UHAKIKI WA KITABU: FALSAFA NA USANIFU WA HOJA - KUTOKA WAYUNANI HADI WATANZANIA(WAAFRIKA).
1. Rekodi za Kibibliografia
Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni “ Falsafa na Usanifu wa Hoja - kutoka Wayunani hadi Watanzania (Waafrika)” na kimetungwa na Dk. Adolf Mihanjo, ambaye ana shahada ya Licentiate na ya Udaktari wa falsafa katika falsafa (Doctor of Philosophy in philosophy) kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Aquino Philippines, amefunfisha vyuo mbali mbali duniani na sasa hivi ni mhadhiri wa falsafa katika chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na mhadhiri mgeni katika Chuo Kikuu kishiriki cha falsafa cha Salvatorian Morogoro. Mchapishaji wa kitabu hiki ni SALVATORIANUM, na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 645 14 3. Kimechapishwa mwaka 2004 kikiwa na kurasa 306.Na anayehihakiki sasa hivi katika safu hii ya Kisima cha ujuzi ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Hiki ni kitabu cha kwanza cha aina yake kinachohusu somo la falsafa kwa lugha ya kiswahili. Katika kitabu hiki Dacta Adolf Mihanjo anachambua kwa makini mawazo ya wanafalsafa kuanzia Thales, Anacimender, Anaximenes, Pythagora, Heraclitus, Parmenides, Atomist, Sophist (Protagora, Georgias, Thrasymuchus), Socrates, Plato, Aristotle, Epicureans, Stoics, Skeptics (Wakushuku) na Neo-Platonists.
Kitabu hiki kina sura sita na kila baada ya sura kuna maswali ya kujadiliana.Mwishoni mwa kitabu kuna vitabu vya rejea, kitu kinachoonyesha kazi muhimu na ya makini aliyoifanya Dk Adolf Mihanjo. Ni jumla ya vitabu 11, vikiwemo: “ The complete Works of Aristotle na the Complete works of Plato”. Kitu kinachovutia zaidi katika kitabu hiki ni orodha ya maana ya baadhi ya maneno (Kiswahili- Kingerea na Kingereza-Kiswahili) anayotuwekea Dk Mihanjo mwishoni mwa kitabu. Ameonyesha jinsi kiswahili kinavyoweza kumudu kupambana na kila aina ya elimu. Yapo meneno mengi ambayo tumekuwa tukiyatumia katika lugha ya falsafa kwa kiingereza, bila kuwa na maneno ya kiswahili.Mfano; Contradiction in terms, contradiction/logical absurdity, contradiction, contradictions,contractory terms na contradict. Dk.Mihanjo anatupatia maneno ya kiswahili:
-Contradictions in terms- utatanisho katika maneno.
- Contradiction/logical absurdity- utatanisho.
- Contradiction- Mkanganyiko
- Contradictions- Matofautisho.
- Contradictory terms – Maneno yasiyo sambamba.
- Contradict- Tatanisha.
Kitabu hiki kimesheheni maneno mengi, ambayo wengi wetu tumezoea kuyatumia kwa kuchanganya kiingereza na kiswahili, kwa kufikiri kwamba hakuna kiswahili chake. Maneno kama: Abstract thinking- akili wazika, abstract thinking- uwazaji mtupu, abstract- dhania/ a kuwazika tu/soweza kushikika, abstract- elimu wazika, abstract- kimawazoni, abstract – kufyonza nk. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu hiki
Kitabu hiki kimetolewa wakati muafaka ambapo katika mazingira ya kidemokrasia na utandawazi nguvu ya hoja ndiyo inayomnadi mtu na siyo hoja ya nguvu.Upeo na ueleo mpana ndiyo kigezo kikubwa cha kukubalika katika jamii ambayo mapokeo hayana tena nguvu za kimamlaka.
Kitabu hiki kinakuja wakati taifa letu liko katika majadiliano ya ni lugha gani itumike katika kufundishia.
Wapo wanosema, tutumie lugha ya kiingereza, na wapo wanasoma tutumie kiswahili. Maswali kama, je, tunaweza kusema kuwa fikara na mawazo ya mtu au jamii yako katika lugha yake na kukomaa kwa fikara za mtu huenda sambamba na kukomaa kwa lugha yake na kwa hiyo kama wazo haliko wazi kwake, haliwezi kupata lugha iliyokuwa wazi?Yatapata majibu katika kitabu hiki. Na swali jingine, kama je,kukomaa kwa fikara ni sharti muhimu la kukomaa kwa lugha?Litapata jibu katika kitabu hiki.
Kitabu hiki kinatoa mwanga kwamba tafsiri, elimu yetu, mawazo yetu na lugha yetu lazima vikue na kuendelea kukotana na maghamuzi yetu.Mawazo yaliyomo katika lugha za kigeni yatasaidia tu kukomaza maghamuzi yetu. Hivyo tafsiri ya maneno ya kisayansi na falsafa katika kiswahili itakuwa na maana tu kama itasaidia kukomaza maghamuzi yetu na kuleta maghamuzi mapya ambayo yatahitaji maelezo mapya.
Kwa umakini wa hali ya juu Dacta Mihanjo anaonyesha namna gani akili na upevu wa binadamu wa kuelewa mambo na uwezo wa kujenga hoja chini ya msingi ya nadharia maalum ulikuwa unakua kutoka hatua moja hadi nyingine.Aidha anaonyesha namna gani nadharia za kifalsafa zilikuwa zinazuka na kutoa maelekeo ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kimaadili katika vipindi na nyakati tofauti.
Walengwa wa kitabu hiki ni Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla, Walimu na vyuo vya ualimu, Wanafunzi wa Sekondari, viongozi wa wananchi na kila mtu mwenye hamu ya kukuza upeo wake wa kuuelewa dhana ziongazo ulimwengu ambamo yeye ni sehemu. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muthasari.
IV. Muhtasari wa Kitabu.
Sura ya kwanza ambayo ni utangulizi wa kitabu hiki ina kichwa cha habari: Historia ya Kupanuka kwa Fikara za Binadamu na Uthibi wa Mawazo Taswira, na imegawanyika katika mafungu saba: Tathmini Tafakari Juu ya Umuhimu wa Falsafa, Maarifa ya Ukweli,Maswali ya Kawaida katika Uwanja wa Falsafa, Hamu ya Kutaka Kujua Masuala ya Utata wa Maisha, Uibukaji wa Uwazaji, Wayunani na Falsafa na Afrika na Falsafa.
Utangulizi huu unatoa mwanga juu ya Falsafa: “ Binadamu,maadamu ni binadamu, hawezi kuwa huru kutoka hali ya kujiuliza maswali.Hii ni hali asilia ya uishi wa roho yake.Roho ya biadamu katika hali yake ya ujiulizo, inataka kwa namna yoyote ile kutengeneza au kuhoji umaana wa uwepo wake.Ni pale tu ambapo roho ya binadamu hupata maana ya uwepo wake, ndipo binadamu huwa “ Mwanafalsafa”, mpenzi wa busara na hekima, huja kuwa ni mtu ambaye hutafuta maaraifa( knowledge) ili aweze kuishi maisha yenye maana” (Uk wa 2).
Tunapata pia jibu la swali: “Sasa, nini hasa maarifa ambayo mwanafalsafa anayatafuta?”, “…Mwanafalsafa anakusudia maarifa ambayo yapo huru kutoka kwenye hali ya undoto… yaani maarifa yanayohusu ukweli kama ulivyo na lengo kabisa la mwisho la kila kitu.Ni elimu inayohusu ukweli kama ulivyo.Na kwa sababu hiyo, hii elimu inajihusisha hasa na maswali ya msingi ya kila kitu na ya kanuni ya uwepo.. Elimu hii kuhusu lengo la mwisho hasa la kila kitu inahusisha hasa maswali ya msingi kuhusu binadamu na ulimwengu na dahana kuu zinazoongoza elimu zote” (Uk wa 3).
Utangulizi, unaeleza chanzo cha mawazo ya kifalsafa kwamba ni Uyunani.Hii ilisababishwa na hali yake ya kijiografia, wingi wa nafasi zakusafiri kwenye nchi kavu na majini, tabia nzuri za kimaumbile na mali tele za kiasili. Utangulizi pia unagusia Falsafa ya Mwafrika: “ Kwa ujumla Wanafalsafa wote wanaotetea uwepo wa Fafsafa ya mwafrika wanaona kuwa Falsafa ya mwafrika inajengwa chini ya misingi ya mila na desturi za mwafrika, ambapo uchambuzi wake wa kina utazaa Falsafa ya mwafrika. Huu uchambuzi ni lazima uzingatie kanuni ambayo inamwongoza mwafrka kufanya vile anavyofanya na kuamini vile anavyoamini.Ugunduzi wa kanuni hiyo ndio utazaa Falsafa ya mwafrika” (Uk wa 15).
Sura ya pili inaangalia mwanzo wa Falsafa: Utafiti wa Ukweli Muhimili(Objective Trurth).Inachambua maisha ya watu wa Ayonia (Ionians) kabla ya Kuzaliwa kwa Falsafa, hawa ni akina Thales, Anazimander, Anaximenes, Pythagoras,Heraclitus, Permanides na Wanaatomi. Wanafalsafa hawa walishughulika na kutafakari chanzo cha kila kitu.Thales, Anazimander na Anaximenes, waliibua swali juu ya chanzo halisi cha kila kitu na walijaribu mara ya kwanza kufanya uchunguzi wa kina na kujaribu kuangalia muundo wa nguvu za asili na chanzo chake, kitu ambacho kilipelekeza utafiti mkubwa wa kisanyansi katika siku zilizokuwa zinafuata.
Pythagoras,alikuza upenzi wa mahesabu. Heraclitus, alikuja na mawazo kwamba vitu vyote viko katika hali ya mabadiliko na Permanides, akajaribu kuonyesha utata wa mawazo ya Heraclitus, ya mabadiliko.Wanafalsafa wa mwisho katika kundi hili ni Wanaatomi, walioongozwa na Democritus na Leccippus, walidai kuwa chanzo cha kila kitu ni atomi.
Sura ya tatu, inajadili jinsi ya Muhimili (Objective Truth) ulivyotiliwa shaka. Wanafalsafa wanaojadiliwa hapa ni Protagoras, Gorgias na Thrasymachus.Kikundi hiki cha wanafalsafa kilijulikana kama MASOFISTI.Kikundi hiki kilisema kuwa, kwa kuwa ukweli kama ulivyo haufahamiki, basi binadamu ndiyo kipimo cha ukweli!
Sura ya nne, inajadili jinsi misingi ya ukweli muhimu ilivyojengwa na wanafikara Adhimu- Socrates, Plato na Aristotle. Hapo ndipo tunapokutana na historia ya maisha ya Socrates, nadharia ya Socrates ya Elimu Pembuzi, Mawazo ya Socrates Juu ya Maadili, Kesi ya na Kifo cha Socrates, kupanuka kwa Mawazo ya Kidemokrasia na Kifo cha Socrates.
Baada ya Socrates, anafuata Plato.Maisha ya Plato, Nadhari Mlingano wa Pango au Asitiria ya Pango,Mstari wa Mgawanyo, Aina nne za Mfumo wa Mawazo kadiri ya Plato, Imani, Nadharia ya Plato ya Mawazo na Mwono wa Plato kuhusu dunia.
Baada ya Plato, anafuata Aristotle, historia yake na mawazo yake pamoja na kazi zote.
Sura ya tano, inajadili kazi mashuhuri za Falsafa baada ya Aristotle.Hapa ndipo tunapokumbana na wanafalsafa kama Epicurus na Stoicism. Yanaibuka mawazo kama: Utimilifu wa Kanuni ya Tamaa au Starehe, Mungu na Kifo, Furaha ya mtu binafsi, Busara na Uthibiti dhidi yaTamaa nk.
Sura ya sita na ya mwisho, inajadili yale yanayosemwa kuhusu Falsafa ya Kiafrika.Dhana yake na kama kweli ipo.Mwelekeo wa Kisasa wa Fikira katika Afrika.Inawachambua wanathiolojia, wanafalsafa hekima, wanafalsafa weledi au mabingwa na Falsafa ya Itikadi.
V. Thathmini ya Kitabu.
Baada ya kuona muhtasari wa kitabu, sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Dk.Mihanjo. Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana na uchochea mapenzi ya Falsafa. Kinatoa mwanga na matumaini ya matumizi ya lugha yetu ya kiswahili.Kitabu hiki kinatoa wingu kubwa lililokuwa limefunika somo hili la falsafa na kulifanya liwe la mapadri peke yao.Lilifundishwa kwenye seminari na kukbaki kwenye lugha ya “Kichawi” na kuwa lugha hii ni watu wachache wanaoifahamu.Dk.Mihanjo, ambaye yeye si padri, amefanikiwa kuoondoa “uchawi” huu. Kwa lugha yetu ya kiswahili, kila mtu anaweza kujisomea na kupata maarifa kutokana na mababa wa falsafa.
Pili,Hiki ni kitabu cha kwanza kuandikwa kwa kiswahili juu ya falsafa. Pongezi nyingi zimwendee Dk.Mihanjo, kwa kufungua uwanja wa falsafa katika lugha ya kiswahili. Kwa vile hadi leo hii ameandika vitabu viwili vya falsafa kwa lugha ya kiswahili amefanya mchango mkubwa ambao unaungana na jitahda nyingine za TUKI, BAKITA na wataalamu wengine wa kiswahili ndani na nje ya Tanzania, kukikuza na kukiendeleza kiswahili ili kiweze kubeba mawazo ya dunia ya leo ya utandawazi.
Tatu, Dk.Mihanjo, ameonyesha kwamba si mwandishi tu wa kitabu ,bali na yeye ni mwanafalsafa.Hii imejionyesha sehemu nyingi katika kitabu, pale anapopenyeza mawazo yake ya kifalsafa: “ Tanzania bila kujua kwa undani kabisa chanzo cha demokrasia, kuibuka kwake na uhusiano uliopo kati yake na mazingira yaliyoiibua hiyo demokrasia.Kuiongelea demokrasia ya Tanzania bila kujua chanzo cha kuibuka kwa neno demokrasia ni kujua ukweli sehemu.Hali hii inaweza kumpeleka mtu kwenye hitimisho potofu.Hivyo , ili kuelewa ukweli unganifu wa neno demokrasia mtu yambidi aelewe kwa undani kabisa namna gani neno demokrasia liliibuka miongoni mwa jamii ya Wagriki hasa nyakati za wanafalsafa waitwao Sophist na za akina Socrates, Plato na Aristotle na namna gani hili neno demokrasia lilitafsiriwa na wanafalsafa waliofuata, na ni kwa sababu gani demokrasia ilionekana na wengi kama ndio mfumo sahihi wa utawala” (Uk wa 85).
Nne,Mwandishi amefanikiwa kukifanya kitabu chake kiwe cha kuaminika kwa kunukuu mistari kutoka katika vitabu vya wanafalsfa mbali mbali na kutumia vitabu vya rejea. Mfano kutumia vitabu vya Plato na Aristotle na kujitahidi kufanya tafsiri ya mawazo yao katika lugha kiswahili,kunaongeza uzito katika kitabu chake.
Tano, maswali ambayo mwandishi anaweka kila baada ya sura, ni changamoto kwa msomaji kuweza kujipima kwa yale aliyoyasoma.Maswali haya ni mwongozo kwa mtu binafsi au kikundi.Yametungwa kwa umakini.Mfano baada ya sura ya tatu inayowaongelea masofisiti akina Protagorasi,Georgias na Tharasymachus, kuna maswali kama haya ambayo yanamsaidia msomaji kuzama kwa kina katika fikara:
- Je hawa Sophist wote watatu wakichukuliwa kwa pamoja wamekusaidia vipi katika harakati zako za kutafakari unafiki wa maisha, matatizo yake na wezekano zake?
- Kuua uwezekano wa kuufikia ukweli jumla (objective truth) ni sawa na kuua misingi ya sayansi (relative truth)? Jenga na tetea hoja zako.
- Ni matatizo gani huweza kutokea pale ambapo watu hingia katika kipindi cha mpito na wakati huo huo hawajaadaliwa kisaikolojia?
Maswali kama haya na mengi mengi yaliyojaa katika kitabu cha Dk.Mihanjo, yanasaidia kuelewa zaidi, kuhoji na kutoa mchango wa mawazo.Falsafa si kitu kilichofungwa, bali ni mwendelezo wa mawazo karne hadi nyingine.
Sita, orodha ya maneno ya Kiingereza- Kiswahili,na Kiswahili –Kiingereza, aliyoiweka mwishoni mwa kitabu ni ishara kubwa ya uwezo wa mwandishi.Ameonyesha ubunifu katika kuunda baadhi ya maneno ya kiswahili ambayo hayakuwepo katika lugha ya kawaida. Maneno haya ni mchango mkubwa, ni changamoto ya pekee kwa wasomi wa kitanzania kwamba kiswahili kinamudu Elimu zote!
VI. Hitimisho
Kwa kuhitimisha basi, ningependa kuwashauri watanzania kukisoma kitabu hiki.Falsafa ni ufunguo wa maisha.Mimi binafsi nilijifunza falsafa mnamo mwaka wa 1975 na 1976, lakini nilipokisoma kitabu cha Dk.Mihanjo, kwa lugha ya kiswahili, nimepata mwanga mpya.Mambo mengi yameonekana kuwa mapya!Ni imani yangu kwamba na kwale waliosoma falsafa kwa kiingereza siku za nyuma, watafaidika sana na kupata mwanga mpya wakiisoma kwa lugha ya kiswahili.
Pia, ningependa kupendekeza kwamba kwa vile Dk,Mihanjo,amefungua uwanja, basi somo la falsafa liwe la lazima kwa shule za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.Ukweli ni kwamba, hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea bila ya watu wake kuzama katika fikara na kujifunza mambo mengi juu ya msingi wa falsafa.
Pamoja na sifa zinazomwendea Dk.Mihanjo,bado kuna changamoto kubwa mbele yake na mbele yetu sote.Changamoto hii ni kazi ya kutengeneza falsafa ya Kitanzania. Kwa kujifunza na kutafakari mawazo ya wengine, tufikie mahali na sisi tutengeneze falsafa ya kutuongoza. Ukisoma kitabu cha Dk.Mihanjo,utagundua kwamba, hakuna Mwanafalsafa anayekubaliana asilimia miamomoja na mwenzake, ama ana mpinga au anajenga juu ya mawazo yake. Lakini daima kitu kipya kinajitokeza kutokana na fikra za waliotangulia. Mwalimu Nyerere, alitengeneza falsafa ya Ujamaa na Kujitemgemea.Falsafa hii imezikwa. Hatukujenga juu ya falsafa hii na wala hatukiipinga na kujenga nyingine, bado tunayumba, hadi leo hii hatuna falsafa inayoeleweka.
Neno falsafa, linaelekea kuwa gumu. Lakini kwa kujisomea vitabu kama hiki cha Dk.Mihanjo, ugumu wa falsafa unayeyuka na mwanga mpya unajitokeza!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment