WAZIRI NCHIMBI, TANZANIA IMEBADILIKA! Mungu, ailaze roho ya mwandishi Mwangosi, mahali pema peponi. Uhai wake umetoka na hauwezi kurudi! Ukatili mkubwa na unyama wa kumfanyia mwanadamu ni kuutoa uhai wake. Ndo maana dunia hii ina mfumo wa serikali, kuhakikisha kuna chombo cha kulinda uhai wa mwanadamu. Hata kama wale waliomvamia, kumpiga na hatimaye kutoa uhai wa mwandishi Mwangosi, watakamatw na kufikishwa mahakamani, haitasaidia kurudisha uhai wake au kushughulikia maendeleo ya familia yake. Uhai wa Mwangosi umetoka na hauwezi kurudi milele. Katika umri wake mdogo, maisha yake yamekatishwa; hakuwa mwizi, hakuwa jambazi na wala hakuwa mchawi: Alikuwa mwandishi wa habari na amekufa akiwa kazini, amekufa na kamera yake mkononi! Ndo maana tunasikitika na kulaani kwa nguvu zote kitendo hiki cha kinyama kilichotekelezwa na Jeshi la polisi. Ndo maana pia tunamshangaa Mheshimiwa Nchimbi, waziri wa mambo ya ndani, kuibuka na kusema kwamba Dr.Slaa akamatwe. Nchimbi, anashindwa kutambua kwamba Tanzania imebadilika? Tanzania ya leo si ile ya jana ya Chama kushika utamu na chama kutoa maagizo bila hata kufuata utaratibu. Akikamatwa Dkt Slaa, tutasimama na kuhoji, tutasimama na kupiga kelele nje na ndani ya nchi; vitendo vya kinyama vinavyoendelea kama kichapo cha Ulimboka na sasa kifo cha Mwangosi haviwezi kuzima sauti za waandishi, sauti za wanaharakati wa kutetea haki za binadamu na sauti za vijana wa sayansi na teknolojia wanaotamani mabadiliko katika taifa lao. Katika hali ya kawaida, au kwenye nchi inayofuata utawala bora, uwajibikaji na demokrasia,kitendo cha Polisi kuonekana wakimpiga Mwandishi wa habari na hatimaye kusababisha kifo chake, Waziri wa mambo ya ndani angezungumza na vyombo vya habari kutangaza kujiuzulu, IGP na RPC wa Iringa wakimfuata; kwa mshangao Waziri Nchimbi, alifanya kinyume! Anaanza hadidhi za kukamatwa kwa Dkt Slaa na kuunda tume. Alipokumbushwa kwamba hana madaraka ya kuunda tume, akasema alinukuriwa vibaya! Yeye alimaanisha kamati! Hata hivyo hawezi kuunda kamati ya kuchunguza kifo! Hili haliko kwenye madarka yake! Kamati ya kuchunguza kifo inaundwa na rais! Hata hivyo Waziri wa mambo ya ndani hawezi kuunda kamati ya wizara yake, ikavuka mipaka ya wizra hiyo kwa kuingiza kwenye kamati yake wanajeshi, majaji na waandishi wa habari. Inaonekana wazi kwamba Waziri Nchimbi, hafahamu anachopaswa kufanya kwenye tukio kama hili la Iringa. Hivyo ni wajibu wetu kumbumbusha: Kitu cha kwanza ni kujiuzulu! Kitu cha pili ni kutoa ushirikiano kwa tume itakayoundwa na Rais kuchunguza kifo hicho. Zaidi ya hapo ni kututangazia kwamba yeye ni mtu asiyefaa kwa uongozi. Kujiuzulu si mwisho wa safari katika uongozi. Mzee Mwinyi, alijiuzulu kwa kuwajibika, lakini hilo halikumzuia yeye baadaye kuwa Rais wa taifa letu. Hata kama Nchimbi, ana malengo ya kuwa Rais wa taifa letu hapo baadaye, asiogope kujiuzulu kwa kuwajibika maana hilo linamjengea jina. Waziri wa Mambo ya ndani anaweza kuunda kamati ya kuchunguza msongamano wa magari, ajali za kila siku zinatokatisha maisha ya watanzania, wahamiaji haramu wanaofia kwenye makonteina, rushwa kutawala Jeshi la polisi na labda anaweza kuchunguza vitendo vya polisi vya kukikumbatia chama chake cha Mapinduzi badala ya kulitumikia taifa. Polisi ni watumishi wa umma, si watumishi wa chama chochote cha siasa. Wakienda kinyume, waziri wa mambo ya ndani anayefahamu vizuri kazi yake ni lazima aunde kamati ya kuchunguza ugonjwa huo na kutafuta mbinu au dawa ya kuuponya. Vyovyoe vile, iwe tume au kamati bado Nchimbi anatapatapa! Ukweli unabaki pale pale kwamba Nchimbi akishindwa kujiuzulu kwa kashifa ya kifo cha mwandishi wa habari kilichotokea mikononi mwa Polisi, basi ajiuzulu kwa kuonyesha wazi kwamba hafahamu kazi yake! Hafahamu kwamba yeye hana uwezo wa kuunda tume yoyote ya kuchunguza kifo. Hiyo ni kazi ya rais! Kama anaanza kuingilia kazi za rais, atamshawishi nani kwamba anafahamu kazi yake na anafaa kwa kazi hiyo? Dkt Slaa, akamatwe kwa lipi? Yeye alitaka Polisi wawalinde watu na si kuwaua watu. Yeye hana polisi na wala hatujasikia akiwaamlisha wafuasi wa CHADEMA kufanya matendo ya kinyama ya kutoa uai wa mtu. Sababu za vifo vyote vinavyotokea wakati wa mikutano ya CHADEMA, ziko wazi kabisa. Jeshi la polisi linaangukia upande mmoja. Jeshi la Polisi linafanya kazi ya kukilinda chama cha Mapinduzi. Kuna mifano mingi ambayo imejionyesha wazi wazi kwamba Jeshi hili linafanya kazi ya kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinabaki madarakani milele. Tumeshuhudia hata wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 jinsi jeshi hili lilivyotumia nguvu nyingi kuhakikisha wagombea wa wa Chama cha Mapinduzi wanashinda uchaguzi. Hivyo wa kukamatwa kwenye matukio haya ya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia ni Jeshi la Polisi na waziri wa mambo ya ndani na wala si Dkt Slaa. Tunaambiwa kwamba ni lazima kutii sheria. Na kosa la Chadema ni kukataa kutii sheria na amri. Hakuna anayepinga hili. Kufuata sheria ni msingi wa utawala bora na nchi zote duniani zinaendelea kwa kufuata sheria. Na jeshi la polisi lina wimbo wake wa “ Kufuata sheria bila shuruti”. Hata hivyo tunajua zote kwamba kuna sheria nzuri na sheria mbaya. Sheria ya ubaguzi wa rangi kule Afrika kusini ilikuwa mbaya na watu walisimama kuipinga sheria hiyo. Kwa kufanya hivyo baadhi walipoteza maisha yao. Sheria za upendeleo zinazokumbatia upande mmoja na kugandamiza upande mwingine, zinakataliwa popote duniani. Tumeshuhudia Polisi wakikataza maandamano ya vyama vya upinzani na kuruhusu maandamano ya CCM. Hivyo kwa wachambuzi wa mambo ya siasa hapa Tanzania, wanaona kuna njama za kuhakikisha vyama vya upinzani havipati nafasi ya kujijenga vijijini kwa kuvizuia kufanya mikutano na maandamano kwa kisingizo cha kuhatarisha usalama. Igunga, Mwanachama wa CCM alipanda kwenye jukwaa la kampeni akiwa na bastola. Juzi tumesikia kwenye mutano wa CCM kule Nzenga, wanachama wa CCM wamekitishiana kwa bastola! Nani anahatarisha usalama? Anayefanya maandamano bila silaa au anayekwenda kwenye mikutano ya siasa akiwa amebeba bastola? Mbona hatusikii Polisi wakizungumza juu ya matukio haya? Mbona hatusikii Jeshi la Polisi likitumia nguvu kubwa kwenye mikutano ya CCM? Siku ya kifo cha Mwangosi, Polisi walizuia mkutano wa Chadema kwa kisingizio cha Sensa. Tungependa kujua kwenye kijiji hicho ni watu wangapi walikuwa hawajahesabiwa kiasi cha kuzia mkutano? Ni watu wangapi walikuwa hawajahesabiwa kiasi cha polisi kutumia nguvu kiasi hicho hata kufikia hatua ya kufumba macho na kumpiga vibaya mwandishi wa habari na kusababisha kifo chake? Ilikuwa ni kutaka kusaidia zoezi la senza kuendelea au ilikuwa ni njia ya kuhakikisha CHADEMA wanasitisha harakati zao za M4C? Tutajenga taifa letu kwa kulinda uhai wa kila raia, hatuwezi kulijenga taifa letu kwa kutoa uhai wa raia. Na ni bora Waziri nchimbi akatambua kwamba Tanzania, imebadilika; Tanzania ile ya ushindi wa mtandao si ya leo! Na, Padri Privatus Karugendo. +255 734 633122 www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment