UHAKIKI WA KITABU: HAINI 1. Rekodi za Kibibliografia. Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni HAINI, Kimeandikwa na Adam Shafi. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Sasa Sema Publications Chapa ya Longhorn Publishers na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 9966 49 766 8. Kitabu kina kurasa 272 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. Utangulizi Haini ni riwaya ya kubuni inayochukua tukio la kihistoria la kuuawa kwa kiongozi mmoja wa Kiafrika mwaka 1972. Baada ya mauaji Hamza, kijana mwandishi wa habari, anakamatwa kwa kutuhumiwa kuwa haini, hasa kutokana na uhusiano wake wa karibu na Hamduni, ambaye amempiga risasi na kumwua Kigogo huyo, kiongozi wa nchi. Sehemu kubwa ya riwaya hii inasimuliwa gerezani ambako Hamza pamoja na wengine waliosombwa na kurundikwa huko gerezani wanateswa, kuthakilishwa na kutendewa unyama wa kila namna. Pamoja na tukio hili la Uhaini, riwaya hii inachunguza matatizo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya nchi za Kiafrika baada ya uhuru chini ya mifumo ya utawala inayojali tu maslahi ya wachache. Ni riwaya inayogusa hisia na kuchochea hasira na uchungu rohoni, hata hivyo ina ucheshi na viliwazo, mfano mwandishi anapoandika hivi: “ Alinyanyuliwa akatupwa nje na baada ya kutua juu ya ile sakafu tu wakammwagia ndoo nzima ya maji kumfufua arudi tena duniani. Walipomwona anazindukana wakaanza tena, ‘sasa utasema”. Riwaya hii imeandikwa na Adam Shafi, mwandishi mkongwe. Mbali na riwaya hii ameandika vitabu vingine vitatu, vyote vikiwa ni riwaya: Kasri ya Mwinyi Fuad ( ambacho kimetafsiriwa kwa lugha za Kifaransa, Kijerumani na Kirusi); Kuli na Vuta nikuvute ( ambacho kilimpatia tuzo ya mwandishi bora nchini Tanzania mwaka 1998). Sasa hivi yuko mbioni anaandika kitabu kingine cha kusisimua Mbali na Nyumbani, kama alivyonielezea tulipokutana katikati mwa Jiji la Dar-es-Salaam: “ Ninaandika juu ya maisha yangu, ujana wangu, harakati za kutafuta elimu na mpango wa kuzamia kupitia Misri kwenda Ujerumani kutafuta maisha na baadaye kurudi hapa Tanzania kuendeleza mapambano ya maisha hadi leo hii”. Alieleza Mzee Adam Shafi. Ukiongea naye, mbali na hekima na busara zilizotulia kwenye kichwa chake ambacho sasa kimejaa mvi, utaburudika na utaalamu wake wa lugha ya Kiswahili, anaongea Kiswahili sanifu, hata akiongea Kingereza na Kijerumani matamshi yake yanaonyesha kwamba yeye ni mtaalamu wa lugha hizo. Adam Shafi alizaliwa mjini Zanzibar mwaka 1940. Baada ya elimu yake ya shule ya msingi alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Seyyid Khalifa ( sasa Chuo cha Ualimu cha Nkrumah) mwaka 1957 hadi mwaka 1960. Alipata Diploma ya Juu katika fani ya Siasa na Uchumi katika Chuo cha Fritz Heckert, katika iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani mwaka 1963. Alipata mafunzo ya uandishi wa habari mjini Prague, nchini Czechoslovakia 9 sasa Jamhuri ya Czech) mwaka 1964 hadi mwaka 1965, nchini Sweden mwaka 1982 na nchini Marekani mwaka 1983. Adam Shafi alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA) kuanzia 1998 hadi 2002. Alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania (BAMVITA) mwaka 2002. Sasa hivi amestaafu na kuendelea na kazi zake za uandishi binafsi. III. Mazingira yanayokizunguka kitabu Kabla sijaanza uchambuzi wa kitabu hiki cha Haini, ni bora nielezee mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Sina uhakika kama kitabu hiki kinauzwa Tanzania Bara. Kitabu hili kilichapishwa mara ya kwanza 2003 na mara ya pili 2010, kule nchini Kenya. Mimi nimepata bahati ya kukipata mwaka wa 2010, nilipokwenda Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu nikiwa Mwangalizi huru wa TEMCO. Nilipoingia kwenye duka la vitabu pale Darajani, nilikikuta kitabu hiki, ingawa bei yake ilikuwa juu kidogo, shilingi elfu kumi na tano ukilinganisha na vitabu vya riwaya tulivyozoea kununua huku bara, sikukiacha. Nilikinunua na kuanza kukisoma. Adam Shafi, aliniambia kwamba aliamua kukichapisha kitabu chake Kenya, baada ya mizengwe ya wachapishaji wa Tanzania. Labda waliogopa kuchapisha kitabu cha Haini? Ni wazi unahitaji ushupavu wa pekee kukichapisha kitabu hiki, hata mimi mwenye nilisitia kukifanyia uhakiki, nilikisoma 2010, ninakifanyia uhakiki 2012! Ni riwaya iliyosheheni ukweli ambao wengi wetu hatupendi kuusikia na tukifikia hatua ya kufilisika kimawazo, ukweli kama huu kwenye riwaya hii ni lazima tuupatie jina la uchochezi! Mwandishi anasema riwaya hii inachukua tukio la kihistoria, la kuuawa kwa Kiongozi kwenye nchi za Afrika. Hapendi kuitaja nchi hiyo na kiongozi huyo. Lakini kwa makusudi au kwa bahati mbaya anasahau kuficha majina ya Pemba, Unguja, Darajani na mengine mengi. Mwisho wake, hata kama msomaji ni zezeta ni lazima atagundua kwamba nchi inayoongolewa hapa ni Zanzibar, na kiongozi aliyeuawa mwaka 1972, si mwingine zaidi ya Marehemu Rais Karume. IV. Muhtasari wa Kitabu Unaweza kufanya Muhtasari wa Kitabu hiki kwa maneno machache: Baada ya kifo cha kigogo, au kwa maneno mengine Kiongozi wa nchi hii isiyotajwa jina na mwandishi, waliokamatwa, wakawekwa ndani, wakateswa na hatimaye baadhi yao wakahukumiwa kunyongwa si waliopanga njama za mauaji. Riwaya inaonyesha na kuweka wazi kwama Kigogo, aliuawa na watu wake mwenyewe, rafiki na ndugu zake waliokuwa wakimzunguka kila siku ya Mungu. Hawa walikuwa na uchu wa madaraka, walitaka Kigogo, aondoke ili wao waingie madarakani, baada ya mipango yao kushindwa, maana nchi hii ilikuwa na nguvu nyingine kutoka nje ambazo zisingeruhusu madaraka kuchukuliwa kwa mtutu wa bunduki, waliona waihadae dunia kwa kuwakamata “washukiwa bandia” na kuwaweka gerezani. Riwaya hii, inatufumbua macho kwamba Haini si Haini. Wale waliopaswa kuitwa Haini kule Zanzibar, walibaki huru na kuendelea kula maisha. Wanyonge na watu baki ndio walikamatwa na kubambikizwa jina hili la Haini. Mfano mzuri ni Hamza, huyu ni mwandishi wa habari. Alikamatwa kwa vile alikuwa ni rafiki wa Hamduni, kijana aliyetekeleza mauaji. Hivyo Hamza na wengine wengi waliokamatwa, hawakuwa na habari za mpango wa mauaji, bali wenye mpango, ambao ndio waliokuwa serikalini, walitaka kuwakamata watu, kuwatesa hadi waungame kitendo cha mauaji. Maungamo yao, yalikuwa salama kwa kikundi kizima kilichotekeleza mauaji. Riwaya inaelezea jinsi baadhi watu walivyokamatwa hata kabla ya kufahamu kilichotokea. Ukurasa wa 7 hadi wa 14 unaelezea jinsi Hamza alivyokamatwa na kupelekwa Gerezani. Kule alikumbana na mateso ya kutisha. Asilimia kubwa ya riwaya ni maisha ya gerezani. Ingawa mwandishi anajitahidi kuficha jina la nchi, lakini majina ya gereza yanamsaliti kiasi mtu anagundua kwamba hizi ni gereza za Zanzibar ambazo hazitofautiani na zile za Tanzania bara. Ukatili na unyama ambao hadi leo hii unaendelea kwenye magereza zote nchini. “Baada ya siku mbili mwili wa Sururu ulivunda, unanyekenya nyekenyeke, unatoja rojo ya usaha. Mgongoni mlifanya mashata ya damu na usaha juu ya misirimbo ya michapo mikali ya fimbo na viboko iliyomzonga mdawari mgongoni kuzungukia mbavuni mpaka tumboni, kama miraba ya pundamilia, kwake kulala kulikuwa ni shida na kukaa pia ni shida, na yote hayo yalimletea mitonesho mikali. Uso ulikuwa umemjaa, umetutumka machoni na mashavuni na domo nalo limeumuka damu bado zinamtoka kwenye lile pengo alilong’olewa meno. Na usoni ndevu zake zilikuwa zikiota kwa haraka, zikashikana na damu iliyokauka zikawa kama vigaga” (Uk wa 21). Ukatili unaosimuliwa kwenye riwaya unatisha. Je mwandishi alionja maisha ya gereza au ni kubuni tu? Ni mateso ya kinyama ambayo kuna ushahidi kwamba mateso hayo ni chakula cha kila siku kwenye magereza yetu mbaya zaidi kwa Haini, anayekisiwa kutoa roho ya Kigogo: “Alimwangalia jinsi anavyohaha, pumzi juu juu, akawaza watu wale walikompeleka Hamza usiku kucha wakamrudisha akiwa na hali ile, si wa dunia hii wa ahera. Aliwaza jinsi binadamu anavyoweza kukosa huruma kwa binadamu mwenzake, akajifanya yeye ni binadamu zaidi kuliko binadamu wengine, akajiweka karibu na Mungu akajipa uwezo wa kuua na kuhuisha” (Uk wa 67) Mbali na mateso, mbinu nyingine nyingi zilitumika ili kuwafanya waungame mauaji, wajinga walianguka kwenye mtego na hao ndio mwisho wa mwisho walihukumiwa kunyongwa. Welevu kama Hamza, ambao walijua fika hakufanya kitu walikwepa mitego hiyo: “ Sisi tunajua kwamba wewe huhusiki lakini ombi letu ni kukutaka ukubali. Ujidai kama vile umo na unawajua wengine. Tuna orodha ya majina hapa tutakupa, na wote hao tumeshawatungia hadithi kuthibitisha vipi wanahusika” (Uk 82). Hamza alikataa ushawishi huo, lakini wao waliendelea kumshawishi “ Hamza usiwe na wasiwasi. Wapo wenzako waliokwishakubali watakuwa mashahidi halafu tutawachilia. Unasemaje, utajiunga na kundi hilo? Tena wao hivi sasa tumewaweka pazuri. Wanakula pilau, chai ya maziwa, mikate, siagi, jam, al-hasil wako burean, alieleza Kanali Mapepe” (Uk 82). Pamoja na yote hayo, Hamza, alijua hakufanya kitu. Alivumilia mateso yote na kukataa kuungama kitu ambacho hakufanya. Wafungwa wengine walijaribu kutoroka, lakini walikamatwa na kurudishwa gerezani au wengine kupotezwa kabisa. Wafungwa wengine walijua kabisa kwamba wameingizwa tu ili kufunika ya wakubwa: “ Sikiliza Kuchi. Haya mambo kuna wenyewe wanaoyajua. Wanayajua utando mpaka ukoko. Kuna wenyewe waliyoyapanga” Alisema Haramia, “ Wenyewe gani?” aliuliza Kuchi “Wakubwa! Wakubwa wenyewe ndio waliyoyapanga haya’ “Unataka kuniambia kwamba Kigogo kauliwa na wakubwa wenzake?” “ Sasa tena!” alitia mkazo Haramia “Vipi?” aliuliza Kuchi “ Wewe Kuchi hebu kaa ufikiri. Silaha zimeibiwa kutoka kwenye ghala ya kutunzia silaha wiki nzima kabla ya siku ya mauaji. Wakubwa wakijua hayo na hakuna lolote walilolifanya” alisema Haramia.( Uk 158). Ili kuonyesha kwamba mauaji yalipangwa na wakubwa, mwandishi anatuingiza kwenye tafakuri ya bure: “ Ile siku ya maziko yake. Kigogo alizikwa kwa heshima zote alizostahiki mtu kama yeye na haukupita muda mrefu mrithi wake akatawazwa. Kanali Bunju ( ambaye ndiye anayeongoza mateso ya wangungwa wa Uhaini) akajikuta kiti kile amekikosa amekikalia mwingine..... Kigogo ameuawa na hakuna mwingine yeyote aliyestahili kiti chake isipokuwa yeye, leo kiti hicho anakikalia mtu mwingie, siye yeye..” ( Uk 161). Baada ya Kigogo, kuuawa, wakubwa walihakikisha wale wauaji wote wanauawa ili wasijetoa ushahidi wa kuwaingiza kwenye kesi. Hivyo hawa wote waliosombwa na kutupwa gerezani hawakuwa na ushahidi wa kujinasua zaidi ya kukubali au kukataa ushawishi wa gerezani. Kesi ya Uhaini ilipoanza kusikilizwa, wale waliokataa kudanganywa ili wakubali waliendelea kusimama kidete kupinga kukamatwa kwao: “ Katika maelezo yangu hayo nimeeleza wazi wazi kwamba mimi sielewi, chochote, wala sihusiki kwa namna yoyote na mpango wa uhaini. Nimekuwa msimamo huo hata baada ya kuhojiwa mara sita katika hali ya vitisho na mateso makubwa, nikilazimishwa nikubali khusika na uhaini kwa kucharazwa kwa mipweke na mpera, kutimbwa kwa mateke ya watu waliovaa viatu vizito vya kijeshi, na kuning’inizwa kwenye kitanzi mpaka choo kibichi kikanitoka” ( Uk 248). Mwandishi anaonyesha jinsi kesi ya uhaini ilivyoendeshwa kwa sheria na kufuata haki. Wale wote waliokataa kudanganywa ili wakubali kutenda kosa waliachiwa huru. Wale tisa waliokubali na kupata maisha mazuri gerezani kwa ahadi ya wakubwa kwamba kesi ikifika wao watakuwa mashahidi, hao ndo kibao kiliwageukia. Kwa kukubali wao wenyewe, hukumu ilipitishwa kwamba walikuwa na hatia. Hivyo watu tisa ndo walipatikana na makosa ya mpango wa kifo cha Kigogo. Kwa maoni ya mwandishi ni kwamba wale waliopanga njama za kifo cha Kigogo, walibaki huru hadi leo hii. Waliokamatwa, kuteswa na kufungwa zaidi ya miaka miwili na hatimaye baadhi yao kupata hukumu ya kifo, ni watu wasiokuwa na hatia. Bahati mbaya riwaya inafikia mwisho bila kufahamu kama kweli hao watu tisa walinyongwa au walikata rufaa? Je historia ya Zanzibar inasema nini kuhusiana na kesi hii ya uhaini? Kuna haja ya kuichimba sasa ili kulinganisha ukweli wa riwaya hii na ukweli wa historia.. V. TATHIMINI YA KITABU. Nianze kwa kumpongeza Adam Shafi, kwa kazi hii nzuri sana aliyoiandika. Kusema kweli hadithi hii inaburudisha, inasikitisha na kufikirisha. Ni hadithi yenye kuchekesha pia. Pili nimpongeze mwandishi kwa kuthubutu kuandika mambo haya ambayo wengi wangeogopa kuyaandika. Inahitaji moyo wa ushupavu kuandika riwaya inayofichua ukweli uliofichika, kwamba wale waliopanga mbinu na njama za mauaji ya Kigogo, walibaki huru wakati walikamatwa watu wanyonge wasiokuwa na sauti. Tatu, ni kumpongeza kwa matumizi ya Kiswahili sanifu na kama ilivyo kawaida yake anapoandika kuiacha ile harufu ya mvuto mzuri wa lugha kiasi kwamba msomaji anatambua pasipo na shaka kwamba mwandishi ni mtu wa visiwani. Nne, ni uhodari wake wa kutengeneza maumbo na kufanikiwa kutoa picha halisi ya kile anachotaka kuelezea. Kwa mtu anayeifahamu Zanzibar, akisoma kitabu cha haini, anajiona kama yuko Zanzibar vile: “ Hamza alijikuta peke yake ameibuka kutoka katika vichochoro vyembamba vya Malindi na kuchomozea katia barabara kuu ya Darajani.. Mtaa wa Darajani ulikuwa umepumbaa kwa kukosa ule uhai wake wa kawaida saa kama zile, saa ambazo kwa kawaida, watu baada ya kusali Swala ya Magharibi, hujitandaza ovyo ovyo vibarazani, wengine wakipiga gumzo kwenye mabao ya wauza kahawa wakibwia mafunda ya kahawa chungu iliyochemka bara bara.” (Uk 2) Tano, mwandishi amefanikiwa kuelezea hali ya uchumi ya wakati huo na ugumu wa maisha: “ Sasa Khadija akaanza kufikiri. Ataupata wapi mchele na siku yao ya ukoo bado haikufika. Hapo duka la ukoo ukienda, kama siku yako haikufika hata ukilia machozi ya damu mchele huupati. Ataupata wapi mkate. Watu huanza kujipanga foleni ya mkate tokea usiku na hukesha hapo hapo kusubiri mkate wa asubuhi. Hata hivyo huo mkate wenyewe kuupata ni bahati nasibu tu. Wakati mwingine hiyo foleni huvurugika watu wakakanyagana na kutiana kabari wakakaribia kuuana” ( 146). Sita, Mwandishi anatufunulia uaminifu na uvumilivu wa wanawake wa Zanzibar. Sura yote ya Kumi na nne, inaonyesha uaminifu wa Khadija juu ya mme wake Hamza, aliyekuwa amekamatwa uhaini kusweka gerezani. Pamoja na ugumu wa maisha na vishawishi vingi kutoka kwa wakubwa wa Serikalini, Khadija akiwawakilisha wanawake wengine wa Zanzibar na labda hata wa Tanzania bara, alibaki mwaminifu kwa miaka yote ambayo mme wake alikuwa kifungoni. Hili ni jambo la kupongezwa, maana kuna baadhi ya waandishi ambao daima wanaonyesha kuwa mwanamke ni dhaifu na hawezi kupambana na maisha magumu na yenye vishawishi. Saba, ni uhodari wa kuficha jina la nchi na Kiongozi. Hapa kuna utata kidogo. Mtu anaweza kujiuliza ni kwa nini mwandishi alificha jina la nchi na kiongozi, lakini riwaya nzima inaonyesha wazi kwamba nchi yenyewe ni Zanzibar na kiongozi aliyeuawa ni Marehemu Rais Karume. Je, angetaja jina utamu wa riwaya ungepungua? Au labda ni ushauri kutoka kwa wachapishaji na watu walioupitia muswada huu? Waliogopa riwaya isilete uchochezi au labda mwandishi kuingia matatani? Inashangaza kidogo na inahitaji majibu. Ni matumaini yangu kwamba baada ya kusoma uhakiki huu mwandishi atatoa majibu. VI. HITIMISHO. Ni wazi ningependa kuwashauri wasomaji wangu kukinunua kitabu hiki na kukisoma ingawa sina uhakika kitabu hiki kinapatikana Tanzania bara. Mimi nilikitafuta siku nyingi na hatimaye kufanikiwa kukipata kule Zanzibar. Pamoja na ukweli kwamba bei ya kitabu hiki ni kubwa, ni muhimu kukinunua na kujisomea yale tunayoyajua na tusiyoyajua. Kama nilivyosema hapo juu, kuna haja mwandishi akaelezea lengo lake la kuficha jina la nchi na kiongozi aliyeuawa, wakati riwaya nzima inaonyesha bila kificho. Akitoa toleo jingine, ni bora kuyakweka majina, ili watu wakapata ukweli na uhondo wa historia na riwaya yenyewe. Pia mwandishi anaweza kufanya jitihada binafsi kuhakikisha kitabu chake kinauzwa Tanzania Bara. Sitaki kuamini kwamba alikuwa akiwaandikia wa Zanzibari peke yao. Mauaji ya Kigogo yaliligusa taifa zima la Tanzania; sote tuwe macho maana tukio kama hilo laweza kutokea tena na mtego wa panya ukawaingiza waliyemo na wasiokuwemo. Wanaotenda kitendo wanabaki huru na kuendelea na maisha, wanakamatwa dagaa, Nyangumi na papa wanaendelea kuelea. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment