chakavu bila kupima vitu hivi vitafany akazi kwenye mazingira gani. Mjadala wa Tanzania kuendele kununua vitu chakavu uliungwa mkono na wabunge wengi wa CCM, tena kwa ushabiki wao uliunga mkono hoja hii kwa kuonyesha jinsi wanavyotumia vichwa vyao kufikiri na si kufuga nywele. Yakitokea maafa ya kutokana na vyombo chakavu, wabunge wetu hatuwasikii tena. Hatusikii wakikemea na kusema wale wote waliosababisha uzembe huu “wanyongwe”. Sauti zao zinasikika kwa kuwalaumu madaktari waliogoma kwamba wanasababisha vifo vya watanzania na kwa kosa hilo madaktari “Wanyongwe” au wafukuzwe kazi. Hatuwezi kukataa kwamba mgomo wa madakrati ulisabisha vifo, tukio ambalo si la madaktari peke yao bali na serikali pia, ila ukilinganisha vifo vinavyosababishwa na ajali za kizembe, huwezi kuwahukumu madaktari “Kunyongwa” kabla ya hukumu ya watu wote wanaongiza bidhaa bandia, watu wote wanaosababisha ajali zinazopoteza maisha ya watu wengi kama hili ya Mv Skagit. Kama tunaweza kuwa wakali kwa madaktari wetu, kwa nini tusiwe wakali kwa serikai yetu ambayo inaendelea kukumbatia vitendo vya kizembe nak uendelea kusababisha vifo vya watu wengi? Tusitafute visingizio na hakuna mchawi! Ajali hapa kwetu zinasabaishwa na uzembe wetu na kwa kiasi kikubwa ni uzembe wa serikai yetu. Tujifunze kuwajibika na kuwajibishana ndipo tutalinda uhai wetu wa kulilinda taifa letu la Tanzania. Na, Padri Privatus Karugendo. www.karugendo.net pkarugendo@yaoo.com +255 754 633122

0 comments:

Post a Comment