MAREHEMU LAURIAN KADINALI RUGAMBWA. Tarehe 6.10.2012, Mwili wa Marehemu Laurian Kadinali Rugambwa, utahamishwa kutoka Kashozi Bukoba, na kuzikwa rasimi kwenye kanisa la Jimbo Katoliki la Bukoba. Mwili huo ulizikwa Kashozi kwa muda mnamo mwaka 1997, kwa vile kanisa la jimbo lilikulinafanyiwa ukarabati mkubwa. Wakati wa Mazishi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba,Mhahsamu Askofu Nestory Timanywa, aliwaambia waumini na wote walioshiriki mazishi hayo kwamba Mwili wa Kadinali, utatunzwa hapo Kashozi kwa muda wa miaka 2, hadi hapo kanisa litakapokamilika. Ni wazi wakati wa mazishi ya sasa, Askofu Timanywa, atawaelezea waumini na waombolezaji ni kwa nini ukarabati wa kanisa la Bukoba, umechukua miaka minngi hivyo. Policarp Kadinali Pengo, kwenye mazishi ya muda, aliwaambia watu wa Bukoba ,kwamba siku ya mazishi rasimi ikifika, wasipomjulisha ili aje kumzika Rugambwa, atawashitaki! Inashagaza kwamba taarifa zinatujulisha kwamba Kadinali Pengo, hataweza kumzika Rugambwa. Eti yuko Roma, kwa kazi maalumu. Mungu, bariki hatawashitaki watu wa Bukoba, maana taarifa ya mazishi ameipata, ila ameshindwa kufika. Nani wa kulaumiwa? Mazishi haya ya pili yanawachanganya wengi. Wanajiuliza maana yake ni nini? Ni kwamba kabla ya kifo cha Kadinali Rugambwa, aliomba “Kwa unyenyekevu” kwamba akifa, azikwe Bukoba kwenye kanisa alilolijenga yeye na kulitolea “Mama”. Hayo ndo yalikuwa mapenzi yake. Na kawaida wosia wa mtu unaheshimiwa. Kuna watu wachache wasiokuwa na busara wanaopuuzia wosia. Kadinali Pengo, aliheshimu wosia wa Kadinali Rugambwa wa kuzikwa Bukoba, ndo maana hakuzikwa Dar-es-salaam, jimbo alilolingoza hadi anastaafu. Kuna mambo mengi ya kuandika juu ya Lauriani Kadinali Rugambwa, kuanzia yeye kuwa Kadinali wa kwanza mwafrika na mengine mengi. T atizo kubwa juu ya Kadinali, ni kwamba hakuandika vitabu. Hivyo ni vigumu kuelezea kwa nukuu yale aliyoyaamini na kuyasimamia. Huwezi kusema alipenda ujamaa au aliuchukia ujamaa, hakuna ushahidi wa kimaandishi. Hakuwa moto na wala hakuwa baridi! Wengine wanasema alikuwa mkimya kiasi cha kuvumilia mateso akubwa wakati wa siku zake za mwisho. Jama yake wa karibu, alihojiwa akilalamika kwamba hali ya maisha ya Kadinali Rugambwa, siku zake za mwisho yalikuw mabaya. Aliishi kwenye ufukara kiasi cha kuvaa nguo zilizochanika! Rugambwa, alikaa kimya. Hakulalamika. Labda tukipekuwa matukio wakati wa uongozi wake tunaweza tunaweza kumfahamu yeye alikuwa ni nani: 1. Kuwashughulikia mapadri wenye matatizo ndani ya jimbo lake. 2. Kuvumilia karama mbali mbali 3. Msimamo wake juu ya padre Nkwera. Kadinali Rugambwa, baada ya kuacha kuliongoza jimbo kuu la Dar-es-salaam, yalijitokeza matatizo makubwa. Wana maombi waliokuwa wanataka kukomunika wamepiga magoti, lilikuwa tatizo kubwa kana kwamba ndo lilikuwa linaanza, wakati hata Rugambwa, akiwa madarakani tatizo hilo lilikuwepo. Huduma ya kuponya ya Padri Nkwera, ilileta gumzo na hatua kali zilichukuliwa kwa wale wote waliomfuata padre huyu mweny karama ya uponyaji. Lakini pia matatizo makubwa ya padre yaliwekwa wazi: Kuanzia magomvi, kwenda kinyume na maadili hadi kufikia hatua ya padre kukamatwa akilawiti. Watu walianza kuwa na maswali mengi juu ya uongozi wa Kanisa Katoliki la Dar-es-salaam. Mbona “Ubaba” wa kionozi ulikuwa unaingia mitini? Mapadri wengi waliacha huduma na wanaendelea kukimbia! Tuaambiwa wakatiwa Rugambwa, kama padre angeenda kinyume na maadili, alisuhgulikiwa kimya kimya bila kuruhusu mambo hayo kuwekwa wazi. Mwenye makosa, alitafutiwa sehemu ya kukaa na kujirudi chini ya uangalizi wa watu wanaoaminika kuwa na maisha bora ya kiroho. Kadinali Rugambwa ,alionyesha moyo wa “kibaba” kwa mapdri wake. Daima alisema “ Mwenye kuhukumu si mimi, bali ni Mungu baba wa Mbinguni” Hata na walei wenye matatizo, aliwaita kwake na kujitahidi kumaliza matatizo yao kimya kimya kabla hayajasambaa na kuwakwaza wengine. Wengine, wanasema kwamba hata viongozi wa serikali, walipata msaanda mkubwa wa ndoa zao. Aliyafanya hayo bila kwenda kwenye vyombo vya habari; yeye alifanya kazi ya kuzigusa roho za watu. Hakupenda kabisa matendo haya yatangazwe, na kwa bahati mbaya wasaidizi wake hawakufikiri haraka kuyaandika matendo haya! Alimwachia Padri Nkwera, kuendelea na huduma yake, maana kama alivyoniambia siku moja kwamba “ Kama huduma ya Nkwera, imetoka kwa Mungu, itaendelea. Kama imetoka kwa shetani itakufa”. Na huu ndo ulikuwa msimamo wake kwa mambo mengine mengi ndani ya kanisa. Hakupoteza nguvu zake na kuonyesha kwamba yeye ndiye mwenye madaraka na mamlaka; aliacha yote yanayotoka kwa Mungu yaendele ya shetani yafe.

0 comments:

Post a Comment