UHAKIKI WA KITABU: IS IT THE FUNDAMENTAL CHANGE? 1. Rekodi za Kibibliografia. Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni IS IT THE FUNDAMENTAL CHANGE?, Kimeandikwa na Bagaya Ibrahim Kisubi na Nyanjura Doreen Mchapishaji wa kitabu hiki ni waandishi wenyewe na wamekipatia kitabu chao namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9970-9069-0-1. Na anwani yao ya parua pepe ni thefundamentalchange@gmail.com Kitabu kina kurasa 137 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo. Ukitaka kukipata kitabu hiki piga simu au tuma sms kwenye namba +255 754 6331 22. Bei ya kitabu hiki ni shilingi elfu 15 za kitanzania. II. Utangulizi Kitabu hiki IS IT THE FUNDAMENTAL CHANGE?, kimeandikwa na vijana wawili wa Uganda. Vijana hawa ni Bagaya Ibrahim Kisubi na Nyanjura Doreen na wote wawili wanasoma chuo kikuu cha Makerere. Wamezaliwa, wakamkuta Rais Museveni akiitawala Uganda; wakasoma shule ya msingi, sekondari hadi chuo kikuu bado Rais Museveni anaendelea kuitawala Uganda. Historia inawambia vijana hawa wawili kwamba Rais Museveni, aliingia madarakani akiwa na ahadi ya kuleta Fundamental Change: Madiliko ya msingi au mabadiliko muhimu katika utawala wa nchi ya Uganda iliyokuwa imeparanganyika wakati wa utawala Idi Amin, ukombozi baada ya Idi Amin, na utawala wa pili wa Obote. Swali la vijana hawa, ni je Museveni kuendelea kukaa madarakani na kuikandamiza demomrasia ndiyo Mabadiliko ya muhimu aliyowahaidi waganda? Vijana hawa ambao wanatamani mabadiliko ya kweli ndani ya nchi yao ya Uganda, wanatumia misemo ya watu watatu wa zamani ili kuelezea vizuri kilicho moyoni mwao. Wanawanukuu Mchungaji Martin Niemoller wa Ujerumani, Martin Luther King na Napoleon. Nafsiri ni yangu: “ Walipowashambulia Wajamaa, nilikaa kimya kwa vile mimi sikuwa mjamaa. Wakawashambulia wa vyama vya ushirika na wafanyakazi pia nikaa kimya maana sikuwa kwenye vyama hivyo. Wakawashambuliwa wayahudi nikakaa kimya, sikuwa myahudi mimi. Wakashambuliwa wakatoliki, kwa vile nilikuwa protestant, nikajikalia kimya. Waliponigeukia mimi na kunishambulia hakukuwa tena na wa kusimama kunitetea” Mchungaji Martin Niemoller. “Maisha yetu yanafikia mwisho siku tunapokaa kimya kwa mambo ya msingi” Martin Luther King. “Dunia inateseka sana, si kwa sababu ya watu wakatili na wabaya, bali kwasababu ya ukimya wa watu wazuri” Napoleon. III. Mazingira yanayokizunguka kitabu Kabla sijaanza uchambuzi wa kitabu hiki cha IS IT THE FUNDAMENTAL CHANGE?, ni bora nielezee mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Tarehe 11 mwezi wa nne ni siku yenye kumbukumbu nzito kwa nchi za Uganda na Tanzania. Tarehe kama hiyo mnamo mwaka 1979, majeshi ya ukombozi ya Tanzania na Uganda (Wapiganaji wa msituni) yalifanikiwa kumtimua Iddi Amin kutoka Kampala, na kuandikwa historia ya kumaliza utawala wa kimabavu uliodumu Uganda zaidi ya miaka tisa. Wakati ule ilionekana Iddi Amin, alikuwa amekaa miaka mingi madarakani. Leo hii Rais Yoweri Kaguta Museveni, anakaribia kufikisha miaka 20 akiwa madarakani. Wameziba midomo ya watu wengine kusema na kuhoji na hili halikuwa ni lengo Rais Museveni, alipokuwa akiingia madarakani. Ingawa ushindi huo wa 1979 ulipokelewa kwa furaha na wanganda pamoja na ndugu zao Watanzania, bado kuna ukweli ambao hadi leo hii bado unaishia ndani ya mioyo ya wanganda. Pamoja na mabaya yote yaliyoandikwa na kutangazwa juu ya Iddi Amin, ukweli unabaki kwamba huyu ni rais pekee wa Uganda ambaye hakuwa na mali binafsi, hakuwekeza fedha nje ya nchi; alitumia fedha ya Uganda kwa maendeleo ya Uganda.Hakuwa na fedha nje ya nchi, aliamini fedha zote ni zake na kama zake yeye Rais, bali fedha ni za waganda. Alipokuwa akiikimbia Uganda, alikuwa na uwezo wa kubeba vitu vingi, lakini hata ndege ya Rais ambayo eti alienda kuinunua akiwa na fedha kwenye mkoba na kuwa mtu wa kwanza kununua ndege kwa mtindo huo, hakuondoka nayo, aliicha maana aliamini si mali yake bali ni mali ya Waganda. Inasemekana kwamba nyumba za Ubalozi wa Uganda katika nchi nyingi zenye uhusiano na Uganda zilijengwa na Iddi Amin. Hata nyumba nzuri za Mapolisi zilijengwa na Iddi Amin. Ingawa Iddi Amin, alikuwa mtu ambaye hakuwa na elimu ya juu, lakini alipenda elimu. Vijana wote waliomaliza kidato cha sita wakati wa utawala wake na kushinda kwa daraja la kwanza, aliwapeleka wote kwa nguvu kujifunza ualimu, ili warudi na kuwafundisha watoto wengine. Walimu wengi walipoikimbia Uganda kwa kuogopa usalama wa maisha yao, Iddi Amin, eti alitumia ndege yake ya Urais, kwenda Ghana, kusomba walimu na kuwaleta Uganda ili wawafundishe watoto wa Uganda. Yapo mengi mazuri aliyoyafanya Iddi Amin, lakini yalifunikwa kwa propaganda za kisiasa. Si lengo la uchambuzi huu kumtetea Iddi Amin, bali ni kutolea mfano wa tarehe 11 mwezi wa nne. Kumbu kumbu nyingine mbaya ya terehe hiyo ya 11 mwezi wa nne ni mwaka huu alipokamatwa na kuwekwa ndani binti mdogo wa miaka 22, Nyanjura Doreen, na kuwekwa ndani kwa kuandika kitabu kinachomkosoa Rais Yoweri Museveni. Furaha ya kumfukuza Iddi Amin, imeanza kuleta machungu na masikitiko katika nchi ya Uganda zaidi ya miaka 31 Iddi Amin kutoka madarakani. Kwa vile Tanzania, ilishiriki kikamilifu kumfukuza Iddi Amin, haiwezi kukaa kimya, historia inapojirudia. Ni lazima watanzania kushirikiana na waganda kulaani kitendo cha serikali ya Uganda kumkamata Binti Mdogo na kumfunga gerezani kwa kitendo cha kuandika kitabu. Nyanjura Doreen na mwenzake Bagaya Ibrahim Kisubi, wameandika kitabu : “Is It The Fundamental Change?” wakilenga kufichua ukweli uliojificha juu ya maisha na utawala wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda. Wanasema Rais Yoweri, alipoingia madarakani, alitoa ahadi ya kuleta mabadiliko ya msingi. Kinachoonekana leo ni tofauti kabisa. Vijana hawa wawili na wengine wengi nchini Uganda, wamezaliwa wakati Rais Yoweri akiitawala Uganda, wamekuwa wamesoma hadi chuo kikuu, bado Rais ni Yule Yule. Na hili ndilo swali lao kubwa, kwamba mabadiliko ya msingi yanaweza kuwa na maana yoyote ile kwa kumtengeneza Rais wa maisha? Kwa kuizika demokrasia na kunyamazisha vyama vya siasa vya upinzani? Walichofanya vijana hawa ni kukusanya maneno ya Rais Museveni mwenyewe, na kuhoji ukweli wa yale yote aliyoyatamka siku akiingia madarakani hadi leo hii. Na jibu ni kwamba wakati umefika wa “Mzee” kupisha kizazi kipya. Kitu ambacho Rais Museveni na serikali yake hawako tayari kukisikia, na ndicho kisa cha Kumkamata na kumuweka Doreen na mwezake ndani. Unapofika wakati vijana wakawa tayari kwa lolote, ni hali ya kuogopesha. Kwanza vijana ndiyo asilimia kubwa ya watu duniani. Siku vijana wakikubaliana kuungana na kuwa na sauti moja na kuamua kuingia mitaani; viongozi wanaotaka kuzeekea madarani watapata taabu kubwa sana. Watajikuta nje ya Bunge na ni jambo la kusikitisha kwamba huko vijijni hawatapokelewa Nilikutana na Nyanjura Doreen,mwaka huu jijini Mwanza siku ya Pasaka, akiwa na nakala chache za kitabu chake cha “Is it The Fundamental Change?” Ni vigumu kuamini kwamba msichana mdogo kama Doreen, anaweza kuwa na maneno ya kuongea; maneno ya kuwaomba viongozi waliokaa muda mrefu madarakani, waachie ngazi vijana chipukizi. Doreen Nyanjura,aliniomba nikifanyie uhakiki kitabu chake na kukiweka kwenye magazeti ya Tanzania. Lengo lake kubwa lilikuwa ni kukisambaza kitabu hicho kabla ya kukizundua Jijini Kampala tarehe 11.4.2012. Nafikiri alijua wazi kwamba uwezekano wa serikali ya Uganda kukizuia kitabu hicho kisizinduliwe na kusambazwa ni mkubwa, hivyo aliamua kusambaza nakala chache nchi jirani. Na huo ulikuwa ujumbe tosha kwa Serikali ya Uganda kwamba mbinu za kizamani za kuzuia vitabu kusomwa, kuzuia vitabu kuzinduliwa, zimepitwa na wakati. Sasa kitabu kimefika Tanzania, kutoka hapa kitasambaa Kenya, Rwanda , Burundi na nchi nyingi za kiafrika hata na Ulaya na Amerika. Na kitendo cha kuwakamata waandishi wa kitabu hiki na kuwaweka ndani ni mtindo wa kizamani usiokuwa na tija. Hata mtu ambaye alikuwa hana habari juu ya Nyanjara Doreen, sasa amemfahamu na atataka amfahamu vizuri kwa kutaka kufahamu ni kwanini binti mdogo kama huyo akamatwe na kuwekwa ndani, kutafanya kitabu hicho kitafutwe kwa udi na uvumba. Wakati akinipatia nakala ya kitabu chake alisema “ Karugendo, nisaidie kukitangaza kitabu hiki, maana najua yaliyo mbele yangu. Museveni, atanikamata na kuniweka ndani. Pia anaweza kuamua kuvichoma vitabu vyote”. Nilimsihi kwa vile alikuwa Tanzania, na ana hofu ya kukamtwa, basi abaki Tanzania kama mkimbizi wa kisiasa. Jibu laki lilikuwa “ Siwezi kuikimbia nchi yangu, ninajua nina haki zote za kutoa maoni yangu, ni haki yangu kutetea haki na kuhakikisha demokrasia na mabadiliko ya msingi yanatendeka nchini Uganda. Ni bora nikamatwe, nifungwe na hata ikibidi niifie nchi yangu”. Nilishangaa kuona binti mdogo wa miaka 22, akiwa na ushupavu wa kutisha. Na kweli siku mbili baada ya kukutana naye Jijini Mwanza, alikamatwa siku ya kukizindua kitabu chake na kutupwa gerezani. Uzinduzi wa kitabu chao ulikuwa ni waina yake. Waandishi walivalia nguo za wasomba taka taka na kushikilia mifagio na vyombo vya kukusanyia takataka na kuelekea kwenye uwanja wa Katiba wa jijini Kampala ili kuusafisha waweze kuzindua kitabu chao kwenye uwanja ulio safi. Polisi waliwakamata wakiwa njiani kuelekea kwenye uwanja wa Katiba. Nyanjura Doreen na Bagaya Ibrahim Kisubi, hawakupenda kuwa kimya; walitaka kuyashughulikia mambo ya msingi: Kutetea demokrasia, kutetea haki za binadamu, kutetea uhuru wa kujieleza na kumweleza wazi wazi rais Museveni kwamba amekaa sana madarakani wakati umefika wa kuwaachia wengine nafasi ya kuliongoza taifa la Uganda. Pamoja na ukweli wa kujua kitakachotokea; kukamatwa, kupigwa, kuwekwa ndani na wakati mwingine kupoteza maisha yao, bado waliendelea na mipango yao ya kukizindua kitabu chao kwenye uwanja wa katiba. Hili linashangaza ni ujumbe si kwa Rais Museveni peke yake, bali kwa marais ya Afrika ya mashariki na Afrika nzima: Kwamba mabadiliko ya msingi yataletwa na Kizazi kipya. Matumizi ya silaha yanapitwa na wakati. Mbele yetu ni nguvu ya kizazi kipya mbayo kuizuia ni lazima mtu awe tayari kuwekwa kwenye rekodi ya mauaji ya kimbali. Nilipomshawishi Nyanjura Doreen, kubaki Tanzania kama mkimbizi wa siasa, alikataa kabisa. Kwa maneno yake mwenyewe alisema: “ acha niende kufungwa, acha nife kama ni kufa kwani mimi ni bora zaidi ya nani? Septemba I 2009 zaidi ya vijana 40 waliuawa, hawa ni pamoja Kauma Joseph, Nakazi Deborah, Nahumma Brenda, Katum Richard, Kalamba Ronald, Kamoga Sula, Aliwo Abed, Nabakoza Christine, Bisso Steven,Ssango Kyobe, Ikongo Samuel, Mayanja Bruno, Bukenya Faisal, Mukwanga Kaziru, Benjamin Parnot Ateere, Batiibwe Badru, Muganga Huzair,Busulwa Hassan, Bwesigwa, Grace Sserunjogi, Joseph,Muganga Hakim, Kafuma Frank, Nampijja Jackie, Magembe Ali, Lukwago Sulaiti, Karungi Annet, Erimweya Mawanda, Nsereko Robert, Batibwe Abdullah, Nampijja Beatrice, Nahumma Brenda, Ngaba Moses. Vijana wote hawa isipokuwa Batiibwe Badru aliyekuwa na umri wa miaka 39, walikua kati ya miaka 2-25. Na wengine walikufa kwenye Makaburi ya Kasubi, Masaka, Kampala, Gulu, Jinja, Mbale na sehemu nyinginezo”. Alinielezea haya kwa uchungu mkubwa. Akilalamika kwamba vijana ambao wangepaswa kuwa shuleni wakisoma, wanakamatwa na kuwekwa gerazani. Yeye Doreen na Mwenzake, wako mwaka wa mwisho kwenye chuo kikuu cha Makerere. Waswahili wana msemo wa “Mwenzako akinyolewa wewe tia maji” Sisi watanzania tunajifunza nini kutokana na tukio la Serikali ya Uganda kuwakamata na kuwashitaki waandishi? Baada ya kuona mazingira yanayokizunguka kitabu hiki kilichoandikwa na vijana hawa wa Uganda, sasa kwa kufupi tuone muhtasari wa kitabu chenyewe. IV. Muhtasari wa Kitabu Kitabu hiki kina sura sita. Katika sura ya kwanza tunaelezewa historia ya Uganda, kuanzia Ukoloni, utawala wa kwanza wa Obote, utawala wa Iddi Amin, utawala baada ya kumfukuza Iddi Amin na hatimaye Museveni kuingia madarakani. “ Mwaka 1966... ilishangaza sana Iddi Amin, alipotoka DRC na dhahabu kubwa na kuiuza kwenye Benki ya Uganda na kujipatia fedha ipatayo paundi 17 elfu...” tafsiri yangu.Uk 20 Obote, alimtumia Iddi Amin, kuvuruga utawala wa Kabaka na hatimaye Iddi Amin, akumwondoa Obote madarakani. Uk 22- 23.Inaonyesha wazi kwamba kama Obote, angelikuwa mwangalifu angemshutukia mapema Iddi Amin. Hatimaye Iddi Amin, akawafukuza wahindi kutoka Uganda, kwa kisingizio cha kuinyonya Uganda, huku wakipeleka fedha nje ya nchi. Uk 24. Sura yote ya kwanza inaelezea matatizo ya uongozi yaliyoikumba Uganda hadi kufikia hatua ya Iddi Amin Kuivamia Tanzania, na kosa hilo likasababisha Iddi Amin kufukuzwa Uganda. Sura ya pili inaelezea jinsi Museveni alivyoingia madarakani tarehe kama ile ya Iddi Amin kuingia madarakani. Vijana hawa wanaonyesha tarehe hiyo inavyokuwa na aina fulani ya kuwafananisha Museveni na Iddi Amin. Katika sura hii ya pili ndo tunavyosikia Museveni,aliyeingia madarakani akiwaahidi waganda Mabadiliko ya muhimu, alivyoanza kufanya mbinu za kubaki madarakani kwa kuongeza mihula ya utawala wake. Hadi leo hii baada ya zaidi ya miaka 20 madarakani, Museveni hana mpango wa kuondoka madarakani. Sura ya tatu inaelezea mambo ya ukweli na muhimu juu ya Museveni: Katika kitabu hiki vijana hawa wanasisitiza kwamba kuna mambo mengi muhimu yasiyojulijana juu ya Museveni: Umri wa Rais Museveni ni utata mtupu, hadi yeye hafahamu alizaliwa lini(Uk 54). Kwa maoni ya vijana hawa ni kwamba hata Museveni akitaka kugombea urais 2016, hakuna wa kuhoji juu ya umri wake, maana hata yeye mwenyewe hafahamu umri wake. Wazazi wake nao wana utata. Kwa uhakika mama yake ni Esteeri Kokundeka. Lakini mtu anayejulikana kama baba yake Amos Kaguta, kuna mashaka kama huyu ni baba yake (Uk 54). Ni kwamba familia ya Museveni, haikuwa na uwezo wa kumsomesha, hadi familia ya Byanyima, ikajitosa kumsaidia kusoma. Maelezo ya vijana hawa kwenye kitabu chao ni kwamba Museveni hakuwa na akili za kipekee darasani, ndo maana alipomaliza sekondari hakuweza kupata nafasi ya kusoma Makerere. Alitafutiwa nafasi Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam. Maisha ya kisiasa ya Museveni, yalianzia Dar-es-salaam. Na baada ya kumaliza masomo, Museveni, alipata kazi kwenye serikali ya Obote, sehemu ya usalama wa taifa – kitengo kilichokuwa kinamsaidia Obote, kuendelea kubaki madarakani kwa mabavu. Iddi Amin alipopindua Uganda, Museveni , hakuwa na njia nyingine zaidi ya kukimbia. Hakukimbia kwa moyo wa kizalendo bali alikimbia kuiokoa roho yake ( Uk 55). Tunaelezwa kwamba, kwa kazi yake ya usalama wa Taifa, wakati wa Obote, Museveni, ambaye kwa wakati ule alikuwa kijana alikuwa na fedha nyingi, kiasi kwamba baada ya kukimbilia Tanzania alikuwa na fedha za kutosha kiasi cha kuponda maisha. Aliponda maisha na msichana ambaye baadaye ndiye alifunga naye ndoa, Janet Kataha. Maisha ya starehe ya ya Museveni hayakuchukua muda, kwa vile hakuwa na kazi. Alihangaika kutafuta kazi Tanzania nzima bila mafanikio, hadi akalazimika kufundisha Chuo cha Ushirika Moshi.Mshahara kiduchu alioupata kwa kufundisha Chuo cha ushirika Moshi, ndo ulimsaidia kufunga ndoa na Janet mnamo mwaka 1973. (Uk 57). Baada ya kujiingiza kwenye ukombozi wa Uganda Museveni, alijawa na uchu wa madaraka.Aliamini matumizi ya nguvu kuingia madarakani. Hadi leo hii lugha yake ni “Mauaji” ili kulinda utawala wake. Kwa kulinda utawala kwake, Museveni anaua hata watu waliokaribu yake. Hii ina ushahidi wa miaka mingi. Rafiki zake wa karibu kama Mwesiga Black, Raiti Omongin na V. Rwaheru, walikufa kwenye mazingira ya kutatanisaha ( Uk 60). Ilishangaza kwamba Iddi Amin, alinunua ndege ya rais kwa dola alizokuwa amebeba mfukoni mwake, ukweli ni kwamba hata Museveni anaposafiri nje ya nchi anabeba dola mfukoni kana kwamba hatarudi tena Uganda. Jamaa wa Museveni wanaishi kwenye nyumba za serikali na kupata mshahara (Uk 72). Sura ya nne, inaelezea juu ya siasa za Uongo za Museveni. Tunaelezwa mambo yote kumi ambayo Museveni, aliorodhesha kuyatekeleza alipoingia madarakani mwaka 1986. Mambo haya mengi ni kinyume na jinsi alivyoahidi mbele ya waganda. Mabadiliko ya msingi, yamekwama! Museveni, aliwashambulia viongozi wa Afrika waliokuwa wakienda kwenye mikutano ya kimataifa na ndege zao za kifahari wakati watu wao wakifa kwa njaa, ni viongozi wa ovyo! Leo hii yeye ana ndege ya kifahari ambayo inatumika kuihudumia familia yake. Waganda walishuhudia ndege hii ikimbeba mtoto wa Museveni kwenda Ujerumani kujifungua. Sura ya tano inajadili mzimu wa Luwero. Ukweli ni kwamba watu wengi walikufa Lowero ukilinganisha na wale waliochinjwa na Iddi Amin. Museveni, amekuwa kilaumu uongozi wa Obote, kuendesha mauaji ya Lowero, lakini ukwei ni kwamba Museveni, ndiye chanzo cha mauaji haya! Sura ya sita inajadili vuguvugu la mabadiliko na jitihada za Museveni kunyamazisha nguvu hizi za vijana. Kitabu hiki ni sehemu ya vuguvugu hizi. V. TATHIMINI YA KITABU. Nianze kwa kuwapongeza vijana hawa wawili kwa kujitosa kuandika kitabu hiki huku wakijua hatari kubwa iliyo mbele yao. Ukweli ni kwamba kazi hii ni nzuri sana . Kitabu hiki kinaburudisha, kinasikitisha na kufikirisha. Pili niwapongeze vijana hawa wawili kwa kuthubutu kuandika mambo haya ambayo wengi wangeogopa kuyaandika. Inahitaji moyo wa ushupavu kuandika kitabu kinayofichua ukweli uliofichika, juu ya kiongozi aliyemadarakani mwenye vyombo vyote vya usalama na madaraka makubwa juu ya uhai wa kila raia ndani ya taifa lake. Tatu, ni ule uzalendo wa kuwa tayari kufa kwa kulitetea taifa. Wakati watu wazima wanaogopa kujitokeza kupinga utawala wa mabavu, vijana wadogo wenye umri wa miaka 23, wanajitokeza kuwa msatari wa mbele kuongoza mapambano. VI. HITIMISHO. Ni wazi ningependa kuwashauri wasomaji wangu kukinunua kitabu hiki na kukisoma. Nimeelekeza namba za simu ambazo ni +255 754 6331 22 ili kukipata kitabu hiki. Pamoja na ukweli kwamba bei ya kitabu hiki ni kubwa, ni muhimu kukinunua na kujisomea yale tunayoyajua na tusiyoyajua. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment