UHAKIKI WA KITABU: MZIZI WA CHUKI
1. Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni Mzizi wa Chuki, Kimeandikwa na Novati
Rutenge Mchapishaji wa kitabu hiki ni Mwandishi mwenyewe na amekipatia namba
ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987- 467- 01 –6. Kitabu
kina kurasa 81 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri
Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Mwezi wa kwanza mwaka huu, Wanyambo wa Karagwe walikuwa na siku ya kuonyesha
utamaduni wao pale Nyumba ya Makumbusho. Mimi pia nilishiriki maonyesho hayo,
na rafiki yangu alinunulia kitabu cha Mzizi wa Chuki. Sina uhakika kama vitabu
hivi vilikuwa vinauzwa pale Nyumba ya Makumbusho au kitabu hiki alikinunua
sehemu nyingine na kuniletea. Kwa vile nimejenga utamaduni wa kusoma kila kitabu
kinachopita machoni mwangu, nilianza kukisoma kitabu hiki na kukimaliza ndani ya
siku moja!
Inawezekana kwamba hata mwandisi wa kitabu hiki alikuwa kwenye maonyesho ya
Wanyambo, maana naye ni mnyambo wa Karagwe. Bahati mbaya sifahamiani naye, hivyo
sikuweza kukutana naye. Nimefanya uchambuzi wa kitabu chake kuendeleza utamaduni
niliouanzisha wa uhakiki wa vitabu, kwa lengo la kujaribu kuwashawishi
watanzania kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu. Lakini pia nimefanya uchambuzi
wa kitabu hiki kuendeleza mchango wangu wa maonyesho ya siku ya wanyambo; Kitabu
chenyewe kimeandikwa na Mnyambo na kinazungumzia mazingira ya Karagwe.
Siku ya utamaduni wa Mnyambo, ilisaidia kutoa utata uliokuwa unaendelea siku
nyingi juu ya Kabila hili. Watu walio wengi walifikiri kwamba Wanyambo ni
wahaya. Kumbe ukweli ni kwama haya ni makabila mawili tofauti. Kila Kabila lina
mila na desturi zake na Kila kabila inajitegemea. Hata mwandishi wa kitabu hiki
anajaribu kuonyesha ukweli huu katika hadithi yake.
Kuna ukweli kwamba Karagwe, haijazalisha waandishi wengi wa vitabu. Ukiachia
mbali vitabu vya kitaaluma kama kile cha Profesa Katoke, cha Karagwe Kingdom, na
vile vya Profesa Josephat Rugemalila vya Kamusi ya Kinyambo na sarufi ya
kinyambo hakuna vitabu vingi vya hadithi vilivyoandikwa na Wanyambo. Hivyo
uhakiki wa kitabu hiki umelenga pia kuwachochea wanyambo kuandika vitabu juu ya
utamaduni wao, mila na desturi; na haya yanaweza kuelezewa vizuri katika vitabu
vya hadithi.
Kabla ya kufanya uhakiki wa kitabu hiki ningependa kuelezea mazingira
yanayokizunguka.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
Riwaya hii ya Mzizi wa Chuki, iliandikwa miaka mingi ya nyumba wakati mwandishi
akiwa kijana. Kwa bahati mbaya hakuweza kuichapisha kwa sababu wakati ule
uchapajji wa vitabu ulikuwa mgumu sana.
Riwaya imeandikwa enzi za Azimio la Arusha. Hivyo inafunua wazi migongano ya
kijamii na kisiasa katika enzi ambazo taifa hili lilikuwa limeamua kujenga
ujamaa. Ndwano ambaye ndiye mhusika mkuu, anawakilisha tabaka la watawala ambalo
baada ya kuaminiwa na kukabidhiwa madaraka, lilitumbukia katika ufisadi wa
kufuja fedha za umma na kuwaharibu watoto wa kike.
Wale wenye umri wa kutosha, watakumbuka tabia iliyokuwa imejengeka ya kuandaa
blanketi la viongozi wakati wakitembelea mikoani. Msichana mzuri aliandaliwa
kumliwaza kiongozi. Mtu aliyepingana na tabia hii ni Marehemu Sokoine,
aliyewakemea wale waliokuwa wakimwandalia blanketi.
Tena bado tuna viongozi ambao waliaminiwa na Mwalimu, ili waendeleze mapambano
ya kujenga Ujamaa katika taifa letu, lakini walikumbwa na kirusi cha tamaa ya
mali na kuubadilisha Ujamaa kuwa Ubepari uliopitiliza.
Mwandishi anadokeza kwamba ingawa mazingira ya riwaya yake ni ya kipindi
kilichopita, lakini yawezekana kuwa ufisadi unaopigiwa kelele sasa hivi ni
matunda ya mbegu iliyopandwa na kupaliliwa wakati huo.
Tumeshuhudia wenyewe jinsi wale waliokuwa wafuasi wa mwalimu, wakivaa kama
mwalimu, wakiongea kama mwalimu; sasa hivi wanavaa suti za Kizungu na kuongea
lugha tofauti na ya mwalimu.
Lakini pia hivi saa kuna vuguvugu la kutaka kurudisha Azimioa la Arusha. Wale
wanaolitamani, ni bora wakafahamu upande mwingine wa shilingi; kwamba hata
katika mfumo wa Ujamaa, ufisadi ulipenyeza hadi ukawa Mzizi wa chuki.
Mwandishi wa riwaya hii ni wakili wa kujitegemea, aliyezaliwa zaidi kidogo ya
nusu karne iliyopita huko Mabira, wilayani Karagwe katika mkoa wa Kagera.
Aliwahi kufundisha katika shule za sekondari za Karagwe (KARASECO) NA Kishoju
(Balimi), Muleba. Pia amewahi kufanya kazi kama wakili wa serikali na katibu wa
Shirika la Madini la Taifa.
Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.
IV. Muhtasari wa Kitabu
Riwaya, inaonyesha jinsi Ndwano ambaye ndiye mhusika mkuu, anavyoyatumia vibaya
madaraka yake. Fedha za umma, zinamchochea kuoa wanawake wengi na kuwachezea
watoto wa kike. Ndwano anakwenda mbali hadi kufanya mapenzi na msichana
aliyekuwa mchumba wa kijana wake.
“Ndwano aingiapo katika penzi jipya, watu wote hujua. Alipofika nyumbani siku
hiyo hakuna aliloona zuri. Wake zake wote walikuwa na makosa. Wanawake wote
hawakuwa na adabu…… Ngesho, mke wake alishajiweka tayari kupambana na mume wake
ili asimwoe Koku – mtoto wa kike aliyekuwa kipenzi cha mwanawe Magezi” Uk. 3
Itaendelea.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment