UHAKIKI WA KITABU: MISINGI NA MAARIFA YA UTAFITI
1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA
Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni Misingi na Maarifa ya Utafiti na kimetungwa na Dkt Ladislaus Nshubemuki. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Dar es Salaam University Press LTD na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9976 60 4017. Kimechapishwa mwaka wa 2004 kikiwa na kurasa 202. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. UTANGULIZI.
Kitabu hiki kilitolewa mara ya kwanza mnamo mwaka 2004. Bahati mbaya kilikuwa na kasoro za hapa na pale za uchapishaji. Mwandishi, amezipitia kazoro hizo na kuwashauri wachapishaji wake kukirekebisha kitabu hiki. Marekebisho hayo yamekamilika.
Misingi na Maarifa ya Utafiti ni mchango unaofuata Istilahi za Elimumisitu (KAD Associates/TFC, 1999) zilizotayarishwa kwa kushirikiana na Profess H.J. Mwansoko na Profesa A.G. Mugasha. Hii ni katika azma ya kupanua matumizi ya Kiswahili katika taaluma na taamuli za ngazi na viwango mbalimbali. Wengi wetu hufikiri kuwa tafiti zenye uelekeo wa kilimo na tafiti nyingine zingezungukwa na ngome isiyopenyeka! Hatima yake ni matumizi madogo ya utafiti kwa kushiriki au kutafsiri. Kitabu hiki kinalenga kudhihirisha kuwa dhana hii si sahihi kwa wakati wote. Kazi hii itachochea matumizi ya utafiti katika shughuli zetu za kila siku jambo ambalo litachangia utendaji wa uhakika, na hatimaye kuchangia maendeleo ya haraka katika taifa letu.
Kitabu hiki kinazo sura saba, marejeo, Istilahi na nyongeza mbili. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na thamini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.
III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU.
Mwandishi wa kitabu hiki amejitahidi kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Kwanza, anajaribu kuelezea maana, umuhimu na namna ya kufanya utafiti.
“Inafahamika kuwa kabla ya utayarishaji wa sera yenye marefu na mapana, ipo haja ya kufanya utafiti au kutumia matokeo ya utafiti huo. Ikiwa sera hiyo inahusu kilimo, hapana budi kazi hiyo ijihusishe na mausala ya ustawi wa jamii”( Utangulizi xi).
“Utafiti ni udadisi, na kila binadamu wa kawaida anayo sifa hii. Tuendapo kwenye sehemu ya kuuzia pombe aghalabu tunaonjeshwa na wauzaji wengi kabla ya kufanya uamuzi kuhusu ni pombe ipi inunuliwe. Kadhalika, mama aendapo sokoni kununua mchele au maharage huchukua sampuli na kuzichunguza kwa makini kabla ya kuamua mchele upi ataununua. Hivyo katika maisha yetu ya kila siku tunafanya vitendo vyenye uelekeo wa utafiti ingawa baadhi ya vitendo hivyo hufanyika hivi hivi bila ya kusudi maalumu la kufanya utafiti. Hivyo, wafanyao utafiti siyo lazima wawe watu wenye akili nyingi. Lililo muhimu ni kuwa na msingi mzuri wa elimu katika mada inayofanyiwa utafiti, kujenga uzoefu, na kujizatiti….. utafiti ni jambo la lazima kwa maendeleo yetu kwani chochote tutumiacho sasa kinaweza kuongezwa ubora wake ili mradi kifanyiwe utafiti”(Utangulizi xi).
Pili, amejitahidi kuonyesha kwamba hata lugha yetu ya Kiswahili inaweza kumudu tafiti za kitaalamu, mfano tafiti za Elimumisitu na kilimo.
Kwa siku nyingi sasa tumekuwa na mjadala kama kweli kishwahili kinaimudu sayansi. Dkt Nshubemuki, amejitahidi kutumia maneno mengi yanayotokana na msamiati ambao umepitishwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA). Na ameweka tafsiri ya istilahi zote nyuma ya kitabu mara tu baada ya marejeo. Hivyo kitabu hiki ni kama kichocheo cha kuwazoeza watu matumizi ya istilahi za kisayansi.
Mfano maneno kama kiwanjatofali kwa kumaanisha “Block”, Lushabo kwa kumaanisha “Silt”, Nakilitendea kwa kumaanisha “Replications”, Saniijaribio kiwanjatofali nasibu kwa kumaanisha “Randomised block experimental design”, Saniijaribio mraba wa Kilatini kwa kumaanisha “Latin square design experiment”, Unamu kwa kumaanisha “Texture”, Utafiti menyu kwa kumaanisha “Pure Research”, Ziro isonasibu kwa kumaanisha “Non-arbitrary zero” yametumika na kuongeza changamoto ya Kiswahili kuimudu sayansi.
Fomyula na vifupisho abavyo ilibidi viwekwe kando ya maelezo vimeachwa katika lugha za kigeni. Mfano ukokotoaji wa eneo la duara , imeachwa ilivyo. Sababu kubwa ni kukwepa athari za kutafsiri fomyula na hali inaweza kuwa ngumu zaidi ikiwa tafisi ya fomyula katika maneno ya Kiswahili ni ndefu. Ufumbuzi wa tatizo hili unahitaji muda, majadiliano na makubaliano ya kitaalamu.
Ladislaus Nshubemuki, alizaliwa mwaka 1950. Alisomea elimumisitu katika Chuo Kikuu cha Makerere na alitunukiwa shahada ya B.Sc (Misitu) mnamo mwaka wa 1980. Mwaka 1990, alipata shahada ya uzamili (M.Sc- Misitu) kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam. Mwaka 1998 alipata shahada uzamifu (Kilimo na Misitu) kutoka Chuo Kikuu cha Joensuu, Finland. Ameandika zaidi ya mada 60 zihusuzo elimumisitu, mazingira, na ushauri wa kitaalam. Baada ya maelezo haya saa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.
IV. MUHTASARI WA KITABU
Muhtasari wa kitabu hiki unabebwa na misemo miwili anayoitoa mwandishi kwenye hitimisho ya kitabu chake. Msemo wa kwanza ni ule wa Shaaban Robert,usemao: “ Uchi wa Binadamu ni Kutojua Vitabu”. Pia msemo wa Kilatini usemao hivi: “ Bila ya elimu uhai ni alama ya ufu” ( Nam sina doctrina vita est quasi mortis imago).
Sura ya kwanza inaongelea juu ya Sifa za Mtafiti na Maandalizi ya Utafiti. Hapa tunaambiwa kwamba:
“Mtafiti ni mwindaji au mchunguzi wa data/takwimu na taarifa mbalimbali kuhusu mada anayofanyia utafiti. Taarifa hizo hufanyiwa tathimini kabla hajazikubali. Ili mtafiti aweze kuwa mwindaji na mtathimni bora inabidi awe na sifa na afuaate taratibu Fulani katika kazi yake…” (Uk 1).
Zinatajwa sifa za mtafiti ambazo ni kama saba. Baada ya sifa za mtafiti zinafuta taratibu Muhimu katika utafiti, taratibu hizi ziko kama kuminatatu. Baada ya taratibu inafuata uchaguzi wa suala la kufanyia utafiti:
“ Hili ni jambo la maana sana. Ni muhimu kwa mtafiti kujichagulia suala analotaka kufanyia utafiti. Kadhalika mtafiti anaweza kuletewa tatizo, anaweza kupata suala hilo kutoka kwenye taarifa mbalimbali, anaweza kupata mawazo kutoka kwenye maongezi ya watu, au kutoka kwenye makongamano mbalimbali…” (Uk 5).
Baada ya hapo, inafuata kutambua umuhimu wa Suala la kufanyiwa utafiti na utekelezaji maana ni mataifa machache ulimwenuni yenye zana za kutosha na za kuwawezesha watafiti wake kuchunguza kila jambo linalosisimua. Ukweli huo huwa bayana zaidi hasa kwa utafiti unaochukua muda mrefu kuleta matokeo. Hivyo, zipo hatua kadhaa ambazo mtafiti anatakiwa azifikirie kabla ya kuanza na wakati utafiti unapoendelea.
Sura ya pili, inaongelea juu ya Zana za utafiti. Hivi ni vyombo ambavyo mtafiti hutumia kufanyia kazi yake. Matumizi ya vyombo hivyo hutegemea ni wapi mtafiti anafanyia kazi. Katika sura hii tunaelezewa pia matumizi ya Maktaba na namna ya kuitumia maktaba.
Sura ya tatu inaongelea Usimamizi na Ukusanyaji wa Taarifa Mbalimbali. Hapa ndipo tunapoelezwa mbinu za utafiti, uchukuaji sampuli na ssifa zake, ufundi wa kuchukua sampuli, umuhimu wa sampuli na sifa za sampuli.
Pia, katika sura hii tunaelimishwa juu ya ukusanyaji wa takwimu. Zinatolewa mbinu mbali mbali za kukusanya takwimu. Ipo mifano mbali mbali na mwandishi anakumbusha:
“ Bwana mganga anaweza kutoa takwimu za kutisha kuhusu ugonjwa wa kipindupindu vinginevyo hasikilizwi! Hii siyo kumaanisha kuwa maofisa wa Kilimo na Afya ni walaghai. Jambo linalojitokeza ni kwamba kila mtaalam anataka kazi yake ithaminiwe na ikiwezekana ipewe umuhimu kuliko kazi nyigine” (Uk 59).
Fundisho kubwa la sura hii ni kuonyesha jinsi mtafiti anavyoweza kupata data kwa kutumia majaribio, karatasi ya masailiano, masailiano, nyaraka mbalimbali, maono na picha.
Sura ya nne, inaongelea uchukuaji wa vipimo. Mifano inatolewa kuhusu vipimo toka majaribio ya sayansi menyu na sayansi ya jamii. Kuna aina kuu nne za vipimo ambavyo hutumika katika sayansi za jamii: Kipimio uwiano, kipimio nafasi, kipimio kioneshacho taratibu za kufuatana na kipimio jina.
Sura ya tano, inafundisha uchambuzi wa takwimu: “Yapo maoni kadhaa kuhusu uchambuzi wa takwimu. Kundi la kwanza linashikilia kuwa uchambuzi lazima uwe umeelemea taaluma, yaani takwimu zinazojihusisha na kazi hiyo. Kundi hilo linaongezea kuwa mchambuzi lazima awe anajua kutumia kompyuta. Kundi hili linafikia hatua hata ya kudharau taarifa ambazo hazioneshi takwimu, au zenye takwimu rahisi rahisi. Kundi la pili linaafiki kuwa matumizi ya taaluma ya takwimu au matumizi ya kompyuta katika uchambuzi hasa ule uhusikanao na data nyingi kama zile za sensa ni muhimu. Lakini bado uchambuzi ambao hutumii fomyula (njia) ngumungumu au kompyuta unayo nafasi yake katika utafiti” (71).
Sura hii pia inafundisha mbinu za uchambuzi na upangaji wa takwimu zilizokusanywa katika utafiti. Wakati wa kuchambua na kupanga takwimu zilizokusanywa katika utafit, mtatifi hana budki kujiliza maswali yafuatayo: je, takwimu zinachunguza suala gani? Je, takwimu zinakidhi malengo ya utatiti? Kama malengo ya utafiti yamefikiwa, takwimu zitathibitisha vipi hali hiyo? Katika njia anazokuwa nazo mtafiti, ni ipi ielezayo kwa urahisi zaidi kipengele ambacho kinachotayarishiwa jedwali?
Pia katika sura hii tunapata somo juu ya baadhi ya vipimo vitumikavyo katika uchambuzi wa takwimu. Mfano kuna vipimo vinavyoonesha uelekeo wa kuja pamoja na uelekeo kati: Wastani,kati na modi. Aina zote hizi zimetolewa mifano katika kitabu. Mwandishi, anaendelea kufafanua juu ya vipimo vioneshavyo mtawanyiko/mweneo wa takwimu: Achano sanifu. Fomyula zinatolewa na kuwekewa maelezo.
Pia kuna maelezo juu ya vipimo vilinganishavyo takwimu: Maono yasiojozi na maono jozi. Mifano na fomyula, vimetolewa.
Jambo linalosisitizwa kwenye sura hii ni kuwa njia zote za uchambuzi wa takwimu hazikutajwa. Ila zile zinazoweza kuhitajika katika uchambuzi wa takwimu zinazohusika na maisha yetu ya kila siku zimegusiwa. Hata hivyo ikumbukwe kuwa uchambuzi wa takwimu ni taaluma ya aina yake hivyo bado upo umuhimu wa kuongezea juu ya yaliyogusiwa katika kitabu hiki.
Sura ya sita inafundisha namna ya uandikaji wa ripoti. Jambo linalosistizwa hapa ni kwamba kabla ya kuandika ripoti inabidi mtafiti ajiulize maswali yafuatayo:
- Je, utafiti nilioufanya unachunguza habari juu ya nini? Swali hilo likijibiwa mtafiti anatakiwa aendelee kujiuliza.
- Je, taarifa/uchunguzi uliofanyika unakidhi matakwa kwa mujibu wa mpango wa utafiti? Mtafiti inabii awe na jibu la ndiyo ili awe na uhakika wa jambo analotaka kulifanya. Pili inamsaidia kuwa na picha kamili ya kukamiisha kazi.
Katika sura hii tunaelezewa kwamba kuna ripoti za aina nyingi kwa mfano ripoti za kitaalamu, ripoti zinazohusu utoaji wa bidhaa, ripoti za maendeleo ya utekelezaji, ripoti zinazotathimini miradi na mada zenye uchambuzi wa kisayansi. Taratibu zinazotakiwa kufuatwa wakati wa kuandika mada za kisayansi zinatumika kuandika ripoti nyingine. Hivyo zinaelezwa taratibu na kutolewa mifano, pia inaonyweshwa tofauti kati ya ripoti na ripoti.
Sura ya saba inatoa mawaidha zaidi juu ya utafiti. Mfano uendeshaji wa shughu za utafiti, ushirikiano wa kitaifa na kimataifa katika utafiti, utayarishaji wa pendekezo la suala la kufanyiwa utafiti. Sura hii ndiyo yenye hitimisho:
“ Katika nchi zinazoendelea utafiti lazima ujihusishe kwanza na masuala ya msingi kwa maisha ya kila siku. Utaalamu mpya utokeapo, hatuna budi tuutumie. Hii ni kwa sababau mtafiti mwenye uzoefu mkubwa anajua mengi lakini wakati huohuo anafahamu kuwa hajui kila kitu, na hivyo yuko tayari na kwa wakati wote kupata uzoefu mpya, kwa sababu ni kutokana na uzoefu huu anafahamu kuwa yote ajuayo hayajafikia kikomo cha ubora; hivyo yuko tayari kutazama maoni yake upya, na hata kubadilishana kauli iwapo ni lazima, kwani mtafiti mwenye uzoefu lazima awe na uzoefu wa kupata uzoefu. Mtumiaji wa matokeo ya utafiti anatakiwa kuwa na msimamo huohuo” (Uk 153).
Sampuli tatu za mada za uchambuzi wa kisayansi zinakutwa mara tu baada ya istilahi zilizotumika kitabuni. Na mwisho kabisa ni nyongeza mbili. Nyongeza ya kwanza ni ya mifano ya mada za uchambuzi wa Kisayansi na nyongeza ya pili ni ile majedwali ya uenezaji.
V. TATHMINI YA KITABU
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Dkt Lasislaus Nshubemuki.
Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kimefanikiwa sana. Kama nilivyosema kwenye utangulizi kwamba, kitabu hiki kina lenga vitu viwili: Kufundisha utafiti na kuweka istilahi za Elimumisitu katika mazoezi. Kama anavyosema kwenye hitimisho : “ Unapomfunza mwanafunzi kuendesha gari, mpe usukani”. Na kweli, mwandishi anatoa usukani.
Pili, mwandishi amefanikiwa kuonyesha kwamba Kiswahili kinaiweza sayansi. Ingawa bado kuna matatizo ya hapa na pale, mfano kwenye fomyula na mengine machache, bado kwa kiasi kikubwa anaoneysha uwezo wa lugha yetu ya Kiswahili.
Tatu, kwa kutumia Istilahi za Elimumisitu, katika kuandika kitabu cha Utafiti, mwandishi amejipatia changamoto yeye mwenyewe na wenzake akina Profesa H.J.Mwansoko na Profesa A.G. Mugasha, BAKITA, TUKI na wengine wote wanaojishughulisha na istilahi za Kiswahili, kubainisha ugumu ulipo wakati wa kuunda maneno. Imejitokeza mara nyingi kwamba neno linaswahilishwa. Hii ni changamoto kubwa!
Nne, Istilahi na maelezo yake nyuma ya kitabu, inakifanya kitabu kiwe cha kuvutia. Kwa mtu ambaye amekuwa akitafuta maneno ya kisayansi na hesabu katika lugha ya Kiswahili, atavutiwa kukisoma kitabu hiki. Pia Istilahi hizi zinaweza kuzua mijadala na hatimaye kuleta ubora katika kuuna maneno ya kutumia katika lugha ya kisayansi.
Tano, Dkt Nshubemuki, anatuingiza katika tafakuri kubwa. Je, tunaweza kufupisha baahi ya maneno? Maana mengine yanakuwa marefu kiasi cha kumchanganya mtu. Mfano: Cyclical fluctuations= Mfululizo nyakati wa maandamano na mafuatano. Inaeleweka vizuri, lakini inakuwa ndefu sana. Au Measures of dispersion= Vipimo vioneshavyo mtawanyo, Measures of association= Vipimo vishirikishavyo takwimu, Least squares principle= Kanuni ya kima cha chini cha namba mraba,nk. Inawezekana kuunda maneno mafupi kwa maana ile ile. Hii ni changamoto kwetu sote. La muhimu ni kwamba inawezekana na wanafunzi wanaweza kuelewa zaidi kuliko kutumia lugha za kigeni.
Sita, kitabu kinatuonyesha kwamba bado kazi ipo. Kwani haiwezekani kupata neno jingine badala ya “fomyula”, “Fosforasi”, “Grafu” “Sitolojia”, “Bibliografia” “Ploti” nk. Haya yameswahilishwa. Lakini tukifikiri zaidi, tunaweza kupata maneno yenye kumaanisha kitu kilekile, lakini kwenye lugha ya Kiswahili au lugha za kibantu zinazotengeneza Kiswahili.
Saba,mwandishi kuelezea maana, umuhimu na namna ya kufanya utafiti kwa lugha ya kiswahili ametoa mchango mkubwa katika taifa letu. Watu walio wengi watatambua umuhimu wa utafiti na kufanya utafiti kabla ya kufanya maamuzi mbali mbali. Kwa vile hatufanyi utafii, utakuta watu wanaanzisha maduka matano ya madawa katika kijiji kimoja, au kijij kimoja kinakuwa na daladala nyingi kuliko wingi wa watu. Serikali inasema vijana waondeoke mjini na kwenda kulima vijijini, je kuna utafiti uliofanyika na kuonyesha jinsi vijana hawa watakavyoanza kilimo, watalima nini na mazao watakayoyalima yatauzwa wapi? Utafiti ni muhimu katika harakakati za kuleta maendeleo.
VI. HITIMISHO.
Kwa kuhitimisha, ningependekeza kitabu hiki kisomwe na kila mtanzania. Ukiondoa sehemu ambayo ina mahesabu na fomyula, kitabu hiki kinasomeka kirahisi na kinaeleweka. Lakini pia kitabu hiki kingeweza kutumika shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.
Kama nilivyotaja kwenye tathmini, mwandishi na wengine wanaojali lugha yetu ya Kiswahili kutumika kufundishia, wanachangamoto ya kutafuta istlahi za kutosha, na hatimaye kuondoa maneno kama “fomyula” na mengine yanayobeba lugha za kigeni.
Mwisho, kabisa ni pongezi nyingi kwa Dkt Ladislaus Nshubemuki, kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuandika kitabu hiki cha Misingi na Maarifa ya Utafiti. Kama kawaida yangu, ninawahimiza watanzania kukisoma kitabu hiki na kuanza kufanya utafiti katika nyanja mbali mbali.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
MHARIRI WA TANZANIA DAIMA.

0 comments:
Post a Comment