MWANA MAMA. BIBI TITI MOHAMED Tunapotaja waasisi wa Taifa letu, majina yanayosikika ni ya wanaume. Lakini ukweli ni kwamba hata wanawake walitoa mchango mkubwa wakati wa kupigania uhuru wa taifa letu. Kati ya wanawake wanaotajwa ni BibiTiti Mohamed. Ingawa kuna jitihada za makusudi kuhakikisha jina hili linafutika na kusahaulika, bado mzimu wa mama huyu unajitokeza na kuendelea kutuchokoza ili tuendelee kuchimba, kutafiti hadi ukweli uwekwe wazi na mama huyu apate heshima na nafasi kubwa miongoni mwa waasisi wa taifa letu. Bibi Titi Mohamed ni mmoja wa viongozi wazalendo waliokuwa na nguvu, uwezo mkubwa na umuhimu wa pekee nchini Tanzania. Wale walio waaminifu wa historia ya taifa letu, wanasema baada ya Mwalmu Nyerere, alifuata Bibi Titi, kwa mvuto, uwezo wa kuongoza, upeo na uzalendo. Alizaliwa Dar-es-salaam mwaka 1926, baba yake alijulikana kama Mohamed bin Salim, alikuwa mfanyabiashara na mama yake Hadija Binti Salim, alikuwa mkulima na mama wa nyumbani. Hawa wazazi wa Bibi Titi, walitokea Rufiji, mama yake alijulikana kama Mmatumbi mwenye nguvu za kuogofya. Bibi Titi alisoma shule ya msingi kwa miaka minne tu. Hilo halikuwa jambo la kawaida hata kidogo kwa msichana wa Kiislamu katika miaka ya 1930. Wakati ambapo wasichana wa kizazi chake walishiriki katika vikundi vya ngoma, ni wachache mno walioweza kuwa waimbaji na kuigiza pamoja na haiba kubwa. Hivyo, pamoja na kwamba alikuwa ni mwanamke wa kawaida wa mjini, Bibi Titi alikuwa na silika iliyomwezesha kushirikiana na kukaa na wenzake, na hivyo kuweza kuwahamasisha na kuibuka kuwa kiongoizi. Alipokuwa Dar-es-salaam, ambapo ni kwao,Bibi Titi aliweza kutambua uwezo wake, na baada ya kufanya hivyo, kuondoa wasiwasi na kujiimarisha kwenye jukwaa la siasa za mjini. Kufikia mwishoni mwa mwaka 1955, Bibi Titi Mohamed alikuwa kiongozi muhimu wa TANU. Alikuwa ameonesha wazi uwezo wake wa kuhamasisha makundi makubwa ya Waafrika walioishi Dar-es-salaam ili kuunga mkono harakati za kizalendo. Bibi Titi alipohutubia mkutano wa kwanza wa Kitengo cha Wanawake cha TANU, Julai 8,1955, wanawake 400 walijiunga na chama. Kufikia Oktoba mwaka huo walishafika wanachama 5,000 walioingizwa kwenye chama na Bibi Titi. Aliwahamasisha wanawake kujiunga na chama: “Nawaambieni kwamba tunataka uhuru, na hatuwezi kupata uhuru kama hamtaki kujiunga na chama. Tumewazaa wanaume wote hawa. Wanawake ndio nguvu ya duni hii. Sisi ndio tunaozaa dunia. Nawambia kwamba inatubidi kujinga na chama kwanza..” (Bibi Titi – Wanawake wa Tanu uk 37) “Niliweza kusafiri kwa miezi mitatu mfululizo, Ningeweza kuwa Mwanza, halafu nikaenda Musoma ambapo ningepata telegram iliyonitaka niende Dodoma. Nikiwa Dodoma Napata telegram nyingine kwenbda Mbeya…” “Mimi sikujinga na TANU nikitarajia chochote… Rafiki zangu walikuwa wananiuliza, unataka kuwa malkia wa nchi? Sikutaka kuwa malkia. Nilitaka kuwa huru. Sikutarajia chochote zaidi. Nilitaka kujenga nchi yangu, kufanya maisha yetu yawe bora, nilitaka elimu kwa watoto wetu, na nilitaka kupata ardhi… Wazungu walikuwa na mashamba makubwa na sisi tulikuwa vibarua tu. Vibarua katika nchi yetu? Kwa nini? Hilo mimi sikulipenda… nilitaka maendeleo kwa watu..” (BibiTiti –Wanawake wa TANU uk 41). Hivyo Bibi Titi, alitembea nchi nzima ya Tanzania, akiwahamasisha wanawake na wanaume kujiunga na TANU. Alifanya kazi bega kwa bega na Mwalimu Nyerere na wapambanaji wengine wa wakati ule wa kupigania Uhuru wa wa Tanganyika. Alifanya kazi kubwa kuzidi hata wanaume wengine waliokuwa wakipigana kwa kujificha ili wasipoteze kazi zao serikalini. Ndoa yake ilivunjika kwasababu ya kujihusisha na siasa “Boi mwenyewe aliniruhusu kuingia TANU, tena ndiye eliyenunua kadi yangu ya uanachama. Sio hivyo tu, TANU ilimwandikia barua kumwomba nisaidie katika shughuli za TANU. Lakini mwishowe hizi safari zilimshinda. Nilikuwa nakaa nje ya nyumbani kwa miezi mitatu, na nikirudi naweza nisikae hata siku kumi kabla sijasafiri tena. Boi akaniambia kwamba anataka kuoa mke mwingine. Nikamwambia sawa, niache na kazi yangu kwasababu nimeshaizoea…Kwa hiyo Boi akamuoa Khadija, lakini walishindwana, wakaachana. Akaniambia kama nampeda niache hiyo kazi. Nikamwambia siwezi, kama unataka kuoa tena, endelea. Akakataa ,akasema nawezi kuoa tena. Nilifunga mizigo yangu nikaondoka..” (Bibi Titi- Wanawake TANU uk 45). Katika maadhimisho ya uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Waingereza, usiku wa Desemba 9,1961, Bibi Titi Mohamed na Julius Nyerere walikaa kwenye jukwaa moja, wakiwa pamoja na waheshimiwa wengine. Kufuatana na wachambuzi wa historia ya Tanzania, ni kwamba wakati wa kupata uhuru yawezekana kuwa Nyerere na Bibi Titi walikuwa ndio viongozi pekee waliojulikana nchi nzima wakati Tanganyika inapata uhuru. Uhuru wa kisiasa ndo ulikuwa lengo kuu kwa Bibi Titi na wanawake wanaharakati wa miaka ya 1950. Hata hivyo, uzalendo na nguvu waliyowekeza katika TANU haikuishia katika kuwapa nguvu ya dola. Waliwekwa pembeni na kushauriwa waingie jikoni, kutunza nyumba na kuwalea watoto. Hata hivyo Bibi Titi, aliponzwa zaidi na uwazi wake na msimamo wake wa mawazo. Alijisimamia na hakuwa na unafiki. Azimio la Arusha, lilijenga ukuta mkubwa kati yake na Nyerere na viongozi wengine wa TANU. Yeye alikuwa wazi kuelezea wasi wasi wake juu ya Azimio la Arusha. Wengine, na hasa wanaume walilikubali Azimo la Arusha kwa unafiki na matokeo yake wanaume hao hao walizika kule Zanzibar. Kama kuna kosa kubwa alilolifanya Mwalimu Nyerere, ni kushindwa kugundua unafiki wa viongozi wanaume waliokuwa wamemzunguka na kushindwa kutambua na kukubali uwazi na uaminifu wa watu kama Bibi Titi waliokuwa na mawazo tofauti, lakini ya kizalendo na ya kujenga. Tunaweza kusema kwamba Bibi Titi, ni kati ya watu waliopigania uhuru lakini hawakufaidi matunda ya uhuru. Wakati wenzake wakifurahia uhuru na kujilimbikiza mali kwa unafiki huku wakijificha nyuma ya siasa ya Ujamaa, yeye alikuwa gerezani. Alipotoka gerezani hakuweza kufurahi maisha, maana jamii ilikuwa inamnyanyapaa. Dosari ya kuingizwa kwenye uhaini ilimchafua kiasi cha kujikuta anaishi bila kuwa na marafiki. Hata na wale walioshirikiana naye kupigani uhuru, walimwogopa. Ni vigumu pia kuthibitisha kama maisha ya ukimya aliyoishi Bibi Titi nje ya siasa kwa miaka mingi baada ya kuachiwa, aliyachagua ama alishurutishwa kufanya hivyo. Katika mahojiano na Ruth Meena baada ya kutoka kifungoni, Bibi Titi alieleza kuwa hakuwa huru sana kushiriki na wenzake kwa sababu walikuwa waangalifu mno wakiwa naye. Alitania akisema, “Mtu angeweza kufikiria kwamba nilikuwa na ugonjwa wa kuambukiza” Bibi Titi alionesha kutoridhika kwake na sera ya chama wakati alipopinga kutofuatwa kwa demokrasia katika mchakato ulioambatana na kutangazwa kwa Azimio la Arusha Februari 1967. Pia, hakukubaliana na kipengele (a) sehemu ya 5 ya Azimio kilichohusu maadili ya uongozi. Hususan, hakukubaliana na kipengele kilichosema kwamba kiongozi wa TANU au serikali hawezi kumiliki au kupangisha nyumba. Hakukataa kwa siri, na hivyo alijiuzulu kutoka Kamati Kuu ya Chama kwa mujibu wa maadili ya uongozi, kuliko aachie haki yake ya kujipatia kipato. Jambo hili lilielezwa katika vyombo vya habari, vikitoa picha iliyomwonesha Bibi Titi kuwa alithamini zaidi faida ya biashara na idadi ya nyumba zake kuliko kazi ya siasa chini ya TANU. Lakini Bibi Titi mwenyewe, alijitetea kwamba alinunua nyumba moja kwa kuuza vito vyake vya dhahabu na nyumba ya pili alinunua kwa mkopo. Yeye alikuwa ameamua kujipatia hifadhi,kwake na kwa binti yake kwa njia hii, wakati washiriki wenzake waliamua kuoa wake wengi na kunywa pombe. Msimamo huu wa wazi ulimwingiza matatani hadi akaingizwa kwenye mkumbo wa uhaini. Aliwekwa ndani miaka miwili na nyumba zake zilitaifishwa. Alipoachiwa kutoka ndani aliishi maisha ya taabu sana na kufanya biashara ya kuuza mafuta ya taa. Baadaye nyumba zake zilirejeshwa na mwaka 1985, Mwalimu Nyerere, alionyesha dalili za kumsamehe. Hata hivyo, jina lake na mchango wake mkubwa wa kupigania uhuru vilipotea na kufunikwa! Ni wajibu wa watanzania kufufua majina kama haya, ili vizazi vijavyo vipate historia isiyopinda ya taifa letu. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment