INDIA WANA KITU GANI AMBACHO SISI HATUNA? Nakumbuka miaka ya nyuma, viongozi wetu walikuwa wakipata matibabu yao nchi za ulaya. Hata baadhi ya watu wenye fedha zao walikwenda kutibiwa Ulaya. Ubaguzi wa rangi ulipoanguka kule Afrika ya kusini, safari za matibabu ya Ulaya zikapungua na kuelekea Afrika ya kusini. Tulianza kusikia sifa za hospitali nzuri za Afrika ya kusini na huduma za hali ya juu zilizokuwa zikitolewa kule Afrika ya kusini. Viongozi na baadhi ya watu wenye fedha zao walianza kuelekea Afrika ya kusini kupata matibabu. Serikali ilianzisha mfumo wa kuwatuma wagonjwa kutibiwa Afrika ya kusini. Siku za hivi karibuni mambo yamebadilika tena kuhusu matibabu nje ya nchi. Sasa viongozi na watu wenye fedha zao wanakwenda India kwa matibabu na serikali imeendelea na mfumo wake wakuwatuma watu India kutibiwa na hasa kwenye hospitali za Appolo.Ni vigumu kufahamu vigezo vinavyotumika serikari kufikia hatua ya kumpeleka mgonjwa kutibiwa India; hata hivyo leo hii kuliko kule nyuma idadi kubwa ya wagonjwa inakwenda kutibiwa India kwa kulipiwa na serikali. Tunasikia sifa za matibabu mazuri yanayopatikana India. Ugonjwa ukishindikana kwenye hospitali zetu hata na Hospitali kubwa ya Taifa Mubimbili, wagonjwa wanatumwa India. Na kusema ukweli kasi ya kwenda India ni kubwa zaidi ya ile ya Ulaya na Afrika ya kusini ya miaka iliyopita. Nimekuwa nikijiuliza swali, India wana kitu gani ambacho sisi hatuna? Hospitali ni nzuri? Wana wataalamu wazuri? Wana vifaa vya kisasa? Huduma ni nzuri? Au ni kitu gani wanacho sisi hatuna? Madaktari wao wanasoma vyuo gani ambavyo madaktari wetu hawezi kwenda kusoma? Vifaa vya kisasa wanavipata wapi ambako dhahabu yetu haiwezi kuvinunua? Tuna almasi, tuna Tanzanite, tuna mbuga za wanyama, tuna mazao ya biashara kama kahawa, pamba, korosho na mengine; tunaweza vipi kushindwa kununua vifaa vya kisasa kwenye hospitali zetu? Kama tunaweza kununua mashangingi ya mawaziri, makatibu wakuu, wakurungenzi na viongozi wengine kama wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, tunashindwa kununua vifaa vya kisasa vya hospitali zetu? Kama huduma nzuri ndo inazifanya hospitali za India kusifika, “Huduma” hiyo inanunuliwa wapi ili na sisi tukainunue? Jumatano ya tarehe 6.6.2012, nilipopanda ndege ya Qatar, kumpeleka mtoto wangu mchanga kwenye matibabu India, swali hili lilirudia tena na tena kwenye kichwa changu “ India wana kitu gani ambacho sisi hatuna?”. Roho yangu ilinisuta kusafiri mbali hivyo kwa matibabu ya mtoto. Kwa nini hakutibiwa na kupona ndani ya nchi yangu? Binafsi nina imani tuna madaktari wazuri sana, ila inashangaza inafika mahali wanaamua kuwatuma wagonjwa nje ya nchi. Nakumbuka kuwasikia madaktari wetu wakilalamika kwamba hawana vifaa vya kisasa. Kwa maneno mengine wangeweza kufanya vizuri zaidi kama wangekuwa na vifaa vizuri. Hata hivyo huduma nzuri ya matibabu inategemea tu vifaa vya kisasa au kuna zaidi ya hapo? Kama vile kujenga utamadui wa kujituma, kujenga utamaduni wa kupenda kazi, utamaduni wa kutanguliza kuyaokoa maisha maana maisha yakiondoka hayarudi tena; kutanguliza huduma kabla ya kutanguliza mshahara? Wakati ninatafuta msaada kutoka kwa ndugu, marafiki na jamaa zangu kuniwezesha kwenda India kwa matibabu ya mtoto wangu, rafiki mmoja kutoka Amerika aliyekubali kunichangia fedha nyingi baada ya kunisuta alisema “ Privatus, nina imani kuna watoto wengi Tanzania, wanakufa kwa kutopata matibabu… ningekuwa na uwezo ningesaidia wengi zaidi ya kumsaidia mtoto wako. Lakini mimi ni mmoja na nimetokea kumfahamu Privatus. Basi pokea msaada wangu na umpeleke mtoto kwenye matibabu..” Nikiwa kwenye ndege, maneno ya huyo rafiki yangu yalirudi tena kichwani mwangu. Mimi nimefanikiwa kumpeleka mtoto wangu kwenye matibabu na wengine je? Watoto wengi wanakufa kwa kutopata matibabu. Wakati mimi nampeleka mtoto wangu India, kuna watoto wanakufa kwa malaria na kwa ugonjwa wa kuharisha. Mwezi wa tano nilikuwa wilaya ya Nkasi, ambako kuna vijiji havina hata mawasiliano ya simu. Gari la wagonjwa liko umbali wa kilomita 90. Mgojwa anayehitaji huduma ya haraka anafia njiani akipelekwa hospitali. Niliwaona watoto wengi kule Nkasi, wenye ulemavu ambao ungeweza kurekebika; watoto ambao ulemavu wao usigewazuia kwenda shule kama wangekuwa sehemu yenye huduma nzuri. Bahati mbaya watoto hawa hawana uwezo wa kufika Namanyere kwenye hospitali ya wilaya,sembuse Chennai India! Ingawa safari ya kwenda India ilikuwa na lengo la kuyaokoa maisha ya mtoto wangu, kwa njia moja ama nyingine yalilenga pia kufanya uchunguzi wa : India wana kitu gani ambacho sisi hatuna? Nilitamani safari hii kwa siku nyingi; naipata wakati mgumu wa kuuguza mtoto, lakini kama ilivyo mpango wa Mungu, nimebarikiwa kwa njii hii ili niweze kupata jibu la swali ambalo limekuwa likinisumbua kwa siku nyingi. Tulitua uwanja wa Chennai India, saa kumi Alfajiri. Moja kwa moja tulipelekwa hospitali na matibabu ya mtoto yakaanza. Hakukuwa na kupumzika kwanza. Hatukujua ulikucha lini; watu hawa wanafanya kazi bila kuangalia hata na muda. Ndani ya masaa nanane , nilishaelezwa matatizo ya mtoto wangu. Nilishangazwa sana na utendaji kazi wa watu hawa. Mimi nilifikiri tungepokelewa na kupelekwa hotelini kwanza, ili tuoge na kupumzika na kesho yake ndo tuje hospitali. Kumbe kwa wahindi ni “Kazi kwanza” mengine ni baadaye. Ugonjwa ambao sikuelezwa nyumbani ndani ya miezi miwili, niielezwa hapa India, ndani ya masaa manane! Swali bado ni lile lile India wana kitu gani ambacho sisi hatuma? Nyumbani niliambiwa matatizo ya mtoto wangu yataisha jinsi mtoto anavyoendelea kukua. Sikupenda jibu hili maana sayansi daima inatoa jibu la Kwa nini? Madaktari wa India, wamesema vile vile kama walivyosema madaktari wa Tanzania, lakini baada ya kugundua tatizo ni nini! Wale wanaonipenda na kunijali, walipendekeza niende kwenye maombi. Wengine walipendekeza niende kwa TB Joshua kule Nigeria, ili mtoto aombewe na kuponyeshwa kimiujiza. Sikuwakatalia, ila nilitaka nijue mtoto ana matatizo gani. Sasa hivi hata nikienda kwenye maombi,nitakuwa ninajua ninaomba mujiza wa aina gani. Pamoja na furaha ya kufahamu kwa undani ugonjwa wa mtoto wangu, sikuacha kutafiti: India wana kitu gani ambacho sisi hatuna. Swali hili niliwatupia ndugu zetu kutoka Nigeria niliokutana nao hapa Chennai. Kumbe wanaokimbilia India, si watanzania peke yao.Kuna watu kutoka Nigeria, Oman na nchi nyingine. Kwa upande wa Afrika Nigeria inaongoza kiasi kila mtu mweusi anayonekana kwenye hospitali za India, anachukuliwa kuwa Mnageria! Kwa watu wa kawaida mitaani hapa Chennai, Tanzania yetu haijulikani! Kwa hospitali na hasa upande wa malipo, Tanzania inajulikana kwa kutuma watu wengi wanaolipiwa na serikali na sifa kubwa ni serikali yetu kutofuatilia malipo. Bili zote zinalipwa bila kuhoji. Ukisema unatoka Tanzania, unaulizwa kama unalipiwa na serikali. Jibu ni muhimu kwa chumba utakachopata na huduma; ingawa huduma zote ni sawa, lakini malipo yanatofautiana. Wale wanaotumwa na serikali hudma yao iko juu ukilinganisha na wale wanaojilipia. Mnageria kijana, aliyejitambulisha kuwa anafundisha chuo kikuu kule Nigeria, alilijibu swali langu: India wana kitu gani ambacho sisi hatuna kwa kujiamini: “… ndugu yangu, wahindi wanafanya kazi kwa kujituma, wanapenda kazi na wanafanya kazi ili kufikia malengo fulani. Wahindi ni tofauti na sisi waafrika ambao tunafanya kazi ili tupate mshahara”. Huyu kijana kutoka Nigeria, aliendelea kulijibu swali langu kwa kusema kwamba “ … ingawa hapa India kuna rushwa, lakini ni tofauti na kule kwetu Afrika; sisi tunadai rushwa kabla ya kazi, na wakati mwingine mtu anakula rushwa na kazi haifanyiki, lakini India, ikitokea mtu akaomba rushwa atafanya hivyo baada ya kufanya kazi. Kule kwetu daktari, atataka umpatie rushwa kabla ya kukutibu, lakini hapa India, daktari anaweza akataka “tip” baada ya kukutibu”. Kijana huyu aliendelea kunielimisha juu ya mafanikio ya India “…nafikiri India, wamewekeza kwenye Afya. Wamegunduga kwamba huwezi kulijenga taifa kama watu hawana afya njema. Ndo maana wanatumia fedha nyingi kununua vifaa vya matibabu vya kisasa. Wameamua kuwalipa madaktari mshahara mzuri ili kuwashawishi wasikimbilie nchi za nje”. Hili wazo la kuwekeza kwenye Afya, lilinikumbusha kauri mbiu ya “Kilimo kwanza”. Wakati sisi tunakazana na Kilimo kwanza, India wanakwenda mbele na “Afya kwanza”. Wakati sisi Kilimo kwanza umebaki wimbo wa kisiasa, hawa wenzetu “Afya kwanza” wameweka kwenye matendo. Ingawa lengo lao kubwa lilikuwa ni kuokoa maisha ya wahindi na kuhakikisha India ina watu wenye Afya nzuri, “Afya kwanza” kimwekuwa kitegauchumi kikubwa. Kwa vile wametengeneza hospitali nzuri na zenye huduma za uhakika, watu wanatoka nchi mbali mbali kuja kutibiwa India. Gharama za matibabu ziko juu, hivyo “Afya kwanza” inaingiza fedha nyingi za kigeni. Mwanzilishi wa Hospitali za Appolo, ambaye pia ni daktari anasema alianzisha Hospitali hizi baada ya yeye kushindwa kumsaidia jirani yake aliyekuwa anaumwa. Vifaa alivyokuwa navyo daktari huyu havikuwa na uwezo wa kuyaokoa maisha ya jirani yake. Msaada mkubwa ungepatikana nje ya nchi na labda Ulaya. Jirani wa daktari hakuwa na uwezo wa kusafiri kwenda Ulaya, hivyo alikufa kwa kushindwa kupata matibabu. Tukio hilo lilimsukuma daktari huyu kuanzisha hospitali nzuri. Anasema alifunga safari kuzunguka dunia nzima akiwatafuta madatari wahindi na kuwashawishi warudi nyumbani India kuokoa maisha ya watu. Aliweza kuwapata na kufungua hospitali. Leo hii Appolo wana zaidi ya hospitali 50 na nyingine imefunguliwa Dar-es-salaam Tanzania. Afrika ina madaktari wengi na wazuri, wanafanya kazi nje. Hawa wakishawishiwa kurudi, na serikali za nchi za Afrika zikakubali kuwekeza kwenye Afya, tunaweza kuwa na hospitali nzuri kama za hapa India. Tanzania, tuna madaktari wazuri ambao wametumkia Botswana, Namibia, Amerika na Ulaya. Akijitokeza mtu akawakusanya na kuishawishi serikali yetu kuwekeza kwenye Afya na kuanzisha kampeni ya “Afya kwanza”, ni imani yangu kwamba tunaweza kuwa na hospitali nzuri kiasi cha kuwashawishi watu kutoka nchi nyingine kuja na kutibiwa kwetu. Nafikri India hawana kitu chochote ambacho sisi hatuna! Tumeshindwa kuwekeza kwenye elimu, tumeshindwa kuwekeza kwenye viwanda, tumeshindwa kuwekeza kwenye teknolojia, tumeshindwa kuwekeza kwenye kilimo, basi tuwekeze kwenye Afya, maana Mtu ni Afya. Na, Padri Privatus Karugendo. +255 754 6331 22. www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment