MSIPOTEZE MUDA KUIUMIZA MIILI YETU; KAMA MNAWEZA SHUGHULIKIA ROHO ZETU! Makala hii ni kwa yeyote anayehusika; yeyote ambaye ana madaraka makubwa juu ya wengine; yeyote anayefikiri yuko juu ya sheria; yeyote anayefikiri anaweza kutoa uhai wa binadamu mwenzake pale anapotaka na kufikiri kwamba yeye ataishi milele; yeyote anayefikiri kuutesa mwili hadi kifo ni mwisho wa kila kitu; kwamba kama ni matatizo yatakwisha. Makala hii ni kwa viongozi wetu waliotufikisha hapa tulipo; tumefika hatua ya Liwalo na Liwe: Kila mtu akizingatia hilo tumekwisha! Tumekuwa tukiimba amani na utulivu kwa miaka mingi, lakini upepo unavyoanza kuvuma tunaelekea mwisho wa Amani na utulivu. Makala hii inaandikwa na wale wote wanaotetea haki za binadamu, wanaotetea haki zao na wale ambao daima wanajitokeza kuwasemea wengine. Tumekuwa tukisema, na sasa tunasema na tutaendelea kusema hata kama wale wa kusikia wanayaziba masikio; tuna imani kelele zetu ziyazibua masikio yao. Yale yaliyomtokea Dakt Ulimboka, yanaweza kumkuta yeyote Yule awe mwalimu, mwanafunzi, mkulima, mfugaji, mwananchi wa kawaida anayepigania haki za kiwanja chake, mwananchi wa kawaida anayepigania haki za ajira yake au machinga anayepigania haki zake. Kuna dalili zote za kutaka kuwatisha watu wanaopigania haki zao. Vishawishi vya kuwaziba midomo vinaposhindwa, nguvu za ziada ziananza kutumika. Inatisha, inakatisha tama, lakini yule atakayevumilia hadi dakika ya mwisho ndiye atakayetetea haki zake na haki za wengine. Makala hii inaandikwa kwa masikitiko makubwa; ni makala ya majonzi, ya kuomboleza, kulaani, kukemea na kutukana unyamaa huu unaoanza kujitokeza kwenye taifa letu. Tulitegemea kwamba jambo hili la unyama huu mpya katika taifa letu lingejadiliwa Bungeni. Tumewachaguwa wabunge kutusemea na kutuwakilisha; lakini baada ya kusikia Spika wa Bunge letu akisema Jambo la Dakt Ulimboka na sakata zima la madaktari haliwezi kujadiliwa Bungeni kwa vile kesi iko mahakamani; Ingawa kujadili sakata hili si kujadili ushahidi wala kujadili kesi inayoendelea. Ukweli ni kwamba madaktari bado wanaendelea na mgomo; watu hawana huduma na mbaya zaidi Dakt amekamatwa, amepigwa na kuumizwa; Bunge likae kimya? Liwe Bubu wakati unyama unaendelea? Ni Bunge la wananchi au Bunge la viongozi na vigogo wachache? Vitisho vinaendelea na labda watu wengine watakamatwa na kupelekwa msitu wa mateso; hatua hii imetufanya kukata tamaa na kubakia na njia ya kutoa maoni kupitia kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Tutajadili vijiweni, tutajadili kwenye daladala na kwenye sehemu zetu za kazi maana huko hakuna Spika wa kuzuia majadiliano. Hatari ya mijadala isiyokuwa na spika wa mwenyekiti, inajulikana duniani kote, moto ukianza kuwaka, kuuzima ni vigumu. Ujumbe wa makala hii ni mfupi: Ni ujumbe kwa yeyote anayehusika kama nilivyotaja hapo juu: Msipoteze muda kuiumiza miili yetu; kama mnaweza shughulikia roho zetu! Tafuta njia, mfumo na mbinu za kuziteka roho zetu! Mwili unakufa, unaoza, unanuka. Hata miili yenu pia itakufa, na kuoza. Lakini roho inabaki na kudumu! Mwenye busara, mwenye hekima, hawezi kupoteza muda wake kuutesa mwili; bali atatafuta njia ya kuiteka roho ya mtu. Kuna njia nyingi za kuiteka roho, na njia hizi ni za wazi na wala si za kificho, njia hizi ni za kukomaza fikra za wananchi kulipenda taifa lao, kulitumikia, kulilinda na kuhakikisha taifa lao linabaki salama kwa vizazi vijavyo. Kiongozi bora ni yule anayetafuta njia zote za kuteka roho za wananchi; akifanikiwa kwa hili anakuwa ametoa mchango mkubwa kwa taifa lake. Kiongozi wa ovyo ni yule anayepoteza muda kuitesa miili ya wananchi wake au kuitukuza miili hiyo. Mwili ni mapambo tu kwenye uhai wa mwanadamu. Mwili unakufa na kuzikwa; hivyo kuutesa na kuufanyia mambo ya kinyama kama alivyofanyiwa Dkt Ulimboka, ni aibu kubwa kwa mtu yeyote mwenye akili timamu. Kwa nini kupoteza muda na nguvu kushughulikia kitu kinachopita na kukiacha kile cha muhimu kama vile roho? Viongozi wa ovyo walioshughulikia miili ya watu na kushindwa kuzishughulikia roho za watu, wamebaki kama vinyago katika historia ya Mwanadamu. Wanatukana na kupambwa na sifa ya mauaji; dunia inawalaani na kubaki kwenye orodha ya watu wa ovyo kupata kutokea hapa duniani. Wale wanaotaka kujiunga na orodha chafu waendekeze utamaduni huu mchafu wa kuwatesa watu wanaotetea haki zao. Orodha chafu ni pamoja na Hosni Mubarak, katika uzee wake amehukumiwa miaka mingi jela, Saddam Hussein, aliyenyongwa hadi kufa kama alivyofanya kwa wapinzani wake, Pol pot, Idi Amin, Mobutu Sese Seko, Nicolae Ceausescu, Slobodan Milosevic, Jean-Claude Duvalier, Ferdinand Marcos, Fulgencio Batista, Antonio Salazar, Alfredo Stroessner, Benito Mussolini na Adolf Hitler. Wote hawa heshima yao ilishushwa na vitendo vyao vya kinyama kuitesa miili ya binadamu. Walishindwa kuziteka roho za watu wao. Hata katika misaafu tunaonywa: “ Basi, msiwaogope watu hao. Hakuna cho chote kilichofunikwa ambacho hakitafunuliwa, wala kilichofichwa ambacho hakitafichuliwa. Ninalowambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong’nezwa, litangazeni kwa sauti kuu. Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja roho...” Matayo:10:26-28. Hapa Tanzania, hakuna mtu mwenye uwezo wa kuangamiza mwili na roho. Hata kwa Dkt Ulimboka, pamoja na mateso yote aliyopatiwa hadi kupoteza fahamu, bado roho yake imebaki imara. Waliutesa sana mwili wake, lakini wakashindwa kuifikia roho yake. Roho haifikiwi kwa vitendo vya kinyama, bali vitendo vya ubinadamu; Haki, wema na huruma. Wakati anapelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi bado alikuwa akisisitiza wenzake kuendeleza mapambano ya kudai haki zao. Mateso ya kinyama aliyoyafanyiwa hayakuigusa roho yake. Uwezo wao unaishia kwenye kuutesa mwili, lakini uwezo wa kuiangamiza roho haupo kwa yeyote yule. Na kama tulivyosikia kutoka kwenye msahafu, kwamba kila kitu kitafunuliwa; je serikali ya kidemokrasia ina siri gani? Serikali ya wananchi, inayochaguliwa na wanachi na kuwekwa madarakani na wananchi ina siri gani kiasi cha kufikia hatua ya kuwakamata watu na kuwatesa? Serikali ya wananchi ina wajibu mkubwa wa kulinda usalama wa taifa, uhai wa wananchi. Na usalama wa taifa, hauna maana ya usalama wa mtu mmoja mmoja, bali usalama wa watu wote. Usalama wa taifa si kumaanisha usalama wa viongozi, ni usalama wa wananchi wote. Usalama wa taifa unapogeuka kuwa wa mtu mmoja au wa viongozi, tunakuwa tumepoteza kabisa maana nzima ya usalama wa taifa. Hoja inayoyejengwa hapa ni kwamba, kama kuna siri ya aina yoyote ile inayolindwa na serikali, ni kwa manufaa ya wananchi wote. Hivyo hakuna sababu ya mtu mmoja kuteswa kwa lengo la kulinda siri za taifa. Hata hivyo kuutesa mwili hakuna maana yoyote ile, maana bila kuigusa roho ni kazi bure. Mfano mzuri, Dk Ulimboka, amepigwa, ameteswa na labda atakufa! Lakini mapambano ya madaktari kudai haki zao yako pale pale! Tumeshuhudia jinsi madaktari walivyokuwa wakisema kwamba tukio la kumpiga mwenzao limewapatia moyo wa kundelea kudai haki zao. Na kama tukiwa wakweli kwa historia; hakuna popote pale duniani ambamko vitendo vya kuutesa mwili vilifanikiwa kubadilisha mawazo ya watu. Viongozi waliotawala kwa mabavu, walijaribu kuwapiga watu, kuwatesa na kuwaua, lakini hawakufanikiwa kufuta roho ya kudai haki. Hata pale ambapo wengine waliendesha mauji ya kimbali bado roho ya kudai haki ilibaki na kudumu. Kumpiga na kumumiza Dkt Ulimboka ni kati ya vitendo vya kinyama vinavyofanywa na binadamu asiyefikiri. Maana mtu anayefikiri vizuri hawezi kumpiga binadamu mwenzake kwa nia yoyote ile; ukimpiga unaumiza mwili wake na roho yake inabaki salama, ukimpiga risasi akafa, unakufa mwili, lakini roho yake inabaki salama. Hadi leo hii tuna roho za watu waliokufa, wako kaburini lakini roho zao ziko salama na zinaishi miongoni mwetu. Roho ya Baba wa Taifa bado tunaishi nayo; roho ya Mkwawa bado tunaishi nayo, roho za mashujaa wote waliokufa wakitetea heshima na maisha ya watanzania bado tunaishi nazo; wao walikufa ili sisi tuweze kuishi kwa uhuru na salama. Hivyo hivyo na sisi lazima tufe tukipambana kulinda uhuru na usalama wa vizazi vijavyo, kinyume na hapo tutakufa na miili yetu na roho zetu! Hivyo kwa kiongozi anayetaka kuiongoza Tanzania, afahamu kwamba kuwapiga watu, kuwakamata na kuwafunga au kuwaua si msaada wa kumsaidia kuwaongoza vizuri. Njia hii imetumiwa na wengi na wameshindwa. Makaburu wa Afrika ya kusini, walimkamata Mandela na kumfunga na kumtesa zaidi ya miaka ishirini na nane, lakini kwa vile hawakufanikiwa kuigusa roho yake, wafuasi wake waliendeleza mapambano hadi alipofunguliwa. Makaburu walifikiri kumfunga Mandela ni kumaliza tatizo, kumbe mbegu ilikuwa imepandwa na inakua kwa kasi ya kutisha. Pamoja na nguvu za jeshi la Arika ya Kusini, hawakufua dafu mbele za nguvu ya Umma. Lakini pia tuko kwenye zama za Demokrasia, mtu anayechaguliwa kuitawala Tanzania, anakuwa na kipindi cha miaka mitano. Baada ya hapo anaweza kuendelea au kuondoka. Na kufuatana na katiba hawezi kupata vipindi zaidi ya viwili , katika hali kama hiyo kuna haja gani kuwa na vyombo vya kuwakamata watu, kuwatesa na kutoa uhai wao kwa lengo la kutafuta maadui wa utawala? Wakati namalizia kuandika makala hii Rais Jakaya Kikwete, anahutubia taifa na kukana kata kata kwamba Serikali haina mkono katika mateso ya Dkt Ulimboka. Na wala sikutegemea Rais, akubali jambo hili la kinyama; na hata akikubali kama ilivyotokea kwa Mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge, hatimaye waliokamatwa na kufikishwa mahakamani waliachiwa huru! Hata kwa Dkt Ulimboka, ni wazi watakamatwa, maana yeye aliwatambua baadhi, ambo hadi sasa inasemekana ni Usalama wa taifa. Kuna mashaka makubwa kama haitakuwa kama ile ya wafanyabiashara wa Mahenge. Hata kama serikali haiusiki na mateso ya Dkt Ulimboka, kwa yeyote anayehusika, apate ujumbe huu kwamba asipoteze muda wake kuitesa miili yetu, bali azishughulikie roho zetu. Lakini ikiwa ni mwendo wa Litakalo na liwe, basi miili yetu iko tayari kupokea mateso ya kutetea haki, ukweli na usawa na roho zetu zitabaki imara! Na, Padri Privatus Karugendo. pkarugendo@yahoo.com +255 754 633122 www.karugendo.net

0 comments:

Post a Comment