UCHAMBUZI WA KITABU: AZIMIO LA ARUSHA. 1. Rekodi za Kibibliografia. Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Azimio la Arusha na Siasa ya Tanu Juu ya Ujamaa na Kujitegemea. Kilitolewa na idara ya Habari ya TANU, Dar-es-Salaam 1967. Kilipigwa chapa na kiwanda cha Uchapishaji cha Taifa. Kijitabu hiki kina kurasa 40, na anayekihakiki hapa ni Mimi Padri Privatus Karugendo. 11. Utangulizi Tunakumbuka kifo cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa letu la Tanzania. Kila mwaka tumekuwa tukifanya hivi kwa heshima yake, tukiwa na imani kwamba Mwenyezi Mungu, anasikiliza sala na maombi yetu na hapana shaka kwamba atampatia nafasi nzuri miongoni mwa watakatifu wake. Kuna mengi ya kukumbuka juu ya Mwalimu; mafundisho yake, maandishi yake, uadilifu wake, utu wake, unyenyekevu na roho ya kusamehe na kuchukuliana. Na mwaka huu, ni wa uchaguzi mkuu. Hivyo ni bora kujikumbusha mawazo ya Mwalimu kupitia kwenye maandishi yake na hasa hoja yake nzito iliyojipenyeza kupitia kwenye kitabu hiki kidogo cha Azimio la Arusha, ambacho yeye alikifananisha kama msahafu au ndugu yake na msahafu, maana alisema daima alitembea na vitabu hivyo viwili; Biblia na Kijitabu hiki cha Azimio la Arusha. Kitabu hiki kimegawanyika katika sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza inaongea juu ya Imani ya TANU, Sehemu ya pili inaongea juu ya Siasa ya Ujamaa. Sehemu ya tatu inaongea juu ya siasa ya Kujitegemea. Sehemu ya nne inaongea juu ya uanachama na sehemu ya tano ndiyo inaongea juu ya Azimio la Arusha. Ni kitabu kidogo sana, mtu unaweza kukiweka mfumoni na kutembea nacho. Ni kidogo, lakini kimesheheni hekima, busara, dira na mwongozo wa kuelekea Mabadiliko ya kweli katika taifa letu la Tanzania. 111. Mazingira yanayokizunguka kitabu Baada ya Uhuru kulikuwa na changamoto nyingi kwa nchi changa za Afrika. Mapinduzi ya kila mara yalikuwa yakizikumba nchi hizi. Ubeberu ulikuwa ukikodolea macho Afrika, na wakoloni walitaka kuenendelea kuitawala Afrika kutokea mbali. Wakati huo kukiwa na pande mbili zinazopingana. Upande wa mabepari ukiongozwa na nchi za Ulaya Magharibi na Amerika na Ukomunisti ukiongozwa na Urusi na China. Tanzania kwa kuamua siasa ya ujamaa, ilijikuta inawekwa kwenye kapu la wakomunisti, ingawa msimamo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa wazi wa siasa za kutofungamana na upande wowote. Hata hivyo alijiweka wazi kupambana na Ubeberu na ukoloni mambo leo. Viongozi wa Afrika walikuwa na uchu wa mali, na kutaka kuishi maisha kama ya wakoloni. Walitaka mishahara mikubwa, walitaka kuwa na hisa kwenye makampuni na walitaka kufanya biashara. Hali hii iliogopesha. Kulikuwa na hatari ya viongozi vijana wa wakati huo kuliuza taifa letu kama walivyofanya jirani zetu wa Congo. Mwaimu Nyerere, aliona hatari ya kuruhusu viongozi kuiga maisha ya wakoloni waliofukuzwa. Alifikiri njia pekee ya kuwahakikisha Tanzania, inaendelea kwa pamoja kwa kuwainua watu wa chini ni kuanzisha mfumo wa kuongoza mapambano hayo. Azimio la Arusha lililenga kujenga na kusimika Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea katika Taifa letu. Ilikuwa njia ya pekee ya kuhakikisha tunabaki salama, kwa amani na utulivu. Azimio la Arusha, halikupata mafanikio makubwa, kwa vile halikuungwa mkono na watu wengi. Walio wengi walifanya kazi ya unafiki. Hawakufuata Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kutoka moyoni. Hivyo juhudi zote za Azimio la Arusha, za kutaifisha njia kuu zote za uchumi kuwa mikononi mwa Umma, kwa kuanzisha Mashirika ya Umma, zilishindwa vibaya sana na uchumi ulididimia. Bila mjadala wa Kitaifa Azimio la Arusha, lilikufa na kuzikwa kule Zanzibar. Kilichofuata hapo si Ubepari – bali Ubeberu wenye kunakshiwa na Utandawazi. Kilio cha leo baada ya kugundua njama za wenye uroho wa mali na uchu wa madaraka ni kwamba turudishe siasa ya Ujamaa na Kujitegemea! 1V. Muhtasari wa Kitabu. Sehemu ya kwanza ya kitabu hiki inaeleza Juu ya Imani na Madhumuni ya TANU. Imani zote ni muhimu, lakini kwa uzito wa uchambuzi huu ni bora tukataja ya (h) na (i) ambazo zinasema hivi; “ Kwamba ili kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakwenda sawa. Serikali lazima iwe na mamlaka kamili juu ya njia muhimu za kuuza uchumi; na Kwamba ni wajibu wa Serikali, ambayo ni watu wenyewe kuingilia kati kwa vitendo maisha ya uchumi ya Taifa ili kuhakikisha usitawi wa raia wote na kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine au kikundi kimoja kunyonya kikundi kingine na kuzuia limbikizo la utajiri kufikia kiasi ambacho hakipatani na siasa ya watu wote kuwa sawa” (uk 2). Na sehemu hii naungana na sehemu nyingine upande wa Madhumuni ya TANU, inayosema hivi: “ Kuona kwamba Serikali ya nchi yetu inasimamia barabara njia kuu za kuzalisha mali na inafuata siasa ambayo itarahisisha njia ya kumiliki kwa jumla mali za nchi yetu” (uk.4) Sehemu ya pili ya kitabu hiki inaelezea juu ya Siasa ya Ujamaa: Kwamba katika Siasa ya Ujamaa hakuna Unyonyaji; “ Nchi yenye Ujamaa kamili ni nchi ya wafanyakazi: Haina ubepari wala ukabaila. Haina tabaka mbele za watu: tabaka ya chini ya watu wanaoishi kwa kufanya kazi, na tabaka ya juu ya watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi...” (uk.5) Kwamba kwenye ujamaa njia kuu za uchumi ziko chini ya wakulima na wafanyakazi; “ Namna ya pekee ya kujenga na kudumisha ujamaa ni kuthibitisha kuwa njia kuu zote za uchumi wa nchi yetu zinatawaliwa na kumilikiwa na wakulima na wafanyakazi....” (uk.6) Kwamba kuna Demokrasia: “ Nchi haiwi ni ya Ujamaa kwa sababu tu njia zake kuu au zote za uchumi hutawaliwa au humilikiwa na Serikali. Sharti Serikali iwe inachaguliwa na kuongozwa na Wakulima na wafanyakazi wenyewe” ( Uk. 7) Kwamba Ujamaa ni Imani: “ Lakini ujamaa hauwezi kujijenga wenyewe. Kwani Ujamaa ni Imani. Hauna budi kujengwa na watu wanaoamini na kufuata kanuni zake.” (uk.8). Sehemu ya Tatu ya Kitabu hiki inaelezea juu ya Siasa ya Kujitegemea. Kwamba tunapigana vita na Mnyonge hapigani kwa fedha. Vita yenyewe ni ya kujikomboa maana: “ Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi; mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe tena, tusinyonywe tena na wala tusipuuzwe tena” (uk.9). Kwamba “ kujitawala ni kujitegemea. Kujitawala kwa kweli hakuwezekani ikiwa Taifa moja linategemea misaada na mikopo ya taifa jingine kwa maendeleo yake..” (uk 19). Kwamba maendeleo yataletwa na viwanda na Kilimo na ni lazima kumkazania mkulima wa vijijini. Na kwamba masharti ya maendeleo ni Juhudi na Maarifa. Hivyo ili tuendelee tunahitaji vitu vinne: - Ardhi na Kilimo - Wananchi - Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea( Siasa safi) na - Uongozi bora. Sehemu ya nne ya Kitabu hiki inaongea juu ya Ubora wa Chama na wanachama. Kwamba wakati wa kupigania uhuru ilikuwa lazima kuwa na wanachama wengi iwezekanavyo. Lakini baada ya uhuru la msingi ni ubora wa chama na wanachama. Ni lazima mwanachama apimwe kwa Imani ya chama, madhumuni, sheria na amri za chama. Na la msingi ni kukumbuka kwamba TANU ni chama cha wakulima na wafanyakazi. Sehemu ya Tano, ni juu ya Azimio la Arusha, ambayo imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inaongelea Viongozi na sehemu ya pili inaongea juu ya Serikali na vyombo vingine. Hapa ndipo kuna masharti ya kuwabana viongozi na vyombo vya serikali kufuata Siasa ya Ujamaa na kujitegemea. V. Tathmini ya Kitabu Kama alivyosema Marehemu Baba wa Taifa, kwamba daima alikisoma kijitabu hiki na kugundua kwamba hakukuwa na kosa lolote. Ndivyo msomaji makini mwenye uzalendo wa kweli atagundua baada ya kukisoma kitabu hiki cha Azimio la Arusha. Kilitungwa kwa umakini mkubwa na watu ambao walikuwa hawana uchu wa madaraka bali uchu wa maendeleo ya Taifa letu. Kwa kiasi kikubwa kitabu hiki ni muhtasari wa mafundisho yote ya Baba wa Taifa. Ni vision ambayo ingeweza kulivusha Taifa letu vizazi na vizazi. Kitabu hiki kinaonya juu ya misaada ya nje. Na kusema kweli sote tumeona hatari ya misaada ya nje. Hata wasomi wenye madigrii mengi, wanafungwa midomo na misaada ya nje. Hata wanasiasa machachari wanafungwa midomo na misaada ya nje. Inajionyesha wazi kwetu na majirani zetu kwamba Uhuru ni kujitegemea. Mtu usipojitegemea, una amriwa la kufanya kufikia hatua ya kukuchagulia hata lugha ya kutumia na wakati mwingine hata mavazi ya kuvaa. Utamaduni unawekwa pembeni kwa kisingizo cha ustaarabu wa kisasa. Bila kujitegemea uhuru unapungua. Kwa kutupilia mbali Siasa ya Ujamaa na kujitegemea, tumekaribisha Ubeberu uliofunikwa na utandawazi. Lugha ya sasa ni Utandawazi na malengo ya maendeleo ya Milenia. Yote ni ubeberu unaoendeshwa na fedha za wafadhili. Wao wanaamua la kufanya na la kuacha. Na daima wanafanya lile lenye manufaa na ya nchi zao. Wakitoa msaada wa Elimu, wanalenga elimu wanayotaka watoto wetu wapate, ili wasifahamu baadhi ya vitu, ili baadaye walete wataalamu kutoka kwao kujazia nafasi hizo ambazo watoto wetu hawawezi kujazia. Au wanataka watumie vitabu na vifaa vingine vya elimu vilivyotengenezwa kwenye nchi zao. Wakitoa msaada wa dawa, watahakikisha ni dawa zinazotengenezwa na viwanda vya kwao. Kufanya hivyo viwanda hivyo vinaendelea kuzalisha, na wafanyakazi wanapata kazi na mshahara. Hawawezi kutusaidia kwa lengo la kutusaidia, hata hivyo hakuna sababu ya kutusaidia maana Juzi walikuwa wakoloni wetu na leo hii kuna jema gani la wao kutusaidia? Kitabu hiki kidogo cha Azimio la Arusha ni msahafu wa Watanzania wazalendo wanaolipenda taifa lao. Ni mwongozo mzuri wa kumwezesha kila Mtanzania kusimama imara kulitetea Taifa lake na kuhakikisha Tanzania inasimama imara katika Jumuiya ya Kimataifa ikiwa na sera na siasa yake inayoeleweka na kuelezeka. VI. Hitimisho. Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma, hasa vijana wa kizazi hiki ambao hawakufanikiwa kuishi wakati wa Azimio la Arusha. Ni kitabu kinachoweza kuwapatia mwanga na dira ya Taifa letu. Ni kitabu kinachoweza kuwasaidia kusema hapana kwa Ubeberu na utandawizi. Ni kitabu kinachoonyesha jinsi tanzania tulivyokuwa na dira, ikapotelea Zanzibar. Wale walioliua na kulizika Azimio la Arusha bado wako hai, hivyo vijana wana nafasi nzuri ya kukisoma kitabu na kuwahoji watu hao na ikibidi wafikishwe mahakamani, maana walitelekeza Dira nzuri ya Taifa letu. Pia waulizwe, baada ya kulitelekeza Azimio la Arusha, walileta kitu gani badala yake? Kuomba na kuwapigia Wazungu magoti wakati tuna kila kitu katika Taifa letu? Kuwakaribisha “wawekezaji” wanaokuja na Bfriefcase na kuondoka makontaina? Au wananufaika na kutibiwa Ulaya na kuwasomesha watoto wao nje ya nchi? Wana lipi la kueleza juu ya kutupilia mbali Azimio la Arusha na kukumbatia Ubeberu? Lakini, kwa upande mwingine ninawashauri viongozi wetu, hasa wale wa CHAMA cha Mapinduzi, kilichotokana na TANU na ASP, kurejea tena kukisoma kitabu hiki ili kugundua pale walipopotea njia. Katika familia ya Kiafrika, baba mwenye nyumba kwenda kuomba chakula kwa jirani, ni aibu kubwa. Sisi viongozi wetu wanatembea vifua mbele kwamba tunapata misaada kutoka nje! Wanacheka na kushangilia kuomba, aibu imegeuka kuwa sifa. Kama si laana ni nini? Ni aibu kubwa na kumfedhehesha Baba wa taifa tunayemkumbuka kila Mwaka. Hata viongozi wa vyama vingine vya siasa wana wajibu wa kukisoma kitabu hiki ili watambue hitaji la watanzania. Kitabu hiki kitawasaidia kuwa na msimamo wa wazi. Wajue kwamba ni lazima kuchagua moja; Uhuru wa Taifa na Siasa ya Ujamaa na kujitegemea, au kuchagua Ubeberu na ukoloni mambo leo uliorembwa na maneno matamu ya Utandawazi. Ni vyema sote kukisoma kitabu hiki na kutambua kwamba Mabadiliko ya taifa leu yataletwa na : Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi Bora. Watu tunao, Ardhi ipo ( ingawa inatishiwa na mashirika na makampuni makubwa kutoka nje – ubeberu) tatizo letu ni siasa safi na Uongozi bora. Mungu, ailaze roho ya Baba wa Taifa, kiongozi wetu mwenye siasa safi na uongozi bora, aliye acha ombwe la uongozi nyuma yake, mahali pema peponi. Na, Padri Pivatus Karugendo. 0754 633122.

0 comments:

Post a Comment