UHAKIKI WA KITABU: SUGU, MUZIKI NA MAISHA: From The Streets To Parliament. 1. Rekodi za Kibibliografia. Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni SUGU, MUZIKI NA MAISHA:From The Streets To Parliament, Kimeandikwa na kuchapishwa na Sugu na amekipatia kitabu chake namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 9987 9491 1 3 .Kitabu kina kurasa 147 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. Utangulizi Hiki ni kitabu kinachoyaelezea maisha ya Mheshimiwa Sugu: Joseph Osmund Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya mjini kupitia chama cha CHADEMA. Ndani ya kitabu hiki anaelezea vizuri jinsi Muziki ulivyoyajenga maisha yake na jinsi alivyoibuka kutoka mitaani kuelekea kwenye Bunge. Sugu mwenyewe anasema: “ Nilipokuwa mdogo sikutarajia kabisa kama siku moja ningekuja kujulikana na kuwa maarufu kiasi hiki na kwa jina la Sugu... Jina hili hapo nimelipata kuitpita muziki wa Rap au Bongo Flava, lakini historia halisi inaonesha wazi kuwa ninastahili na kwa kweli nimelipenda sana kwa maana naamini linaendana na mimi hasa...Nahani kwamba nililipenda jina la Sugu kuliko haa niavyoyapenda majina yangu mengine ya mwanzo niliyowahi kuyatumia... Naamini kuwa nimeweza kufika hapa nilipo kisanii, hata kimaisha kiujumla kwa sababu ya kuwa Sugu, maisha yangu yote nimejitahidi kuwa Sugu, Nimekuwa Sugu kwa vikwazo mbali mbali maishani.” Ingawa kitabu hiki kimeandikwa na Mheshimiwa Mbunge, tena kutoka chama cha upinzani, si kitabu cha siasa. Mwandishi anaelezea jinsi alivyopambana na maisha na jinsi anavyoendelea kupambana na maisha. Ni mbunge aliyotoka kwenye mazingira ya watu wa kawaida; hakutoka kwenye familia ya Kisiasa na wala hakubebwa kwenye nafasi yake kama tulivyozoea kuwaona viana wengi wakibebwa na baba zao, jamaa zao au rafiki zao kuingia katika siasa na wakati mwigine kupata nafasi za juu serikalini. Kitabu kina sura 11 na zote zinaelezea mapambano ya maisha. Pia kitabu kina picha nyingi zinazoonyesha maisha ya Sugu, kuanzia shuleni, harakati zake za Muziki na hatimaye kuingia Bungeni. Kwa kurasa zinazofuata nitakifanyia uhakiki kitabu hiki, baada ya kuelezea kidogo mazingira yanayokizunguka kitabu chenyewe. III. Mazingira yanayokizunguka kitabu Hiki ni kitabu cha kizazi kipya. Hata lugha iliyotumika ni ya kizazi kipya! Bila kuwa makini mtu atafikiri ni kitabu cha kiuni. Ukweli ni kwamba lugha iliyotumika kwenye kitabu hiki ndiyo lugha ya vijana wengi. Ni lugha ya wakati uliopo, itakuja na kupita na hakuna haja kugombana nayo maana wakati ukuta. Misemo kama vile: ‘Mbongo’ ‘siriaz’ ‘wangenimaindi’’stori’ ‘mademu’ na mingine mingi imejaa kwenye kitabu hiki. Twaweza kusema kwamba si kiswaili sanifu, lakini ndo lugha ya vijana. Kama tunataka kuwasiliana na vijana, hatuwezi kukwepa Lughaya vijana. Misemo hii inaleta mvuto wa kipekee kwenye kitabu hiki ambacho mwisho wake ni kutoa ujumbe mzito kwa vijana wa Tanzania na kwa wananchi wote wa Tanzania. Kitabu hiki ambacho kinayaelezea maisha ya Sugu kinakuja na falsafa mpya: Maisha ni ubishi!: “Maisha nivile unavyoishi, inakubidi uwe mbishi...”. Na huu ni msemo wa kizazi kipya. Maana yake ni kutokukata tamaa na kuendelea kupambana hadi kinaeleweka. Sugu, anaelezea mapambano yake na walimu, mapambano yake na maisha hadi kusafiri hadi kusini mwa Afrika akitafuta maisha. Katika safari ya maisha yake, anatuonyesha falsafa hii ya “Maisha ni ubishi”. Ameteleza mara nyingi na kuanguka, lakini daima alisimama na kusonga mbele. Kitabu hiki kinakuja wakati watanzania wengi hawajajenga tabia ya kusoma vitabu na kuandika vitabu. Wengine wanasema ukitaka kuificha siri kwa mtanzania, iandike siri hiyo kwenye vitabu. Hakuna atayeiona maana wengi hawasomi. Tuna wabunge wengi, na wengi wao ni wasomi, ni wangapi wameandika vitabu? Ni wangapi wameandika juu ya maisha yao? Kwa kiuandika juu yamisha yake, inaonyesha jinsi Sugu, alivyomsomaji wa vitabu IV. Muhtasari wa Kitabu Kwa kifupi kitabu hiki cha Mheshimiwa Sugu, kinaelezea maisha yake kuanzia utotoni, maisha ya shule, harakati ya kutafuta maisha, maisha ya kufanya kazi, maisha ya muziki, wivu kwenye fani ya muziki, manyanyaso ya mapromota, wizi wa kazi za wasanii na hatimaye maisha ya kisiasa. Yeye mwenyewe amefanya muhtasari wa kitabu chake kwa maneno : Muziki na Maisha: From The Streets to Parliament. “Jina langu halisi ni Joseph Osmund Mbilinyi. Nilizaliwa 01.05.1972 katika Hospitali ya Serikali ya Mkoa ya Ligula mjini Mtwara... Mimi ni mtoto wa kwanza kwa mama yangu nikiwa na wadogo zangu wanne..” (Uk 1) “ Kuna wakati niliishi maisha mazuri ya ‘kiushuani’, yaani ‘dingi’ mambo safi ambapo nyumbani kila kitu cha muhimu kilikuwa kinapatikana kwa familia, wengine wanaita familia yenye neema au familia bora au hata familia ya mboga tatu!... Kuna wakati niliishi maisha halisi ya uswahilini. Haya ni masiha ya shida ambapo mimi na wadogo zangu watatu wakati huo tulilala chumba kimoja...” (uk 1&2). “Maisha yangu ya utotoni yalikuwa ni ya kuhamahama kutokana na kazi ya baba yetu ambaye alikuwa mwajiriwa, hali hii imesababisha niwe na marafiki wengi wa utototni ambao nilisoma nao shule za msingi na sekondari katika mikoa ya Arusha, Mtwara, Da-es-salaam na Mbeya” (Uk 2). “Hapa tulifanya utundu wote mpaka kuvuta “ganja”! Sishauri vijana na hasa wanafunzi wajihusishe na mam bo haya leo na nakemea kwa nguvu zote, lakini nakiri tulipitia ile kiti aisee” (Uk 7). Inashangaza sana kuona unyoofu wa Sugu. Kutaja hata mabaya aliyoyafanya utotoni. Anayaandika maisha yake kwa uwazi wa kupitiliza. Ni watu wachache wenye ushupavu huu wa kukubali kujivua nguo mwenyewe. Baada ya kuelezea maisha yake ya utotoni, Sugu, anaelezea “Ubishi wake wakati wa kusoma shule” Na kuonyesha kwamba daima alipigania haki na hakuwa na woga wa kusema ukweli na kuusimamia. “Nikaondoka kuelekea bwenini ambapo nilitoa mizigo yangu na kusaidiwa na wanafunzi wa vidato vya chini, walikuwa ananipenda kwa kuwa niliongoza kampeni ya kuzuia wanafunzi wa vidato vya hcini kuonewa hasa wale wa form one, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku wao kutumwa kufua nguo za wanafunzi wa vitadto vya juu, kampeni hii tuliiendesha na Gibbo pamoja na Bonny” (Uk 11). Anaelezea alivyotetea haki wakati akiwa shuleni, hakukubali kuonewa wala mtu mwingine kuonewa. Baada ya kumaliza kidato cha nne, alijaribu kwenda Bondeni, bila mafanikio. Anaelezea safari yake ya kwenda Bondeni, ambayo linafanana zile nyingi tunazozikia, jinsi vijana wanavyojaribu kutoroka kwenda Bondeni kutafuta maisha. Yote hayo yako kwenye falsafa ya Sugu, kwamba “Maisha ni ubishi”. Maana yake ni lazima kupambana bila kurudi nyuma. Sehemu inayovutia sana katika kitabu chake ni maisha yake ya Muziki. Hapa kuna vituko vya mafanikio, kushindwa, kudhurumiwa, kunyanyaswa, kuoneana wivu na vituko vya “Wadosi” (wahindi) jinsi wanavyowanyanyasa wasanii wa muziki. Sugu, amefichua malalamiko ya wasanii ya siku nyingi kwamba kazi zao zinaibiwa na wala serikali haifanyi mpango wowote ule kutunza haki za wasanii. Wadosi, wanavyatua kanda na DVD za wasanii na kuziuza, bila wasanii kupata faida yoyote ile. Safari za Sungu nje na ndani ya nchi zina mvuto wa kipekee katika kitabu hiki. Anaonyesha wazi jinsi Muziki ulivyomsaidia kusafiri sana nje ya nchi na kumsaidia kupanuka kifikira. Pamoja na kwamba yeye aliishia kidato cha nne, lakini kuzunguka sehemu mbali mbali duniani kulimfanya aonekane msomi wa kutupwa. “Mwezi Oktoba mwaka huo, nikiwa tayari nimekaa Uingereza kwa miezi takriban miwili nilipata taarifa toka ‘Bongo’ kwamba nilitumiwa mualiko kwenda Sweden kushiriki tamasha la muziki la WOMEX lililotarajiwa kufanyika Stockholm mwaka 1998” (Uk 73). Pamoja na kupata nafasi nyingi za kwenda nje, Sugu, hakupenda kukaa nje ya nchi. Alirudi nyumbani kuendelea muziki wake na hatimaye kufanikiwa kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chama cha CHADEMA. V. TATHIMINI YA KITABU. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Sugu, kwa kazi aliyoifanya ya kuandika kitabu juu ya maisha yake. Ni watu wachache ambao wanafanikiwa kuandika maisha yao. Hata wasomi, wanashindwa kuandika maisha yao. Mara nyingi maisha ya watu wengi yanaandikwa na wengine baada ya wao kutoweka hapa duniani. Ukweli ni kwamba kazi hii ni nzuri sana . Kitabu hiki kinaburudisha, kinasikitisha na kufikirisha. Pili, nimpongeze kuyaandika maisha yake kwa uwazi bila kificho. Penye sifa ametaja bila kuongeza chumvi, penye lawama amesema bila kificho. Ameelezea tabia zake mbaya na nzuri. Kawaida ni kazi ngumu mtu kujichambua mwenyewe. Mara nyingi kazi hii inafanywa na watu wengine, si mtu mwenyewe. Maana kuna hatari mtu kujipendelea na kuficha mengine ambayo ni mabaya. Lakini Mhesimiwa Sungu, amefanya kazi hii kwa kunyoofu mkubwa. Ukizingatia hatua aliyopo hivi sasa, angeweza kuficha tabia nyingine kama kuvuta ganja na kuwapenda mademu kupindukia. Tatu, ni pongezi kwa kazi ya kufichua manyanyaso ya wasanii wa Muziki. Kumekuwepo malalamiko ya wizi wa kazi za wasanii, lakini Mheshimiwa Sugu, amefichua wizi huu kwa kuuelezea vizuri. “Nilipopata taarifa za kuenea kwa kanda feki za album yangu niliamua kuanza uchunguzi na hatimaye nikapata habari kwam ba dula la Congo Corridor lililoko Kariakoo walikuwa wakitengeneza na kuuza kazi zangu bila ya makubaliano yoyote na mimi...Siku moja niliamua kujitutumua na kwenda dukani kwao, nilipania kupambana kulinda haki yangu, nilipofika niliingia dukani ambapo nilimkuta ‘mdosi’ mwenyewe na wafanyakazi wake, niliulizia ile kanda lyangu nikapewa, baada ya kuhakikisha kwamba ilikuwa feki nilijitam bulisha mimi ni nani na nikawauliza kwanini walikuwa wanauza album yangu bila kuwaruhusu... yule mdose alinifokea kwa dharau na kunitishia kuita polisi ...” ( Uk 57) “Wadosi, wamelidhibiti game, wanafanya wanavyotaka wao kwa msaada wa wadau wachache wazalendo wasio na uchungu wa wasanii wa naoteseka akiwemo Ruge. Wakati sisi walikuwa wakitufuata Sinza, leo hii kila siku wasanii wanajazana kwenye mabenchi nje ya ofisi zao utadhani wagonjwa wakiwa kwenye foleni hopspitali. Kutokana na hali hiyo, hata kama msanii mmoja au kume watajaribu ‘kuwakomalia’ wapate haki zao, kuna wenzao zaidi ya mia watawapelekea kazo zao tena huku wakilia na kubembeleza hivyo kukwamisha juhudi za mtu mmoja mmoja katika kujikwamua” (Uk 84) “Kwanini tunasema ‘wadosi’ ni wezi? Tunawaita wezi kwa kuwa tunaamini wanafaidika na mfumo mbovu wa biashara ya muziki na pengine hata wanautetea na kuulinda mfumo huu uendelee kuwepo kwa kuwa una faida kwao....” (Uk 84} Wasanii wa muziki wanapata shida sana kuuza kazi zao. Mawakala, ambao wengi wao ni “wadosi” wanawanyanyasa na kuwaibia kazi zao. Wakati mwingine msanii wa muziki analazimika kuuza kazi yake yote kwa fedha kidogo, wakati aliyenunua anatengeneza fedha nyingi na wakati mwingine kwa kufyatua kanda na CD feki. Nne, Mheshimiwa Sugu, ameelezea vizuri manyanyaso wanayoyapata wasanii wa muziki kutoka kwa mapromota. Amewataja mapromota hao kwa majina yao na jinsi wanavyowanyanyasa wasanii wa muziki. Na hapa anaunganisha na vyombo vya habari kama vile Radio na TV. Vyombo hivi vinafanya kazi ya kuzitangaza kazi za wasanii kwa kuzirusha kwenye Radio na TV. Lakini kufuatana na maeleoz ya Mheshimiwa Sugu, kwenye kitabu chake ni kwamba bila kutoa rushwa kazi yako haiwezi kuingizwa kwenye kwenye Radio au TV. “Nakumbuka rushwa hii ilianzia kwenye redio na wasanii wakaona mkombozi wao alikuwa ni TV, hasa Channel 5, lakini mdudu wa rushwa alipoingia na huko ikawa balaa zaidi, mimi mwenyewe ni muathirika wa tatizo hili nakumbuka niliporudi kwenye game kwama 2004 nilipeleka vido yangu kwa ‘Moto chini’ pale, dada mmoja aliyekuwa anahusika akaipokea vizuri kabisa na kuisifu baada ya kuiangalia. Video ile ikapigwa silku chache na mara ikaingia kwenye top ten, ikaendelea kupanda kidogo naghafla itatolewa kwenye ite top ten na hata ikawa haipigwi kwenye vipindi vingine, nilishangaa mazingira iliyotolewa... Sikuamini alichosema! Aliniambia live kwenye simu kuwa nyimbo yangu ilitolewa kwenye chati na hata kuacha kupigwa kwa kuwa mimi sikuwa natoa ushirikiano na sikwenda ‘kuwaona’, yaani maana yake slikwenda kuwapelekea pesa” (Uk114). Tano, mwandishi amefanikiwa kutumia lugha ya vijiweni ili kufikisha ujumbe wake. Anasema ametokea mitaani kuingia mjengoni, ametumia lugha hiyo ya mitaani kuyaelezea maisha yake. Hata hivyo na kwa umri wake, yeye ni kizazi kipya. Kizazi hiki kina mambo yake, kina lugha yake. Kama niivyosema mwanzoni, wengine watafikiri ni kuivuruga lugha na si kiswaili sanifu. Lakini ndo hivyo jamii inapiga hatua na kupitia hatua mbali mbali. Kuna kazi wasomi kuhakikisha kiswahili sanifu, kinabaki na kutunzwa; lakini pia kuna haja ya kukubali lugha ya vijana. Na hatimaye ni pongezi kwa maelezo yake juu ya Ubunge wa Mbeya. Haikuwa kazi raihisi. Yalikuwa mapambano na kufuatana na falsafa yake ulikuwa ni “Ubishi”. Akafanikiwa kuingia Mjengoni, lakini kwa kuwa yeye anakumbuka alikotokea: kutoka mitaani hadi kuingia mjengoni, anaukumbuka Muziki na anaendelea kutumbuiza hadi leo hii VI. HITIMISHO. Ni wazi ningependa kuwashauri wasomaji wangu kukinunua kitabu hiki na kukisoma. Kwa vijana ambao wanakata tamaa na maisha, wajifunze kutoka kwa Sugu, kwamba maisha ni ubishi. Kwa kusoma kitabu cha Sugu, kuona jinsi alivyopambana na maisha na hatimaye kufanikiwa kuingia mjengoni, nao wafuate nyayo. Namshauri mheshimiwa Sugu, pindi akitaka kutoa toleo la pili la kitabu chake, atafute wahariri wazuri, warekebishe makosa ya hapa na pale, ili kitabu kiwe kizuri zaidi. Hata sasa kitabu chake si kibaya, ingawa kuna makosa madogo ya hapa na pale. Si makosa ya kukichafua kitabu, bali yakiondoka itakuwa vizuri zaidi. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment