UHAKIKI WA KITABU: KILIMO CHA PAMBA TANZANIA 1. Rekodi za Kibibliografia Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Kilimo Cha Pamba Tanzania na kimetungwa na Pius B. Ngeze. Mchapishaji a kitabu hiki ni Tanzania Educational Publishers LTD na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN) 978 9987 07 022 0. Kimechapishwa mwaka huu wa 2010 kikiwa na kurasa 85. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mim Padri Privatus Karugendo. II. UTANGULIZI Kitabu hiki kimekuja wakati muafaka. Leo hii wimbo wetu ni Kilimo kwanza. Hatuwezi kuanzisha mbio hizi za kilimo kwanza bila kuwa na ujuzi wa mazao yetu ya biashara. Kwa vile hatujafanikiwa kuwa na mabwana shamba wa kutosha kuenea nchi nzima, kitabu hiki kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa zao hili la pamba. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa pamba ilianza kuonekana kwa mara ya kwanza Tanganyika mwaka 1858 wakati Bwana John Speke alipokuwa katika safari yake ya kutoka Bagamoyo kwenda Ujiji, Kigoma. Lakini, Tanganyika (sasa Tanzania) ilianza kupanda pamba mnamo mwaka 1900 na ilianza kuiuza nje ya nchi mwaka 1920. Takwimu za uzalishaji zinaonyesha kuwa mwaka 1922 marobota 7,250 yalipatikana. Uzalishaji bora wa pamba ulianza Ukiriguru mwaka 1932 na mwaka 1947 ukaanza Ilonga. Kazi iliyofanywa na vituo hivi viwili vya Utafiti ni kubwa sana na ya kusifika. Bila kutumia matokeo yao ya utafiti, pamba isingekuwapo nchini, hasa kutokana na wadudu waharibifu ambao ni wengi na waharibifu kweli kweli. Pamoja na hayo, uzalishaji kwa kila mpamba na kwa eneo bado uko chini sana kutokana na wakulima kutofuata sawa sawa Kanuni kumi za kilimo bora cha pamba. Kanu hizo zimeelezwa katika kitabu hiki. Mwandishi wa kitabu hiki Mzee Pius Ngeze, ni mwanasiasa mkongwe aliyeamua kustaafu katika uwanja wa siasa na kujikita katika kuandika vitabu. Ameandika vitabu vingi na mwaka huu pekee, ametoa vitabu zaidi ya kumi na vitano. Yeye pia ni mtaalamu wa Kilimo, ndo maana ameamua kuwashirikisha watanzania wenzake elimu hii ili tuweze kwa nguvu zote kushiriki wimbo wetu wa Kilimo kwanza. Kitabu hiki kinazo sura saba. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na thamini yake. III. MUHTASARI WA KITABU Sura ya kwanza ya kitabu hiki inaongea juu ya mchango wa utafiti katika maendeleo ya kilimo cha pamba nchini Tanzania. Hapa ndipo tunaelezwa historia ya maendeleo ya uzalishaji bora wa pamba nchini ; utafiti wa wadudu waharibifu wa pamba; uzalishaji bora wa mbegu zinazostahimili mashambulizi ya wadudu; njia za kudhibiti wadudu wa pamba ambazo ni: Karantini, kung’oa na kuchoma miti ya pamba, usafi wa mazingira, muda wa kupanda na kuvuna na maumizi ya viuawadudu. Pia katika sura hii tunaelezwa juu ya utafiti juu ya kanuni za kilimo bora za Pamba ambazo ni: Utayarishaji wa shamba, wakati wa kupanda, idadi ya mimea katika kila shimo, kupalilia mashamba na kuhifadhi rutuba ya udongo. Nyongeza katika sura hii ni juu ya utafiti juu ya magonjwa ya pamba ambayo ni kama ifuatavyo: Bakteria, myauko fuzari; na Utafiti katika kanda ya mashariki kuhusu uzalishaji bora wa pamba, wadudu, magugu, mbolea na utafiti kuhusu ubora wa nyuzi za pamba. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba bila kutumia matokeo ya utafiti, pamba isingekuwapo nchini, hasa kutokana na wadudu waharibifu ambao ni wengi na waharibifu kweli kweli. Sura ya pili ninaongea juu ya hali ya uzalishaji wa pamba nchini; hali ya uzaishaji wa pamba tangu mwaka wa 1922 hai leo hii 2010. Pia tunaelezwa sababu za kushuka kwa uzalishaji wa pamba nchini na mbinu za kuendeleza zao la pamba ambazo ni pamoja na kurutubisha ardhi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa ardhi, utafiti wa pamba, ushauri wa huduma kwa wakulima na viwanda vya pamba na zana za kilimo. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba Zao la pamba hivi sasa hulimwa katika mikoa 13:Shinyanga,Mwanza, Kagera, Mara, Tabora, Kigoma, Singida, Mbeya, Morogoro, pwani, Tanga, Kilimanjaro na Arusha yenye jumla ya wilaya 41. Uzalishaji wa pamba unaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kufikia kilele cha marobota 693,809 mwaka 2005/6. Sababu kubwa zilizofanya ongezeko hilo ni kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ununuzi wa pamba, uzalishaji wa pamba kimashindano, upatikanaji wa ardhi mpya, upatikanaji wa zana za kilimo na pembejeo. Sura ya tatu inaongea juu ya mmea wenyewe wa pamba, umuhimu wake, mahitaji ya kimazingira, uotaji wa mbegu na kazi za virutubisho. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba mmea wa pamba huitwa mpamba. Pamba ni nyuzi zitokanazo ya vitumba vya mipamba. Kutokana na mazoea tu, neno “pamba” linaonekana kuchukuliwa kuwa na maana ya mimea na nyuzi zake. Pamba huwapatia wakulima fedha, huipatia nchi yetu fedha za kigeni, mafuta ya chakula, chakula cha mifugo, hutoa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu vya kutengeneza nguo na mafuta na hutoa ajira kwa watu wanaoajiriwa na viwanda hivyo na vinu vya kuchambulia pamba. Inapendekezwa kwamba pamba ilimwe kwenye udongo wenye kina kirefu, wenye rutuba na unaoshikilia unyevunyevu. Hustawi katika maeneo yanayopata milimita 500-750 za mvua kwa mwaka, mradi kiasi hicho kitawanywe vizuri wakati wa kipindi cha ukuaji. Na pia ustawi wake unahitaji mwinuko wa mita 90 hadi 1,200 kutoka usawa wa bahari. Mwanga wa jua ni muhimu sana kwa ukuaji wa mmea, hasa mwanzoni mwa kipindi cha ukuaji na wakati wa utoaji maua. Mpamba unahitaji virutubisho ambavyo ni : Nitrojeni, fosferasi, potasi, kalisi, magnesi, salfa, boroni, manganizi na Zinki. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba Mpamba ni mmea wenye manufaa makubwa katika uchumi wa Mtanzania. Hivyo ni lazima kuutunza na kuhakikisha unatoa matunda mengi na ya kutosha. Sura ya nne inaongea juu ya mahitaji, matumizi na dalili za ukosefu wa virutubisho; matumizi ya samadi, mbolea za viwandani, dalili za ukosefu wa virutubisho, muundo wa mbolea kuu za viwandani zinazotumika kustawisha pamba. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba katika hali fulani, ikiwa kanuni moja au zaidi zinazohusu kilimo bora cha pamba hazikufuatwa, mbolea za viwandani haziwezi kuongeza mavuno hata kidogo. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kanuni wakati wa maandalizi ya kilimo cha pamba na kilimo kwa ujumla. Sura ya tano inafundisha juu ya wadudu wa pamba. Imegawanywa kwenye sehemu kuu tatu: makundi ya wadudu waharibifu, Njia za Jumla za udhibiti na njia za kunyunyizia Viuawadudu. Tunafafanuliwa juu ya wadudu waharibifu ambao ni Nondo wa vitumba: Helioti, Eria, Plateda, Dipora; Wadudu wafyonzao: Kidusufi, Kalidia, Vijasidi, Vidukari, Kapsidi,Kiduru, Kasende, utitiri mwekundu, moshi wa chungwa, mdudu wa mbegu. Mchwa unaelezewa peke yake na pia kuna wadudu wengine wasio na madhara makubwa, wanaoshambuliwa miche, majani, maua na vitumba. Na njia za jumla za udhibiti: Kung’oa na kuchoma masalia ya mipamba, Usafi, Karantini, Kupanda na kuvuna mapema, Udhibiti wa kibiolojia na kutumia viuawadudu. Pia mwandishi anatuelezea njia za kunyuzia viuawadudu: Kwa kutumia ndege, kwa kutumia trekta na kwa kutumia mikono. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba bila kupambana na wadudu, ni vigumu kupata mavuno bora na mengi. Hivyo ni muhimu kuwafahamu na kufahamu njia za kuambana nao. Mwandishi ameweka picha za kila mdudu anayeshambulia mipamba. Sura ya sita imejikita juu ya magonjwa yanayoshambulia mipamba, ambayo ni: Bakabakteria, mnyauko fuzari, mkonomweusi, ukoga wa pamba, kuoza kwa vitumba, magonjwa ya miche, mnyoofundo na mdoajani. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kama ule wa sura iliyotangulia, bila kupambana na magonjwa yanayoshambulia mipamba, ni vigumu kupata mavuno mengi na pamba nzuri. Hivyo ni lazima kupamba na magonjwa haya na wakulima wote wafahamu magonjwa haya na dalili zake. Mwandishi ameweka picha ili kuonyesha magonjwa haya yanavyofanana na athari zake. Sura ya saba inaelezea kanuni kumi za kilimo bora cha pamba, ambazo ni: Kutayarisha ardhi ya shamba mapema, kutumia samadi na mbolea za viwandani, kupanda mbegu mapema, kupanda mbegu kwa mistari kwa kufuata nafasi maalumu, kupanda mbegu tatu kwenye shimo moja, kupunguza miche shambani, kudhibiti magugu na kwa wakati, kudhibiti wadudu na magonjwa, kuvuna mapema na kuichambua pamba vizuri na kung’oa na kuchoma masalia ya pamba. Ujumbe muhimu katika sura hii ni kwamba ili nchi iweze kunufaika zaidi kutokana na kilimo cha pamba, wakulima sharti wazalishe pamba bora nyingi zaidi kuliko miaka iliyopita. Baada ya utafiti wa kitaalamu wa miaka mingi, imeonekana kwamba wakulima wakitimiza Kanuni Kumi za Kilimo Bora cha Pamba na hali ya hewa ikiwa nzuri, basi wanaweza kuwa na uhakika wa kupata mazao mengi na bora. Ili mkulima aweze kufanikiwa vizuri katika kilimo cha pamba ni lazima atimize kanuni zote kumi. Huwezi kuacha moja na kutegemea kwamba utafaulu. Kila kanuni ni lazima itimizwe kwa wakati wake. Mwisho wa kitabu kabla ya marejeo, mwandishi anatuwekea tafsiri ya baadhi ya maneno: Dipora ni Red Bollworm Eria ni Spiny Bollworm Helioti ni Heliothis armigera Kapsidi ni Capsid Kabarili ni Carbaryl Kasende ni Stem Girdler Kiduru ni Heliopeltis Kilidia ni Bluu bug Kijasidi ni Jassids Kimwagaute ni Cersonspora gossyii Kiyogakombe ni Ascochyta gossypii Kidusufi ni Cotton stainers Plateda ni Pink Bollworm Paramoto ni Red spider mite. IV TATHIMINI YA KITABU Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliyoifanya Mwandishi Mzee Pius Ngeze. Ni lazima tuanze tathimini yetu kwa kumpongeza Mee Ngeze kwa jitihada anazozifanya kuielimisha jamii. Mzee huyu alipotangaza kuachana na siasa, kila mtu alishangaa ni kwa nini aliamua kufanya hivyo akiwa na nguvu na wakati wenzake wote bado ndio kumekucha. Kumbe alitaka apate nafasi ya kutumia ujuzi wake kuwaelimisha watanzania wenzake. Na huu basi ungekuwa mwito kwa wataalamu wetu wote wanapostaafu, wasikae tu kuifurahi pensheni yao, bali watumie lugha nyepesi kuandika vitabu katika fani zao. Mzee Ngeze, ameandika upande wa Kilimo, tuna wazee wengine wengi kwenye fani mbali mbali za Afya, Elimu, Ufundi n.k. Kitendo hiki cha kuandika vitabu ni cha kupongezwa na hii inaonyesha kwamba Mzee huyu ni kiongozi wa kweli. Tunavyofahamu Kiongozi, anaonyesha njia, anafundisha na kuelekeza. Kitabu cha Kilimo cha Pamba Tanzania, kinafundisha na kuelekeza. Badala ya viongozi wetu kupenda kuendelea kubaki madarakani, ni bora wakaiga mfano wa mzee Ngeze wa kukaa pembeni, kushauri na kuelekeza. Vitabu vingi vya kilimo vimeandikwa kwa lugha kingeleza na kwa mfumo wa kitaalamu sana, kiasi kwamba mtu wa kawaida hawezi kukifaidi. Mzee Ngeze, ametuandikia kwa lugha nyepesi ya Kiswahili na kwa mfumo wa kueleweka kwa kila mtu, hata wazee wasiofahamu kusoma, watoto wao wanaweza kuwasomea yaliyoandikwa. Katika taifa ambalo halijafanikiwa kuwasambaza maofisa kilimo katika kila kijiji, kitabu hiki ni msaada mkubwa. Mkulima anaweza kujisomea na kufuata aliyoyasoma na kufanikisha kilimo chake. Pia ubunifu wa mwandishi kutumia picha kuelezea magonjwa na wadudu wanaoshambulia mipamba ni wa kusifia. Uk. 35 kuna picha mbili zikionyesha ukosefu wa boroni na kwamba ua kushindwa kuchanua ni dalili tosha za ukosefu wa boroni, picha ya pili inaonyesha dalili za mapema za ukosefu wa magnesi katika mmea. Kwa kuangalia picha hizi, mkulima anaweza kuchukua hatua za mapema. Uk. 40 kuna picha ya Buu akijilisha kwenye kitumba. Buu anaweza kuwa kijanikibichi, manjano, hudhurungi au cheusi na naweza kutambuliwa kwa mstari mweupe chini kila upande. Uk.43 kuna picha ya Eria, inaonyesha Buu huyu mwenye nywele anavyojilisha kwenye shina la mpamba mchanga na kuua kichipukizi kinachokua, baadaye hujilisha kwenye vijipukizi vya nchani, maua na vitumba. Uk. 45 kuna picha ya Dipora na Uk. 48 kuna picha zinazoonyesha Kidusufi katika hatua mbalimbali za ukuaji wake. Pia zinaonyesha Kidusufi akifyonza kitumba. Uk. 49 kuna picha ya Kalidia. Uk. 52 kuna picha inayoonyesha Vijasidi kwenye pamba; kingo zake hugeuka kuwa za bizari, halafu nyekundu kisha hujikunja kwa ndani. Uk. 68, 69, 70, 71, kuna picha zikionyesha magonjwa mbali mbali ya pamba. Kitabu hiki kilivyoandikwa kinafaa kufundishia elimu ya kilimo katika shule za msingi na sekondari. Lakini pia kinafaa kwenye vyuo vyetu ambavyo mara nyingi masomo yanafundishwa kwa kingeleza, lakini maafisa kilimo wanakwenda kuwaelekeza wakulima kwa lugha ya Kiswahili. Hivyo kitabu hiki kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa maofisa wa kilimo. V. HITIMSHO. Kwa kuhitimisha, ningewashauri watanzania wakitafute kitabu hiki na kukinunua a kukisoma. Hasa ile mikoa inayolima zao la Pamba, ni muhimu sana kuwa na kitabu hiki. Lakini pia kwa vile sasa hivi tunaimba wimbo wa Kilimo kwanza, huku tukishindwa mbinu za kuendesha kilimo kwanza, naishauri serikali kununua vitabu vingi vya Kilimo cha Pamba Tanzania, na kuvisambaza nchi nzima. Hatuwezi kuimba Kilimo kwanza bila ya maandalizi. Na si kwamba kilimo kwanza kitakuja kama vile mvua za masika. Ni lazima watu wajitokeze kama alivyofanya Mzee Pius Ngeze, waandike vitabu, na wengine wafundishe, na wengine wabuni mbinu za kuenesha kilimo kwa njia za kiteknolojia. Kwa njia hii tunaweza kusonga mbele. Na, Padri Privatus Karugendo. Simu: 0754 633122 www.karugendo.com

0 comments:

Post a Comment