UHAKIKI WA KITABU: JUMUIYA NDOGONDOGO ZA KIKIRISTO. 1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA. Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Jumuiya Ndogondogo za Kikristo: Changamoto kuelekea Ukomavu na kimetunga na Padri Stephano Kaombe, wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Ecoprint Ltd na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987-474-01-02. Kimechapishwa mwaka 2006 kikiwa na kurasa 196. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. UTANGULIZI Kitabu hiki kilichozinduliwa siku ya Jumapili ya tarehe 17, Agosti,2006, katika kituo cha Msimbazi jijini Dar-es-Salaam, ni kitabu kwa ajili ya Wakatoliki wa rika zote, na watu wote katika jamii, maana mwandishi anajadili maswali mbali mbali yanayohusu watanzania wote. Mfano anajadili uwezekano wa Mkristu kufunga ndoa na Mwisilamu na mahusiano ya dini mbali mbali na kugusa maisha ya kila siku ya Mtanzania.. Kitabu hiki kinaelezea hali halisi ya Jumuiya ndogondogo kuanzia zilizo hai, zilizo vuguvugu mpaka zinazodorora katika azima ya Wakristo kuwa chumvi ya ulimwengu. Kitabu hiki kimeandikwa katika mtindo unaofanana sana na ule aliotumia Mtakatifu Thomas Aquinas katika kitabu chake maarufu kwa jina la “ A Summary of Thology”.Kitabu hiki kinazo sura 3 na viambatanisho 7. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na thamini yake, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU. Tangu miaka ya 1970 Maaskofu Katoliki la AMECEA waliamua kwamba Jumuiya Ndogondogo ziwe ndiyo vitovu vya uenjilishaji ndani ya Kanisa. Baadhi ya maaskofu walijitosa kuanza zoezi hili na wengine walibaki kuangalia na kusikiliza wanayofanya wengine. Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, alijitosa kiasi kizima na kuanzisha Jumuiya ndogondogo katika jimbo lake la Rulenge. Jumuiya hizi zilivuka mipaka ya kusali tu na kuingia katia nyanja za maisha yote. Mwoleka, alilenga kukamilisha kile ambacho Padri Kaombe, ananukuu katika kitabu chake kutoka katika tamko la AMECEA 1979, juu ya jumuiya ndogondogo: Ni njia kwayo Kanisa linaletwa chini toka katika mfumo ambao karibu upo mtupu, wakufikirika, kwenda katika maisha ya kila siku, yanayowagusa waamini, furaha na majonzi ya watu wanapoishi kabisa, wanazaliwa, wanapenda, wanafanya urafiki, kazi, kulala, wanasherehekea, wanaomboleza na kufa. Ni njia kwayo watu wanawezeshwa kutambua fumbo la Kristo aliyeko katikati yao, anayeonekana kwao kwa njia ya sura ya jirani. Ni Jumuiya ambazo watu wanasaidiana katika kumtafuta kwao Mungu kwa pamoja, katika njia yao ya mateseko ya kufuata njia ya Kristu, ambayo katika hiyo msamaha, upendo na uaminifu vinawasilishwa katika kina cha maisha ya kila siku” ( Uk.4). Mbali na Jimbo la Rulenge, Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam nalo limekuwa mbioni kutekeleza mpango wa Jumuiya Ndogondogo, kufuatana na mfumo anaouelezea Padri kaombe, katika kitabu chake. Aidha mwaka jana Julai 15,2005 Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ilizindua kitabu kiitwacho “ Kompendia ya Mafundisho ya Kanisa Kuhusu Haki za Binadamu” pale Kurasini makao makuu ya ya TEC na kuweka mkakati wa kuyafanya mafundisho haya sehemu ya uenjilshaji katika ngazi zote za Parokia na katika Jumuiya ndogondogo Ni katika muktadha huu, Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam lilitangaza kuwa toka Sherehe ya Mt.Yosef Mei Mosi mwaka 2006 hadi sherehe hiyo tena mwaka 2007 kuwa ni mwaka wa Jumuiya Ndogondogo, lengo likiwa ni kutathmini ubora wake, udhaifu wake, na hatimaye kuamua namna ya kufanya maboresho stahili. Kwa ajili ya tathimini hii, Padri Kaombe aliamua kutumia Kipindi cha Zingatia katika Redio Tumaini ambapo waamini walialikwa kuuliza maswali na kutoa mapendekezo mintarafu uhai wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, wakifanya hivyo kwa njia ya meseji za simu. Kitabu hiki ni matokeo ya zoezi hili chini ya uratibu wa Padri Kaombe. Inaelekea, amekuwa mwaminifu kuyapokea maswali na mapendekezo ya wachangiaji na kutoa majibu kadri alivyoweza. Ameonyesha ujuzi wake wa hali ya juu katika ufahamu wake wa Jumuiya Ndogondogo, ujuzi wake katika theolojia, imani yake isiyoyumba na hasa moyo wake wa kuwasikiliza watu. Majibu yake yana mantiki na kuvutia. Inaonyesha wazi kwamba yeye ni msomi, ni padre, ni kijana na ni mtu anayeutambua ulimwengu wa leo. Ni mchungaji anayefaa sana katika ulimwengu wa leo wa utandawazi. Wakati huu anafanya Shahada ya Uzamili katika Taalimujamii (Sociology) kwenye Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Masomo haya hayamtengi na kazi zake za kiroho na majukumu mengine ndani ya Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam. Ameandika vitabu mbali mbali kikiwemo na kitabu juu ya falsafa kwa Kiswahili. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari. IV. MUHTASARI WA KITABU Sura ya kwanza inaongelea Mfumo wa Jumuiya Ndogondogo (Uk.2-29) na inayo majibu kwa maswali 17. Majibu haya yanafafanua maswali kuhusu maana ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo; tamko la uongozi wa Jimbo kwa waamini wasiohudhuria Jumuiya Ndogondogo; mwongozo wa Jumuiya Ndogondogo; faida za Jumuiya ndogondogo; sifa za viongozi wa Jumuiya hizi; na kadhalika. Ujumbe muhimu katika sura ya kwanza ni: Jumuiya Ndogondogo “ Ni familia ya Mungu inayosali na kubadilisha uzoefu wa imani na kusoma neno la Mungu na kulitafakari kwa pamoja na kujadili mambo mengine ya kijamii ya kiuchumi kulingana na mazingira yao” (Uk 3). Sura ya pili inaogelea Maisha ya Jumuiya Ndogondogo (Uk, 30-91) na inayo majibu kwa maswali 28. Majibu haya yanafafanua maswali kuhusu umuhimu wa mahudhurio ya baba, mama na watoto katika Jumuiya Ndogondogo; wajibu wa Jumuiya Ndogondogo kwa wagonjwa wa ukimwi; ufafanuzi kuhusu masomo yanayofaa kusomwa katika mikutano ya Jumuiya Ndogondogo; ushiriki wa wanajumuiya katika shughuli za vifo na mazishi; na kadhalika. Ujumbe muhimu katika sura hii ni: “kutojua maandiko matakatifu ni kutomjua Kristo” (Uk.56) kwani maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundisha ukweli, kuonya, kusahihisha makosa na kuwaongoza watu waishi maisha ya maadili.” (Uk.61). Sura ya tatu inaongelea Katekesi ya jumuiya Ndogondogo (Uk.92-162) na inayo majibu kwa maswali 36. Majibu haya yanafafanua maswali kuhusu nafasi ya msalaba wakati wa Ibada; umuhimu wa Sala ya Salamu Maria katika Jumuiya Ndogondogo; msimamo wa ki-Biblia kuhusu pombe; kuabudu sanamu; kutoa pepo na kuponya magonjwa kwa njia ya maombezi; nafasi ya maungamo kwa padre; maana ya sakramenti na visakrament; nafasi ya desturi katika Misa; na kadhalika. Mojawapo ya ujumbe wa kufurahisha katika sura hii ni kupitia swali hili: “ Je, katika nyumba yeu tunaweza kuweka msalaba chooni?” (Uk.122). Ni lazima kusoma kitabu hiki, ili upate jibu la swali hili. Jew ewe unaweka msalaba chooni? Baada ya sura ya tatu vinafuata viambatanisho saba ambavyo ni: Ibada ya wanajumuiya kwa wagonjwa; mwongozo wa kuadhimisha sakramenti mbalimbali; Nukuu ya Biblia katika kitabu cha Kutoka 18: 13-23; Ishara ya Umoja katika Adhimisho la Misa. Viambatanisho vingine ni Sala ya kuomba fadhila ya unyenyekevu; sala ya mwaka wa Jumuiya Ndogondogo; na hatimaye ni shairi kuhusu Jumuiya Ndogondogo za Kikristo likiwa na kibwagizo cha maneno: “ Wewe ni mwamini hai, au wewe ni goi goi?” ambapo maneno haya yanapishana na maneno “Wewe ni mwamini hai, au wewe ni hoi hoi” ubeti hadi ubeti. Kwa ufupi, shairi hili murua linawahimiza waamini kuchukua nafasi zetu katika kuitakatifuza nchi, na hasa nchi hii, kupitia ushiriki wetu katika Jumuiya ndogondogo! Nchi ikitakatifuka, inakuwa salama kwa kila mtu, awe Mkristu au asiwe Mkristu! Ndo maana kitabu hiki kinawafaa watu wote! V. Tathmini ya Kitabu Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Padre Stefano kaombe. Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana kutokana na mtindo alioutumia mwandishi. Ni mtindo wa maswali na majibu yenye kusheheni utani mwingi, na tena maswali yanayotokana na waamini wenyewe kwenye Jumuiya ndogondogo ambako ndiko walengwa wa kitabu hiki wanapatikana. Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake, yaani kubainisha na kisha kutoa majibu kamilifu kwa changamoto zinazowakabili waamini kuelekea ukomavu wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Tatu, mwandishi ambaye ni mtaalimujamii amefanikiwa, japo kwa njia ya mzunguko inayoambatana na ucheshi na utani mwingi, kufanya tathmini ya Jumuiya Ndogondogo kwa mtazamo wa kitaalimungu (teolojia) na pia kwa mtazamo wa kitaalimujamii(sosholojia). Katika hili lazima nimpongeze kwa sababu sayansi za jamii kama vile sosholojia, uchumi na zingine bado hazijapewa nafasi ya kutosha katika mchakato mzima wa uenjilishaji ndani ya Kanisa. Yeye ametoa mfano hai. Nne, mwandishi pia, bali na kujieleza kwa njia ya utani na vichekesho vingi, ameonyesha umahiri wake katika kujieleza kwa njia ya ushairi. Mashairi ni njia mojawapo kati ya njia muhimu za kufundishia kutokana na ukweli kwamba ni sanaa inayoruhusu wazo la msingi kurudiwa rudiwa mara kadhaa mpaka likashika mizizi akilini. Wazungu husema “repeation is the mother of learning”! Tano, mwandishi amefanikiwa kukifanya kitabu chake kiwe cha kuaminika kwa kutumia mbinu mbalimbali. Kwa mfano amefanikiwa kuthibitisha hoja zake kwa kunukuu mistari ya kutosha kutoka katika maandiko matakatifu(uk. 61, n.k.), maandiko ya mababa wa kanisa(uk. 56, n.k.) na wasomi maarufu katika elimu dunia(uk.4, n.k.). Na sita, mwandishi ameonyesha ubunifu mkubwa katika kuzindua kitabu chake! Aliwaalika watu maarufu kama vile Kardinali Pengo na Askofu Methodius Kilaini. Kardinali Pengo katika kutoa maoni yake juu ya kitabu hiki alionekana kukifagilia sana. Kwanza alisema kwamba katika utafiti wake kwa ajili ya shahada yake ya uzamivu alikuwa anatafiti juu ya Jumuiya Ndogondogo huko Jimboni Rulenge Kagera chini ya uongozi wa hayati Askofu Chrstopha Mwoleka. Aidha, Kardinali alisisitiza kwamba Askofu Mwoleka ndiye anapaswa kuitwa mwanzilishi wa Jumuiya ndogondogo hapa tanzania. Pia alifafanua kwamba Jumuiya Ndogondogo ni sawa na Basic Christian Communities huko Amerika Kusini ambako ni chimbuko la theolojia ya ukombozi. Kwa maneno haya hakuna mtu angeweza kushindwa kuona ubora wa kitabu kilichokuwa kinazinduliwa. Hata hivyo, kwa kuwa Jumuiya Ndogondogo ndicho kitovu kikuu cha uenjilishaji, na kwa kuwa mafundisho ya kanisa kuhusu haki za binadamu ni sehemu ya mchakato huo, kama ilivyotamkwa wakati wa kuzindua Kompendia ya Kanisa Katoliki Kuhusu haki za Binadamu mwaka jana, basi ni mawazo yangu kwamba kama kitabu hiki kingeeleza namna elimu ya haki za binadamu inavyoweza kupenyezwa kwenye “medulla oblongata” za waamini kupitia Jumuiya ndogondogo basi kingepata asilimia 101, badala ya asilimia 100 za sasa! VI. Hitimisho Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri wanajumuiya wakipate na kukisoma kitabu hiki ili waweze kufahamu sababu za msingi za mafanikio, mapungufu, na namna ya kufanya maboresho panapostahili. Lakini, kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya jambo moja zaidi katika machapisho mengine ya kitabu hiki katika siku za usoni. Waamini tutafaidika sana ikiwa ataeleza namna ambavyo yale mafundisho ya kanisa katoliki kuhusu haki za binadamu, kama yanavyopatikana katika Kompendia ya Kanisa Katoliki Kuhusu haki za Binadamu, yanavyoweza kupenyezwa na kufundishwa mpaka yakaeleweka kupitia Jumuiya Ndogondogo. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment