UHAKIKI WA KITABU: ADUI WA UMMA. 1.REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA Jina la kitabu kinachohakikiwa hapa ni: Adui wa Umma.Kitabu hiki ni tafsiri ya “Enemy of the People”, kilichoandikwa na Henrik Ibsen, miaka zaidi ya miamoja iliyopita. Kimetafsiriwa na Elias.K.Maarugu.Mchapishaji wa tafsiri hii ya kiswahili ni EK International Publishers na amekipa namba ifutayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 8824 12. Kimechapishwa 1992 kikiwa na kurasa 95.Na anayekihakiki sasa hivi ni mimi Padri Privatus Karugendo. II. UTANGULIZI Adui wa Umma ni tafsiri ya mchezo wa kuigiza ujulikanao kwa jina la “An Enemy of the People”. Mchezo huu ulitungwa mnamo mwaka 1882 na Henrik Ibsen wa Norway, na umetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili na Ndugu Elias K.Maarugu, mnamo mwaka 1982; miaka mia moja baadaye. Mchezo wenyewe una maonyesho matano. Onyesho la kwanza ni sebuleni mwa Dk. Stockmann, onyesho la pili ni kama lile la kwanza. Onyesho la tatu ni Ofisini mwa mhariri wa Gazeti la The Herald.Onyesho la nne ni chumbani katika nyumba ya Kapteni Horster na onyesho la tano ni chumba cha faragha cha Dr.Stockmann. Wahusika katika mchezo huu ni: Dk.Thomas Stockmann, ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji, Bibi Katherine Stockmann, ambaye ni mke wa Dk. Stockmann, Petra, ambaye ni binti wa Dk.Stockmann na ni mwalimu wa shule, Eilif na Morten, ambao ni watoto wa kiume wa Dk.Stockmann, Peter Stockmann, ambaye ni kaka wa Dk.Stockmann na ni Meya wa Mji, Mkuu wa Mgambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Hamamu, Morten Kil, ambaye ni mmilikaji wa Viwanda vya ngozi na ni babamkwe wa Dk.Stockmann, Bwana Hovstad, ambaye ni mhariri wa gazeti la “The Herald”,Bwana Billings, ambaye ni mhariri msaidizi, Kapteni Hoster ambaye ni Kapteni Mkuu wa meli, Bwana Aslaksen ambaye ni mchapishaji mkuu wa mitambo ya magazeti na kuna kundi la wanaume na wanawake wa mchanganyiko kimaslahi na wanafunzi wachache. Maonyesho ya mchezo yanachukua siku nne mfululizo za mwanzoni mwa majira ya vuli mwaka 1882, Mji mmoja kando ya Bahari Kusini mwa Norway. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya mchezo, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayoitangulia tafsiri hii ya kiswahili. III. MAZINGIRA YANAYOKIZUNGUKA KITABU. (TAFSIRI YA KISWAHILI). Bwana Elias K.Maarugu, alifanya kazi ya kutafsiri kitabu hiki mnamo mwaka 1982, lakini kwasababu ya kushindwa kupata pesa za uchapaji, alikaa na muswada kwa kipindi cha miaka 10! Mwaka 1991, Bwana Maarugu, aliombwa na Mama Keti Kamba, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa UWT enzi hizo, amwakilishe katika warsha ya Elimu ya Mazingira.Warsha hiyo ilimwezesha Bwana Maarugu, kukutana na Bw.Peter Martin, ambaye alikuwa Afisa Elimu Mfawidhi (World Wide Fund WWF for nature UK). Bw.Peter Martin, katika risala yake ya kuelezea umuhimu wa warsha hiyo ya elimu ya mazingira, kwa wanawarsha, aligusia maudhui yanayojitokeza katika kitabu cha Isben “An Enemy of the People”, kwa kutoa mfano jinsi ambavyo maslahi binafsi ya wanasiasa wenye uroho wa fedha, yanavyoweza kuvuruga mipango ya miji na kuleta maafa kwa masuala ya mazingira siku za uzoni. Bwana Maarugu, alitumia mwanya huo kuongea na Bw.Peter, juu ya mswada wa Adui wa Umma, alikokuwa amekaa nao zaidi ya miaka kumi bila kuchapishwa. Kuanzia hapo mwanga mpya wa kukichapisha kitabu ulipatikana.Bw.Peter, kupitia WWF, alitoa pesa za kuchapa kitabu cha Adui wa Umma. Pesa zilizotolewa, ziliweza kuchapisha vitabu elfu tano. Ingawa kitabu hiki kilichapishwa mwaka 1992, sasa ni zaidi ya miaka kumi, kitabu hiki hakijasambaa nchi nzima. Hakipatikani kwenye maduka ya vitabu.Bwana Maarugu, nafikiri aliamua kukisambaza yeye mwenyewe na bila shaka kazi ilikuwa ngumu kwake. Hivyo anayekitaka kitabu hiki, amtafute Mheshimiwa Maarugu, Mkuu wa Wilaya ya Mishenye –Kagera. Nami nilipata bahati ya kukipatakitabu hiki nilipomkuta Bwana Maarugu, Magu, akiwa mkuuu wa Wilaya. Lakini pia kwa vile sasa hivi watu wanajadili mswada wa Habari, ni vyema watu wakakisoma kitabu hiki wakaona jinsi mapambano na Ya Jamii, Serikali na Waandishi wa habari, yalivyo ya siku nyingi. Pia mtu anaweza kuona vizuri ugumu wa kuwa mhariri wakati mwenye gazeti anatetea maslahi binafsi.Mchezo huu umetungwa zaidi ya miaka miamoja iliyopita lakini ujumbe wake ni waleo hii! Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muthasari. IV. MUHTASARI WA KITABU Adui wa Umma ni mchezo wenye vitendo vitano.Ni mchezo wenye dhamira za kisiasa.Aidha unatokana na mgogoro kati ya msema kweli mmoja aitwaye Dk.Stockmann, na Meya wa Manispaa, Peter Stockmann.Kwa kifupi ni kwamba, Manispaa hii ilikuwa imejenga “hamamu” kwa ajili ya shughuli za starehe na utalii.Mradi huu ulibuniwa na Dk. Stockmann na Peter Stockmann, Meya wa Manispaa.Matokeo ya mapato haya yalikuwa makubwa kwa wakazi wote wa jiji: kulikuwa na nafuu ya kodi kwa wananchi, na viongozi walifurahia matunda ya kazi yao. Kwa bahati mbaya, kulijitokeza magonjwa Fulani ambayo, Dk.Stockmann, Bwana Afya wa Manispaa, alidhani kuwa yanatokana na maji ya “Hamamu”. Alifanya uchunguzi na kuthibitisha jambo hilo.Uchafu uliokuwa unatoka kwenye kiwanda cha ngozi ulikuwa unaingia kwenye mabomba yaliyokuwa yakielekea kwenye “hamamu”. Dk.Stockmann, alichukua hatua za kuwaeleza viongozi wenzake. Meya wa jiji hakupendezwa na ukweli huo.Dk Stockmann pia, alishauri mabomba yatolewe yalipo na yatandikwe upya.Hali kadhalika ushauri huu haukukubaliwa na Meya.Basi watu hawa walikubaliana kutokukubaliana. Dk.Stockmann alisimama upande wa utaalam wake na ukweli.Naye Meya Peter Stockmann aliuona ushauri na msimamo huo wa ukweli kama shambulizi la moja kwa moja kwa uongozi wake na yeye binafsi. Mvutano huu ulisababisha mapambano kadhaa.Dk.Stockmann, alitarajia kuchapisha ripoti ya uchunguzi wake katika gazeti la “The Herald”.Hakufaulu kwani gazeti hili lilimilikiwa na kufadhiliwa na ongozi wa manispaa.Kuchapisha ripoti hiyo kungesababisha kufungwa kwa gazeti hilo. Uwanja mwingine wa mapambano ulikuwa mkutano wa hadhara. Pande zote mbili zilieleza tatizo hili. Dk. Stockmann alikuwa akisema ukweli.Hakusikilizwa na badala yake alizomewa na kudhihakiwa, kitu ambacho kilisababisha kugawanyika.Upande wa Peter Stockmann ulikuwa ukimshitaki Dk.Stockmann, kuwa ni shabiki, mchafuzi wa amani ya umma na kwa hiyo ni adui wa umma. Swali ambalo lingekuwa la kwanza kuulizwa ni hili: ni nani kweli adui wa umma? Dk. Stockmann au Peter Stockmann? Je adui wa umma ni yule anayeamua kusema ukweli na kufichua aibu na mizizi ya magonjwa katika jamii, au yule ambaye ni mnafiki, anayeficha uozo kwa ajili ya kulinda maslahi yake binafsi ya kikazi.Je adui wa umma anaweza kuwa ni yule mwenye nia ya kuondoa maovu, rushwa, ujinga na uongo, umaskini na uchafu uliomo katika Jamii? Hadi mwisho wa mchezo tunamwona Dk,Stockmann akisimama peke yake na akisimamia ukweli mtupu bila ya kujali kama anaungwa mkono na watu wengine au la!Kwa maneno yake mwenyewe anasema hivi: Dk, Stockmann: “ Ndiyo,- uvumbuzi wenyewe ni huu –mwanaume shupavu duniani ni yule anayeweza kutetea msimamo wake peke yake hata kama haungwi mkono… uk 92” Katika kusema na kutetea ukweli Dk. Stockmann,alikuwa na changamoto nyingi.Yeye na kaka yake Peter Stockmann, walibuni hamamu.Na kweli zikawa kitegauchumi cha mji.Mapato ya mji yalipanda sana na wenyeji wa mji walipunguziwa kodi.Ukweli kwamba hamamu hizo zilikuwa na wadudu wanaosababaisha magonjwa ya binadamu kungesababisha kufungwa kwa hamamu, Na kuporomoka kwa mapato.Meya wa mji ambaye alikuwa kaka yake Dk.Stockmann, angeingia matatani na labda kupoteza umeya.Alimtaka mdogo wake kuuficha ukweli ili kulinda cheo chake!!Na kulinda kipato cha mji.Mabishano yao yalikuwa hivi: Peter Stockmann: Ndiyo maana unafanya juu chini kuhakikisha kuwa unapokonya mji huu chanzo pekee cha kujipatia mapato,sivyo? Dk. Stockmann: Hi huelewi? Chanzo chenye sumu, bwana! Umekuwa mwehu? Tunaendesha shughuli za utalii kwa kuuza uchafu na maradhi; kwa nini ustawi wa maisha yetu utokane na uongo… uk36. Peter Stockmann: Hizo ni ndoto tupu na za hatari.Mtu ye yote ambaye anaweza kutoa ushauri wa kupotosha kama huu kuhusu mji wake si mtu wa amani, bali ni adui wa umma…uk36 Meya wa mji ambaye ni kaka yake Dk.Stockmann, alimtishia kumfukuza kazi kama angefichua ukweli wa vijidudu kwenye maji ya hamamu. Alimshauri akae kimya kuwasikiliza wakubwa zake: Peter Stockmann: Kwa kuwa u mtumishi wa kamati, huna haki ya kufuata mawazo yako binafsi…. Si katika wadhifa wako wa kikazi.Ungalikuwa mwananchi wa kawaida, hili lingekuwa jambo jingine. Lakini maadamu u mfanyakazi mwenye madaraka ya chini, huna haki kutoa mawazo ambayo yanapinga na yale ya wakubwa wako..uk.33 Changamoto nyingine kubwa iliyokuwa mbele ya Dk.Stockmann, ni kwamba vile viwanda vya ngozi vilivyokuwa vikizalisha uchafu uliokuwa uaingia kwenye mabomba ya hamamu vilikuwa vya Baba mkwe wake, Bwana Morten Kil. Kufichua ukweli wa uchafu huo ilikuwa ni kupiga vita viwanda vya Baba Mkwe wake.Bwana Morten Kil, alikuwa ameandika urithi wake kwenda kwa binti yake; mke wa Dk Stockmann na watoto wake. Sasa alikuwa akitumia urithi huo kumzuia Dk. Stockmann, kusema ukweli: Morten Kil: Na jana usiku ulisema kwamba kiwanda chagu cha ngozi ndicho kinaongeza uchafu. Kama hivyo ndivyo iliyo, basi baba yangu, na babu, wamekuwa na wanautia mji huu uchafu kwa karne nzima.Kama malaika watatu waharibifu.Huwezi ukafikiri kwa dakika moja tu kwamba sitavumilia kashafa ya namna hiyo ikivumishwa dhidi yangu bila kuchukua hatua yoyote- unafikiri hivyo?… uk 84 Morten Kil: Vema, sina budi kuondoka.Lakini lazima unifahamishe kwa njia moja ama nyingine.Na iwapo hutafanya hivyo, hisa zote zitakwenda kwenye misaada ya huru mchana huu…uk 85. Pamoja na shinikizo la Baba Mkwe, kwamba Dk,Stockmann, akae kimya ili apate urithi wa viwanda vyenye kuzalisha uchafu na vijidudu – alikataa na kuendelea na mpango wake wa kusema ukweli.Mke wake alijaribu kumshawishi.Alimkumbusha kwamba wana watoto watatu.Wawili walikuwa bado wanasoma shule. Akifukuzwa kazi – wangeshindwa kuwasomesha. Lakini Dk.Stockmann, alisimama kidete: Dk. Stockmann: Kate! Umepagawa! Yaani kwa sababu mtu ana mke na watoto watatu aongope kutangaza ukweli, kuwa raia wa manufaa- asitimize wajibu wake katika maisha..uk.50 Marafiki zake wahariri wa gazeti la “The Herald, waliogopa kuchapisha makala yake.Gazeti hili lilimilikiwa na kufahdiliwa na uongozi wa manispaa. Wangechapisha makala ya Dk. Stockmann, hamamu zingefungwa na uchumi wa mji ungekwenda chini.Kodi ingepanda.Watu wangeacha kununua magazeti.Na gazeti lingefungwa.Hivyo wahariri hawakuangalia ukweli.Walizingatia mishahara na maslahi yao binafsi! Binti mkubwa wa Dk. Stokmann, Petra, alifukuzwa kazi, kwa sababu ya ukweli wa baba yake.Alikuwa anafanya kazi ya ualimu.Watoto wake wawili wavulana walifukuzwa shuleni walikokuwa wanasomea.Yeye mwenyewe Dk.Stockmann, alifukuzwa kazi na kufukuzwa kwenye nyumba na kupachikwa jina la Adui wa Umma. V. Tathmini ya kitabu. Bwana Elias K.Maarugu, alifanya kazi nzuri ya kuutafsiri mchezo wa Ibsen, “An Enemy of the people” katika lugha ya kiswahili. Ni imani yangu kwamba watu wakiusoma mchezo huu wa Adui wa Umma.Tutagundua kwamba Adui wa Umma si Dk.Stockmann, bali kaka yake Peter na viongozi wengine wa Manispaa.Adui wa Umma ni wahariri wa magazeti wanaoogopa kuandika ukweli ili kulinda biashara yao. Mchezo huu ni wa maana kwetu, ukizingatia kwa sasa hivi viongozi na wanasiasa wanatanguliza maslahi binafsi na wanakuwa na uroho wa fedha, hii inaweza kuvuruga mipango ya miji yetu na kuleta maafa kwa masuala ya mazingira siku za usoni.Watu wanagawiwa viwanja vya kujenga majumba ya makazi na mahoteli bila kujali hifadhi ya mazingira.Vyanzo vya maji vinaharibiwa.Mahoteli yanajengwa bila mpango kwenye ufukwe wa babari. Ingawa mchezo huu umetungwa zaidi ya miaka 100, lakini unafaa sana kwenye mazingira ya leo na hasa hapa Tanzania, kama nilivyodokeza mwanzoni, ni kwamba sasa hivi kuna muswada juu ya vyombo vya habari.Pia tumeshuhudia kila siku matumizi mabaya ya vyombo vya habari, tumeshuhudia jinsi wahariri waliyotumiwa vibaya ili kulinda maslahi ya wenye vyombo hivyo. Tunalilia uzalendo.Mchezo huu, unaonyesha mfano wa mtu mzalendo.Mtu huyu ni Dk.Stockmann, anasimama kidete, hadi anapoteza kila kitu kwa kusimamia ukweli.Watoto wake walipofukuzwa shule, aliamua kuwafundisha yeye mwenyewe akisaidiana na binti yake mkubwa Petra: Dk.Stockmann: Na tutaanzisha shule yetu katika chumba kilekile walimoniita mimi adui wa Umma.Lakini nyinyi wawili tu hamtoshi hatuna budi tuwe na vijana kama kumi na wawili wa kuanzia… Vema! Baadaye mtaenda mitaani mkawalete mtakao waona.Kwa majaribio tutaanza na watoto wa ombaomba – kwa safari mmoja tu – matokeo yanaweza yakawa ya kufurahisha-uk.92 Mtoto mmoja aitwaye Morten, aliuliza swali kwa baba yake: Lakini Baba tutafanya nini baada ya kukua na kuwa wenye mawazo mapana na walio mashujaa..Uk 92, Dk.Stokmann: Wafukuzeni hawa mbwa mwitu wote…92. Hata hapa Tanzania, kazi ya wanamapinduzi, kazi ya wazalendo na kizazi cha leo, ni kuwafukuza mbwa mwitu wote. Wale wote wanaoshughulikia maslahi binafsi bila kuaanglia maslahi ya taifa zima, ni lazima wafukuwze kabisa! Hivyo mchezo huu ni muhimu kwetu sote maana anayesema viongozi wanakula rushwa ndiye anaonekana kuwa adui wa umma.Kila msema kweli hapa kwetu ni adui wa umma. Na wasema ukweli wote wanapata mashinikizo kama ya Dk. Stockmann.Mashinikizo ya kaka, dada, mjomba, wanandugu, wanaukoo, wakwe, kabila, ukanda hadi kwa wanamtandao.Na yeyote anayetoa shinikizo kwa msema ukweli, anaangalia maslahi yake na tumbo lake.Haweki mbele maslahi ya watu wengine na ustawi wa taifa zima.Kwa maneno mengine Adui wa Umma, ni adui wa matumbo ya watu wachache wanaopenda kuneemeka kwa gharama ya maisha ya watu walio wengi. VI. HITIMISHO. Pamoja na pongezi zangu kwa Bana Maarugu, ningependa kuwahimiza watanzania kukizoma kitabu hiki, maana kuna mengi ya kujifunza na kulinganisha na yale yanayotokea katika taifa letu. Mfano mtu akifanya utafiti juu vipodozi, akasema vipodozi ni hatari kwa ngozi, kwamba vipodozi vinasababisha magonjwa ya ngozi na hata kasa.Wenye viwanda vya vipodozi, wenye maduka na wenye salooni, watamnyoshea kidole mtafiti huyo na kumpachika jina la adui wa umma.Wenye salooni, viwanda na maduka ya vipodozi wanashirikiana kwa karibu sana na viongozi wa serikali - na wakati mwingine ni mali za viongozi.Hivyo ukweli wa usalama wa vipodozi hautegemei mtafiti.Unategemea tamko la serikali.Mtafiti akikazana kuonyesha ukweli- atanyoshewa kidole na kupachikwa jina la Adui wa Umma. Gongo ni pombe ya hatari.Ni sumu tupu na hatari kwa afya ya binadamu.Inatengenezwa kienyeji na vyombo vinavyotumika kuitengeneza kama mapipa yenye kutu na mirija iliyotengenezwa kwa vyuma si salama.Hapa Tanzania, tuna sheria ya kuzuia pombe hii ya gongo.Sheria hii imekuwa kama pazia la maafisa watendaji wavijiji na mapolisi kujipatia hongo.Watu wanaendelea kunywa gongo na kujaza sumu mwilini.Mtu akijitokeza na kupendekeza sheria ya kuzuia gongo ifutwe- atanyoshewa kidole na kupachikwa jina la Adui wa Umma.Kuzuia gondo ni kuziba riziki: polisi ameangalia hapo, mtendaji pia!Watu wanasomesha watoto, wanajenga nyumba na kumili mashamba makubwa kwa kutumia pesa ya gongo.Wanastawi kwa kuuza na kueneza sumu katika jamii. Kuna mifano mingi inayoonyesha jinsi maadui wa Umma, wanavyoshughulikia maslahi binafsi na kulitelekeza taifa. Wao wanajiona wanafanya vizuri, na kuwageukia watetezi wa ukweli kuwa wao ndo maadui wa umma.Pia ningependa kumshauri Bwana Maarugu, afanye mipango ya kukisambaza kitabu hiki.Kukiacha vunguni mwa kitanda, ni sawa na kusema alifanya kazi bure maana kitabu kilicho vunguni hakiwezi kusambaza maarifa katika jamii. Na, Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment