UHAKIKI WA KITABU: MAISHA NA HARAKATI ZA KAZIMOTO 1. Rekodi za Kibibliografia. Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Maisha Na Harakati za Kazimoto:Nekemia Musa Kazimoto. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Tanzania Educational Publishers LTD, katika mpango wake wa kutoa vitabu vya Watu Mashuhuri wa Mkoa wa Kagera. Hiki ni kitabu cha pili katika mpango huu na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani(ISBN): ISBN 978 9987 07 035 0. Kimechapishwa mwaka jana wa 2011 kikiwa na kurasa 223. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni Mimi Padri Privatus Karugendo. II. Utangulizi Kitabu hiki kinahusu maisha ya Mzee Nekemia Musa Kazimoto, Mwafrika, Mtanzania na Mnyambo wa Karagwe; mwanafamilia,mwanaharakati,mfanyabiashara na mkulima. Ni kitabu kinachoelezea maisha ya mtu ambaye bado yuko hai, mwenye mafanikio na anendelea kutoa mchango wake katika kulijenga taifa letu la Tanzania. Kitabu hiki amamekiandika yeye mwenyewe, ni tofauti na vitabu juu ya maisha ya watu vinavyoandikwa baada ya wahusika kutoweka hapa duniani. Mzee, Kazimoto anasimulia mwenyewe maisha yake tangia utotoni hadi kulitumikia taifa katika ngazi mbali mbali, kazi za kijamii, kazi za kifamilia hadi leo hii anapoendesha biashara yake na kuendelea kutoa mchango mkubwa katika jamii nzima ya watanzania. Mzee Kazimoto, anayachukulia maisha kama Mlima. Ni kama mtu anapanda mlima, akitafuta kilele cha mlima. Anaamini katika maisha yake yameupanda mlima na anaendelea kuupanda hadi atakapofikia kileleni. Ni kati ya wazee waliofanikiwa kupanda mlima bila kupinda wala kutizama nyuma. Mafanikio yake ni kioo cha jamii, ndo maana watu wanaomfahamu akiwemo na mchapishaji wa kitabu hiki Mzee Pius Ngeze, walimshauri kuandika kitabu juu ya maisha yake, ili kizazi hiki chetu na vizazi vijavyo wajifunze kutokana na maisha ya mtu aliyekuwa mwaminifu kwake, mwaminifu kwa familia na mwaminifu kwa jamii nzima ya Tanzania. Mwandishi mwenyewe anasema “ Nimelazimika kuandika kitabu hiki si kwa lengo la kujikweza, kwa kuwa najua wapo watu wengi muhimu wenye simulizi za kuvutia sana, bali ni baada ya kushawishiwa na marafiki na watu wa kawaida waliopata kunifahamu. Kwa hiyo, naamini kuwa wasomaji wataelewa kuwa maandishi haya hayana lengo la kujionesha kwao kuwa pengine mimi ni mtu aliyefanikiwa sana au mwenye bahati mbaya sana ili nihusudiwe ama kuonewa huruma, bali ni kwa nia ya kuweka kumbukumbu ya maisha yangu yanayoweza kutoa mafunzo ya aina fulani kwa kizazi kilichopo na vizazi vijavyo katika kupambana na maisha ya changamoto zake” Pamoja na Utangulizi, kitabu hiki kimegawanywa katika sura kumi na tatu: Sura ya kwanza inaainisha Asili, Wazazi na Maisha ya Utotoni. Sura ya pili ni Maisha ya Shule. Sura ya tatu ni Harakati za Ajira. Sura ya nne ni Harakati katika Vyama vya wafanyakazi. Sura ya tano ni kupinga Unyanyasaji na Ubaguzi. Sura ya sita ni uongozi. Sura ya saba inahusu Uwakilishi na Ushiriki ndani ya nchi. Sura ya nane inaainisha Anga za Nje. Sura ya tisa inahusu Shughuli Binafsi za Kilimo, Mifugo, Biashara na Ujenzi. Sura ya kumi inaelezea Familia ya Kazimoto, Ndugu na Marafiki. Sura ya kumi na moja ni watu wengine wanavyomzungumzia Mzee Kazimoto. Sura ya kumi na mbili ni Wosia wa Mzee Kazimoto kwa kizazi hiki. Kitabu kinafungwa na sura ya kumi na tatu ambayo ni shukrani. III. Mazingira yanayokizunguka kitabu Wakati Taifa letu limegubikwa na misamiati kama Ufisadi, rushwa, uzembe na kutowajibika, wakati zinajengeka fikira kwamba hakuna watanzania waadilifu, ni jambo la kutia moyo kukisoma kitabu cha Mzee Nekemia Musa Kazimoto. Ukifika Wilaya ya Karagwe, ambayo sasa hivi imegawanyika katika wilaya mbili za Karagwe na Kyerwa, ni lazima utalisikia jina la Kazimoto. Pamoja na ukweli kwamba Kazimoto ni jina la ukoo mkubwa, aliyelijenga jina hili kuwa miongoni mwa watu waadilifu wa Tanzania, si mwingine bali Nekemia Musa Kazimoto. Maana ya neno Kazimoto, ni kufanya kazi moto moto, kufanya kazi kwa bidii na kufanya kazi kwa malengo ya kuleta mafanikio si ya mtu binafsi bali ya jamii nzima. Nekemia Musa Kazimoto, ameishi jina hili la familia na kuonyesha maisha ya kufanya kazi moto moto. Simulizi yake na watu wanaomfahamu akiwemo na mchambuzi wa kitabu hiki ni ushuhuda wa kutosha wa Nekemia Musa Kazimoto kuishi maisha ya kufanya kazi moto moto. Mzee Pius Ngeze, mchapishaji wa kitabu hiki na ambaye alipewa heshima ya kuandika dibaji ya kitabu hiki anasema “ Ni kazi kubwa kuandika Dijabi ya kitabu cha mtu mwenye historia iliyotukuka kama ya ndugu yangu Nekemia Musa Kazimoto..... Nimesikia Mzee huyu tangu 1962, lakini, kumfahamu ni tangu 1977. Lakini kumbe, nilikuwa simfahamu wala kumwelewa sawasawa. Baada ya kusoma kitabu chake hiki, sasa naweza kutamba kuwa ninamfahamu. Hata hivyo si mimi peke yangu ambaye nilikuwa najidai kuwa ninamfahamu wakati simfahamu. Tuko wengi..” Bwana Nekemia Musa Kazimoto, alizaliwa mwaka 1937. Amewahi kufanya kazi katika mashirika ya umma, serikalini na vyama vya wafanyakazi alikopanda hadi kuwa Rais wa Tanzania Federeation of Laboru (TFL). Ni mfanyabiashara aliyefanikiwa, mkulima na mfugaji bora. Pia, amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika chaWilaya ya Karagwe, taasisi na asasi za dini na zisizokuwa za serikali. Ni mcha Mungu. Ana mke mmoja na watoto kumi na nne( Saba wa kike na saba wa kiume). IV. Muhtasari wa Kitabu Kitabu hiki kinahusu Harakati na Maisha ya Kazimoto: Nekemia Musa Kazimoto; utakapomaliza kukisoma, utagundua siri ya mafanikio yake kwamba ni kufanya kazi kwa motomoto, yaani,Kazimoto. Sura ya kwanza, mwandishi anaelezea juu ya asili yake, wazazi wake na maisha yake ya utotoni. Anaelezea baba yake na ukoo wake, mama yake na ukoo wake. Kwa upande wa watu wa Karagwe, sura hii inawafumbua macho kufahamu ni nani anahusiana na nani, na ni ukoo upi unahusiana na mwingine. Wale watakaosoma kitabu hiki, na hasa vijana huu ni mwongozo wa kuwasaidia ndugu na ndugu wasioane au ndugu na ndugu kufahamiana na kujenga uhusiano mkubwa zaidi. Lakini pia kwa upande mwingine sura hii inatufumbua macho kwamba waafrika tunahusiana kutokea Uganda, Karagwe,Bukoba hadi Mtwara. Katika sura hii Mzee Kazimoto anatufahamisha kwamba ukoo wao wa Abaihuzi, ulichimbuka kule Abisinia (Ethiopia) na kusambaa hadi Uganda,Bukoba,Karagwe na Mtwara. Hii pia ni changamoto kwa wanahistoria kuangalia ukweli wa jambo hili. Kwa vyovyote vile watu hawa, “Abaihuzi” watakuwa na vitu fulani vinavyofanana, sura, lugha au utamaduni. Fundisho jingine katika sura hii ni familia za zamani kuishi kwa mshikamano na upendo. Mama wa kambo kuwalea watoto ambao si wake wa kuzaa kwa upendo mkubwa. Ma Josephina, anaonekana kuwa mama mwenyew upendo mkubwa ambaye aliwalea baada ya Baba yao kuachana na mama yao. Pia yeye Mzee Kazimoto anatoa mfano wa mke wake pili alivyowatunza watoto wake baada ya mke wake wawa kwanza kuaga dunia. Sura ya pili, ni simulizi juu ya maisha ya shule. Hapa tunapata fundisho juu ya shule za zamani. Zilikuwa mbali na wanafunzi walisafiri kwenda mbali kutafuta elimu. Lakini muhimu zaidi hapa ni jinsi urafiki wa shuleni ulivyokuwa unadumu hadi uzeeni. Mwandishi, anatutajia watu aliosoma nao shule ya msingi, kama Mzee Nsherenguzi, ambao hadi leo hii ni marafiki. Je sisi tunadumisha urafiki? Hili ni jambo la kujifunza. Inaonekana mwandishi analisisitiza, maana mwishoni mwa kitabu ametaja marafiki wa watoto wake, marafiki wa wajukuu wake na marafiki wa mke wake. Ni kama anawapatia swali... Je urafiki utadumu kama yeye alivyodumisha urafiki hadi uzeeni? Sura ya tatu ni simulizi juu ya harakati za Ajira za Mzee Kazimoto. Hapa tunasikia alivyoanza kufanya kazi kwenye shirika la Reli. Na baadaye kufanya kazi Idara ya ujenzi ya Serikali (Public works Department). Kufanya kazi kwenye vyama vya wafanyakazi vya TFL na TUPE. Kazi kwenye kampuni ya kusindika Unga ya Tanganyia, Ajira kwenye Halmashauri ya Jiji la Dar-es-salaam, Kazi kwenye viwanda vya sukari vya Kilombero na Kagera na mwishowe uamuzi wa kuachana na kazi za kuajiriwa. Tunachojifunza kwenye sura hii ya tatu, ni juhudi ya kutafuta kazi na kufanya kazi kwa uamiifu. Tunashuhudia msimamo wa Mzee Kazimoto, wa kusimamia ukweli na kutetea haki. Jinsi alivyo leo hii, hakuna tofauti na kule nyuma. Alitaka uwazi kazini na alichapa kazi bila kuangalia nyuma kwa maana ya kufanya kazi motomoto. Sura ya nne ni simulizi juu ya harakati katika vyama vya wafanyakazi. Hapa tunasikia Mzee kazimoto akiwa Rais wa Tanganyika Federation of Labour. Na pia katika sura hii tunasimuliwa safari za nje za Mzee Kazimoto, alizozofanya akiwa kazini. Safari ya Uingereza, Ujerumani na kwingineko. Pia hapa ndo anatusimulia juu ya migomo ya wafanyakazi, ambayo ilikuwa silaha kubwa kwa wafanyakazi kudai maslahi yao na kuchangia kwa harakati za kudai uhuru kwa kiasi kikubwa. Na pia katika sura hii ndipo tunasikia juu ya kuzaliwa kwa Azimio la Arusha. Sura ya tano inasimulia juu ya harakati za kupinga Unyanyasaji na Ubaguzi: “ Baada ya Uhuru, mnamo mwaka 1963, nilipokuwa ziarani Mbeya katika harakati zangu za kuhimiza usawa katika vyama vya wafanyakazi, nilishangaa sana kukuta vibao chooni vikieleza hii ni “Choo ya waafrika tu”, “ Choo ya Waasia tu” na “ Choo ya Wazungu tu” (Uk 52) Anaendelea kuelezea juu ya Ubaguzi. “ Nilipomaliza ziara ya Mbeya na kurudi Dar-es-salaam niliitisha mkutano wa waandishi wa magazeti na kulaani vitendo hivyo. Magazeti yote kesho yake yaliandika habari hizi. Gazeti la Ngurumo pamoja na redio vilitangaza katika vichwa vya habari “ ACHA UBAGUZI WA MAVI KAZIMOTO” (Uk 52). Sura ya sita ni simulizi juu ya uongozi alioushiriki mzee Kazimoto: Uongozi kwenye vyama vya wafanyakazi, Uongozi katika siasa, uongozi katika vyama vya ushirika, matatizo katika uongozi wa ndani ya KDCU, Kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa KDCU, jinsi alivyokabiliana na matatizo ndani ya KDCU, matatizo kwenye vyama vingine vya Ushirika Tanzania, jinsi alivyofikia hatua ya kungatuka KDCU, Uongozi katika chama cha Saidia wazee Tanzania (SAWATA), Uongozi katika KAPETFU, Uongozi katika Saidia wazee Karagwe na uongozi katika mfuko wa misaada kwa wazee. Sura ya ya saba ni uwakilishi wake ndani ya nchi. Hapa anaelezea sehemu zote alizofanya kazi ya uwakilishi, kwenye siasa, asasi zisizokuwa za serikali na kwenye dini. Kuwa kwenye bodi za shule na vyuo hadi kwenye bodi ya KAMEA inayoiendesha Radio Karagwe. Sura ya Nane, anaongelea nchi mbali mbali alizozitebelea wakati anafanya kazi hata baada ya kustaafu. Nchi hizo ni kama: Algeria, Misri, Ethiopita, Mali,Moroko, Rwanda, Zambia, Zimbabwe, Uganda, Albania, China, Chekoslavakia, Ujerumani, Hungari, Israel, Uingereza, Urusi na Marekani. Sura ya tisa, anasimulia shughuli binafsi za Kilimo, Mifugo, Biashara na Ujenzi. Hapa tunasikia juu ya Kilimo na mashamba yake, mashamba ya miti na utuzanji wa ma zinginria, ufugaji wa Kuku, Ng’ombe,Mbuzi na mifugo mingineyo. Pia katika sura hii anaongelea juu ya biashara; chimbuko la kuanzisha biashara, biashara yake ya kwanza ya karanga na kibanda kidogo,mashine ya kusaga nafaka, biashara ya ushonaji na biashara ya maduka, KAZCOM, nyumba za kupanga, Tabora, Mwanza na Dar-es-salaam. Ujenzi wa nyumba ya familia na nyumba nyinginezo. Sura ya kumi ni simulizi juu ya familia ya Kazimoto, ndugu na marafiki. Tunasikia juu ya ndoa yake ya kwanza, mke wake wa kwanza aliyezaa watoto 7, na ni marehemu. Mke wake pili ambaye naye amemzalia watoto 7. Tunaelezwa juu ya watoto wote wa mke wa kwanza na watoto mke wa pili. Mwandishi anasimulia juu ya wajukuu zake, ndugu na wanaukoo wa Karibu, marafiki wa karibu wa Kazimoto, Marafiki wa utotoni na shuleni, marafiki wa kwenye maisha kwa ujumla, marafiki sehemu za kazi na ujirani, marafiki katika Biashara na marafiki wa familia kupitia kwa wake zake, watoto na wajukuu. Sura ya kumi na moja ni juu ya wengine wanavyozungumza juu ya Kazimoto, wanavyomfahamu. Sura ya kumi na mbili ni wosia wa Mzee Kazimoto kwa watoto wake, wajukuu, marafiki ndugu na jamii nzima: “ Tujaribu kupima mienendo na tabia zetu kwa kuangalia matendo yetu na marafiki tunaoongozana nao. Tusiige mambo mabaya, bali tutafute na kuchukua mazuri yaliyofanywa na wenzetu waliofanikiwa. Tufikiri na kutaka maneno mazuri kila wakati ili vichwa na matendo yetu vivutiwe nayo. Hii ni pamoja na kuwapatia watoto wetu na wenzetu majina mazuri. Ninaamini jina “Kazimoto” alilopewa baba yake na ukoo mzima tukalirithi, linatulazimu wanaukoo waliolikubali kufanya kazi motomoto...” Katika wosia Mzee Kazimoto, anaendelea kusema “ Ninawaasa wasomaji wangu, mwendeleee kumwoba Mungu awasaidie na kuwaongoza, mjitahidi kutengeneza maisha yenu kwa kujali ubinadamu na kuleta maendeleo kwa familia, ukoo na jamii zenu kwa ujumla. Mkifanikisha hivi, hata kama ni kwa vikundi vidogo kwa kuanzia, basi mpanue maendeleo kwa jamii na mwishowe mtaiona dunia inayowazunguka kuwa nzuri...” (Uk 212). Wosia wa Mzee Kazimoto unakuwa changamoto pale anapogusia usawa wa kijinsia “ Ninajua mambo fulani yanayombeza mwanamke katika biblia na baadhi ya tamaduni za kiafrika. Lakini, ukweli ni kwamba, wanawake ama watoto wa kike, kwa kusema ukweli, wana msaada mkubwa kwa wazazi kuliko watoto wa kiume na wakiwezeshwa wanaweza. Kwa asababu ya asili yao, watoto walio wengi wa kike wana huruma na ubinadamu mkubwa, hivyo kuwa na msaada mkubwa kwa wazazi kuliko watoto wa kiume...” ( Uk 214). Sura ya kumi na tatu ni shukrani. Mzee Kazimoto anawashukuru watu mbali mbali waliyoyafanikisha maisha yake na anamalizia kitabu chake kwa sala. V. TATHIMINI YA KITABU. Nianze kwa kumpongeza Mzee Nekemia Musa Kazimoto, kwa kazi nzuri aliyoifanya kutuandikia maisha yake. Hii ni historia ambayo ingefukiwa kama angefikia mwisho wa maisha yake bila kuandika chochote. Inawezekana kwa vile ameshiriki harakati nyingi za kuleta maendeleo, angejitokeza mtu kuandika juu yake; tofauti na yeye alivyoandika, mwandishi mwingine angeweza ama kupotosha au kusifia kuvuka mipaka. Kwa kuandika mwenyewe, amejiwekea kipimo. Hata akitokea wa kuandika juu ya maisha yake, wasomaji watampima mwandishi huyo na yale aliyoaandika Mzee Kazimoto mwenyewe. Pili, nimpongeze Mchapishaji wa kitabu hiki Mzee Pius Ngeze, kwa kuwasukuma na kuwashauri wazee wenzake kuandika maisha yao. Amefanya kazi nzuri na kuleta mabadiliko makubwa katika fikra za watu. Walio wengi waliamini maisha au historia ya mtu inaandikwa baada ya kifo chake. Kumbe ukweli ni kwamba hata mtu ambaye bado ni hai anaweza kuandika maisha yake. Kwa vile Mzee Pius Ngeze, ana nyumba ya kuchapa vitabu, kazi hii ya watu kuandika maisha yao imekuwa nzuri na kuleta changamoto mkoa wa Kagera na taifa zima kwa ujumla. Tatu. mwandishi amefanikiwa kuyaelezea maisha yake kwa ufupi, kwa uwazi na unyenyekevu mkubwa. Mzee huyu ni miongoni mwa watu Mashuhuri Mkoani Kagera. Watu wengi wanamfahamu, ila nina mashaka kama walifahamu historia yake. Mimi ninayeandika uhakiki huu, nimemfahamu siku nyingi na ni mzee wangu wa karibu, nimekuwa karibu na watoto wake hasa mvulana wake wa kwanza Andrew, lakini sikufahamu mengi juu yake kama yanavyosimuliwa kwenye kitabu , na wala sikufahamu kama mali aliyonayo aliipata kwa mahangaiko makubwa, lakini la muhimu zaidi ni jinsi Historia yake inavyoifunua historia ya mkoa wa Kagera, ambayo nimekuwa nikiipigia kelele siku nyingi. Nimekuwa nikidai kwamba, mtu wa Mkoa wa Kagera, ambaye hana chimbuko Rwanda, Burundi na Uganda, si mwenyeji wa Kagera. Hivyo swala zima la uhamiaji haramu katika Mkoa wa Kagera, ni lazima liendeshwe na watu wenye akili nzuri, wenye hekima na busara. Vinginevyo wenyeji wote wa Mkoa wa Kagera, watabatizwa “wahamiaji haramu”. Tumesikia jinsi ukoo wa Abaiuzi, ulivyochimbuka Ehthiopia, ukasambaa Bukoba, Karagwe hadi Mtwara. Mtu atakayesoma kitabu hiki atakuwa mwangalifu kuongelea uhamiaji haramu mkoa wa Kagera. Nne ,mbali na kufafanua mambo ya familia yake na historia nzima ya maisha yake ya utumishi, siasa , asasi za kijamii , kitabu hiki pia ni fundisho kwa vijana kwamba mafanikio katika maisha hayaji kwa njia za mkato. Yanakuja kwa kutoa jasho. Mtu anaweza kufanikiwa bila kujiingiza kwenye magendo, rushwa, ufisadi au kuuza madawa ya kulevya. Mtu anaweza kufanikiwa, akiaacha tabia za kukaa vijiweni bila kufanya kazi. Tano, Mwandishi, anaonyesha jinsi anavyoshirikiana na watanzania wote bila kujali dini zao. Hili ni fundisho maana, kuna hatari ya kuachia dini zetu zitutenge na kutuelekeza ni mtu gani wa kushirikiana naye. Mjadala wa mahakama ya kadhi, unataka kutugawa kidini na kuna vuguvugu hasa upande wa Zanzibar wa kuanza kuleta choko choko za kidini. Ni lazima tujifunze kutoka kwa wazee wetu, jinsi walivyoishi pamoja na kushirikiana, bila kujali utofauti wa dini zao. Sita, vyamba vya ushirika na muhimu kwa wakulima wadogo wadogo. Kwa Karagwe, KDCU ni muhimu kwa wakulima. Katika kitabu chake Mzee Kazimoto, ameelezea matatizo yanayovikumba vyamba vya ushirika. Tukimsikiliza na kusahihisha matatizo yaliyopo sasa hivi, Karagwe inaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kutumia vyama vya ushirika. Saba, familia ya watoto 14, ni kubwa. Kufanikiwa kuiongoza bila matatizo makubwa, kama anavyoaandika na kama tunavyoshuhudia ni jambo la kupongezwa. Watoto wa mama wawili tofauti, kuungana na kuishi kwa kushirikiana ni jambo la kupongezwa pia. Hivyo familia ya Mzee Kazimoto ni ya mfano, kwa Karagwe, Kagera na Tanzania nzima. VI. HITIMISHO. Kwa kuhitimisha basi, ninawashauri watanzania wakitafute kitabu hiki na kukisoma. Watachota hekima za mzee huyu.Kwa watu wa Karagwe ni muhimu wote kukisoma kitabu hiki. Mbali na hekima nyingi iliyojaa humo, ni vyema watu wakatambua umuhimu wa kuelezea mahusiano, ili kuepusha jamaa wa damu kuoana na kutambua mahusiano haya ili kujenga jamii inayoheshimiana, na kuchukuliana. Lakini pia ninawaomba wazee wetu wengine waliobaki wayaandike maisha yao kama alivyofanya Mzee wetu Nekemia Musa Kazimoto. Kuna wazee kama vile Mzee Gabriel Kasesene wa Bushangaro, Mzee Deogratias Tigalyoma, Mzee Laurent Ishungisa, Mzee Theobard Kagande, Mzee Anthony Bijura, Mheshimiwa Balozi Ferdinand Kamuntu Luhinda, Askofu Mstaafu Paulo Mkuta, Askofu Mstaafu Kazoba, Mtume Nzalombi Marehemu Mzee Tinamanyile, Marehemu Mwalimu John Kahatano wa Isingiro na wengine wengi wana historia ambayo haijaandikwa. Wakisoma kitabu hiki cha Nekemia Musa Kazimoto, watashawishika nao kuanza mchakato wa kuandika maisha yao. Taifa letu lina watu mashuhuri ambao maisha yao hayajaandikwa. Hivyo mradi wa Tanzania Educational Publishers LTD, wa kuandika maisha ya watu mashuhuri wa Mkoa wa Kagera, ni muhimu na ni wa kuungwa mkono. Na ni vizuri mradi huu ukijitandua nchi nzima. Watu mashuhuri kama Marehemu Mwadhama Laurian Kadinali Rugambwa, maisha yao hayajaandikwa.Marehemu Askofu Josia Kibira, Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, historia ya maisha yake haijaandikwa. Wako wengi kama Marehemu Kichwabuta na wengine wengi. Hivyo kitabu hiki cha Maisha na Harakati za Kazimoto ni mwendelezo wa njia aliyoifungua Mzee Alhaji Abubakari Rajabu Galiatano, ambaye naye kitabu cha maisha yake kilichapwa na Tanzania Educational Publishers LTD na wengine wafuate. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment