UKWELI UTATUWEKA HURU, UKWELI UTATUKOMBOA. Msema ukweli ni mpenzi wa Mungu, sote hata wale ambao hawana imani na dini za kigeni, wanamwamini Mungu. Tunaambiwa Mungu huyu ni mpenda ukweli na daima huwapatia waja wake uhuru kamili na ukombozi timilifu pale wanapoishi na kutembea kwenye ukweli. Watu wote wanaompenda Mungu na kumtumainia, ni lazima kusimama na kukemea uongo bila woga wowote ule. Tunaambiwa kwamba woga ni hatari hata kuliko risasi; woga ni adui mkubwa wa binadamu. Hivyo watu wa Mungu ni lazima waushinde woga, ni lazima watamani kuwa na uhuru wa kweli na ukombozi uliokamilika. Naandika makala hii kwa mwito huo wa kusimama na kuutetea ukweli. Naandika makala hii kuwakemea wale wote wanaopenda kukwepesha ukweli na kuruhusu uongo kutawala. Wakati duniani kote watu wanaulilia ukweli na kujitahidi kuupenda ukweli, sisi Tanzania tunafikiri tunaweza kupata uhuru kamili kwa kuendeleza uongo. Matukio mengi yanayotokea kwenye taifa letu, yanatawaliwa na uongo. Wakifa watu kumi, tunasema watatu, akipigwa mtu risasi tunasema ametupiwa kitu chenye ncha kali, tukitaka kuficha ukweli tunakimbilia mahakamani na kusema hakuna ruhusa ya kujadili suala lililo mahakamani. Mahakama badala ya kuwa chombo cha kulinda na kuutetea ukweli, kimegeuka kuwa kandamizi na kuwapokonya wadau uhuru wa kujadili mambo yanayogusa hisia kwenye jamii yetu ya Kitanzania. Tunasema Dr.Slaa, aliongoza vurugu kule kikijini Iringa wakati wa kufungua tawi la Chadema, wakati siku hiyo ya tukio Dr.Slaa, alibaki Iringa mjini wala hakwenda kijijini kwa kuzingatia zuio lililokuwa limewekwa na jeshi la polisi. Ukweli huu hautajwi na magazeti yote ya taifa letu na wala hakuna redio inayowafafanulia wananchi yale yaliyomsibu Amekufa Mwangosi, tukaeneza uongo kwamba alikufa kwenye vurugu cha CHADEMA. Polisi zaidi ya nane, walimvamia Mwangosi na kumpiga vibaya, sasa tunasema muuaji ni mmoja na ndiye amefikishwa mahakamani: Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Mashuhuda wa tukio hilo ni kwamba Mwangosi, alivamiwa na polisi, kupigwa hadi mauti baada ya vurugu. Watu walishasambaa, na Mwangosi alikuwa amebaki na baadhi ya waandishi wa habari wakiendelea kufanya kazi zao. Tunawashukuru wapiga picha, waliojitahidi kuchukua tukio zima la mauaji ya Mwangosi. Ni ushahidi mkubwa kwamba Mwangosi, alifikwa na mauti nje ya urugu; hakuna picha hata moja inayomwonyesha Mwangosi akiwa anapigwa katikati mwa kundi la wananchi. Anaonekana anapigwa yeye peke yake na kuzungukwa na polisi.Hakuna mwananchi anayeonekana kwenye picha hizo. Kwa mtu anayepata ujumbe kutoka kwenye picha atashangaa na kujiuliza maswali mengi: Kama polisi walikuwa wanatuliza vurugu za wananchi, mbona hakuna hata mwananchi yeyote anayeonekana kwenye tukio. Kwa maoni ya wale walioshuhudia(Majina yapo), ni kwamba tukio la kifo cha Mwangosi, ni magomvi kati ya polisi na Mwangosi na wala hayana uhusiano wowote na ufunguzi wa matawi ya Chadema. Kufuatana na tukio zima, ina maana hata kama si siku hiyo, ingekuwa siku nyingine, maana inaelekea polisi hawa walikuwa na chuki na Mwangosi. Suala la bahati mbaya halina nafasi hapa. Polisi walitumwa kijijini kusambaratisha wanachama wa Chadema waliokuwa wakifungua matawi yao. Hawakutumwa kumpiga mwandishi ambaye si mwanachama wa Chadema na ambaye hakuwa na silaha yoyote ile zaidi ya kamera. Hata kama polisi waliokuwa Iringa, walikuwa wageni kiasi cha kutomtambua Mwangosi kama mwandishi wa habari, kitendo cha kuwa na kamera mkononi, kilitosha kutoa taarifa kwamba huyo alikuwa mtu wa amani. Hivyo hapa mshitakiwa hawezi kuwa mmoja. Tumesikia kwenye vyombo vya habari kwamba mtu mmoja mwenye jina la Pasficus Cleophase amefikishwa mahakani na yeye amekubali kutenda kitendo cha kukatisha maisha ya Mwangosi bila kukusudia. Wale polisi wengine, walioongoza kipigo cha mwandishi mbona hawatajwi? Au ni danganya toto, ili kesho na keshokutwa tusikie kwamba Bwana Pasficus, yuko huru baada upande wa mashitaka kushindwa kuhakikisha pasi na makosa kwamba huyo ndo muuaji. Sote tunakumbuka kesi ya Zombe; ilichukua muda mrefu, lakini hatimaye Zombe alishinda kesi. Ingawa si kawaida maiti kupambana na mtu na ikashinda. Wakati mwingine kuna ushahidi wa kutosha lakini kwa sababu maiti hasungumzi tena, hawezi kuleta ushahidi na kutuhakikisha kwamba yeye, askari walikuwa na magomvi ya muda mrefu: Aliyekufa, amekufa, la msingi ni kukazania utawala wa kisheria na kwamba jambo kama hili halitokei tena kwa mwandishi yeyote ule Najua, hata tukifanya utafiti wa namna gani, si msaada wowote kwa Mwangosi, amekufa na kuzikwa. Maisha yake yamekatishwa na hayarudi kamwe. Watoto wake wamebaki wakiwa, na mke wake amebaki na mzigo mkubwa kuwalea watoto hawa. Lakini ili jambo hili lisitokee tena ni lazima tujiulize chanzo cha chuki kati ya polisi na mwandishi wa habari. Je, ni chuki na Mwangosi au ni chuki na waandishi wote? Je waandishi wataendelea kuwa salama? Je wataendelea kuandika kwa uhuru bila kuogopa yale yaliyomtokea Mwangosi? Na kama kuna chuki kati ya polisi na waandishi wa habari, chuki hii itamalizika vipi? Haiwezekani chuki hii kumalizika kwa kuutunza uongo na kuuficha ukweli. Chuki hii haiwezi kuisha kwa baadhi ya wahariri na waandishi kujipendekeza na kujikomba kwa viongoji wa juu kwenye jeshi la polisi. Kuna ulazima wa kufanya utafiti wa kina na kufichua yote yaliyofichika. Na swali jingine linaloweza kutusaidiasana ni je, siku hiyo ya mauaji ni watu wangapi walikuwa hawajashiriki sensa kiasi cha RPC wa Iringa kufikia hatua ya kutuma Jeshi la Polisi katika eneo hilo la tukio? Je kama Chadema wangelifanya mkutano wao wa ndani tatizo lilikuwa wapi? Yeyeyote Yule aliyetuma polisi kijijini ndiye chanzo kikubwa cha mauaji hayo yaliyotokea kinyama. Kama maagizo hayo yaliagizwa na wanasiasa, kuna ulazima wa kumfikisha mwanasiasa huyo mahakamani ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania analindwa na kuedelea kuulinda kuutetea UHAI. Ili utafiti wetu ufanikiwe, ni vyema kama wale polisi wote waliomvamia Mwangosi na kumpiga wawajibishwe, RPC wa Iringa awajibishwe, OCD wa Iringa awajibishwe na waziri wa Mambo ya ndani awajibishwe. Haya nayarudia, maana niishayasema kwenye makala iliyopita. Lakini kwa vile mpaka sasa hakuna hatua iliyochukuliwa hatua ni lazima niendelee kupiga kelele hadi masikio ya wakubwa yakisikie kilio hiki. Ni lazima tushirikiane kwa pamoja na kupaaza sauti zetu tukisema “Hapana” “ hapana”. Ni lazima tujenge mazingira ambayo viongozi watatambua kuwa wale waliochini yao wakifanya makosa, ni lazima viongozi kuwajibika. Kwa njia hii viongozi hawa watawasimamia wale waliochini yao kwa umakini mkubwa. Watabuni mfumo wa kuhakikisha kila mtu anafanya kazi kwa ufanisi. Tujenge utamaduni wa kuwajibika na kukumbushana kwamba Ukweli utatuweka huru na kutuletea ukombozi uliotukuka! Na, Padri Privatus Karuge. +255 754 633122 pkarugendo@yahoo.com

0 comments:

Post a Comment