WILLIAM E. MKUFYA, MWANDISHI WA UA LA FARAJA NA ZIRAI NA ZILANI William E. Mkufya aliyezaliwa mwaka 1953 wilayani Lushoto, Tanga, nchini Tanzania ni mmo-jawapo wa waandishi wakongwe wa riwaya za Kiswahili. Hadi hii leo amechapisha riwaya nne. Miongoni mwa riwaya hizi nne ni Ua la Faraja na Ziraili na Zirani. Kwa nyakati tofauti nimefanya uhakiki wa vitabu hivi viwili. Ziraili na Zirani kwenye gazeti la Rai na Ua la Faraja kwenye safu ya Kisima cha Ujuzi gazeti la Mtanzania. Aidha, William Mkufya ameandika vitabu kumi na viwili vya watoto na kutafsiri baadhi ya vitabu, kama vile riwaya ya Kiu ya Mohamed Suleiman Mohamed. Riwaya za Ziraili na Zirani na Ua la Faraja zimeshinda Tuzo ya Fasihi ya Kitaifa Tanzania katika kiwango cha Muswada Bora wa Riwaya mnamo 1999 na 2001. Mwaka 2004, Januari, LUTZ DIEGNER, alifanya mahojiano na William Mkufya juu ya uandishi wake na hasa juu ya kitabu chake cha Ziraili na Zirani. Ingawa nilishafanya uhakiki wa kitabu hiki ni vizuri kusikia mwandishi mwenyewe anavyosema juu ya uandishi wake. Ni matumaini yangu kwamba kwa njia hii wasomaji wanapata mwanga zaidi juu ya vitabu na waandishi. Na sasa tumwangalie Mkufya na uandishi wake wenye wingi wa tafakuri juu ya dini na maisha kwa ujumla na hasa kwenye kitabu chake cha Ziraili na Zirani. Mimi mwenyewe nimefanya maongezi mengi na Mkufya, hivyo kwa kusaidiana na mahojiano ya Lutzdiegner niliyoyapata kwa njia ya mtandao, ninawaleteeni Mwandishi mashuhuri William Mkufya. Swali: Lini na kwa nini ulipata mbegu ya kuandika Ziraili na Zirani? Jibu: Sasa, unajua, nina hadithi ndefu kuhusu lini na kwa nini niliandika riwaya hii. Kuandika Ziraili na Zirani ilikuwa ni lazima ningeiandika, ila mimi mwenyewe nina historia ya muda mrefu kuhusu mtazamo wa imani. Kwa hiyo lini? Ni mwaka 1981, tuseme hapo ndiyo nilipo-anza kuiandika hiyo Ziraili na Zirani. Niliiandika kama hadithi ya kurasa mia moja tu. Lakini kabla ya hapo nilikuwa na mtazamo wangu kuhusu imani, na nilikuwa najua tu, siku moja nitaandika kazi itakayosema ninavyoamini mimi. Unaona? Kwa hiyo kuanza kuiandika ni mwaka 1981 tuseme. Nikaiwasilisha. Kuna rafiki yangu mmoja alikuwa anafanya kazi hapo Oxford University Press, alikuwa anaitwa Anthony, An-thony Majengo. Sasa yeye akaipeleka Chuo Kikuu na profesa mmoja akaisoma aka-comment kwamba ni nzuri sana na inachokoza mawazo ya mtu. Lakini wakati huo ilikuwa inazungumzia tu, incidence ya mtu mmoja alivyofariki, alivyofika kuzimu na akawa na matatizo katika kujikabidhi kwenye hukumu. Baada ya pale yale maoni yaliyotolewa na yule Profesa, nika- yarekebisha nikaiandika upya. Sasa… Swali: Alikuwa profesa yupi? Jibu: Nadhani alikuwa Prof. Mbunda. Sina uhakika. Huwa wasomaji wa miswada hawapendi kuacha majina yao yajulikane kwa mwandishi. Sijui kwa nini. Nikarekebisha yale aliyoelekeza. Nilivyokwisha kuyarekebisha nikaipeleka Oxford University Press Nairobi. Kule alikuwepo mhariri wa siku nyingi sana, sasa hivi ni marehemu. Anaitwa Brian Hocking. Basi yeye, ile kazi ikamfurahisha sana. Ikamfurahisha, akampa mhariri. Kawaida publisher akishasoma muswada anawapa wasomaji wa ziada walioko nje ya ile kampuni wausome muswada kisha watoe maoni yao. Akampa. Nadhani huyo aliyepewa muswada ule alikuwa mtu mwenye imani kali. Kwa hiyo akaikatakata kwa wino mwekundu, akasema… ninazo zile nakala za maoni yake. Lakini yeye ame- nisaidia sana. Yale maoni yake yalikuwa makali, na kwa hiyo Oxford University Press wakasema hawawezi kuichapisha. Lakini yeye hajui kwamba alinisaidia sana kwa yale maoni yake, kwa sababu nilijua kwamba nikiandika bila kuwa mwangalifu, itawaathirije wale wenye imani ya namna ile. Kwa hiyo nikawa nimepata nafasi ya kujieleza zaidi. Halafu yeye, Mzee Brian Hocking akaniuliza kama nimesoma Dante na Milton, nikajibu ndiyo kwa sababu hata wakati nilivyokuwa nikiandika, nilikuwa nimeshasoma Dante na Milton. Lakini Milton, Paradise Lost, nilikuwa sijaielewa vizuri, kwa sababu ni utenzi mgumu, hata Divine Comedy ya Dante pia niliuona mgumu. Lakini nilikuwa nimezipitia tu kama kijana, nikazielewa nusunusu. Kwa hiyo akaniuliza umezisoma hizi? Nikamwambia nimezisoma. Akaniambia kazisome tena. Kwa hiyo nikaenda nikazisoma tena. Sasa nikawa mimi mwenyewe nina msimamo wangu. Wakati ule nilikuwa na mtazamo wa Kimarx, kwa hiyo baadhi ya hoja za Milton kwenye Paradise Lost, hasa pale, nadhani ni Raphael, anapomuusia Adamu, sikukubaliana nazo. Unaona? Bado hadi leo sikubaliani. Lakini ile sanaa, ile epic handling ya hizo hoja na matukio nilikuwa nimezifurahia sana. Kwa hiyo akaniambia kazisome tena. Ndiyo nikaanza sasa kuzisoma na ndipo nikaanza kuandika upya ile kazi. Ni kama niliichanachana na kuiandika upya kabisa. Ule ulikuwa ni mwaka 1981. Baada ya mwaka huo nikaenda Budapest, Hungaria kwenda kusoma glass technology kwa muda wa miezi tisa. Wakati huo nilikuwa nafanyakazi NDC. Kwa hiyo nikawa sijapata muda wa kuendelea nayo. Nilivyorudi nikawa fundi mkuu wa kiwanda cha NDC cha kutengeneza chupa kwa ajili ya hizi tube lights na balbu. Lakini sasa huo muda ukaniruhusu nikitoka kiwandani napata muda wa kusoma fasihi na falsafa kwa umakini zaidi. Kwa hiyo katika hicho kipindi cha karibu miaka minane nafanya kazi Light Source Manufacturers Ltd nikawa naendelea tu kusoma falsafa na kuzidi kujiimarisha na Marxism kuiangalia from the other angle pia. Kipindi kile wafuasi wa Umarx walikuwa wengi. Ni muda mrefu, nimeiandika kwa muda mrefu. Swali: Na ulimaliza mwaka tisini na nane, kwa sababu ilitoka tisini na tisa? Jibu: Ee. Nilimaliza tisini na nane kui-typeset na nini... Lakini ndiyo kwenye tisini na nane hiyo nilimaliza. UWAVITA walinifadhili. Walinipa shilingi laki nne nikaenda kijijini kwetu kuiandika upya. Kwa ujumla, nimeiandika karibu mara sita: yaani naandika, naandika upya, na- andika upya zaidi ya mara sita. Kwa hiyo hata kila neno la ile riwaya nimelichagua. Si kwamba yameangukaanguka tu kwa kusimuliwa! A-a. Yaani kila mstari au sentensi imekaguliwa kwa umakini na umantiki, ili kuwe na muunganiko wa msuko wa matukio. Swali: Umekusudia kumfikia nani kwa riwaya ngumu kama hiyo? Jibu: Kwa kweli sikutaka, sikukusudia iwe ngumu, ila yale yanayoongelewa kwenye riwaya ya namna ile ni magumu. Kwa hiyo mimi mwenyewe ningependa iwe rahisi sana. Na ndiyo utaona kwamba hata Kiswahili nilichotumia nimefanya makusudi kiwe chepesi, mtu yeyote anayekisoma, aweze kukielewa kile Kiswahili. Kitakachomtatiza ni zile concepts. Yale mashauri yanayojadiliwa mle ndiyo yatakayomtatiza, lakini ni kwamba nilitaka nihadithie kwa lugha inayoeleweka kwa kiwango kikubwa. Swali: Lakini baadhi ya maneno ya msamiati pia ni magumu kidogo, au unafikiri watu wanaoitwa wa kawaida wanayaelewa yote? Jibu: Ndiyo sababu nakwambia mle kila neno limewekwa kwa sababu lilingane na hoja au tukio. Kama utakuta neno gumu lina sababu ya kuwekwa mle, kwa sababu neno lingine la rahisi lingerahisisha ile dhana iliyoko mle ndani. Si kwamba nimetumia neno gumu kwa makusudi tu ya kumbombast mtu, a-a, ni kwamba likiwa mle, lina sababu ya kuwemo mle. Na siyo mengi sana hata hivyo. Swali: Je, katika kumuumba mhusika Zirani, ulimchanganya na maisha yako? Jibu: Ndiyo. Ndiyo. Zirani, unajua, kile kichwa cha ile riwaya ni Ziraili na Zirani. Yule mtu anaitwa Fikirini Zirani. Ndilo jina lake. Kuzira Kiswahili ni kususa. Kwa hiyo nawaambia watu kwamba: Fikirini mzire! Mkifikiria haya mambo ni heri mzire. Ni heri msusie, msusie hizo dini, kwa sababu haziwasaidii. Ndiyo jina lake yule Fikirini Zirani. Nimemchanganya na maisha yangu kwa kiwango fulani, kwa sababu mimi nimekuwa natatanika sana kuhusu hizi imani. Kwa muda mrefu nimekuwa nazira. Hivyo, kama nilivyokueleza, kwamba nimekuwa nazitazama na naona kwamba kwanza zinaathiri maisha ya watu, nazo zenyewe zinaji-contradict. Lakini bado watu wanalazimika kuwa nazo, halafu hawana jinsi yoyote ya kuziepuka. Hili ndilo tatizo kubwa. Swali: Tunaweza kusema kwamba mada kuu ya riwaya hiyo ni uchunguzi wa dhana ya dini pamoja na mikinzano inayotokana na waumini na wasioamini, na mikinzano baina ya waumini wa dini tofauti. Hapo umetia mkazo kwenye dini za Uislamu na Ukristo. Ulikusudia zaidi kuzingatia mikinzano baina ya dini hizo mbili, au lengo lako lilikuwa kuijadili misingi ya dini zote? Jibu: Ukifika kwenye ile sura inayohusu vita ilipokuwa inapiganiwa kule mbinguni, unaona nilijaribu kuwaita wote, hata mashetani wa Kihindu, mashetani wa Kizoroaster, niliwahusisha mle. Kwa maana ya kwamba ile vita ni vita yote ya jamii yote, na ya jamii zote za kibinadamu zinazoamini. Kwa hiyo, maana yangu hapo ni kwamba ninakusudia kuzisema dini zote zinazoamini uungu. Ila kwa sababu hadhira yangu mimi ni ya Waislamu na Wakristo, hapa eneo letu la Afrika Mashariki, Afrika kwa ujumla na sehemu kubwa sana ya ulimwengu, hadhira yangu kubwa zaidi ni ile, halafu mimi mwenyewe sijawa na ufahamu wa kutosha kuhusu dini za mashariki ya mbali, za Kihindu, Kibuddha, na hizi nyingine, kwa mfano za Japani. Kwa hiyo kama ile riwaya ingeanza kuzijadili hizo ingekuwa mbali mno na hawa wasomaji. Ningeanza kwa mfano kuweka miungu ya Kishinto au imani za Kishinto, au hekima za imani ya Confucius, riwaya ingejitenga mno na hawa wasomaji wa kawaida. Kwa hiyo ni heri nilivyozijadili zile ambazo tunazo japokuwa kusudi ni imani zote kwa ujumla. Mawazo mawili makuu yanayopingana katika riwaya hii yanawakilishwa tayari katika ma- dondoo ya mwanzoni mwa riwaya. Wazo la kwanza la Mfalme Ashoka linasema kwamba dini zote ziheshimiane na kwa kuheshimiana huko, zipevuke na zipevushane. Wazo la pili la Bertrand Russell linasema kwamba uwingi wa dini tofauti unadhihirisha kwamba hakuna hata dini moja iliyoweza kuwa kweli. Anaongeza kwamba msingi wa dini yoyote ile ni woga. Swali: Katika riwaya yako tunasoma dondoo lifuatalo juu ya asili ya dini yoyote ile: —“Woga huu unapopevuka unabatizwa na kufinyangwa kimantiki na falsafa na kuitwa dini. (ZZ Mo- toni V).” Ukiangalia hayo mawazo mawili makuu ya mwanzoni, wewe uko upande gani? Jibu: Mimi yale mawazo mawili yote nayapenda, kwa sababu usitegemee hoja moja kutekelezwa mara moja, labda kwenye mapinduzi , lakini kama unataka transformation, social transformation, inaenda kwa ngazi. Kwa hiyo kikweli kwa hivi sasa, hali tuliyo nayo, hoja ya Mfalme Ashoka ni nzuri, kwamba sasa hivi ni upuuzi kuanza kukatana mapanga kwa sababu ya tofauti ya Mkristo na Mwislamu zile imani zinapotofautiana. Sasa ngazi ya pili ya transformation ya binadamu ni ile hoja ya Bertrand Russell. Ukiniuliza nakubaliana na lipi ni vigumu kusema kwa sababu hiyo ni ngazi. Hatuwezi sasa hivi kuiambia jamii maana imeshaathirika. Tumekuwa wagonjwa, yaani jamii ya Kitanzania na Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, infact dunia nzima, ni wagonjwa, wameathiriwa na huo ugonjwa wa imani. Na tukiita dini ugonjwa, tutawaudhi watu. Huko nyuma dini ilikuwa na manufaa mengi hasa ya maadili. Hatuwezi kuyapuuza. Lakini kwa sababu sasa hivi dini zinapoanza kukaribiana na kugongana huleta madhara mengi, basi unaweza kuita imani: ugonjwa. Kule nyuma kote labda imani hazikuwa ugonjwa, ilikuwa ni lazima mtu awe na imani. Lakini sasa hivi imani za dini ni ugonjwa. Sasa hatuwezi kuponya huo ugonjwa kwa dawa moja ya ghafla na kusema: —Acha!“ Ni kama leo baada ya tatizo la ukimwi ukiwaambia watu —Msifanye sex!“ Wameshakuwa watu wa utamaduni wa ki-leo, utamaduni wa kisasa. Sex is part of the way of looking at life. Sasa huwezi kuwaambia —Acheni!“ Itakuwa kama wako jela. Kwa hiyo ni lazima uanze labda kuwashawishi waanze kupunguza, kupunguza, kupunguza na hatimaye waone ni upuuzi kama anavyoona mhusika Alyosha wa Dostoyevski akiwa na Grushenka kwenye Brothers Karamazov, kwamba kuendekeza ngono ni upuuzi. Haina maana, haina manufaa, kama it‘s just a playing around! Lakini kwa hivi sasa ukiangalia tele-visheni, na vijana wanavyochangamkia sex, huwezi kutoka tu ghafla ukawaambia —Acheni!“ Kwa hiyo ndivyo vile hata na hizo imani. Lakini nafikiri kuna tofauti baina ya jambo hili na jambo la dini. Bahati mbaya nimeihusisha na kitu ambacho dini zenyewe zinakichukia. Ngoja, katika Ua la Faraja ninazungumzia tatizo moja la hilo neno sex. Katika Ua la Faraja ninazungumzia ukimwi, lakini dhamira mojawapo ni kwamba: tuiheshimu sex. Na kuiheshimu sex, siyo kusema ni kuiacha, au siyo kusema ni mbaya na kuiita shetani, au vilevile si kuitukuza na kuifanya kama riadha! Uliniambia kwamba nimelinganisha vibaya msukumo wa kuendelea na imani na msukumo, katika nafsi za mwanadamu, wa kuendekeza sex; yaani ile analogy haifai. Sasa ndiyo nikakwambia kwamba mbona na hizo imani zinaiogopa sex? Kwa sababu sasa hivi kwa Mkristo au Mwislamu sex ni kama shetani yaani sex ni kama jitu, kitu kibaya sana. Katika Ua la Faraja nasema kwamba sex ni kitu muhimu sana kwa mwanadamu na ni kitu sacred, ni kitu cha kuheshimika, cha kutukuka. Sisi Waafrika kikwelikweli tunaitukuza sex. Si kwamba tunaitukuza kwamba tunaifanya mno... fanatically, a-a, yaani tunaiheshimu. Ni kama ni sacred thing. Na ukienda kwenye majando na unyago, wanafundishwa hivyo kwa yale ya asili, siyo ya sasa hivi, kwa sababu yale ya sasa hivi yameathirika pia na ile sexist fanatism. Lakini yale hasa ya jadi, zamani, yalikuwa yanatukuza sex kwa sababu ndiyo njia pekee ya kufanya jamii iendelee, idumu isipotee. Kwa hiyo kile ni kitu cha kutukuza. Kwenye imani za Kikristo na za Kiislamu sex inaogopwa mpaka inakuwa kama yenyewe ina uovu ndani yake. Swali: Tukirejea kwenye Ziraili na Zirani: Katika riwaya hiyo, umetumia wahusika wengi na kutaja majina mengi sana, hasa ya wanafalsafa na mashujaa wa kihistoria kutoka dini mbalimbali Jambo hili halirahisishi usomaji wa riwaya. Halafu umeyarudia baadhi ya hayo majina mengi katika sura nyingine. Kwa nini umetumia majina mengi namna hiyo? Jibu: Ile riwaya nimekusudia kuwa na muundo wa epic, kwa hiyo approach au staili yake ya uandishi ni hasahasa ile. Siyo epic katika hii modern concept ya epic kwamba unaweza kuwa na prose epic. Lakini nilijaribu kutumia ile ile style aliyoitumia Vergil kwenye Aeneid, Milton kwenye Paradise Lost, na kadhalika, ambapo mashujaa au waoga hutajwa kwa majina yao yale yale. Epic inazungumzia hata zile za nyuma na ina uhusiano wa karibu sana na tukio la kweli. Ni masimulizi kuhusu kukabiliana na jambo na kumsifu aliyeweza kukabiliana nalo mpaka akaliweza. Yule aliyekabiliana na jambo, kama ni jambo dogo, tena la kwake pekee, sasa nd‘o unapata zile epics kwa mfano za Homer. Ni kwamba yule mkabilianaji na hilo jambo ni huyo mmoja. Odysseus anakabiliana na vita, vita yake, halafu anapata masaibu, anakabiliana nayo, anayaweza. Unapotoka kwenye ile primary epic ya akina Homer, unaingia kwenye secondary epickama ile ya Vergil. Kwenye Aeneid, ni taifa la Urumi lilivyoweza kuhama kutoka hapo lilipo-kuwa mpaka lilipokwenda kuji-establish nchi ngeni, humo njiani likiwa linapambana vita na kukabiliana na matatizo mengi. Sasa pale hawezi kuwepo shujaa mmoja. Ni mchango wa watu wote kufanya hilo jambo liwezekane, au siyo? Unapoitazama Secondary epic nyingine, ile ya Milton, The Paradise Lost, pia hayo maanguko ya mwanadamu yalielemezwa mno kwa Adamu. Ingawaje Adam alikuwa ndiye mhusika mkuu, tena wa pekee, hayo masaibu aliyokuwa anapata Edeni, yeye mwenyewe binafsi, na jinsi yalivyomwangusha, hakustahili abebe lawama ya wanadamu wote. Kusema kweli kwenye Paradise Lost mimi huwa nasema kwamba “ Ah! Kwani ni kweli Adam ndiye mhusika wa vita ile?” Maana inakuwa kana kwamba kulikuwa na vita kati ya mashetani na malaika huko jehanamu. Hapakuwa na vita, ila kulikuwa na maanguko ya Adamu kwenye Paradise Lost. Maanguko ya Adamu, alivyoweza kushawishika na shetani kwa kupitia kwa Hawa. Lakini mle kwenye masimulizi aliyopewa Adamu kuhusu kilichotokea pia wanatajwa wahusika wengi, miungu ya Mesopotamia mingi imetajwa. Imetajwa miungu ya Misri, wametajwa watu mbalimbali, muhimu katika historia ya theolojia ya magharibi. Mimi naona hii ni kawaida ya epic, kwa mashujaa kutajwa kwa majina yao. Na kusema kweli jambo ambalo ninalishughulikia kwenye Ziraili Na Zirani, ni jambo muhimu na nyeti kuhusu suala tata la dini – umuhimu wa kuwa au kutokuwa nayo. Linahusu watu wengi katika historia waliowahi kulijadili. Kwa hiyo ni lazima niwahusishe wengi ili hoja zangu ziwe na uzito na zisionekane kwamba ndiyo mimi wa kwanza kuzijadili. Kesi sharti iwe na ushahidi au iwe na mifano ya aina kesi za namna hiyo zilizowahi kutokea. SWALI: Unapokosoa dini inadhihirika kwamba unatia mkazo zaidi kwenye kukosoa dini ya Kikristo. Kwa nini? Jibu:Kwa sababu mimi mwenyewe nilikuwa Mkristo, na nilizaliwa katika mazingira ya Kikristo. Kwa hiyo ninaufahamu Ukristo zaidi. Kabla ya sababu ya pili, inabidi nikiri kwamba Wakriso si wageni katika kujadiliwa. Pengine ni kwa sababu wamepitia katika mabadiliko ya kifikra ya muda mrefu yaliyokuwa yanaendelea huko Ulaya kuanzia karne ya kumi na tano. Kwa hiyo walishazoea kustahamili hoja zinazowazungumzia. Halafu pili: Waislamu huwa hawapendi dini yao ijadiliwe kwa namna hiyohiyo ilivyojadiliwa ile ya Wakristo. Yule mwanamke wa Bangladesh aliyeandika kuhusu haki za wanawake zinavyoathiriwa na sheria za dini, ingawaje ametoa hoja za msingi lakini alipata matatizo makubwa. Kwa hiyo hilo pia limesababisha nisiwe muwazi sana. Nilisoma Qurani na kuielewa kama msomaji mwingine asomavyo tafsiri ya biblia na kuielewa kabla sijaandika hiyo Ziraili na Zirani. Kwa hiyo kusudi halikuwa kwamba niwajadili Wakristo peke yao. Kama utaitazama ile riwaya hii leo, utakuta kwamba Wakristo wamewekwa kwa kuwakilisha dini zote….. SWALI: Katika sura iitwayo Dhahara unasawiri dilemma ya kimsingi ya binadamu kuwa amegawanyika baina ya hiari na haja. Tunasoma dondoo lifuatao: “Tamaa haziepukiki japo zinatawalika” (ZZ Dhahara V 107). Unafikiri kweli kwamba dilemma hiyo ina suluhisho lililoweza kutawaliwa na hekima kiasi hicho? JIBU: Hiari, haja, na hekima. Freud aliyatenganisha kama The Ego, the Id and the Super-Ego. Hata Hazrat Ahmad mwanzilishi wa Ahmadia Movement anazizungumzia kwenye The Teaching of Islam. Naye amezitenganisha kwa namna inayokaribiana na hiyo. Anaziita nafsi i-amarah, nafsi i-lawama na nafsi i-mutmainna. Nafsi i-amarah ndiyo hiyo Ego, na nafsi i-lawama, nadhani ni hiyo Id, na nafsi i-mutmainna pengine ndiyo Super-Ego. Kusudi hasa la kusema hivi ni kwamba hizi zote ni dhana kuhusu muundo wa nafsi ya mwanadamu. Muundo wake ni kwamba una sehemu hiyo inayohusu haja za kimwili ambazo Freud anaziita libidinous part ya mwanadamu. Halafu iko hii sehemu ambayo inahusiana na hekima– any-way tuache kwanza hekima- inayohusiana na busara zake, yaani the rational part, halafu kuna ile ya hiari. Unaona? Huo muundo wa nafsi nimeuweka hivyo: haja, hekima na hiari. Sasa kuhusu swali lako linalohusiana na hilo dondoo: “Tamaa haziepukiki lakini zinatawalika”: Inawezekana! Ukienda kwenye ile sura ambapo Zirani ameingizwa kwenye kambi ya mashetani, kwenda kwenye mafunzo, wakawa wanajadiliana. Muhutasari wa mafunzo yale umewekwa katika ukurasa 52 na 53. Sehemu moja ya ile hoja ni kwamba mwanadamu anaishi muda mfupi mno. Mwili wake una tamaa, lakini zinatawalika kama akili itapata muda wa kukua, busara ikakua. Lakini muda wa kukua busara ni mfupi. Jamii zile ambazo watu wake wana muda mfupi wa kuishi, kwa mfano miaka sitini, hata busara hazipati muda wa kukua na kuenea ukilinganisha na jamii ambazo wazee wanakuwa wengi na wana muda wa kujadiliana na kueneza hekima zao. Mifumo ya maisha ya jamii zenye muda mfupi wa maisha huwa michanga na ghafi. Jinsi mwanadamu anavyoweza kuishi miaka mingi ndivyo atakavyoweza kutawala hizo tamaa. SWALI: Mojawapo ya tata za misingi ya dini tofauti kama inavyotajwa katika riwaya yako ni kwamba waumini wanaamini kwa chochote wanachokitenda duniani, watahukumiwa mbingu (tz ZZ Zirani VI). Binadamu angeamini zaidi kwamba tahukumiwa papa hapa duniani, asingetenda kama anavyotenda. Unaona suluhisho gani kwa tatizo hili? JIBU: Kwamba utahukumiwa mbinguni- mimi siamini hivi. Hakuna kuhukumiwa mbinguni. Kwa hiyo la muhimu sasa hivi ni kuikataa hii hoja nyingine. Watu waelewe kwamba pa kuishi na kuhukumiwa ni hapa hapa duniani. Mimi naona kuna umuhimu wa kuwa na kosmolojia mpya. Kosmolojia inayozingatia ufupi wa maisha ya hizi nafsi na tatizo la utu wa nafsi. Kwani dini ni nini? Mimi naona kusudi lake ni lile ya kutamani immortality. Kusudi ni kujenga hofu ya mauti, na kuzusha matumaini ya maisha baada ya kifo ambayo siamini kama yapo. Sasa la muhimu ni kuweza kuukubali na kuustahamili ukweli kwamba tunakufa. Lakini kikwelikeweli hatufi na kufutika. Na hiyo ndiyo hoja ya Ua la Faraja. Hiyo ndiyo dhamira kuu kama nitafikia kwenye hizo ngazi ya tatu ya Maua. Lakini nitawezaje na mazingira magumu ya uandishi? Bado naona kama sitaweza kufika mwisho wa hoja yangu. Jinsi ya kufika huko, sijui kama itaniathiri vipi. Hoja yangu ni kwamba kwanza mwanadamu ameshajua, ameshaanza kujua au kukubali ukweli kwamba hakuna mbinguni tulikokuwa tunakutamani hapo zamani. Baadaye hata watoto watapuuza. Unaona? Ni hatari! Kwa sababu, kwa mfano katika kitabu cha Dostoyevski, kuna mhusika anasema kwamba mwanadamu akishaanza kukataa kwamba kuna immortality, hapo anaweza kufanya uovu wowote anaoutaka. Kwa sababu sasa haogopi kama kuna adhabu mbele yake. Ni kweli kwamba kuna hatari hiyo kwamba sasa hivi jinsi tunavyokaribia kuelewa ule ukweli kwamba hatuna mustakabali mwingine tunaweza tukaingia kwenye janga kubwa la kutisha. Dhana ya absurdity au utomaana wa maisha itakuwa imepaa juu mno. Na watu watakata tamaa, watafanya mambo ya ajabu kabisa. Sasa kwa nini pasiwe na suluhu? Bila shaka utatokea usharika wa wanafalsafa utakaozua mbinu ya kuepusha janga kama hilo. Ng’ombe hajutii kuwepo kwake, hajutii kuendelea kulishwa na mwanadamu halafu atiwe kisu naye, aliwe, anyang’anywe maziwa ya mtoto wake, halafu yaende kuuzwa. Hajutii. Tatizo la mwanadamu ni kule kujua, kujitambua na kujidadisi. Tumeshajitambua. Kwa hiyo tunatakiwa tuwe na suluhu ya matatizo ya kuutambua ukweli. Kwenye Ua la Faraja nitajadili uwezekano wa suluhisho. Sitausema sasa hivi, kwa sababu uko katika kuumbwa. Sitaki kutoa mapendekeo yoyote mpaka niwe na uhakika nayo. SWALI: Kwa tashtiti fulani inatajwa katika riwaya yako kuwa dini za ulimwengu zinachukulia kwamba asilimia tisini ya binadamu ni watenda dhambi, kwa hiyo motoni ni pahala pa uvundo mkubwa panapojaa tele (tz ZZ Motoni 1). Ungetathmininje athari za dhana ya dhambi kwa historia ya binadamu? JIBU: Dhambi! Labda niseme hambi ni uovu, kwa sababu dhambi ni kama jambo linalostahili adhabu vile. Yaani ukisema dhambi, una maana kuna hakimu – Mungu. Unapoanza tu kusema dhambi ina maana kwamba unaenda kinyume cha sheria fulani zilizowekwa. Kwa hiyo mimi huwa silipendi hilo neno ‘dhambi’. Kwa sababu sioni kwa nini kuwe na kitu kama hicho, mtu aliyeweka sheria, yaani Mungu au kitu kingine, ila iwe tu kwamba mtu atambue kwamba kwenda kinyume cha mfumo wa maadili itakuathiri. Ile karmic vision ya Kihindu au ya Kibuddha kwamba ukienda kinyume cha matarajio ya mfumo wa maisha, utapatwa na athari; ukienda sahihi na mfumo wa maisha, utapata furaha. Sasa dhambi huwa si neno bora zaidi, naona ni bora kuwe na sheria, law of nature, kitu kama hicho. Kwa hiyo liwepo neno bora zaidi la Kiswahili badala ya dhambi. SWALI: Ndiyo. Lakini ile dhana ya dhambi, watu wengi wameishikilia na wameitathmini sana, halafu hii ilikua na athari kubwa nafikiri. JIBU: Ni sahihi kabisa. Ile dhana kwamba kosa ni dhambi imewaathiri. Kwa mfano kuogopa kufanya jambo kwa kudai kwamba ni dhambi. Hata kukosoa tu baadhi ya hoja za kidini ni dhambi. Sasa huwezi kuboresha maelekezo yake. Kufuru ni dhambi, kwa dini zote tulizo nazo. Lakini kutokubaliana na desturi za imani fulani ikiwa imewekewa mwiko huo wa “kufuru” ina maana watu wataogopa hata kutoa mapendekezo yaliyo bora zaidi. Inawezekana mengine zamani yalikuwa yakiitwa dhambi, lakini sasa hivi si dhambi tena. Mfano Wayahudi walikatazwa kula nguruwe, lakini Wakristo sasa wanakula. Kwa hiyo miiko imezuia watu kufikiria uboreshaji. Hata hicho kipindi cha mageuzi ya kifikira huko Ulaya wakati wa akina Diderot na Descartes ni kwamba walianza kuonekana kama wao ni watenda dhambi, ni watu wabaya, kwa kuwa walianza kusahihisha. Hata Galileo alipogundua darubini ya kuona nyota kwa ukaribu zaidi ilionekana kama dhambi, ilichukuliwa kama kufuru. Kwa hiyo, dhana ya dhambi imesababisha kukandamizwa kwa uhuru wa kufikiri. SWWALI: Ukikosoa dini, hasa zile ziabuduzo Mungu mmoja tu, linajitokeza suala la dini barani Afrika: Ukristo na Uislamu zote mbili zimeletwa na wageni. Kwa kutoa mfano wa Kin-jeketile unaonesha jinsi ambavyo alisilimu kijuujuu, lakini bado anamwabudu Mungu wake Bokelo (tz ZZ Motoni IV). Tunaweza kuhitimisha hoja mbili: Ama nafasi ya imani za kijadi itambuliwe ipaswavyo na wakuu wa dini za Ukristo au Uislamu, ama Ukristo na Uislamu ziachwe kwa sababu hayahusiani na utamaduni wa kiasili wa Waafrika. Ungependelea hoja ipi binafsi, na kwa waafrika kwa ujumla? JIBU: Katika hiyo sura kuna mahali ambapo Kinjeketile anaambiwa na Zirani na wenzake walioenda kumtembelea kule motoni “Sasa acha!” Kwa sababu walimwuliza maswali “Mbona huyo Mungu wako haji kukutetea huko huko motoni?” Mwisho kina Zirani wanamwambia Kinjeketile, “Basi, jiunge na sisi tuachane na mambo ya imani.” Kuna mmoja mle kuzimu walimwambia hivyo akawatukana na kuwafukuza. Lakini huyu Kinjeketile akawaambia “Nendeni nifikirie.” Wakaondoka. Alivyofikiria jibu lake alileta lini? Ile riwaya imeungamana, matukio yanahusiana. Unapofikia kwenye ile sura ya vita, kundi la Kinjeketile lilikuja vitani. Kama lilikuja vitani ina maana alikubaliana nao. Kule vitani shetani mmoja aliwatania, akawaambia “Na nyinyi mnaokula nyama za vidudu mmekuja hapa? Lakini ndivyo hivyo inavyojidhihirisha kwamba na yeye Kinjeketile amekubali kuingia kwenye hiyo vita ya kupinga imani zote. Nilikuwa upande wa Kinjeketile kuhusu imani za Kiafrika. Lakini, kwa Kinjeketile naye kukubali kujiunga na vita, hoja yangu ni kwamba hata hizo za Kiafrika pia si muhimu kwa sasa. Ninachosema ni kwamba hapakuwa na sababu Waafrika waletewe imani nyingine. Hapakuwa na sababu. Na ni haki kabisa kwamba Kinjeketile alikuwa anasema, “Hatukusilimu uchi. Nilisilimu nikiwa tayari na vazi langu la hadhi.” Kuletwa kwa imani nyingine hakukuwa na haja. Ingawa hata hizo za Kiafrika zilizopo sasa, kwa mazingira ya sasa hivi nazo hazina umuhimu. Ndiyo sababu ya lile kundi la Kinjeketile, pamoja na kwamba lilikuwa linataka imani zao za asili ziheshimiwe, na wao wenyewe waliamua kujiunga na vita. Ina maana kwamba na ile imani ya kwao pia wameikana. SWALI: Sasa hii zaidi ni hoja yako kama mtu binafsi, au ungepenelea kwamba Waafrika wote wangefikiri hivyo? Tukisema katika siku za karibuni au katika hali ya sasa hivi, unafikiri inawezekana kweli kwamba Waafrika watambue jambo la kwamba tuache dini zote – zikiwa za jadi au zisizo za jadi, haina tofauti – tuziache zote, au ni kama hatua ya mbele? JIBU: Kwanza hiyo ni hadithi, ni riwaya; si kwa Waafrika peke yao. Hiyo ni hadithi, ni universal epic on faith. Kwa hiyo kusudi si Waafrika peke yao. Ndiyo sababu nasema kwamba hata wale wa Kinjeketile walijiunga kwenye ile vita maana yake tatizo lote ni kwa wanadamu wote. Siyo tatizo la Mwafrika peke yake. Ingawa historia ilikowapitisha wao walienguliwa, walinyimwa nafasi ya kuonyesha imani za kwao, kama vilevile Waskandinavia walivyoathiriwa na Ukristo. Jinsi Waafrika walivyo na tatizo hilo ndivyo walivyo nalo Wataliano, Wahispania, Waingereza, Wajerumani, wote wana hilo hilo tatizo kwamba ni imani ya Mesopotamia imeenea mpaka kule kwao. Tatizo ni kwa watu wote. Lakini Mwafrika sasa hivi akisema “Mimi narudia dini za jadi”, atakuwa kama ameruka mkojo amekanyaga tope! Itakuwa ni kichekesho kurudi na kuanza kushika pembe ya uganga, na kuanza kuiuliza maswali ili ikutatulie matatizo yako! Schopenhauer anasema kwamba haoni tofauti kati ya yule ambaye ni Mkristo, na yule ambaye anaabudu mizimu. SWALI: Jambo linalohusiana na swali lililopita ni kwamba tamaduni za kimagharibi zinatambua na kuhusudu kwa kiasi fulani tangu zamani dini nyingine za duania kama Ushinto, Utao, Uhindu na nyingine, lakini hawazitambui sembuse kuziheshimu dini na imani za kijadi za Kiafrika (tz ZZ Mzingo wa Vita IV). Unafikiri kuwa licha ya ubaguzi wa rangi vile vile kuna phenomenon kama ubaguzi wa dini? JIBU: Kikweli ni kwamba unaposema hivi sasa kwamba wanaziheshimu imani za Mashariki: wanaofanya hivyo sasa hivi ni wale Wazungu wa Magharibi wa leo…. SWALI: …lakini imeanza zamani. Hata akina Goethe kwetu Ujerumani, na wengine wameanza zamani sana kufanya utafiti kuhusu hizi dini za Mashariki, kuzipenda sana na kuziheshimu sana kama utamaduni mwingine. Lakini kumbe kuhusu dini na imani barani Afrika hakukuwa na kitu kama hicho, kulikuwa tu kwamba “Ah! Ni upuuzi. Tusambaze Ukristo, basi.” JIBU: Kwanza tukubaliane kwamba, mfano sayansi, kuna kwingine ambako ilipewa nafasi ya kuendelea na kukua vya kutosha. Kuna kwingine ilikandamizwa isikue. Kwa hiyo, huwezi kusema kwamba utafiti wa kisayansi katika dunia uko katika usawa mmoja. Kuna ambako mazingira yaliruhusu sayansi ipanuke au irefuke zaidi. Au si ndiyo hivyo? Basi hata hizo dini. Kuna dini ambazo zilipata fursa ya kupevuka zaidi kuliko nyingine, na hiyo inahusiana na maendeleo ya binadamu. Kwa mfano upevu wa Ubuddha, hata Ukristo unaweza ukazidiwa nao. Au ukichukua tu hata upevu wa Uislamu, kwa sababu Mwislamu kaanzia pale Mkristo alipoishia, alipata nafasi ya kupevuka zaidi. Tarehe ya Kuruani iko mbele ya tarehe ya Ukristo. Kwa hiyo Wakoloni walivyotukuta sisi, ni kama walivyofanya Amerika Kusini. Waliwakuta watu kule, walikuwa na tamaduni zao pevu kama Wainka. Pengine walikuwa na miungu yao, au siyo? Waliwafanyaje? Waliwatukana na kuua hizo imani zao; waliona kwamba walichoamini ni upumbavu? Inaonyesha kwamba heshima waliyo nayo watu wa magharibi kwa hizi imani za mashariki ni kwa sababu walikuwa wameshangazwa na upevu wake walioukuta. Bahati ikawa wakati huo ndio wakati wa mapinduzi ya kifikira huko Ulaya ndiyo sababu walikuwa na udadisi wa namna watu wa mashariki walivyoabudu. Baada ya akina Descartes kuanza kutilia mashaka imani ndipo wakaanza kuuheshimu ule upevu wa imani za mashariki. Hata akina Schopenhauer walipoweza kuyasoma yale waliyoyasoma walikuwa tayari wamekubali kwamba tunaweza kujiuliza maswali ya kudadisi ukweli wa imani. SWALI: Sidhani kwamba tunaweza kusema kwamba imani za Kiafrika hazijapevuka. Nafikiri katika kesi nyingi tatizo ni kwamba hatujui mambo mengi kuhusu imani hizo. JIBU: Sasa nilikuwa sijamaliza. Ndiyo sababu. Mimi ninapozungumzia upevu wa Ubuddha siushabikii kwa sababu yoyote. Au ninapozungumzia upevu wa imani za Warumi, sipendelei kwa sababu ya kwamba ni ya Kirumi. Au kwa mfano ninapozungumzia upevu wa imani za Uchina, si kwa uishabikia ila nina maana kwamba imani hiyo ina kiasi cha ubora wake ambao unaweza kunufaisha mambo kadha ya kisasa kuhusu maisha. Kila utamaduni una kiasi cha manufaa ya aina fulani yenye uwezo wa kumsaidia mwanadamu kukabiliana na mambo yenye utata. Mfano Ying yang ya Wachina ina vichocheo vya fikra vya hali ya juu. Waafrika pia wanaweza kuwa na vichocheo vya kifikra vya aina yake. Lakini kujibu hilo swali lako ulilouliza ni kwamba ubaguzi wowote unapokuwepo, yule anayebaguliwa, lolote alilo nalo linalomhusu litabaguliwa. Pakishakuwa na ubaguzi; nikishakubagua wewe, chochote utakachosema nimekibagua, nimekipuuza, maana pengine nakubagua kwa kukuogopa usinikaribie. Chochote unachosema nitakibagua. SWALI: Ni kweli, lakini India imekuwa colonized pia. Na hawajabagua Uhindu kiasi hicho. Na swali jingine ni: hudhani kwamba imani za Kiafrika pia zilikuwa zimepevuka sana, lakini hatujui sisi Wazungu hatujui – vya kutosha? Na hatuwezi kutathmini au tuseme ni vigumu sana kupata vigezo vya kusema huu ni upevu, na ule si upevu. Nakubali kwamba tunakuta upevu mkubwa kwa mfano katika Ubuddha, lakini kwa nini katika imani za Kiafrika tusiseme kuna upevu mwingine? JIBU: Unajua mimi mwenyewe hapa nilipo ukiniuliza, juzijuzi tu ndipo nilienda nyumbani kwa kusudi la kimila. Mwaka juzi, nilikwenda nyumbani kwetu kufuatilia kama tambiko fulani limefanyika. Kulikuwa na tambiko, tuna tambiko linaloitwa ‘Fika’. Sasa nilikwenda kushirikiana na wazee kwenye Fika hiyo. Siku nyingi sana tambiko hilo lilikuwa halijafanywa. Kwa kushirikiana na baadhi ya wanandugu tukachanga pesa ili kukamilisha mahitaji yote yanayohitajika: ng’ombe, vifaa vingine vya tambiko na vyakula. Kweli tulifanikiwa. Ile Fika ikafanyika. Nikiangalia kusudi halikuwa kushiriki peke yake, kwamba mimi pia nina imani ile ile, ndiyo sababu nikafurahia ifanyike. Si hivyo tu. Kusudi pia lilikuwa kupinga kutofanyika kwa Fika ile. Na pia kupinga kwamba Fika ile iliachwa kufanyika kwa sababu ya Uislamu au Ukristo. Kwa hiyo nikachangia kuhimiza mpaka ikafanyika. Bahati mbaya sikuwa na kamera ya video, lakini nilichukua picha. Sasa hivi naandika, naandaa kumbukumbu kuhusu jinsi ya kuifanya ile Fika ili hata watoto huko baadaye waweze kuirudia kuifanya. Kwa hiyo mimi ukiniuliza imani za Kiafrika – mimi mwenyewe sizijui! Kwa sababu ziliachwa kufanyika muda mrefu. Hata hao wasomi wa sasa hivi wanaotetea Uafrika, wengi wao maskini hawaujui, kwa sababu wameshatenganishwa na Uafrika wao halisi kwa muda mrefu. Wazazi wao, au kuanzia kizazi cha juu, generations tatu zimeshapita, hawafanyi matambiko. Kama unavyosema, pengine zilikuwa zimepevuka. Hata kama hazikuwa zimepevuka, ni nani alitakiwa kuzipevusha kama si Waafrika wenyewe? Kwa mfano, kama umesoma Facing Mount Kenya ya Mzee Jomo Kenyatta. Walikuwa na matambiko yao waliyofanya. Nafikiri udugu na umoja wa Maumau ulileta na msukumo mkubwa sana wa kitaifa uliotokana na mtazamo wa kiimani wa Kikikuyu. SWALI: Kabla ya vita baina ya waumini na wasioamini pamoja na mashetani kuzuka, Zirani anaota ndoto ambapo mzee anamweleza kwamba aikubali tu ulimwengu kama unavyoumbwa, asijaribu kuufahamu (tz ZZ Mzingo wa Vita III). Baadaye Zirani anaifikiria sana ndoto hiyo. Je, katika yaliyosemwa na mzee, yamo maoni ya mwandishi mwenyewe? JIBU: Kwa kiwango fulani. Kwa sababu ya tatizo la imani yenyewe, halafu tatizo hasa la kuwa kwetu ulimwenguni, existence, ni fumbo gumu. Na, kwamba tulifikirie; ni lazima tulifikirie, kwa sababu tupo. Tulifikirieje? Hilo ndilo swali. Na tulifikirieje ili lituathirije? Hilo ndilo tatizo. Lakini kwamba tukilifikiria tutapata ufumbuzi wake, ni vigumu kutabiri. Ndiyo maana ninafananisha na sisimizi aliyeko kwenye msitu wa nywele kwenye kichwa cha mtu. Sisimizi anapoupanda ule unywele anauona kama mnazi. Halafu eti umwulize, “Mtu huyu mwenye hiki kichwa ana sura nzuri au mbaya?” (vicheko vikubwa) Atakuwa hakuelewi kabisa! Hata umwelezeje; hata utumie karne ngapi kumweleza hatakuelewa kwamba haiba ya mtu huyo ikoje. Kwake yeye haielezeki. Ndivyo yule mzee anavyomweleza yule mwota ndoto, kwamba: “Ni heri tu mlikubali umbile lenu. Mkubali uumbwa wenu. Na mnaweza kuamua kuabudu. Kuabudu kusudi lake si kwamba unamtukuza yule aitwaye muumba. Isiwe hiyo! Kusudi lisiwe kumtukuza ili mpewe zawadi ya mbingu au pepo. Hapana. Kusudi ni kwamba muwe na mfumo. Muweze kuwa na jinsi ya kuyarahishisha maisha yenu, ili kuwa kwenu ulimwenguni katika muda huu mfupi kupate umaana na urahisi. Muweze kuendesha maisha yenu bila vikwazo, na yawe na furaha angalau. Kusiwe na matatizo mengi kama vita na kadhalika. SWALI: Zaidi ya hayo, mwisho mwa riwaya Zirani anaishia kumwita Mungu (tz ZZ Kiama III). Je, ulitaka kusema kwamba binadamu hata akijitahidi kwa nguvu zake zote kumkana Mungu, atakapokuwa hatarini ndipo atakaporudi kwake? JIBU: Unajua swali hilo aliniuliza Profesa Madumulla. Akaniambia “Bwana wewe, umeianza riwaya yako vizuri”. Hata Privatus Karugendo anayeandika makala kwenye gazeti la Rai, kama Madumulla, wote wakaniambia, “Wewe umeanza vizuri hiyo riwaya, sisi tunajua wewe ni mwanamapinduzi au mfuasi wa ki- Marx, sasa imekuwaje kule mwishoni ukarudi kwenye idealism tena? Umejisaliti kwa kurudi kwenye idealism”. Nikamwambia Privatus Karugendo ambaye ni Padri, “Bwana, unajua? Tatizo la mwanadamu ni kwamba anakufa. Halafu anapokufa hatima ya hapo baada ya kufa inaweza kuwa ni wazi kwamba ni sufuri, eh?” Sasa hiyo sufuri yenyewe ni kioja! Yaani ile hali kwamba utakuwa sufuri. Unaweza kufikiria? Wewe kuwa sufuri? Inakera! Hakika inasumbua akili! Muuliza swali: Nitakuwa sufuri tu! Minyoo watanila. Likija bomu hapa likalipuka. Baah! Kisha ghafla ukatoweka! Sasa tunapofika hapo hakuna mwenye jawabu. Hata sasa hivi ingawa tunasema unazaliwa na utakufa, basi, hakuna aina yoyote ya kuwepo baada ya mauti, lakini sasa kuikaribia ile hali ya kuwa sufuri yenyewe inaudhi sana. Inakera sana ukiifikiria. Halafu kufikiria kuwemo kwenye hali ile ya sufuri yenyewe inaliza au siyo? (vicheko) Muuliza Swali: Mimi nawafikiria minyoo. Watakuja na kunila. Jibu: Unamkumbuka yule Meursault, mhusika mkuu wa The Outsider ya Albert Camus, mwanzoni hilo jambo la kifo lilikuwa halimsumbui sana lakini alipokuwa anaenda kunyongwa, sasa anakaribia kitanzi, ikawa inamsumbua. (NB: Sahihisho: Mersault alihukumiwa kukatwa kichwa)Mwanzoni alikubali kwamba hajali, ni mto-kujali, lakini alipozidi kukaribia kifo… Kwanza, mchungaji akamwendea kutaka amsalishe. Akamfukuzia zake mbali kama pia alivyofanya Bigger Thomas wa The Native Son ya Richard Wright. Akamwambia “Kwenda zako sitaki kukusikia!” Unaona? Ni kwamba haoni sababu. Anaamini kwamba hakuna uwepo wa aina yoyote baada ya kifo, la sivyo asingemkataa mchungaji. Kama angekuwa muumini kweli, si angekubali aendelee kusalishwa ili akiri tu makosa yake, aweze kuingia mbinguni? Sasa amejua kwamba hakuna mbingu. Lakini bado ilikuwa ni tatizo kwake mpaka mwisho wa ile riwaya kwamba anaikaribia ile hali ya kuwa sufuri. Hiyo ni tatizo tupu! Sasa unaposema kwenye Ziraili Na Zirani alimwita Mungu mwishoni. Mungu si lazima awe Mungu Mkristo, Mungu Mwislamu au mungu kitu chochote. Maana yangu ya maneno: “Ni mimi kwa kuwa ni mimi” niliyonukuu kwenye Ziraili na Zirani ambayo nimeyatoa kwenye Biblia ni hilo fumbo lisilo na utatuzi. Ile hofu ya kioja cha kuikaribia hali ya usufuri ipo ama kwa kuitabiri kwamba: mbele kuna maisha, au kwa jinsi yoyote ile; au kwamba ni sifuri yenyewe kabisa, hofu hiyo ipo kwa kila mtu. Kwa hiyo tuikubali kwamba ipo na tuwe na mfumo, au jinsi yoyote ya kukabiliana nayo bila kufadhaika kiasi cha kuweza kuiruhusu iturudie na kutudhuru. Ikiturudia ina maana watu wanapoukaribia uzee wataweza kuanza fujo au kupiga watu ovyoovyo tu, kwa sababu wanajua wanakufa. Wanaweza kuleta maafa makubwa zaidi. Kwa hiyo ni lazima tuwe na kitu, mfumo ambao utaipoza hali kama hiyo. SWALI: Katika riwaya yako tunamkuta mwanafalsafa Voltaire akizungumza juu ya kuwepo kwa Mungu mmoja tu, juu ya uraia wa kidunia na kuwa dunia ni kama kijiji kimoja tu (tz ZZ Motoni VI). Je, hapo Voltaire amekuwa mtabiri wa uwezekano wa utandawazi kuwa kitu kizuri? JIBU: (vicheko vikubwa) Uwepo utandawazi usiwepo – hata huo utandawazi tulio nao sasa hivi unawezekana kwa ufanisi wake zaidi kutokana na mawasiliano ambayo yamerahisishwa sasa. Lakini imerahisishwa kwa kiwango gani? Kwa sababu inategemea kiwango cha sayansi kilichofikiwa. Kwa mfano inasemekana baadaye watu wataweza kuwepo mahala pawili kwa wakati mmoja. Pengine ngazi hiyo itafikika. Lakini tangu hapo, dunia ni kijiji kimoja. Hata kabla ya haya maendeleo ya mawasiliano kufikiwa. Bado dunia ilikuwa ni kijiji kimoja. Ila hatujawa na muda wa kukitazama kama kijiji kimoja! Kwani dunia ina ukubwa gani wa ajabu kama utafikiria ukubwa wa cosmos au hata wa hii mbingu moja (galaxy) wanajimu wanayoita Milky Way? Kadunia ni kadogo tu! Ni kwamba tulikuwa hatujaitazama dunia kwa udogo huo. Sasa hivi tunapata nafasi ya kuweza kuitazama kama kitu kimoja. Unaposema Voltaire alikuwa mtabiri – hapakuwa na hata haja ya utabiri kwa sababu tayari dunia ilikuwa kama kijiji kimoja, muda mrefu tu. Ila ufahamu wa wanadamu hapo kale haukuwa na macho au nyenzo za kuiona hivyo…. Kwa mfano leo ukimwuliza simba aliyeko Manyara kuhusu simba aliyeko India habari zake (kicheko) – kwake simba kitakuwa ni kitu cha ajabu sana. Lakini kwa sisi wanadamu si tunafahamu kwamba wapo simba huko India? Kwa hiyo kama simba wa India ana matatizo kama ugonjwa sisi tunaweza kuushughulikia kama wanadamu kwa kuwa tumewazidi wanyama. Kwa hiyo kulingana na kiwango cha ufahamu hata kabla ya huyo Voltaire, kulikuwa na umuhimu wa dunia kuwa kijiji kimoja. Mhusika Ahab wa Moby Dick ya Herman Melville, kuna mahali anapolitukana jua akiliambia: “Mimi Bwana namtafuta yule nyangumi mweupe, namtafuta Moby Dick, wewe nina uhakika kwamba, hapo alipo unamwona– kwa nini huniambii?” Maneno yake hakuyapanga kwa namna hii, lakini maana yake ilikuwa kwamba, pale alipokuwepo, hakika jua lilikuwa linamwona yeye, na yule nyangumi alipokuwepo pia jua lilikuwa linamwona. Lakini yeye Ahab alikuwa na upungufu wa kibinadamu kutoweza kumwona huyo nyangumi akiwa mbali. Jua lingeweza kumwambia kwamba yuko wapi yule nyangumi. Kwa hiyo lile suala la imani linakuja tena kwamba tunatamani kigekuwepo kiumbe chenye uweza mkuu ambacho kingeweza kuitazama dunia kama kijiji kimoja. Hata hapo nyuma, miaka mingi iliyopita, tamaa ya kuwepo kwa kiumbe mkuu ambaye angetusimamia bila shaka ilikuwepo kwa matumaini ya yeye kuuongoza huo ukijiji wetu mmoja. Hii ni dhana ngumu mno kuiepuka hata kama haiwezi kuthibitishwa. SWALI: Nafasi ya wanawake katika riwaya yako ni ndogo. Unawataja akina Clara, Roza na Emma (tz ZZ Mzingo wa Vita II) ambao hapo baadaye tunaelezwa kwamba ni Clara Zetkin, Roza Luxemburg na Emma Goldman (tz hapo IV). Walakini, wanawake hao hawachukui nafasi kubwa kama mashujaa wa kiume. Je, unafikiri mikinzano ya kifalsafa na ya kidini ilitokea kama ilivyotokea kwa sababu uwingi wa wahusika wakuu walikuwa wanaume? JIBU: Pale nyumbani kuna kitabu sijakimaliza kukisoma. Kinaitwa Gender and Genius2, Kimeandikwa na mwanamke mmoja wa Kiingereza. Ni kazi ambayo imejaribu kuchukua tatizo la hulka ya watu kuhusu vipaji. Watu wanasema uwezo wa kufikiri kwa kiwango kikubwa uko kwa wanaume pekee. Mwandishi wa kitabu hicho anapinga tabia hii. Kwa mfano anasema kwamba mke wa Beethoven alikuwa hodari sana wa kupiga muziki kwenye piano. Lakini amefunikwa, hakujitokeza. Kivuli cha Beethoven kilimfunika. Kumbe na mke wa Beethoven alikuwa genius wa kiwango chake. Sasa kwa nini vipaji vikubwa vinapozungumziwa mwanamke hapewi uzito, hata kama alijitokeza kwa upungufu kiasi katika mazingira ya magwiji? Au tumchukue John Stuart Mill. Mke wake amechangia sana kwenye kazi zake, na katika maendeleo yake ya kifikra. Hata kwenye utangulizi wa kazi zake amemtaja. Kwa mfano kwenye utangulizi wa kitabu chake On Liberty, amemsifia mke wake kwamba amechangia kwa kiasi kikubwa kujadiliana naye kuhusu maoni yake. Lakini heshima inayotolewa kwa mchango wa yule mwanamke ni ndogo. Sifa yote anapewa John Stuart Mill mwenyewe. Tuendelee sasa kuhusu swali kako. SWALI: Hili ni suala la genius. Lakini sasa ukiangalia suala la mikinzano na vita …..? JIBU: Vita ni ya wanaume, kwa muda mrefu sana. Nikizungumza vita, na nikizungumza mashujaa wa vita, nazungumza wanaume. Na ndio utamaduni wa wanadamu kwa muda mrefu sana. Mwanamke hutajwa kwa uzuri wake, hasa kwa Waingereza. Kama anavyoukejeli George Bernard Shaw katika tamthilia zake. Anazungumzia uzuri wa mwanamke wa Kiingereza wa enzi hizo alizoandika tamthilia hizo kwamba ni ule unyongenyonge wake na ulimbwende wake. Unaona? Hazungumzii ushupavu. SWALI: Lakini kulikuwa na wale wapiganaji wa Amazones… JIBU: Anaposifiwa mwanamke wa aina hiyo, anasifiwa kwa ubaya. “Mbaya kama amazones” yaani….. SWALI: Wanasifiwa kivita pia, kwa sababu walikuwa wapiganaji hodari sana kama watu wanavyosema. Lakini niliuliza kwamba kama unafikiri mikinzano ya kifalsafa na ya kidini ilitokea kama ilivyotokea kwa sababu uwingi wa wahusika wakuu walikuwa wanaume? JIBU: Si kwa sababu uwingi wa wahusika wakuu walikuwa wanaume ndiyo sababu ya kuwepo kwa ile mikinzano, ila mikinzano ilikuwepo, lakini wanawake hawakuhusishwa au hawakujihusisha nayo kwa wingi kama waliyojihusisha wanaume. SWALI: Tofauti na riwaya ya Nagona ya Euphrase Kezilahabi, umeingiza zaidi nafasi na mchango wa Waafrika katika historia ya kitamaduni, kisiasa na kifalsafa katika riwaya yako. Umeyataja makundi mbalimbali ya Kiafrika kama Wayoruba, Wazulu, Waashanti, Wakamba, Wagikuyu, Wasambaa na Waluhya na mashujaa kama Fanon, Nkrumah, Lumumba, Mondlane, Machel, Cabral na Neto. Umekusudia nini katika kufanya hivyo? JIBU: Hata wao walishiriki. Kwa muda mrefu tunapozungumzia mtazamo wa mwanadamu, tunamtazama mwanadamu kwa kutotutambua sisi Waafrika. Siku hizi tunaanza kuitazama dunia kwa mitazamo ya ki-mashariki na ki-magharibi. Na kwa kweli huwa tunaanza kutazama jambo kwa mtazamo wa ki-magharibi, halafu tunasema ngoja pia tuliangalie kwa mtazamo wa ki-mashariki. Ni mara chache unapoona jambo linatazamwa kwa mtazamo wa Amerika ya kusini, mtazamo wa ki-Australia, na pia ni mara chache tunapouhusisha mtazamo wa ki-Afrika. Kwa hiyo riwaya hii imeandikwa na mtu ambaye yuko Afrika, na hawezi kusahau kuwataja wale ambao wanahusika katika mtazamo wa ki-Afrika wa jambo linalojadiliwa. SWALI: Kuna sehemu chache tu katika riwaya yako zinazoonesha kwamba zina uhusiano fulani na mazingira ya Tanzania, kwa mfano kutaja kwamba kisiwa cha Nguu kiko karibu na kisiwa cha Mafia (tz ZZ Duniani (I) II), au kutaja chakula aina ya kachumbari katika wimbo fulani (tz ZZ Zirani IV). Tukiangalia uchache wa madokezo ya namna hiyo, je, ulifanya hivyo makusudi? JIBU: Kachumbali imetumika kwenye hizo nyimbo kwa ajili tu ya kuichangamsha lugha. Nisingesema goulash soup kwa sababu sijui supu ya goulash inavyotengenezwa. Halafu, kama kweli shetani yupo, basi angependa kachumbari vilevile. (kicheko kikubwa) Ukiwa Afrika, Lutz, ukimpa kachumbari ataifurahia tu, kama watu wengine walioko Afrika wanavyoifurahia. (kicheko kikubwa) Lakini akienda Hungaria atapenda goulash soup, kwa sababu ni chakula cha huko. Au siyo? (kicheko) SWALI: Kwa hiyo yuko universal. JIBU: Enhe, kama kweli shetani yuko, basi yuko universal. (kicheko) Sasa kisiwa cha Nguu nimekitaja kwa sababu gani? Ni cha kufikirika. Kama umekikuta ulipokwenda Tanga basi ni vizuri lakini ni cha kubuni katika hiyo riwaya. Siwezi kwenda mbali, ni cha kubuni. Bahati nzuri tu kilihusiana na neno ‘Mafia’. Kuna ‘Mafia’ ya Waitaliano, ile Mafia ya Sicilia. Lakini ‘Mafia’ maana yangu ni ile Mafia ya hapa Tanzania. Labda ungeniuliza swali la vita ya Mwendashari na Sharihaswa. Muulizaji: Lingalikuja hilo swali. Sasa hilo lina uhusiano wa karibu sana na Tanzania, vita walivyovipigana Watanzania na Waganda. Lakini nayo pia nimeitumia kwa sitiari nikimaanisha ingeweza kutokea popote duniani. SWALI:Unajua nimefikiri nini? Nimefikiri unadokeza vita vya Ethiopia na Eritrea. JIBU: Na maana hiyo hiyo. Kwa sababu kichwani nilipoandika vita ya Mwendashari na Sharihaswa nilikuwa nafikiria vita ya Kuwait na Iraq. SWALI:Umedokeza hivi? JIBU: Mle hamna majina ya Kuwait wala Iraq. Kwenye hiyo riwaya hayamo, lakini nataka tu nikuonyeshe kwamba vita ya namna hiyo ndiyo iliyopo kokote kwingi. Kwa mfano vita ya Kuwait na Iraq ilisababisha maangamizi ya watu wa Iraqi. Vita ya Uganda na Tanzania, au vita hiyo unayosema, ya Eritrea na Ethiopia, au vita vya Yugoslavia, Kosovo nkt, – si vyote vilishusha gharika ya mabomu ya Marekani? Kwa hiyo ile vita ya Mwendashari na Sharihaswa ni symbolic. Maana ya Mwendashari ni mtu anayeendesha maisha kwa shari, maisha yake yanaongozwa na shari. Na maana ya jina la yule mhusika mwingine, Sharihaswa ni: “Ukitaka shari, mimi pia ninayo haswahaswa”. SWALI: Lakini kudokeza Tanzania ya wakati ule wa Mwalimu Nyerere na Uganda wa Idi Amin, kuwaita Mwendashari na Sharihaswa ki-spontaneously inanishangaza. JIBU: Aha. Ni kweli Nyerere alikuwa na kusudi jema kabisa. Lakini Idi Amin alivamia. Alipovamia majeshi yetu yakampiga. Sababu kulikuwa na kutoelewana baina ya Tanzania na serikali ya Idi Amin kwa muda mrefu. Lakini pamoja na kwamba Idi Amin alikuwa mwendashari na Nyerere alikuwa anajibu tu, ule uchokozi – mtu aliyekuweko pale Bukoba anapopatwa na adhabu ya vita ile, hajui hizo historia za kutoelewana kwa watawala; hajui hayo masuala ya kisiasa yaliyosababisha. Wewe unapoisikia vita ya Kuwait na Iraq kwenye magazeti au kwenye televisheni, ni tofauti na mtu, mzee kijijini pale Kuwait anapoangamizwa na mshindo wa mabomu! Yeye hajui ubora wa hao watawala, hajui uadilifu wao, haujui. Yeye anachojua ni kwamba ndege zilikuja zikawaua. Basi. SWALI: Je, ulipobuni nchi ya Bloblaha ulikusudia kuudokeza Uganda? JIBU: Kuna nchi ya Bloblaha ya Mwendashari, na nchi nyingine Porojoro ya Sharihaswa. Sifa za nchi hizi, kiuchumi, ni kwamba wale wengine walikuwa hodari sana wa kuongea, lakini hawajui kutekeleza. Halafu wale wengine walikuwa na neema ingawaje neema hiyo ilikuwa mikononi mwa wachache. Maana yake mojawapo ni zile nchi za kiafrika zilizodai ni za kijamaa ambazo zilikuwa zinaweza tu kuhubiri mambo ya mapinduzi na nini, lakini hawana lolote, kiutekelezaji. Lakini wale wengine wakaamua heri kuwa mabepari kabisa. Na wakawa wanaendesha mambo yao kibepari. Kwa hiyo hao walikuwa wana shibe na wale wa Bloblaha waliishia kwenye bla-bla. SWALI:Kwa nini umetumia ‘Fuvu la Kichwa’ kama jina la mahali fulani (tz ZZ Mzingo wa Vita VIII)? JIBU : Katika riwaya ‘Fuvu la Kichwa’ inawakilisha Golgota. Yaani mahali Yesu alipouliwa. Ndiyo sababu ile jiografia ya kuzimu umbali wake umeelekezwa kwa kutumia umbali wa muda kutoka ‘Fuvu la Kichwa’. Kama historia isemavyo ‘before Christ (B.C.)’ na ‘after Christ (A.D.)’. ‘Fuvu la Kichwa’ imetumika kama kirejeo cha muda na umbali baina ya matukio ya kihistoria katika vita ile ya kwenye riwaya. Katika ile jiografia ya kuzimu, kila kitu pale ni istiari, kwa mfano kile kitivo cha Aquinas, ni kitivo cha falsafa za Thomas Aquinus. Kuna sehemu inayataja majabali matatu ambayo ni istiari ya matukio ya kihistoria ya mji wa Makka au ngome ya Uislamu. Kwa hiyo kama kuna sehemu inaitwa ‘Fuvu’ inahusiana na kalenda ya sasa inayotambua kuanza kwa Ukristo kama kirejeo cha historia ya ulimwengu. SWALI: Ingawa maudhui ya riwaya yako ni mazitomazito, nafasi ya ucheshi pia imo, kwa mfano unapomchora Lusifa (tz ZZ Ziraini II 38) au mwishowe ambao Lusifa anakiri kwamba amechoka na kazi ya ushetani na kuomba apewe kazi nyingine. Unaonaje wewe mwenyewe nafasi ya ucheshi katika riwaya yako? JIBU: Nimekusudia. Kwa sababu ni lazima kisa kifurahishe, mkasa uhuzunishe. Ni lazima watu wacheke. Na mwingine anachekesha, kwa sababu hiyo nafasi ya Lusifa kuitwa shetani, na Gabrieli kuitwa mtakatifu – ni arbitrary. Kwa hiyo ni kichekesho kwamba wajibu huo wa kimalaika unapotazamwa kwenye maisha ya watu, huhusishwa kwelikweli na ubaya au wema. Ziraili wanamwogopa, Gabrieli wanampenda na Lusifa wanamchukia. Katika ile sura ya Motoni, kwenye zile hotuba kuna mhusika anayesema: “maovu ya mwanadamu ni mengi, na yamekuwa ni ya muda mrefu. Kama tungemlaumu shetani, tutazidi kuonyesha upumbavu wetu sisi wenyewe. Kwa sababu mwovu siyo shetani ila ni sisi wenyewe”. SWALI: Fantasia inachukua nafasi kubwa katika riwaya hiyo vile kwamba sehemu nyingine zinafanana na ngano au fasihi ya kubuni ya kisayansi, kwa mfano jinsi unavyomchora Alalu (tz ZZ Zirani III). Msukumo au kariha ya kuandika namna hiyo umeipata wapi? JIBU: Mimi nadhani fantasia iliyoniathiri zaidi kwenye hii kazi ni hizo mbili ya Dante na ya Milton. Hii fantasia ya ngano za kisayansi nimezisoma zamani sana. Habari za kwenda kwenye mwezi, za kwenda katikati ya dunia, Jules Verne, The Blue Planet. Unajua mimi, ujana wangu, riwaya ilikuwa ni kimbilio langu. Nilikuwa nazipenda riwaya hizi. Kwa hiyo sijui jinsi gani zimeniathiri. Sijui. Lakini nakubali kwamba katika kazi hii nimeathiriwa na fantasy ya Dante ambayo hata hivi sasa bado si hodari sana kuielewa. Nilipoisoma, niliipita kama mtu anayepita gizani, mengine anayachukua, mengine anayaacha. Hivyo hivyo. Sasa kwa mfano nilivyosimulia kuhusu kulivyo mbinguni inaweza kuwa ni kama kusoma riwaya ya ki – sayansi: Man On Mars. Zaidi ni shetani ndio niliowachora: Nilivyokuwa mtoto nilisoma kitabu kilichoitwa Moyo wa Mtu. Nilikisoma nikiwa mtoto wa miaka kama minane. Nilikipenda sana hicho kitabu. Mwandishi alichora moyo wa mtu ulivyoathiriwa na Ibilisi. Kilionyesha kwamba humo kwenye moyo wa mtu kuna mashetani wa aina nyingi. Kuna shetani wa uvivu, kuna shetani wa pesa, kuna shetani wa uasherati, ulevi na kila uovu. Sasa tuliposoma kitabu hicho tulikuwa tunaambiana “Ah! Wewe unafanana na huyu!” Tena kiliandikwa kwa lugha ya Kisambaa. Siyo Kiswahili. Bila shaka nakala ile iliyoko kule kwetu ni tafsiri. Kwa hiyo bila shaka iko nakala ya Kijerumani ambako ndiko ilipo ngome ya Waluteri. Ukitazama katika ile sura inayozungumzia maandalizi ya kwenda vitani. Wanakuja aina mbalimbali za shetani. Anakuja Beelzebabu, Maimoni, , Asmodeus na kimada wake Lilitu. Hizo ni baadhi za sitiari za ushetani. Kwa hiyo fantasia hii imeathiriwa na ile kumbukumbu ya wakati ule. SWALI: Kejeli na tashtiti pia zinachukua nafasi isiyo ndogo katika riwaya yako. Kwa mfano tunasoma hoja au swali lifuatalo: Je, kuumbwa kwa binadamu mwingine kutafanikiwa zaidi (tz ZZ Sherehe 11)? Unaonaje nafasi ya kejeli na tashtiti katika uandishi wako na katika fasihi kwa ujumla? JIBU: Dawa nzuri ya utata ni kicheko. Kwa hiyo ukicheka hata lile lililokuwa gumu mwishoni unaliona “Ah! Basi tu, limeshapita” Sisi Waafrika, hususan sisi Watanzania, kuna kitu kinaitwa utani. Ukiwa na msiba wanakuja watani wako, wanaanza mazungumzo mengine ya pembeni kabisa yasiyohusiana na ule msiba. Nyote mnaanza kucheka na hatimaye hata ule uchungu wa msiba unatoweka. Kwa hiyo kicheko ni kitu kizuri, ni kitulizo cha maisha. Kejeli na ucheshi katika sanaa ni kitu kizuri, kwa sababu kinamfanya msomaji au, kwa ujumla, mwanadamu ayatazame mambo kwa kejeli. Ni kichefuchefu ukiangalia kwamba unazaliwa, unaishi kwa miaka hamsini au mia moja kisha unakufa! Ni heri ucheke, usipocheka utapata matatizo, mfadhaiko! SWALI: Mwisho mwa sura ambapo Zirani anafunzwa katika kambi ya mashetani, yanarudiwa yaliyoelezwa kabla ya hapo (tz ZZ Zirani IV). Kwa upande wa kisanaa haivutii sana kama sauti ya msimulizi inamweleza msomaji maudhui yaliyosawiriwa kabla. Kwa nini uliiandika hvyo? JIBU: Zirani alipelekwa kule kwa makusudi ya kujua kinachoendelea kwenye kambi ya mashetani. Kiistiari, shetani akimweleza Zirani pia anakuelezea wewe, au mimi. Zirani pale anamwakilisha mwanadamu. Shetani anamwambia mwanadamu anavyowaona mashetani, na mashetani wanavyomwona mwanadamu. Kwa hiyo baada ya yale mambo ambayo mashetani walikuwa wanamhubiria Zirani, kila shetani alivyomwambia kwamba wewe uko hivyo, uko hivyo, uko hivyo, na kumsisitizia kwamba alipewa majukumu ambayo hukuyastahili kabisa kuyapewa. Wakamwambia kwamba hapakuwa na haja ya kuwa na mtu kama yeye. Baada ya pale, ni kama ufupisho tu. Yale yote yaliyoongelewa sehemu mbalimbali ufupisho wake ni huu hapa. Zirani aliyatolea muhutasari. Kwa sababu kila mmoja alitamka maoni yake ki-vyake, ule muhutasari ulitakiwa uwepo ili ujenge ujumla wa hoja kuhusu mambo yote yaliyojadiliwa. Jinsi Zirani alivyoelimika na kubadilishwa na hoja hizo katika kuwepo kwenye kambi ile. Kwa hiyo kusudi lilikuwla hilo. Kwa msomaji ambaye anataka kupata ile burduani tu, anaweza kukereka. Lakini kama anafuatisha umantiki wa hoja na matukio kutoka mwanzo, ule muhutasari ni muhimu kuonyesha kambi ile ilivyochangia katika kumjenga mhusika Zirani. SWALI: Katika sehemu kadhaa za riwaya hiyo tunakuta mashairi na nyimbo ( tz ZZ Matukio 5; Mbingu 10;12; Ziraili 28; Zirani 42-43;52; Motoni 90-92; 109-110; Duniani (1) 133-135; Mzingo wa Vita 145; 153; 156-157; 178; 183-184; Mtingisho wa Vita 187-189; 194-196; 200-201; 205-206; Kiama 212-218;221-223;226). Ulikusudia nini kwa kuingiza aina hii nyingine ya matini katika nathari? JIBU: Kuhusu Ushairi- katika hii epic ya Ziraili na Zirani. Ukiangalia sehemu nyingi sana, ingawaje ziko katika nathari, ukizikata unapata mashairi pia. Kusudi ni kwamba, kwa kuwa ni epic, visifa vya jambo lililotokea ni lazima viwe na vichocheo vya utamu wa lugha. Lugha iwe na hamasa, iwe na vibwagizo, ile sanaa ya kiepic inazidi kuimarika pakiwa na ushairi kama huo. Ukieleza kwa nathari ya kawaida tu, masimulizi yanakosa msukumo, yanaanza kuchosha. Lakini hizi nyimbo-nyimbo, vibwagizo-vibwagizo vinasaidia kuipa ule msukumo wa ki-epic. Ningekaa chini ningeiandika kama utenzi. Lakini siku hizi watu wameanza kuchoka kusoma utenzi. Kwa hiyo ilikuwa tu ni mbinu ambayo niliona ingeongeza ule msukumo wa kisanii. SWALI: Kwa mtazamo fulani tunaweza kusema kwamba Ziraili na Zirani inaweza kusomwa kama maendelezo ya riwaya fupi Nagona ya Euphrase Kezilahabi. Katika riwaya zote mbili, falsafa inayojitokeza zaidi ni falsafa ya udhanaishi. Kwa mfano Ziraili anatamka yafuatayo: “Wanadamu wanazaliana mno na wanachelewa kufa. Karibuni dunia itafurika” ( ZZ Ziraili 31). Kuhusiana na hilo nilipewa hoja na mtaalam wa Chuo Kikuu cha Dar-es-salaama,.Alisema ile dhana ya dunia kufurika na wanadamu kuzalianan mno – anaiona ni ubeuzi, kwa sababu tatizo la msingi la biandamu ni ugawaji mali usio sawa duniani. Ugawaji malii duniani ungekuwa sawa, haingekuwa shida kwamba tuko binadamu milioni sita ua saba au nane. Unaonaje suala hili? JIBU: Kwa kweli hili sikubaliani naye. Tutake tusitake, tukikataa kumheshimu Malthus, dunia inaweza kujaa. Si unajua nadharia za Malthus? Kwamba jamii ikiwa mahali fulani inaweza kujitosheleza kwa muda fulani tu, lakini kama idadi yao itaongezeka mno, uzalishaji wa mahitaji ya ile jamii utafika upeo, ambao ile idadi yao ikizidi, itavuka ule upeo, ile optimal balance. Ule uwiano wa uzalishaji na mahitaji utakuwa umevurugwa, hakutakuwa na mlingano tena. Kwa hiyo jinsi idadi inavyoongezeka itaharibu uwiano, itasababisha imbalance ya mahitaji na kiwango cha kuyatosheleza. Hapo ile jamii yenyewe italazimika kujipanga upya, vinginevyo ile idadi ya watu ni lazima ipungue ili mfumo uweze kudumu. Dunia ina mipaka. Ukisema haiwezi kujaa ni kama isingekuwa na mipaka, hapo tungeweza kusema hivyo. Lakini dunia ina mipaka ya anga na ardhi. Kwa hiyo ni lazima inajaa. Kuhusu tatizo la wanadamu kujaa- dunia haitajazwa na watu wenyewe. Pia itajazwa na matumizi yao, vitu wanavyotoa na vitu wanavyoharibu. Hata kule kukata miti kuna athari kwa sababu tuko wengi. Zamani walikuwa hawakati miti mno, lakini sasa tumeongezeka kwa hiyo miti inazidi kupungua. Au magari kutoa moshi wenye sumu kwenye mazingira ya dunia. Kwa hiyo dunia inajaa. Sikubaliani naye kwamba dunia haijai. SWALI: Ndiyo. Sasa tukiyachukulia maoni haya synchronical bila kuangali mbele. Labda amekusudia hivyo. Tukisema “sawa, sasa hivi tuko milioni sita, na tatizo la msingi zaidi ni ugawaji usio sawa wa mali…” JIBU: Ahaa! Basi hiyo kauli ingewekewa neno zaidi. Yaani kwamba, tatizo la msingi zaidi kwa sasa siyo kuwepo kwa wingi wa watu. Ila tatizo la sasa hivi la msingi ni ule ugawaji wa kilichopo. Hapo nakubaliana naye. Hilo ni neno zaidi, kwamba kujaa anakomaanisha ni mlinganisho. SWALI: Eee. Lakini mtaalam huyu alikusudia zaidi kuukosoa uthanaishi kwa ujumla, kwa sababu… JIBU:….Akikosoa udhanaishi, kama hii ndiyo hoja yake kwamba ni matokeo ya ugawaji potofu wa mali za dunia, sio uwingi wa idadi ya watu- hiyo mimi naikataa kwa bababu phenomeonon ya udhanaishi haisababishwi na dhiki au mgawanyo potofu wa mali peke yake. Phenomenon ya udhanaishi inahusiana na mwanadamu kujitambua hatima yake, upeo wake na kadhalika. Hoja kwamba wingi wa watu hautafika mahala ambapo tutashindwa kuongezeka jibu lake ni la kisayansi na halina haja ya kubishana… Nenda tu kwa mfano Hongkong. Kisiwa kimejaa. Kutafika mahala ambapo uwingi wa watu utaathiri maisha yao hata kama wakigawana sawaswa majumba na vitu vilivyomo. SWALI: Unaonaje athari ya riwaya ya Nagona kwa uandishi wa Ziraili na Zirani? JIBU: Sikuwa nimeisoma hiyo Nagona. Nimeisoma juzi. SWALI: Mojawapo ya tofauti baina ya riwaya hizo mbilli ni kwamba Ziraili na Zirani inachunguza historia ya falsafa kwa undani zaidi. Tofauti nyingine ni kwamba sauti ya masimulizi inasikika zaidi kumweleza msomaji ujumbe. Kwa ujumla wewe mwenyewe unaoje ‘ udugu’ baina ya riwaya hizo mbili, au labda unasema hamna ‘udugu’ wowote? JIBU: Udugu unaweza uwepo, unaweza usiwepo. Kwa sababu hata hivyo Nagona nimeisoma juzi, kuna kwingi ambako ninakwama. Nagona ni riwaya ngumu. Ni jamii ya riwaya za kidhanaishi kama The Fall ya Camus au Nausea ya Sartre. Epic ya Ziraili na Zirani, kusudi lake ni kuonyesha kukua kwa mtazamo wa mwanadamu, kukua kwa kosmolojia ya mwanadamu hadi alivyofika kwenye kiwango cha dialectical materialism. Lakini pia maoni ya wahusika ambao bila kukusudia wanawakilisha maoni yangu kama mwandishi, maoni ya wahusika mbalimbali kuhusu hizo ngazi za kukua kwa kosmolojia hiyo, halafu hatima ya maoni yangu mimi mwenyewe, limejitokeza zaidi kwenye sura za mwisho ambazo Zirani anaota ndoto. Kwa hiyo Nagona, nilivyoisoma, ninapata hisia kama nilivyosoma Nausea ya Sartre. Kwa sababu anaanza gizani, anaishia gizani. Na lile giza limo, kote liko giza, kwa sababu kila wakati anaanza na sentesi “Sijui nilikuwa wapi na nilikuwa si-, nilikuwa si-, Yaani kuna ile vagueness. Ni nyingi mno. Kwa hiyo hamna mwanga. Hamna mwanga kwenye Nagona. Hakuna mwanga. Ni giza kutoka mwanzo mpaka mwisho. Si giza tu kwa macho, ni giza hata kwa zile dhana zilizomo mle ndani. SWALI: Isipokuwa kuna ‘askari wa mwanga’ kama motifu…. JIBU: Enhee! Halafu tena hata hao ‘askari wa mwanga’ wanapojitokeza hawana nguvu ya kutoa mwanga wa kutosha. Wale ‘askari wa mwanga’ wenyewe, dhana yake, walivyowekwa mle, wanakuwa wenyewe pia ni abstract, na ile abstractness yake yenyewe inazidi kuongeza giza tena. SWALI: Lakini huyu mhusika msimulizi anapata mwanga mwishoni mwa Mzingile, kwa hiyo ingenivutia sana tukiweza kuzungumza juu ya Mzingile.. JIBU: Mzingile sikusoma. Lakini ninalosema ni kwamba: mimi nilivyosoma Nagona, naona hili gizagiza na vagueness na utusitusi. Kwa sababu liko kutoka mwanzo mpaka mwisho. Nadhani pengine mwandishi alikuwa anataka atuonyeshe kwamba maisha ni utusitusi, ni vague, ni kama ilivyo kwenye Nausea. Ingawa niliisoma Nausea nilipokuwa kijana, lakini nataka niisome upya katika ukubwa. Pale ujanani niliipenda tu kwa tabia za kijana kujaribu mambo magumu lakini kusema kweli nilielewa kidogo mno. Ila niliona hilohilo giza. Kwa hiyo hata kwenye Nagona, ule utusitusi unaanza kuwepo kutoka mwanzo mpaka mwisho. Sasa ndiyo kusudi la mwandishi la kutuonyesha ule utusitusi? Kwamba maisha ni utusitusi? Kama ni hilo, ni vizuri tu, hamna tatizo. Mimi, kusudi la Ziraili na Zirani ni mwanga, kutoka mwanzo kila ukiangalia matukio yanaelekea kwenye mwanga, kusudi ni kumwangazia msomaji… SWALI: Enhee, imekuwa na hiyo spirit ya enlightenment? JIBU: Ndiyo, spirit ya ile riwaya ni kuangaza. Ni kutoa mwanga. Hata ukimtazama Zirani, kazi yake alipoenda motoni, gizani, kusudi ni kutoa mwanga wa mawazo kule gizani. Hata wanapokaa kwenye mkutano wakijadiliana, wahusika wanapoleta hoja za kuyageuza maisha kuwa kioja kwa kutumia imani za kidini, wanatokea akina Voltarie wanawaelimisha. Kwa hiyo kila mahali, kusudi ni kuleta mwanga. Hii ndiyo tofauti kubwa baina ya Nagona and Ziraili na Zirani. Kimoja ninaleta giza, kingine kinaleta mwanga. SWALI: Jambo ambalo linajidhihirisha katika riwaya yako ni kwamba kitabu cha ‘Akirikifuk’ kinadokeza riwaya ya kinjozi ya Kufikirika ya Shaaban Robert. Kwa nini umedokeza hivyo? JIBU: Hiyo nimeipenda, hili jina la Kufikirika. Kwa sababu Kufikirika ni abstract world katika riwaya ya Shaaban Robert. Ziraili na Zirani haizungumzii yaliyomo kwenye ile riwaya ya Shaaban Robert, ila nimetumia jina la kitabu hicho cha Shaaban Robert kwa heshima na pia kwa dhana kwamba mambo ya mbingu ni kufikirika tu. Ndiyo sababu wanapopambana na jambo gumu, wakitamka tu ‘Akirikifuk!’ linatatuliwa. Mwanga ni ile elimu kwamba ugumu huo waliokumbana nao ni dhana tu, siyo kweli, hakuna mbingu. Hata yule shetani alivyowakilishwa kwenye hadithi, alikuwa anachezacheza pale nje ya ngome na kufanya fujo huku akiimba nyimbo zake; kiongozi wa kambi akasema “ Tamkeni ‘Akirikifuk!” Walipotamka neno hilo, lile lango lililokuwa linakataa kufunguka, likafunguka. Maana yangu ni kwamba: dunia au mwanadamu atakapotazama hizi mystifications, atakapozitazama kwamba hizi ni dhana tu, ni kufikirika, ndipo hapo atakapopata mwanga. SWALI: Vilevile unadokeza mara kadhaa Magriots yaani waimbaji wa kijadi wa Kiafrika (tz Motoni 11; Mzingo wa Vita VIII & Mtingisho wa Vita III), halafu na Enugu, na sehemu ya matini ya Christopher Okigbo. Umekusudia nini katika kufanya hivyo? JIBU: Yule kasisi wa Enugu, hakika siyo Christopher Okigbo mwenyewe, ila ni mtu aliyevutiwa na ule utenzi wa Christopher Okigbo. Kwa nini ule utenzi? Ni kwamba, mara nyingi maelezo au masimulizi ya ki-dini huambatana na utenzi. Halafu yanaeleza kitu kilicho ndani kwa kutumia viashiria (symbolism). Pia utenzi wa Christopher Okigbo ukiusoma pale unapotoka kwenye Distances – kuna mahali ambapo anakutana na Mungu, alimkuta anakata kucha. Ni ngazi ya juu kabisa. Ni kama ulivyo kenye Kubla Khan ya Coleridge: Anapofika kule ndani kwenye zile kasri, na kadhalika. Ile ngazi ni kiwango cha juu cha akili ya mwanadamu kutafuta kiini cha ukweli. Je, kuwepo kwetu duniani kuna asili yake? Kwa hiyo nimeuhusisha ule utenzi kama msisitizo, kwa sababu imani zote zina uhusiano na hiyo kiu ya kuupata ukweli, ingawaje ni ukweli-dhanifu. Huu ulimwengu wa ruiya tunaouangalia, jinsi inavyozidi kuuangalia na kuuona kuwa fumbo, ndivyo inavyozidi kuwa poetic. Kutatanika kwetu kunatufanya tuzue lugha ya kishairi. Kwa hiyo ndiyo sababu nukuu kadhaa za washairi zimehusishwa mle na mimi mwenyewe lugha ya hiyo hekaya nimeikoleza kwa ushairi. SWALI: Naomba tuangalie mfano wa wimbo anaouimba mghani wa Enugu (tz. ZZ Mzingo wa Vita III 199).. JIBU: Hii ni elegy. “Rambirambi, midomo imepasuka kwa rambirambi..” (Ubeti wa mwisho wa huu wimbo). Ni wimbo wa rambirambi. Lakini kote alikojitokeza kwenye hii riwaya alikuwa anatabiri akiwaambia wahusika kwamba “ninyi huko mnakoenda mtaenda kupambana na mwanga”. Mtaenda kupasuliwa, mtaenda kupamba na mwanga. Kusema kweli huyu ndiye mhusika wa kitabiri kwenye hii riwaya. SWALI: SIYO VOLTARE? JIBU: Voltaire? Voltaire pia ni mtabiri kwa maana ya kutabiri, yaani kuona kilicho mbele kabla hakijakufikia. Lakini pia kuna prophecy kwa maana kama ile asemayo E.M.Forster kwenye kitabu chake: Aspects Of The Novel, ambayo, kama nilimuelewa, ni ile ngazi ya uandishi yenye mtiririko wa masimulizi unaoelekeza ujumi wa msomaji kuweza kutarajia au kutabiri hatma za ujumuisho na ukamilisho wa plot. Nyimbo za huyu mghani wa Enugu ziliwaandama akina Zirani toka walipoitembelea kuzimu hadi zilipoishia kwenye wimbo wa “rambirambi” pale walipokuwa wanakaribia kuanza vita. Kwa hiyo mhusika wa kitabiri kwenye Ziraili Na Zirani ni yule kasisi wa Enugu. SWALI: Sura mojawapo inazungumzia kisiwa cha kubuni cha Nguu ambapo kuna mradi wa kisiri wa kuwanyima watu viungo vyao kama vile figo na kuviuza na kuvisafirisha nje ya nchi (tz ZZ Duniani (I) (II). Mada hiyo inamkumbusha msomaji riwa ya Vipuli vya Figo (1996) ya Emmanuel Mbogo. Umedokeza hivyo makusudi? JIBU: Sijaisoma hiyo riwaya. Lakini kipindi fulani kwenye magazeti na redio walikuwa wanazungumzia kuhusu jambo hilo. Watu walichukua viungo vya watu na kwenda kuviuza au watu wenyewe waliamua kujitolea kuuza sehemu zao za mwili kama figo. Iliandikwa kwamba huko Bangladesh biashara hiyo ilikuwa inafanyika. Kwenye riwaya hii, jambo hilo limegusiwa kwenye sura za Duniani (I) na Duniani (II). Kwenye riwaya vita ile ilikuwa inapiganika huko mbinguni, lakini masimulizi yakahamishiwa kidogo huku duniani kuona kilichokuwa kinaendelea. Kwa mfano ikasimulia vita zilizokuwa zinaendelea kama ile ya Mwendashari na Sharihaswa. Kuonyesha jinsi watu walivyokuwa wanauana kwa sababu ya tama za mali, mamlaka na viburi vya viongozi wao. Huo ulikuwa mfano mmoja ulioonyesha maisha wanayoishi wanadamu na jinsi ambavyo inaathiri imani duniani. Baada ya huu, ukaja mwingine ambao pia masimulizi yalihamishiwa duniani. Huu ulihusu maendeleo ya sayansi, na jinsi dunia ilivyoendelea hata kufikia kuwa na viwanda vya kutengeneza mashine za kuteketeza wanadamu. Makampni makubwa ya Marekani yanauza silaha duniani kote. Kusudi ni nini? Binadamu anapenda kujiangamiza. Sasa hii ni biashara ya kishetani pia. Shetani kwa maana halisi ya ushetani. Mtu mwenye uovu uliokithiri anapofikia kuwa na nia ya kuuangamiza u-anadamu. Siyo ushetani wa kidini ambao uovu wake hasa ni ule wa kumkosea Mungu, siyo! Uovu huu ni ule uovu wa kuu-kosea u-anadamu. Hayo ndiyo maendeleo potofu ya sayansi . Utafika muda ambao tumefika mahala pa kutoa uamuzi mgumu. Baada ya kuuana kwa muda mrefu tutakuwa tumebaki wachache. Tunafika mahala ambapo tumemalizana na uovu unazidi kututuma kwamba hatuwezi kuwepo wote. Pengine sasa itabidi tuchague mmoja abaki. Sasa atabaki nani? SWALI: Nani atashika bao la mwisho tukizama? JIBU: Enhee, ndiyo hapo sasa. Ukiangalia kwa mfano sasa hivi tunapozungumza kuhusu dunia kuwa kama kijiji kimoja, ni kwamba kutafika muda ambao tumesongana mno na sasa tutasema wabaki nani? Ni nani wapate neema za dunia; ni nani wafaidi neema za dunia? Ndio hiyo ngazi tutakayofika. Na tukifika hapo ndipo mwanadamu atautumia mwili wa mwanadamu mwingine kama kipuli cha kujitengeneza asife, aendelee kuishi. Sasa huyu ambaye mwili wake unatumika kukarabati wa yule mwingine, yeye ana upungufu gani? Kwenye hii riwaya, kuna lile jaribio la kisiwa cha Nguu. Ilibidi madaktari wa lile jaribio wawaharibu wale viumbe wa jaribio nafsi zao kwa kuharibu ubongo. Waliwaharibu nafsi zao makusudi, ili ule u-anadamu wao upungue ndipo waweze kuwa na uhalali wa kutumia vile viungo vyao kwenye mahospitali ya ulimwengu. Lakini hapa kuna swali gumu la kifalsafa kwamba itatokea nini wakati mwanadamu atakapougeuza mwili wake kuwa bidhaa? SWALI: Aidha, imo miingilianomatini mingine katika riwaya hiyo. Unawadokeza akina Shellye, George Bernard Shaw, T.S.Eliot, Christopher Okigbo- umeshamtaja- na Ayi Kwei Armah. Je, tunaweza kuchukulia kwamba hao wamekuathiri zaidi katika uandishi wako? JIBU: Kwa kweli siwezi kusema aliyeniathiri ni yupi. Huwa nasoma kwa mapana na sichagui. Ila utenzi wa Christopher Okigbo niliupenda sana. Nilipokuwa mwaka wa kwanza chuo kikuu, niliuchora huo utenzi. Sijui michoro yangu imepotea wapi! Niliuchora kutoka shairi la kwanza mpaka la mwisho. Jinsi ile hisia ya ushairi ilivyonipata ndivyo nilivyoichora kweye karatasi. Kwa hiyo niliupenda ule utenzi wake. Pengine ndiyo sababu umeuona unajitokeza sana kwenye ile riwaya. Nakubali huyo ameniathiri, kishairi. Lakini naye Christopher Okigbo aliathiriwa na T.S. Eliot. Nimemsoma T.S. Eliot na ikiwa kamuathiri Okigbo basi kwa kiasi fulani ameniathiri. Hata kwenye riwaya nimemnukuu mahala mbapo anawaasa Waafrika kwamba “ Ninyi mmekubali mambo ya kuabudu miti, na mizimu na majoka, sasa mnaona mlikoishia.” Shelley nimemsoma kwa kiwango kidogo lakini ile elevated language ya ushairi wake inanifurahisha. Siwezi kusema kwamba ameniathiri. Labda ungesema S.T.Coleridge. Na Ayi Kwei Armah nimeigusia hoja yake katika kitabu chake Two Thousand Seasons, kwamba sisi Waafrika tulipotoka kwenye mwelekeo wetu wa asili na kwenda pembeni tulikosea. Anasema “There was a way” akimaanisha kwamba hapo mwanzo Waafrika tulikuwa na njia, mwelekeo, lakini tukaenda pembeni. Na upotofu huo umekuja kutuathiri sisi Waafrika. Na yeye kwa kweli anazumguzia kuhusu nafasi ya Afrika katika huu ulimwengu wa leo. SWALI: Na G.B. Shaw? JIBU: G.B. Shaw- nimesoma tamthilia zake nyingi. Ameipa tamthilia sababu, kama Tolstoy alivyoipa riwaya sababu. Ni riwaya zinazofunza, kama hizo tamthilia za G.B. Shaw. Zote zinafunza, zinatoa mwanga. Kwa hiyo napenda sana uandishi wa G.B. Shaw. SWALI: Swali lifuatalo linahusu lugha unayoitumia: kwanini ulianza kuandika kwa Kiingereza, halafu ukaacha na kuandika kwa Kiswahili? JIBU: Niliandika Kiingereza kwa sababu ya heshima unayopata ukiandika Kiingereza wakati ule. Unajua, uandishi wa Kiafrika uliimarishwa sana na Heinemann, katika African Writers’Series. Na sisi wakati ule tulipokuwa vijana ukizungumzia riwaya hasa kama unazungumzia fasihi- siyo kusoma tu riwaya za kujiburudisha kama James Hadley Chase na Ian Fleming, lakini fasihi zinazohusiana na masuala ya Afrika, vitabu vilivyotia fora vilikuwa kwenye African Writers’s Series. Sasa karibu zote zilikuwa riwaya za Kiingereza. Kwa hiyo, kwa sababu wakati ule tulizisoma kwa wingi kama mtindo au mazoea, basi nikaona aha!, Nitapata heshima nikiandika Kiingereza. Lakini baadaye nikaona kwamba uandishi unakuwa mwepesi zaidi nikiandika Kiswahili. Kwa mfano ningeandika Ziraili Na Zirani kwa Kiingereza pengine nisingeweza. Kazi hii nimejaribu kuitafsiri mpaka sasa hivi sijaweza. Kwa sababu Kiingereza ni kigumu. SWALI: Lakini si wakati ule ulipokuwa mwandishi hapa Tanzania, uwingi wa waandishi, tuseme asilimia themanini au zaidi, waliandika kwa Kiswahili tayari? Hii ndiyo sababau ya kukuuliza swali hili, kwa sababu wengi wenzako wameanza moja kwa moja kuandika kwa Kiswahili. JIBU: Mmm. Labda ni hilo suala la kudhani utaheshimiwa ukiandika kiswahili. Ambayo kusema kweli ni dhana potofu. Lakini sibishi kwamba niliona ni heshima zaidi kuandika Kiingereza. Hii ilikuwa ni kasumba tu. Ni vizuri zaidi kuandika kwa Kiswahili. Lakini pia sababu nyingine ni kwamba ile hadhira ya wasomaji wa riwaya za Kiingereza wakati ule ilikuwa kubwa zaidi. SWALI: Swali la mwisho, halafu tutashusha pumzi! Nafikiri umeshajibu sehemu. Katika fasihi ya kiulimwengu, unawapenda waandishi gani zaidi? JIBU: Ni ngumu kuchagua kwa sababu kila mmoja, uandishi wake una utamu wake. Lakini mmoja katika uandishi wa tamthilia ni George Bernard Shaw. Na yeye ameathiriwa sana na Nietzsche. Kwa hiyo kwa kufuata mkondo wa Shaw pia nimemsoma Nietzsche, hasa mchango wake kifalsafa. Nawatumia jinsi ninavyojadili hoja ninazozigusia kwenye Ziraili Na Zirani. Ingawaje mimi mwenyewe pia nina hoja binafsi na muundo wa uandishi ambao si lazima ufanane na wa kwao. Katika ushairi – napenda ushairi wa Coleridge, na Christopher Okigbo, na T.S. Eliot. Kwenye upande wa riwaya – ni vigumu kusema. Kwa sababu ni nyingi, na zote, kila moja ina ladha yake. Hivi sasa nasoma The Brothers Karamazov. Nilipenda sana Crime and punishment, na uhusika wa Raskolnikov. Ukimtazama Zirani wanafanana – ingawa Raskolnikov alikuwa ametenda uhalifu, na alikuwa anaikimbia hukumu ya uovu wake. Unajua uhusika wa Raskolnikov unafanana na ule (wa Mersault) uliopo kwenye The Outsider ya Camus; ndiyo huohuo pia uliopo katika Native Son, yaani yule Bigger Thomas, na pia uhusika huohuo– juzijuzi niliukuta nilipokuwa nasoma Resurrecton ya Tolstoy! Ni uhusika huohuo! Nauona uhusika huu ni ule ambao unawakilisha taswira ya (nafsi ya mwanadamu kijana wa leo) the modern young individual na jinsi anavyoathiriwa na mabadiliko ya maisha. Kwa hiyo ingawa Zirani hakuwa mhalifu, lakini ana sifa hiyo. Katika riwaya zangu zote nadhani nina mhusika wa aina hiyo. Lakini pia Albert Camus napenda sana uandishi wake, hasa kwenye zile riwaya zake mbili: The Plague na The Stranger. Zamani, nilikuwa napenda uandishi wa D.H. Lawrence. Kwa hiyo siwezi kusema ni mwandishi yupi napendelea zaidi uandishi wake. Halafu juzijuzi hapa nimemsoma Hermann Hesse. Ah! Ana uandishi mtamu sana. Natafuta riwaya zake nyingine. Ninayo moja, niliikuta kwenye book sores za barabarani. Sasa natafuta kazi za Thomas Mann na za huyu Hermann Hesse. SWALI: Umesoma Siddharta? JIBU: Siddharta, ndiyo hiyo niliyo nayo nyumbani. SWALI: Na ya Thomas Mann umesoma ipi? JIBU: Sijapata. Ndiyo naitafuta. Herman Hesse, uandishi wake unaburudisha sana, unaliwaza! Ameandika kwa nathari lakini huwa nausoma kama ushairi. Kwa hiyo nikiwa na nafsi iliyoelemewa, mara nyingi huenda kusoma kitabu cha Herman Hesse. Ni kizuri sana. SWALI: Inatuliza sana? JIBU: Ah! Inatuliza sana moyo! Hapa tunafika Mwisho wa mahojiano. Huu ni mwanga kwa wale ambao hawajasoma kitabu hiki cha Ziraili na Zirani. Hata wale waliokisoma, kama mimi mahojiano haya yanaleta mwanga na utamu zaidi. Mtu akisoma mahojiano haya anakuwa na shauku ya kusoma tena Ziraili na Zirani. Lakini pia mahojiano haya, yanasaidia kumtambua vizuri Mwandishi Mkufya na vitabu vyake. Kama anavyosema yeye, vitabu vyake vinaleta mwanga. Ni bora tukavisoma ili tuusambaze mwanga wa elimu kupitia kusoma vitabu. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment