KISIKI KIKAVU
UHAKIKI WA KITABU: KISIKI KIKAVU
1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA
Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Kisiki Kikavu na kimetungwa na Aldin Mutembei. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Limited na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN) 9987 411 347. Kimechapishwa mwaka 2005 kikiwa na kurasa 72. Na anayekihakiki sasa hivi ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. UTANGULIZI.
Hii ni hadithi ya kubuni na mhusika mkubwa akiwa Kalabweli. Mazingira ya hadidhi hii ni Mkoa wa Kagera, Nchi ya Uganda (vita na mpakani) na Dar-es-salaam. Hadithi inafunua historia ya Ugonjwa wa Ukimwi, mkoani Kagera.
Kalabweli alitarajia kuwa angewatunza wazazi wake, dada na wadogo zake. Na kweli Kalabweli alifanikiwa katika biashara, akashamiri, akapenda na kupendwa, akaijua pesa.. Kisiki Kikavu kinatufunulia maisha ya Kalabweli ambayo yamebeba historia ya UKIMWI huko mkoani Kagera. Historia iliyoanzia katika umasikini uliofuatia vita vya Iddi Amin, hali iliyozaa biashara ya magendo na maisha ya starehe iliyokithiri. UKIMWI ukabisha hodi ukapatiwa majina; Juliana, Silimu, Ninja nk.
Kwa maneno ya Profesa F.E.M.K Senkoro, Mwanafasihi wa Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, Kisiki Kikavu kinaweka wazi udhaifu wetu katika kukabili changamoto za maisha. Jinsi mtu anavyozidi kusoma Kisiki Kikavu ndivyo anavyoona kwamba historia, siasa, mila na uchumi vimeshikamana katika kuibua na kutandawaza janga la UKIMWI, na hapo ndipo mtu anapogundua Ukavu wa fikra za mwadamu. Na kwamba hii ni riwaya ya aina yake inayochambua taadhira ya VVU, uelewa wa watu, ukubalifu wao na jinsi tabia zinavyobadilika kwa wakati, mahali na kwa rika.
Kitabu kina sura nane na zimepewa majina badala ya namba. Majina haya ni: Handaki, Kikomela, Ihembe, Juliana, Silimu, Ninja, Kadi Nyekundu na Kisiki Kikavu. Majina yote kwa namna moja ama nyingine yanahusiana na Ugonjwa wa UKIMWI. Ni historia ya ugonjwa huu ulivyoendelea kujifunua miongoni mwa jamii ya watu wa mkoa wa Kagera na baadaye kuenea hadi Dar-es-salaam. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu.
III. MUTASARI WA KITABU.
Sura ya Kwanza, inayobeba jina la Handaki, linaelezea maisha ya watu wa Kagera, mara baada ya vita ya Kagera. Vita iliacha nyuma Mahandaki, ambayo watu walikuwa wakiyatumia kujificha maadui na ndege za Iddi Amin, zilizokuwa zikitupa mabomu. Baada ya vita mahandaki, yakawa maficho ya nyoka na chatu. Familia ya Mzee Kakwezi, inaanza kuonja machungu ya mahandaki. Mtoto Keisho, anamezwa na chatu ndani ya handaki. Katika sura hii msomaji anaonja falsafa ya mwandishi. Maana mahandaki yanakuwa na maana pana zaidi ya mashimo yaliyochimbwa kwa nia ya kujificha maadui.
Katika sura hii, mwandishi anatuaandaa ili tuone matokeo ya vita. Maana si mahaandaki tu, baada ya vita maisha yalikuwa magumu, serikali ilitangaza miezi 18, ya kufunga mikanda. Hali hii ilipelekea chanzo cha biashara ya magendo iliyokuwa ikifanyika kati ya Uganda na Tanzania. Biashara hii, ilileta neema na maafa.
Sura ya pili, inayobeba jina la Kikomela, inatufunulia hali ya biashara ya magendo ilivyofanyika. Kikomela, ni soko lililokuwa likiendesha biashara ya magendo mpakani mwa Uganda na Tanzania.
“ Barabarani, na hasa kwenye njia panda, vile vizuizi vilivyowekwa wakati wa vita kuwashika wapelelezi na maadui wengine, sasa vikageuzwa vizuizi vya kuwashika wafanya magendo. Vizuizi hivyo vilileta kero kubwa kwa raia wasio na hatia” (uk 11).
Vijana waliacha shule na kuanza kufanya biashara ya magendo. Kwa maelezo ya mwandishi, magendo ilileta neema na kuwafanya watu kusahau hali ngumu ya vita. Pesa za magendo ziliwafanya vijana kuponda raha, kunywa na kugeukia uzinzi.
Sura ya tatu, inayobeba jina la Ihembe, inatufunulia wagonjwa wa kwanza kupata ugonjwa wa UKIMWI. Kwa vile wagonjwa mwanzoni ni wale waliokuwa wakienda kufanya biashara kule Uganda, iliaminika kwamba walifanya mambo mabaya kule Uganda, na ndiyo maana walipata “Ihembe” (Aina Fulani ya uchawi:
“ Ndugu zangu zikilizeni. Hapa tumeingiliwa. Hakuna mtu ambaye hajui misiba inayotupata siku hizi. Watu wanakufa, wanakufa mmojammoja. Miili yao haisikii dawa tena. Huu si ugonjwa. Na hospitalini wameshindwa. Hospitali zote, hata kule Bukoba, wagonjwa wanakwenda wanarudishwa. Baada ya muda kifo ‘kifo cha ajabu’. Watu hawa kama nilivyoona, wamewadhulumu wenzao huko kwenye biashara zao. Dhuluma ndiyo imeleta vifo hivi Hiki ni Kisasi. Ni lazima tufanye kafara. Twende tukamwage kahawa katika mto Kagera…” (uk 31).
Sura ya nne, Ukimwi unapata jina la Kwanza. Jina hili ni Juliana. Hii ilitokana na vitambaa vya nguo vilivyojulikana kama Juliana, vilivyokuwa vikitokea Uganda. Vijana waliokuwa wakifanya magendo, waliviuza na kuvivaa vitambaa hivi. Hivyo ugonjwa huu, ambao haukujulikana ukapata jina la Juliana. Hapa watu wengi walianza kuambukizwa na kupoteza maisha kwa ugonjwa huuu wa Juliana.
Katika sura ya tano mwandishi, anatupatia jina pili la ugojwa huu, ambalo lilitokana na namna wagonjwa walivyokuwa wakipungua kabisa na kubaki mifupa. Ugonjwa ukabatizwa Silimu. Na katika sura inayofuata, baada ya ugonjwa huu kusambaa na kuvuka mipaka ya mkoa wa Kagera, ukawa na majina mengine kama vile Ninja.
Sura ya saba na ya nane zinazobeba majina ya Kadi Nyekundu na Kisiki Kikavu, zinaonyesha jinsi ugonjwa wa IKIMWI, ulivyoenea na kuzagaa na kuacha visiki vikavu. Familia ya mzee Kakwezi, iliyoanza kuonja machungu ya maandaki, inampoteza shujaa wa familia Kalabweli, aliyefanya biashara ya magendo, akapata pesa, akaponda raha hadi akahamia Dar-es-salaam, na kuendelea kuponda raha hadi akafa na huku akiacha idadi ya watu wengi wakimfuata nyuma yake.
IV. THAMINI YA KITABU.
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Aldin Mutembei. Awali ya yote lazima niseme kwamba kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki au niseme hadithi hii ambayo ni ya kubuni inasisimua sana. Mwandishi, amefanikiwa kuchora historia ya ugonjwa wa Ukimwi mkoani Kagera na jinsi ulivyosambaa nchi nzima. Inajulikana wazi kwamba mgonjwa wa kwanza hapa Tanzania, aligunduliwa mkoani Kagera.
Pili, mwandishi amefanikiwa kuonyesha jinsi vita vya Iddi Amini, vilivyoleta maafa mengi. Ugumu wa maisha uliofuata baada ya vita, ulisababisha biashara ya Magendo na mwingiliano wa watanzania na waganda ukawa mkubwa. Inaaminika kwamba hiyo ndo ilikuwa njia ya kuingiza UKIMWI, hapa Tanzania. Labda, nani anajua, bila vita, ugonjwa huu, ungeinga kwa namna nyingine, au ungetukuta tumejiandaa na kuwa na elimu juu yake.
Tatu, mwandishi ameonyesha wazi kwamba bila elimu, watu wanaweza kuangamia bila kujua. Mfano unajionyesha kwenye majina ya Ukimwi, mwanzoni walifikirini uchawi, baadaye ikawa Juliana, Sililmu na Ninja. Viongozi wa dini walifikiri ni shetani na adhabu kutoka kwa Mungu. Mwandishi, ameyachora haya vizuri kabisa kiasi cha mtu anaposoma, anajional yuko mbele ya mchungaji akipata mahubiri juu ya shetani anayepitia kwenye ugonjwa wa UKIMWI. Hapa tunapata fundisho kwamba elimu na utafiti ni vitu vya msingi.
Nne, mwandishi amefanikiwa kuonyesha kwamba historia, siasa, mila na uchumi vimeshikamana katika kuibua na kutandawaza janga la UKIMWI.
Tano, mwandishi amefanikiwa kugusa nyanja mbali mbali katika jamii yetu, amegusia vyuo vyetu na maadili yanavyochechemea, amegusia familia, serikali, dini na kuonyesha jinsi kila mtu anavyoguswa na ugonjwa huu wa UKIMWI.
Ingawa hadithi hii ya Bwana Mutembei, inasisimua na kumfanya mtu atafakari mengi na kuwa mwangalifu juu ya ugonjwa huu wa hatari, hadithi yake inaisha bila ya matumaini. Kisiki kikavu, hakina maisha na si dalili za matumaini. Wakati huu, si wakati wa kuongelea Kisiki Kikavu, bali shina linalochipuka!
Kwa namna ya kushangaza kidogo, Bwana Mutembei, ameamua kutogusia kampeni ya Tosheka naye, acha au tumia kinga. Ni kweli mambo haya, hayapunguzi utamu wa kitabu. Bado ni kitabu kizuri kukisoma. Ila hadidhi yake ingenoga zaidi kama angejitahidi kuingiza mambo kama haya. Kwa vile anaelezea historia ya ugonjwa huu, isingekuwa mbaya kuonyesha na hatua nyingine zilizofikiwa hivi sasa. Hata hivyo hadithi yake ni ya hivi karibuni 2005.
Matumaini mengine, ambayo yako sasa hivi ni dawa za kurefusha maisha, dawa za kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, na kuna ukweli kwamba siku hizi maambukizi yanapungua baada ya watu kuanza kuufahamu ugonjwa huu, na kuacha kufikiri kwamba ni uchawi. Kisiki Kikavu, sasa hivi ni shina linalochipuka!
V. HITISMISHO.
Kwa kuhitimisha, ninawaomba watanzania wakisome kitabu cha Kisiki Kikavu, ili wapate mengi kuhusiana na Ugonjwa huu wa UKIMWI. Ingawa, hii ni hadithi ya kubuni, lakini imesheheni mifano hai ya kutusaidia kupambana na ugonjwa huu wa hatari.
Pia ningependa kumshauri Bwana Mutembei, kuandika hadithi nyingine ya Shina linalochipuka. Yeye kama mtafiki wa ugonjwa huu katika mkoa wa Kagera, kwa miaka mingi sasa, anajua ukweli wote kwamba kuna matumaini makubwa. Baada ya giza la Ihembe, Juliana na Silimu kupotea, sasa hivi kuna mwanga mpya na matumaini.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment