KUICHEZEA ELIMU YETU NI DHAMBI KUBWA: TUTAJUTA! Waswahili wanasema majuto ni mjukuu. Serikali inashangilia kwa kuwashinikiza walimu kurudi kazini; wenye upeo mkubwa wa kuchambua masauala ya kijamii na kuona mbali wanasikitika na kusononeka: Kutangaza mgomo kilikuwa ni kilele; nyuma yake kuna mambo mengi. “ Haya mambo mengi” kuyafunika kwa nguvu za dola ni aina fulani ya mabavu ya kijinga. Mgomo wa walimu na hatua za serikali kuitumia mahakama kuubatilisha mgomo huo ni mchakato wa kuichezea elimu yetu na kama wasemavyo waswahili majuto ni mjukuu. Kuichezea elimu ni dhambi kubwa! Ni uchawi mkubwa. Kama sisi tulipata elimu bora kwanini tutake watoto wetu wabaki na ujinga? Wamalize darasa la saba bila hata kujua kuandika majina yao? Tulifundishwa na walimu bora ambao waliipenda kazi yao na kuitekeleza kwa moyo wote. Walimu wetu walikuwa wanafundisha kwenye mazingira mazuri. Kulikuwa na yumba za walimu, madarasa yalikuwa na madawati, tulikuwa na vitabu na vifaa vingine vya kufundishia.Ualimu ilikuwa ni kazi ya kuheshimika katika jamii na sisi tuliwapenda walimu wetu nao walitupenda kama watoto wao. Serikali ya Mwalimu Nyerere ilitoa kipaumbele kwa elimu, leo sisi tunafikiri elimu ni kitu cha mwisho! Huu ni uchawi zaidi ya mtu anayeamua kunyonya maziwa yake mwenyewe na kuawaacha watoto wake wakifa kwa njaa! Hakuna taifa lolote duniani linaloweza kuendelea bila vijana wake kupata elimu bora. Msingi wa maendeleo ni kuwaandaa watoto kwenye msingi bora wa elimu. Kwa maana hiyo, walimu popote duniani ni watu wanaoheshimika na daima wanajengewa mazingira ya kuwawezesha kuendeleza kazi ya kulielimisha taifa. Tanzania tunataka kufanya kinyume; Ingawa Rais wetu anasema serikali inawathamini sana walimu, lakini ukweli ulio mbele yetu ni kinyume kabisa. Walimu wetu hawalalamikii mishahara peke yake, bali nyumba za walimu, madarasa, madawati, vitabu, vyoo na wakati mwingine usafiri wao na wa wanafunzi. Haiwezekani kwamba serikali haina fedha za kununua madawati, kununua vitabu, kujenga madarasa, kujenga nyumba za walimu, kujenga vyoo, kuwapatia usafiri wanafunzi na kuwaongezea walimu mshahara. Serikali itwambie ni kipi kati ya hivyo inakitekeleza kwa ukamilifu? Hadithi kwamba serikali haina uwezo zinachosha masikio ya kila mtanzania. Tuambiwe kwamba serikali haina uwezo wa kuongeza mishahara, lakini shule zote zina madawati, tuambiwe kwamba serikali haina uwezo kwa kuongeza mishahara ya walimu lakini shule zote zina nyumba za walimu, zina madarasa na zina vitabu vya kutohsa. Kuna ujumbe unaozunguka kwenye mitandao ya kijamii ukisema: "Kitaeleweka tu kwa walimu vinginevyo darasani itakuwa hivi: a) 1 + 3 = 13, b) 73-3= 7, c) 3 mara 3 = 333, d) 7 mara 2 = 77, na kwenye physics usiseme kila formula itakuwa reciprocal. hivyo ndo plan B kwa walimu wa science sipati picha kwa wa history, "Binadamu wa kwanza alikuwa NYERERE. Kazi ipo." Ujumbe huu umeanza kusambazwa walimu walipoanza mgomo wao. Wakionyesha kwamba endapo mgomo wao ukaingiliwa na serikali, watakuwa na mpango B. Na kweli sasa Serikali kupitia mahakama ya kazi wameuingilia mgomo huu kimabavu, bila majadiliano na makubaliano kwa pande zote mbili. Ni wazi sasa mpango B wa mgomo baridi utaanza kutekelezwa. Hata kwa mjinga yoyote asiyekuwa na akili ya kufiki na kuchambua mambo, atatambua kwamba tunaelekea kuichezea Elimu yetu na matokeo yake ni kujuta. Kuna ambao wataupuuzia ujumbe huu wa walimu wa kuanza mgomo baridi na kuna ambao ujumbe huu hauwagusi kabisa, maana kama mtoto anasoma shule ya binanfsi kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, au mtoto anasoma nje ya nchi, ujumbe huu si wake kabisa. Lakini kwa wale (ambao ndio wengi) wanaotegemea shule za serikali, ujumbe huu si wa kupuuzwa. Tatizo kubwa tulilonalo ni kwamba wale wanaowasomesha watoto nje ya nchi, wale ambao watoto wao hawasomei kwenye shule zetu hapa nchini, ndio wanafanya maamuzi juu ya elimu yetu. Hawana uchungu kwa chochote wakatakahoamua. Hawana uchungu endapo walimu wataamua kufanya mgomo baridi Walimu walipotangaza mgomo, kuna mwalimu mmoja ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini aliniambia hivi “ Ni kutangaza tu mgomo, lakini ukweli ni kwamba walimu tuligoma miaka mingi”.Ukweli wa mwalimu huyu ni matokeo tunayoyaona kwenye viwango vyetu vya elimu. Tunasikia namba kubwa ya watoto wanashinda mtihani wa darasa la saba, bila kujua kusoma wala kuandika. Mahakama ya Kazi, imetoa hukumu na kuwalazimisha walimu kurudi kazini. Ni wazi hakuna anayefurahia walimu kugoma, lakini pia kushangilia Mahakama kuwalazimisha walimu kurudi kazini bila majadiliano ya kumaliza madai ya walimu kwa njia ya amani ni kujidanganya. Walimu, wataitii mahakama, lakini hawatafanya kazi kwa moyo. Na hii ni hatari kubwa kwa elimu ya watoto wetu. Mgomo baridi ni mbaya kuliko mgomo wa wazi ambao hekima na busara vikifuatwa, mgomo huo unamalizika na walimu wanarudi kazini kama kawaida. Kutumia “Mabavu” kumaliza mgomo wa walimu ni kuliletea taifa letu janga kubwa. Walimu wataingia kwenye mgomo baridi na hata polisi wakitumika, haiwezekani kuwalazimisha kufundisha, na wakilazimishwa watafundisha ovyo ovyo na watoto wetu watamaliza shule bila kuwa na elimu bora. Mabavu yalitumika kuumaliza mgomo wa madaktari. Hadi leo hii kuna malalamiko kwamba huduma kwenye hospitali zetu za Serikali si nzuri. Madaktari wako kazini, lakini kwa vile malalamiko yao hayakushughulikiwa, hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi. Wanaoumia ni wananchi wa kawaida, viongozi wetu hawatibiwi kwenye hospitali zetu, wao wanakwenda kutibiwa nje ya nchi. Ingawa migomo si mizuri kwa maendeleo ya taifa, lakini na kuizima kiubabe si vizuri kwa maendeleo ya taifa letu. Tutaendelea kurudi nyuma kwasababu namba kubwa ya watumishi wa umma wanafanya kazi kwa kulazimishwa na si kufanya kazi kwa mapenzi na moyo wa kizalendo. Si kweli kwamba serikali yetu haina fedha za kuwalipa mshahara mzuri walimu, madaktari na watumishi wengine. Fedha tunazo nyingi na nyingine wajanja wachache wanaendelea kuzichota na kuziingiza kwenye mifuko yao, Mahakama inawatizama tu! Sote tunaishi Tanzania, walimu wanaishi Tanzania, madaktari wanaishi Tanzania.Sote tunashuhudia magari ya kifahari wanayoendesha watoto wa vigogo, tunashuhudia mahekalu ya vigogo, ya watoto wao na vimada vyao; tunashuhudia watoto wa vigogo wanakwenda kusoma nje ya nchi, tunashuhudia vigogo wakipanda ndege kwenda kutibiwa, kupumzika na kufanya manunuzi nje ya nchi. Fedha hizo wanazipata wapi? Zinachotwa hapa hapa Tanzania. Tumeanzisha wilaya za kisiasa, mikoa ya kisiasa bila kuwepo na hitaji la muhimu na haraka kuanzisha wilaya hizi na mikoa hii. Fedha nyingi zitatumika na kwingineko zimeaanza kutumika kuanzisha wilaya na mikoa. Tungekuwa na nia ya kuboresaha elimu yetu, tungeanza kushughulikia kero za walimu kabla ya kuamua kutumia fedha nyingi kwenye mradi huu mkubwa wa kuanzisha wilaya mpya na mikoa mipya. Tuna baraza la mawaziri kubwa bila sababu zozote za msingi. Baraza hili linatumia fedha nyingi ambazo zingeweza kuelekezwa kwenye mishahara ya walimu, madaktari na watumishi wengine wa serikali na kuchochea mambo mengi kufanywa kwa ufanisi mkubwa. Wengi tulitegemea kumsikia Rais Kikwete, akisema kwamba kwa vile Serikali haina fedha na walimu wanadai nyongeza ili wapate motisha wa kuwafundisha watoto wetu, basi serikali inaachana na mpango wake wa kuanzisha Wilaya mipya na mikoa mipya, serikali inapunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, serikali inapunguza matumizi mengine ya serikali yasiyokuwa ya lazima: kama chai, posho na safari nyingine za nje ili fedha zitakazookolewa kwenye zoezi hilo zisaidie kulipa mishahara ya walimu. Badala yake Rais, anasema serikali haina fedha hivyo walimu wanataka wasitake ni lazima warudi kufundisha. Hawawezi kufundisha hawa! Kitakachofanyika ni kuichezea elimu ya watoto wetu. Hitaji la sasa hivi si kuanzisha wilaya na mikoa. Mfano Karagwe, imegawanywa mara mbili kutengeneza Wilaya za Karagwe na Kyerwa. Lakini hili halikuwa hitaji la watu wa Karagwe. Hitaji lao ni maji,hospitali,soko la kuuza mazao yao kwa uhakika, walimu, vyumba vya madarasa, madawati, barabara na umeme. Karagwe kuna tatizo sugu la maji na miaka yote halijapatiwa uvumbuzi, barabara nyingi za wilaya ya Karagwe, zinapitika kwa shida wakati wa mvua, shule nyingi za Karagwe, watoto wanakaa chini na shule nyingi hazina vifaa vya kufundishia. Kuyaweka matatizo hayo yote pembeni na kukimbila kuanzisha wilaya mpya ambayo itahitaji mabilioni kuianzisha ni kuwachelewasha watu kupiga hatua ya maendeleo. Kama tunalipenda taifa letu, kama tunawapenda watoto wetu, kuna umuhimu na hitaji la haraka kukutana na walimu na kujadiliana nao juu ya madai yao. Bila kufanya hivyo walimu hawatafundisha. Ndo maana wameanza kusambaza ujumbe kama huo hapo juu kwenye mitando ya kijamii. Watakwenda shuleni na kufundisha mambo mengine kinyume. Matokeo yake watoto wataingia mitaani kudai haki yao ya kufundishwa. Juzi tumeshuhudia wanafunzi wakiandamana nchi nzima. Serikali inafikiri kwamba watoto hao wanafundishwa na kulazimishwa na walimu wao kufanya maandamano. Kufikiri hivyo ni “Upumbavu”. Watoto hao wanapitia manyanyaso makubwa; wanasafiri kwa shida kwenda shuleni, wanasukumwa na makonda, wanasimama kwenye dalala, wanashinda njaa bila chakula, wanakaa chini, hawana vyoo shuleni. Nyumbani wanashuhudia maisha yanavyopanda, wanasikia wimbo wa mafisadi, rushwa na uporaji wa maliasili. Wakati huo huo wanashuhudia watoto wengine wakipelekwa na mashangingi shuleni na kusomea kwenye shule za kifahari. Hawa ni binadamu na yote hayo wanayaona; hivyo si lazima wasukumwe na mtu, wanasukumwa na jamii yetu iliyofilisika kimawazo. Makala hii ni wito kwa serikali kuachana na mfumo huu wa kutumia mabavu kuwalazimisha walimu kurudi kazini. Pia ni ushauri wa bure kwamba kuitumia mahakama kama chombo cha kuzima sauti za wanyonge ni dhambi kubwa; wanyonge wakitambua kwamba hakuna sehemu yakukimbilia kudai haki zao, wataamua kuingia barabararni na hili likitokea hakutakuwa na sabababu ya msingi ya kumtafuta mchawi au kufikiri kwamba migomo inaendeshwa na vyama upinzani; migomo hii inaratibiwa na serikali iliyo madarakani kwa tabia yake ya kufumbia macho mambo mengi ya ukweli. Tusichezee elimu ya watoto wetu kama tunalipenda taifa letu. Na, Padri Privatus Karugendo. www.karugendo.net +255 754 633122.

0 comments:

Post a Comment