UHAKIKI WA KITABU: FRESHI NA MAISHA 1-4
I. Rekodi za Kibibliografia
Jina la vitabu vinavyohakikiwa hapa ni Freshi na
Maisha, kitabu cha kwanza hadi cha nne na vimetungwa
na Elieshi Lema. Mchapishaji wa vitabu hivi ni E&D
Limited na amevipatia namba zifuatazo katika sekwensia
ya vitabu duniani (ISBN): Freshi ya Maisha 1,
9987-622-64-x, Freshi na Maisha2, 9987-622-65-8,
Freshi na Maisha 3,9987-622-66-6,Freshi na Maisha 4,
9987-622-67-4.Vitabu vyote vinne vimechapwa mwaka wa
2005.Kitabu cha kwanza kina kurasa 34, Kitabu cha pili
kina kurasa 37, Kitabu cha tatu kina kurasa 52 na
kitabu cha nne kina kurasa 64.Na anayevihakiki sasa
hivi ni Padre Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Vitabu hivi vilivyoithinishwa na EMAC tarehe 10 mwezi
wa 5 mwaka 2005 kuwa vitabu vya Ziada kwa ajili ya
Darasa la Tano na la Saba katika shule za msingi
nchini Tanzania, vimeandikwa kwa aina yake.Kila kitabu
kina jina lilelile la Freshi na Maisha,lakini ujumbe
ni tofauti lakini ulioungana katika mwendelezo.
Wahusika ni wale wale. Kitabu cha kwanza kinabeba
ujumbe wa “Jipende”: “ Maisha anaishi katika familia
yenye upendo na amani, ana bidii ya kazi, nyumbani na
shuleni. Maisha ameanza kupata dalili za kukua.
Changamoto mpya zinamkabili. Anakutana na Freshi
anayekuwa rafiki yake. Freshi anamfunulia Maisha
uwanja wa maarifa ya stadi za maisha kuhusu
kujipenda”.
Kitabu cha pili kinabeba ujumbe wa “Jilinde”: “ Freshi
ameendelea kuwa rafiki mkuu wa Maisha.Katika kitabu
hiki Freshi anamwezesha Maisha kuona jinsi mwili wa
binadamu ulivyo wa kipekee, na jinsi ambavyo ni wajibu
wetu kuulinda dhidi yamagonjwa yote, na hasa UKIMWI.”
Kitabu cha tatu kinabeba ujumbe wa “Jijue”: “Mojawapo
ya stadi kuu za maisha ni kufahamu jinsi ya kutumia
akili yako kunufaisha maisha yako, mahali popote
ulipo.Uwe mtendaji,siyo mtedewa, ili ujielewe zaidi,
ujiamini zaidi, ufanye mambo makubwa na udhibiti
mwelekeo wa maisha yako”
Kitabu cha nne kinabeba ujumbe wa “Jithamini”: “
Maisha amefika Darasa la Saba. Amekua kimwili na akili
imepevuka kiasi. Ameanza kujithamini na kutambua
mazingira tofauti yanayomzunguka pamoja na changamoto
zake. Maisha amegundua kwamba wazazi ni wazito katika
kuongea masuala ya ngono na vijana wao. Hali hii
imewaweka vijana njia panda, huku jamii ikiwa
inajiundia ngao ya ukimya kuhusu masuala nyeti kama
haya”.
Vitabu vyote vimegawanywa kwenye sura fupi fupi
zikifuatwa na maswali ya majadiliano na picha mbali
mbali zinazosaidia kufikisha ujumbe. Kitabu cha kwanza
kina sura Saba fupi, kitabu cha pili na cha tatu vina
sura nane ambazo ni vupi pia na kitabu cha nne kina
sura kuminamoja. Katika aya zifuatazo nitatoa
muhtasari na tathmini yake, lakini baada ya kudokeza
mazingira yanayovizunguka vitabu hivi.
III. Mazingira yanayovizunguka vitabu hivi.
UKIMWI ni janga la kitaifa. Taifa letu lina mikakati
mbali mbali ya kupambana na ugonjwa huu. Wataalam
wanakubaliana kwamba kwa kiasi kikubwa ugonjwa huu
unaenea kupitia tendo la ngono. Tendo hili linapendwa
kwa wingi, lakini kilamtu anapenda alifanye katika
uficho. Hakuna aliyetayari kuliongelea kwa uwazi.
Wazazi hawataki kuliongea na watoto wao, ingawa kuna
ushahidi wa kutosha kwamba vijana hadi watoto wadogo
wa miaka 10 wanatenda tendo hili. Nyakati tulizomo,
maadili yameporomoka, ngono kimekuwa kitu cha kawaida.
Mbaya zaidi vijana wetu wameachwa kuogelea bila
mwongozo wa maisha yao. Wazazi wanaogopa kuongea na
kujadiliana na watoto wao juu ya mahusiano, juu ya
mabadiliko katia miili yao, juu ya kupenda na kupendwa
na hasa juu ya kujikinga na ugonjwa huu hatari.
Kama anavyosema mwandishi: “ Lakini kwa sababu ya
mabadiliko ya jamii kiuchumi na kisiasa, pamoja na
mwingiliano wa hali ya juu wa tamaduni na amali za
jamii tofauti, mifumo ya jadi yaliyoongoza mahusiano
katika jamii yamefifia kabisa. Hivyo, katika muda
mwingi, vijana wanajilea wenyewe. Vijiwe vyao vimekuwa
taasisi. Wanajijengea amali zinazoongoza matendo yao
katika mahusiano ya kila siku. Wanabuni lugha yao ya
kujieleza katika jamii iliyojaa utenganisho. Katika
kujilea huko,vijana wengine wanajiona wajanja kwa
sababu ya uzoefu uliojengeka katika kufanya majaribio,
hata kama ni uzoefu potofu. Wanaokuwa na ushawishi
mkubwa na wanawarubuni wenzao kirahisi” Freshi ya
Maisha 4, uk 31-32.
Serikali nayo imeshindwa kuwa na mfumo wa wazi wa
kufundisha maadili na kuwasaidia vijana kujitambua na
kujithamini. Mashirika ya kidini pia yameshindwa.
Hatuoni mfumo wao kuhusu malezi ya vijana na swala
zima la maadili na kujingina na UKIMWI.
Mwandishi wa vitabu vya Freshi na Maisha, aliandika
kitabu cha hadithi ya “Parched Earth”. Kitabu hiki
kina mafundisho juu ya vijana kujitambua, kuwatambua
wengine na kwa pamoja kushirikiana kujenga mahusiano
yaliyo bora kwa lengo la kulinda uhai na hasa
kupambana na ugonjwa wa UKIMWI. Baada ya kukisoma
kitabu hikili, nilimshauri mwandishi atunge vitabu kwa
lugha ya kiswahili, ili viwe msaada wa kuwafundisha
watoto wetu namna ya kujilinda, kujipenda na
kujithamini. Jibu la mwandishi ni zawadi ya vitabu
vinne, vya Freshi na Maisha, ninavyovifanyia uhakiki
siku ya leo. Wakati ninampatia ushauri, kumbe yeye
alishaviandika na vinatumika kwenye shule za msingi!
Huu ni mchango mkubwa na wa kuingwa.
Kabla ya kuviandika vitabu hivi mwandishi alifanya
utafiti wa akina. Alifanya majadiliano nakuongea
nawatu mbali mbali,pia alichimbua vitabu vingi.Hapa
kuna baadhi ya vitabu alivyovitumia wakati akiandaa
Freshi ya Maisha: Choosing Good Health 5&6,Scott,
Forestman& Co.,1983; Soul City: Living Positively with
HIV and AIDS; Family Medical Encyclopedia, An
Illustrated Guide, Hamlyn, 1983; Prescription for
Nutritional Hearing, Avery Publishing Group,1997; All
About the Human Body, Random House,1958.
Ingawa mwandishi ametumia vitabu mbali mbali wakati
akiaandaa Freshi na Maisha,na kufanya majadiliano na
watu wengi, ubunifu wote ni wake na mapungufu yote
yanayojitokeza kwenye vitabu hivi ni mzigo wake
mwenyewe!
IV. Muhtasari wa vitabu
Kitabu cha kwanza; Freshi na Maisha 1, kina ujumbe wa
“Jipende”. Kitabu hiki ndicho kinachofungua safari ya
maisha ya msichana Maisha, anayeishi katika familia
yenye upendo na amani, ana bidii ya kazi nyumbani na
shuleni. Binti huyu ameanza kupata dalili za kukua.
Changamoto mpya zinamkabili.
Maisha, anaanza kutafakari juu ya maisha yake: “Hivi
kukua maanake nini?”, “ Hivi, watu hukua mwili tu, au
sehemu nyingine nazo hubadilika?” (Uk 2).
Wakati Maisha, akiwa amezama kwenye tafakuri juu ya
maisha yake, anakutana na rafiki yake. Huyu rafiki
jina lake ni Freshi. Huyu Freshi, anajitokeza kwa
namna ya miujiza. Anajitokeza katika umbo la jiwe.
Huyu ni rafiki ambaye ni mshauri wa kiroho. Watu
wengine wanampatia jina la kipaji fiche ndani mwa kila
binadamu. Kwenye mazingira Fulani, huyu anaweza kuitwa
malaika mlinzi au roho mtakatifu. Rafiki huyu ni
silika iliyomo ndani mwa kila binadamu yenye nguvu na
ufahamu isiyohitaji kufundishwa. Huyo ndiye Freshi,
rafiki wa maisha, anayemwongoza kujipenda, kujilinda,
kujijua na kujithamini.
Freshi, anamfunulia Maisha, ukweli wa maarifa kwamba
kujipenda ni ufunguo wa safari ndefu ya kila kijana
kuelekea kujilinda, kujijua na kujithamini. Kwamba
kujipenda kunaanza na mtu kuangalia usafi wa mwili
wake, usafi wa mazingira yake na kutambua kwamba mwili
ni muhimu na maalumu, nivyo ni lazima kuulinda dhidi
ya magonjwa.
Maisha, anasikiliza ushauri wa Freshi.Anakuwa msafi
yeye mwenyewe, anatunza usafi nyumbani na sehemu
anakofanyia biashara mama yake. Shuleni anakuwa mfano
wa kuigwa katika usafi.
Kitabu kina maswali mengi ya majadiliano. Kila baada
ya sura kuna maswali zaidi ya matatu. Mfano wa maswali
ni kama: Taja mabadiliko matatu ambayo yanaonesha
kwamba msichana au mvulana amepevuka. Halafu jadili na
rafiki yako: je, kupevuka maana yake ni nini?, Mweleze
rafiki yako, kujipenda maana yake ni nini? Kwa nini
Freshi alimpa Maisha uwezo wa kugeuza takataka na
uchafu kuwa kitisho? Taja madhara matatu unayoyajua
yanayotokana na mazingira machafu.
Kitabu cha pili, Freshi na Maisha 2, kina ujumbe wa
“Jilinde”. Freshi, anaendelea kumpatia Maisha,
maarifa. Maisha anatambua kwamba mwili wa binadamu ni
wa kipekee na kwamba ni wajibu wa kila binadamu
kuulinda mwili dhidi ya magonjwa, na hasa UKIMWI.
“Lakini kwa kifupi, mwili wako ni kama mashine. Sehemu
zake tofauti hufanya kazi kwa pamoja na kwa
kutegemeana. Lakini mwili wako ni mashine hai, yenye
akili asili ya kupanga, kuratibu, kutathmini na
kujilinda” Freshi na Maisha 2 uk 23.
Kitabu kinaelezea kwa lugha nyepesi jinsi mwili wa
binadamu unavyofanya kazi: Mfumo wa mifupa na viungo,
mfumo wa misuli, mfumo wa mzunguko wa damu na hewa,
mfumo wa kusaga chakula, mvumo wa neva, mfumo
unaoshughulikia ulinzi wa mwili na mfumo wa hisia.
Kitabu hiki pia kina maswali ya majadiliano kila baada
ya sura.
Kitabu cha tatu, Freshi na Maisha 3, kina ujumbe wa
“Jijue”. Kitabu hiki kinaelezea kwamba mojawapo ya
stadi kuu za maisha ni kufahamu jinsi ya kutumia akili
yako kunufaisha maisha yako, mahali popote ulipo.
Yaani mtu awe mtendaji, siyo mtendewa ili mtu ajielewe
zaidi, ajiamini zaidi, afanye mambo makubwa na awe na
udhibiti wa mwelekeo wa maisha yake.
“ Kujijua kunaanza na nafsi yako. Unajichunguza wewe
mwemyewe ulivyo, kwa kujiona jinsi unavyoishi na
familia yako, rafiki zako na watu kwa ujumla. Yale
utakayopata kutoka kwa wengine, yanakuongezea maarifa
juu yako, au yanakupa changamoto ya kubadilika, au
yanakazia ukweli unaoufahamu tayari” Freshi na Maisha
3 uk 29.
Katika kitabu hiki, Freshi, anamfunulia Maisha, ukweli
kwamba maisha ya binadamu yanaongozwa na Ubongo.
Ubongo umechorwa na kuonyesha kila sehemu ya ubongo na
kazi zake:
“ Kichwani mwako Maisha, kuna kitu kinachoitwa ubongo.
Ubongo ni ogani ya miujiza tupu. Wasomi wameutafiti
sana, lakini mpaka sasa mambo mengi yanayohusu uwezo
wa ubongo wa binadamu hayajafahamika. Lakini huko
ndiko kila tendo la mwili wako linakoratibiwa,
tanfsiriwa na utekelezaji wake kuamrishwa.” Freshi na
Miasha 3 uk 46.
Kama ilivyokwa kitabu cha kwanza na chapili, kitabu
cha tatu pia kina maswali mengi ya majadiliano.
Kitabu cha nne, Freshi na Maisha 4, kina ujumbe wa
“Jithamini”. Hapa Maisha amefika Darasa la Saba.
Amekua kimwili na akili imepefuka kiasi. Ameanza
kujithamini na kutambua mazingira tofauti
yanayomzunguka pamoja na changamoto zake. Maisha
amegundua kwamba wazazi ni wazito katika kuongea
masuala ya ngono na vijana wao. Hali hii imewaweka
vijana njia panda, huku jamii ikiwa inajiundia ngao ya
ukimya kuhusu masuala nyeti kama haya.
“Vijana wanahitaji stadi za maisha, siyo tu kwa
kujikinga na UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa.
Wanazihitaji stadi hizo kama mhimili wa maendeleo yao.
Stadi za maisha zitakazowawezesha kufahamu wanachotaka
maishani, jinsi ya kukipata na jinsi ya kukilinda na
kukiendeleza baada ya kukipata”Freshi na maisha 4 uk
47.
“ Alaa, sasa naanza kumpatapata Freshi! kumbe
kujithamini ni kufanya vitu kibao.Kujithamini ni
kujifanyia kila jambo zuri: kuwa msafi, kula vizuri,
kuweka mazingira safi, kuwa na uelewa wa mambo muhimu
kwa maendeleo yako, kujijua ili uweze kuwa chachu ya
maendeleo yako na jamii yako, hapo ulipo.” Freshi na
Maisha 4 uk 48.
Kitabu cha nne, nacho kina maswali ya majadiliano.
Swali lenye mvuto katika kitabu hiki ni hili: Taja
mambo mawili abayo siyo rahisi kuyazungumza na wazazi
wako. Jadili mambo hayo na rariki yako, kasha mjaribu
kubuni mbinu ya kuyazungumza na wazazi.
V. Tathmini ya vitabu hivi
Baada ya kuona muhtasari huu sasa nifanye tathmini ya
kazi hii aliyoifanya Mama Elieshi Lema. Niungame
kwamba wakati mwingine ni vigumu kufanya tathmini ya
mawazo ya mtu ambaye kwa kiasi Fulani mnakubaliana kwa
mambo mengi. Nitajitahidi kuwa mwaminifu kwa kile
kilichoandikwa katika vitabu vya Freshi na Maisha!
Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia
hadhira anayoikusudia, vitabu hivi vinasisimua sana
kutokana na mtindo alioutumia mwandishi. Ni mtindo wa
sura fupi fupi, kutumia miujiza ya maisha ya kila
siku, picha na maswali ya majadiliano.
Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza
Lengo Lake, yaani kubainisha na kisha kutoa majibu
kamilifu kwa changamoto zinazowakabili vijana na
walezi wao katika nyakati hizi tulizomo.
Tatu, mwandishi amefanikiwa kutoa mchango mkubwa
katika kufundisha maadili kwa vijana wetu. Amevumbua
kitu ambacho hakikuwepo. Mfumo wa kufundisha kwa
kusoma vitabu, kuuliza maswali na kujadiliana.
Mwandishi anasisitiza kwamba elimu inapatikana kwa
njia ya kusoma vitabu. Msisitizo huu unajitokeza sana
kwenye kitabu cha nne cha Jithamini.
Nne, mwandishi amefanikiwa kutumia lugha nyepesi na
mifano hai kuelezea mambo magumu. Ameonyesha mbinu
ambazo vijana wanaweza kuzitumia kufanya majadiliano
na wazazi wao. Wale wanaoshindwa kuongea na wazazi wao
wanaweza kutumia mtindo wa kuandika kwenye daftari
maswali, na wazazi wanajibu kwa kuandika: “kwa wanangu
Robert na Richard, Hamtaweza kukimbia au kuyachenga
maisha. Mazungumzo ya ana kwa ana yamewashinda.
Tujaribu maandishi. Awapendaye, Mama”. Freshi na
Maisha 4, uk 38.
VI. Hitimisho
Vitabu hivi vinasomwa kwenye shule za msingi. Hivi
vinaitwa vitabu vya watoto. Inawezekana na mwandishi,
aliwaandikia watoto. Lakini ukivisoma kwa makini,
unagundua kwamba hivi si vitabu vya watoto, hivi ni
vitabu vya watanzania wote na hasa watu wazima!
Kwa maoni yangu, vitabu hivi ni muhimu kwa watu
wazima. Ni muhimu kila mzazi kuwa na vitabu hivi
nyumbani kwake, avisome na kuviweka kichwani, baadaye
afanye kazi ya kuwasimulia watoto au asome na watoto
wake na kufanya majadiliano.
Ukiangalia mpangilio wa vitabu vyenyewe: Jipende,
Jilinde, Jijue, na Jithamini, utaona lengo zima la
kutaka familia na jamii nzima ya watanzania kuanzisha
mazungumzo na majadiliano juu ya maadili. Na
mazungumzo haya ni lazima yaanzishwe na watu wazima
wenye uzoefu. Ni lazima yaanzishwe na akina Freshi.
Freshi, rafiki wa Maisha,ni changamoto
kubwa.Mwandishi, amemchora na kumwingiza katika
hadidhi za miujiza.Amefanikiwa vizuri sana na ujumbe
unafika. Ukweli unabaki kwamba Freshi, ni rafiki wa
kila binadamu. Kila mtu ana malaika wake mlinzi, kila
mtu ana kipaji fiche ndani mwake. Kazi iliyo mbele ya
kila mtu ni kukikuza kipaji fiche, ni kukubali
kumsikiliza malaika wake mlizi. Tunaona mambo ya
Maisha, yanakwenda vizuri baada ya kukubali
kumsikiliza rafiki yake Freshi. Fundisho tunalolipata
ni kwamba kila mtu akikubali kumsikiliza malaika wake
mlizi, mambo yanakwenda vizuri. Huu ndio ujumbe mzito
tunaoupata kutoka kwenye vitabu hivi vya Freshi na
Maisha.
Vitabu vya Freshi na Maisha, vina maswali zaidi
150.Maswali haya yakijibiwa, vinaweza kuandikwa itabu
vingine zaidi ya vinne. Huu unaweza kuwa mchango
mkubwa wa kuboresha maadili katika jamii yetu. Kwa
njia hii tunaweza kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.
Mama Elieshi Lema, anatutoa kwenye hatua ya kulalamika
na kunyosheana vidole juu ya maadili na kutuingiza
kwenye hatua ya kutenda. Wakati ni huu, timiza wajibu
wako! Nunua vitabu, soma na watoto wako, fanya
majadiliano na kukubali kumsikiliza malaika mlinzi!
Pongezi nyingi zimwendee Mama Elieshi Lema,
aliyeonyesha ubunifu mkubwa wa kuelezea mambo magumu
kwa lugha nyepesi. Ni matumaini yetu kwamba mto wa
hekima bado unatiririka kichwani mwake, hivyo
tunategemea atuandikie tena Freshi na Maisha 5 hadi
10. Kwa mtindo wake wa kuandika vitabu hivi vinaweza
kuendelea bila ya kikomo!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment