UHAKIKI WA KITABU: CORRECT LINE? UGANDA UNDER MUSEVENI
1. Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni “ Correct Line? Uganda Under Museveni”. Kimeandikwa na Olive Kobusingye. Mchapishaji wa kitabu hiki ni AuthorHouse UK Ltd na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978-1- 4520- 3962- 6 (sc). Kimechapishwa mwaka huu wa 2010 kikiwa na kurasa 213. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Rafiki yangu mganda, aliponipatia zawadi ya kitabu hiki cha Correct Line? Uganda Under Museveni, aliniambia kwamba watanzania wana tabia ya wizi na udanganyifu; wanachakachua kila kitu hadi kura! Lakini ukitupa kitabu hakuna wa kukiokota wala kukiiba! Maana yake kwamba watanzania hatusomi vitabu. Nina imani hata aliponipatia kitabu hiki aliamini sitokisoma. Nami kwa hasira nimekisoma na kukifanyia uhakiki. Nina imani watanzania wataniunga mkono kukitafuta kitabu hiki na kukisoma na kusoma vingine vingi.
Je, umesoma kitabu maarufu cha Museveni “Sowing the Mustard Seed”? Kama bado, basi kakisome kwanza ndo upate furaha ya kusoma Corret Line? Maana kama ulikuwa na mawazo kwamba Obote na Amin, waliitawala Uganda kwa vitisho, mateso na mauaji; Mkombozi Museveni, kama si pacha wa hao waliomtangulia basi ni mzimu wao uliofufuka! Tumekuwa tukisikia kwa mbali malalamiko ya watu wa Uganda, kwamba Museveni hapendi kutoka madarakani; lakini hadi sasa hakuna mtu aliyefanikiwa kuweka wazi ukweli wa Museveni kama alivyofanya Olive Kobusigye, katika kitabu chake cha Corret Line?
Mwandishi, ametumia kitabu cha Museveni “Sowing the Mustard Seed” kuandika kitabu chake; anayatumia maneno mazito ya mwanamapinduzi Museveni, kuonyesha jinsi anavyofanya kinyume. Kitabu kinazo sura kumi na tisa na picha tisa zinazoonyesha matukio ya Uganda chini ya Utawala wa Mwanamapinduzi Museveni. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokitangulia kitabu hiki.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
Historia ya Uganda, inajulikana vizuri kwa watanzania, maana uchumi wetu uliokuwa unaendelea vizuri kwenye miaka ya sabini, uliyumba vibaya na haukurudi katika hali yake hadi leo hii kwa sababu ya Tanzania kushiriki kikamilifu kumwondoa madarakani dikteta Idi Amin wa Uganda. Baada ya kumwondoa Idi Amin, ambaye watanzania na dunia nzima waliamini alikuwa dikteta na mwuaji, Uganda ilitawaliwa kwa kusuasua, hata na utawala wa Obote kwa mara ya pili ulikuwa ni wa kusuasua hadi pale alipojitokeza Mkombozi na Mwanamapinduzi Yowei Museveni.
Hapana shaka kwamba Museveni, aliivusha Uganda kutoka katika hali mbaya ya Uchumi, makundi na kujenga nchi yenye umoja. Hali ya wasi wasi iliyokuwa Uganda, ilianza kupotea wakati wa utawala wa Yoweri Museveni. Tatizo kubwa lililokuja kujitokeza baadaye ni kwamba Yoweri Museveni, hapendi kuondoka madarakani. Uganda wamefanya uchaguzi mkuu mara mbili na sasa mwanzoni mwa mwaka kesho wanafanya uchaguzi mwingine, lakini inavyoelekea Yoweri Museveni, ataendelea kutawala.
Museveni, alipoingia madarakani, alijigamba kwamba vita ya msituni ilifanikiwa kwa vile wao wapiganaji walikuwa wakitembea juu ya mstari ulionyooka, au mstari sahihi. Au kwa maneno mengine njia yao ilikuwa sahihi na ilikuwa amenyooka. Mwandishi wa kitabu, anauliza kwamba mbona njia hiyo, au mstari huu umeanza kupinda? Mbona badala ya kunyooka umekuwa mviringo? Ndo maana ya jina la kitabu Correct Line?
Museveni, aliyeingia madarakani akijigamba kuijenga Uganda yenye demokrasia safi na ya kuigwa barani Afrika, hataki kuondoka madarakani. Anaamini bado ana kazi kubwa ya kuijenga Uganda; akiulizwa kuondoka madarakani anajibu kwa lugha yake ya Kinyankole: “ Niinye nahiigire enyamaishwa yange nkagiita. Mbwenu ngu ngyende! Nzehi?” Tafsiri isiyokuwa rasmi; “ Mimi ndo niliwinda, nikafanikiwa kuua mnyama wangu, sasa wakati wa kula nyama, eti niondoke? Niende wapi?” (Uk 98).
Kitu kisichofahamika kwa wengi, ni kwamba wale wote wanaompinga Museveni, wanakamatwa, wanapigwa na kuwekwa ndani. Wengine wanakufa kama tutakavyosoma kwenye kitabu hiki. Visa vya Museveni, kutaka kuhakikisha anabaki madarakani havina tofauti na visa vya Idi Amin na Obote. Kama tulimchukia Idi Amin, kwa udikteta wake na kukiuka haki za binadamu, tuna sababu gani za msingi kumkumbatia Museveni ambaye baada ya kuwinda anataka madaraka yote ya kuchinja, kupika na kugawa nyama yabaki mikononi mwa mwindaji: ... “All power belongs to the hunter” (Uk 98).
Waliofanikiwa kutoroka wanaishi nje ya Uganda, inakuwa vigumu kuishawishi dunia juu ya “Mwindaji” wa Uganda, maana sifa nzuri juu yake zimezagaa dunia nzima na anajua namna ya kujieleza na kuandika kama vile alivyoandika kitabu chake “Sowing the Mustard Seed” na kile kingine cha “ What Is Africa’s Problem?”.
Mwandishi wa kitabu hiki Olive Kobusingye, ni daktari bingwa wa upasuaji na kuwashughulikia majeruhi. Alisoma Makerere, Chuo Kikuu cha London na Chuo Kikuu cha Jimbo la New York. Ameishi na kufanya kazi Uingereza, Amerika, Kenya, Congo DRC na Zimbabwe. Ameolewa na ana watoto wawili wasichana. Sasa hivi anaishi na kufanya kazi Uganda. Alikuwa shabiki na mfuasi wa Museveni, wakati mstari ukiwa bado umenyooka, baada ya muundo wa duara anafikiri wakati umefika wa mabadiliko. “Mwindaji” lazima apumzike ili walio nyuma yake waendeleze kazi ya uwindaji.
Kitabu kimeandikwa kwa kumbukumbu ya kifo cha Saasi, mdogo wa mwandishi aliyekufa akiwa gerezani kwa kosa la kuonyesha dalili za kupinga utawala wa Museveni usiokuwa na kikomo. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.
IV. Muhtasari wa Kitabu
Dibaji ya kitabu kiki imeandikwa na Profesa J.Oloka-Onyango, kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Makerere. Anampongeza Olive Kobusingye, kuandika kitabu juu ya Utawala wa Museveni. Kwa maoni yake hiki ni kitabu cha kwanza kinachoonyesha upande mwingine wa Museveni, maana vitabu vingine vingi vinavyoandikwa na wasomi wa Uganda, ni vya kumtukuza Mkombozi Museveni.
Profesa Oloka-Onyango, anakubaliana na Olive Kobusignye, kwamba mstari sasa umekuwa duara. Kwamba hakuna mstari ulionyooka wakati Museveni, anatumia jeshi kufanya kila analolitaka hata kuhakikisha uchaguzi mkuu unaendeshwa kwa usimamizi wa Jeshi. Kwamba hakuna mstari ulionyooka wakati Uongozi wa nchi umekuwa ni mali binafsi na mali ya familia. Kwamba mke wa Museveni ni waziri, mtoto wake ana cheo cha juu jeshini, ndugu zake wana vyeo vya juu na ndugu wa mke wake ndo wameshikilia hazina ya Uganda.
Pia, anatuhakikishia kwamba Olive Kobusingye, ni mtu aliyekuwa karibu sana Yoweri Museveni, alikuwa msaidizi wake, alikuwa shabiki wake na alikuwa kada kwa NRM. Hivyo anayoyaandika si ya kubahatisha wala kutunga, ni ukweli wenyewe!
Sura ya kwanza Mwandishi, anaelezea kisa kilichompata wakati wa uchaguzi mkuu wa 2001. Jinsi Jeshi lilivyokuwa likitumika kuwapiga na kuwaweka ndani wale wote waliokuwa wakimuunga mkono mpinzani mkubwa wa Museveni Dr.Warren Kizza Besigye. Ukatili anaouelezea, hauna tofauti na enzi zile za Idi Amin wa Uganda. Tofauti ni kwamba Idi Amin, alichukiwa na vyombo vya habari na vilihakikisha vinasambaza habari zake hata zingekuwa ndogo kiasi gani. Museveni, amehakikisha vyombo vya habari viko chini ya himaya yake. Anafanya hivyo kwa kutumia fedha nyingi za walipakodi wa Uganda. Hivyo yale anayoyaelezea Komusignye katika kitabu chake ni vigumu kuyasikia kwenye vyombo vya habari na taarifa tulizonao ni kwamba kitabu hiki kimepigwa marufuku Uganda.
Sura ya pili inaanza na nukuu kutoka kwenye kitabu cha Yoweri Museveni cha “ What is Africa’s problem”, Museveni anasema; “ Kama serikali haijishughulishi kumaliza matatizo ya wananchi wake, inategemea nini? Inategemea amani” tafsri ni yangu.
Museveni, amekuwa akiutumia msemo huu kuonyesha kwamba serikali za Uganda zilizotangulia zilikuwa hazikushughulikia matatizo ya jamii ya Uganda. Amekuwa pia akimlaumu sana Obote, kutumia jeshi kupigana na Kabaka wa Uganda. La kushangaza ni kwamba Museveni mwenyewe, Septemba 2009, alitumia jeshi kupambana na Kabaka, na watu zaidi ya ishirini walikufa! Na yapo matukio mengine mengi yanayotajwa kwenye kitabu hiki yanayoonyesha jinsi Museveni, anavyotenda kinyume na msemo wake ulioandikwa kwenye kitabu chake.
Sura ya tatu nayo inaanza na nukuu kutoka kwenye kitabu cha Museveni cha “Sowing the Mustard Seed” anaposema hivi “ Kazi yetu ilikuwa ni moja tu; kupigana na kurudisha uhuru wetu, ambao tulimaanisha wananchi wapate nafasi ya kujiamulia maisha yao bila kuburuzwa”
Hapa mwandishi anatuelezea jinsi hayo maneno yaliyoandikwa kwenye kitabu cha Museveni na kuwavutia watu wengi, hayafuati tena. Watu wa Uganda wanaburuzwa na hawapati nafasi tena ya kujiamulia maisha yao wenyewe. Watu waliokuwa karibu sana na Museveni, kama vile Dr. Besigye, waliaanza mipango ya kutaka kumpinga katika uchaguzi baada ya kuona kwamba hataki kabisa kuondoka madarakani.
Sura ya nne pia inaanza na nukuu kutoka kwenye kitabu cha Museveni cha “ What Is Africa’s problem: “ Mfumo unaweza kuonekana ni wenye uhuru, lakini ukiangalia kwa undani unakuta si kweli. Kwa mfano unaweza kutumia ujinga wa wananchi na kuwaburuza kuyaunga mkono yale yanayopingana na uhuru wao. Je huo ni uhuru? Je uhuru una maana ya kuburuzwa? Kuwanyima watu habari na kutumia ujinga wao kama mtaji? Hiyo ndiyo demokrasia? Mimi binafsi nafikiri si kweli”(uk 26) tafsiri ni yangu
Mwandishi anaonyesha kwamba yale aliyoyaandika Museveni na kuutangazia ulimwengu mzima, ni kinyume kabisa na ukweli wa Uganda hivi leo. Mfano uchaguzi mkuu wa 2001, ulifanyika wakati vyama vya siasa vimepigwa marufuku. Kwa maneno mengine ni kwamba watu walikuwa wanaburuzwa kukubaliana na uamuzi wa NRM. Anatoa mifano mingi kuonyesha uongo uliokuwa unaenezwa dunia nzima kwamba NRM, ni mfumo wa demokrasia ya aina yake, au demokrasia ya Waafrika. Ukisoma misukosuko aliyoipata Dr.Besigye na watu waliokuwa karibu na yeye, unajiuliza ni kwa nini Museveni, alikuwa akipinga mfumo wa kuwaburuza watu? Mbona yeye sasa anawaburuza watu? Au baada ya kukaa sana kwenye madaraka mawazo yake yamebadilika? Tuvichome vitabu vyake na kuomba aandike vingine?
Sura ya tano inaanza na nukuu ya Museveni, kutoka kwenye hotuba aliyoitoa kukubali kuteuliwa na NRM kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2001. Alisema hivi: “ Nimekwisha tumikia awamu moja ya urais kati ya awamu mbili zinazopendekezwa na katiba yetu ya 1995, hivyo bado nina nafasi ya kusimama tena kugombea na pia kwa vile nyinyi mmeniomba, lakini pia bado ninaamini kwamba kuna kazi ambazo bado sijazikamilisha. Hivyo ningependa kuwa mgombea wa urais kwa sababu kubwa mbili: Ninaona jeshi letu halijawa na ujuzi wa kutosha, siwezi kuondoka madarakani bila kuhakikisha kwamba jeshi letu ni imara. Nafikiri mimi ndo ninaiweza kazi hii ya kuliimarisha jeshi maana ninalifahamu vizuri. Pili, ni lazima tuwe na mfumo mzuri wa kurithishana madaraka, mimi siwezi kuwa sehemu ya kurithishana madaraka bila utaratibu. Najua tutashinda uchaguzi, na baada ya hapo tutakaa na kupanga nani wa kuvaa viatu vya Museveni...” (uk 34) tafsiri yangu.
Mwandishi anatuchambulia vizuri uongo na kweli wa Museveni, kutaka kubaki madarakani, akisisitiza kwamba yeye ndo anaweza kulifanya jeshi la Uganda kuwa imara. Kufuatana na mifano inayotolewa kwenye kitabu, ni wazi kwamba jeshi la Uganda, linaweza kusimama imara hata kama Museveni, akitoka madarakani. Uamuzi wa mtu wa kuvaa vitatu ya Museveni, ni wa watu wa Uganda wote. Si uamuzi wa NRM peke yake!
Sura ya saba inatuelezea utata wa mwamuzi wa mchezo kuwa mchezaji kwenye timu mojawapo kati ya mbili zinazoshindana. Hili limekuwa tatizo la nchi zote Afrika, ambazo hazina tume huru ya uchaguzi na Tanzania inaogelea kwenye mfumo huu. Kwa maana nyingine ni kwamba Museveni, akiendelea kuwa mwamuzi wa mchezo, ni ndoto upinzani kupata nafasi ya kuiongoza Uganda. Kwenye sura hii pia tunasikia nukuu ya Museveni kutoka kwenye kitabu chake cha “ Sowing the Mustard Seed” pale anaposema hivi:
“ Kutokuaminika ni kikwazo kikubwa kwa kundi lolote lile la kisiasa”
Yaliyojitokeza kwenye chaguzi kuu mbili, yanaweka wazi kwamba uaminifu wa wananchi kwa NRM, umepungua sana. Vituo hewa vilivyotengenezwa ili kuhakikisha NRM, inashinda na Museveni anabaki madarakani, kuwatumia wanajeshi kupiga kura zaidi ya mara tatu na kuwatishia watu kwa nguvu za kijeshi ili wamchague Museveni, matumizi ya fedha nyingi za kununua kura na kupika matokeo ya uchaguzi ni dalili tosha za kuporomoka kwa uaminifu wa NRM.
Sura zote hadi ya kumi na tisa zinafuata mtindo kama wa hizi zilizotangulia, ni nukuu ya Museveni kutoka kwenye vitabu vyake na baadaye mwandishi anaonyesha kwa mifano jinsi Museveni anavyoishi na kutenda kinyume na maandishi yake. Mwandishi amefanya utafiti na kuwahoji watu mbali mbali. Amewahoji watu waliokuwa karibu sana na Museveni na sasa hivi ni maadui wakubwa; amehojiana na watu waliofungwa na kuteswa kizuizini; kitu kinachojulikana kule Uganda kama “Nyumba salama”.
Pia, ameweka picha za matukio mbali mbali ya kuonyesha jinsi jeshi la Uganda linavyotumika kuwanyanyasa, kuwatesa na kuwaua watu.
V. Tathmini ya Kitabu
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliyoifanya Olive Kobusingye.
Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia mwandishi, kitabu kinasisimua, kinafundisha na kinafikirisha kutokana na mtindo alioutumia mwandishi. Mtindo wa kuanza kila sura na nukuu kutoka kwenye vitabu vya Museveni. Hii inavutia, maana marais wengine wa Afrika, wanafanya makosa bila kuwa na ushahidi wa kuwabana. Museveni, ni tofauti. Yeye aliandika na kulaani uongozi usiokuwa wa kidemokrasia, amelaani ukiukwaji wa haki za binadamu, amelaani wananchi kuburuzwa na mengine mengi ambayo leo hii ameyakumbatia na kuwa kinara wa kupinga demokrasia kwa nguvu zote.
“ Usalama wa raia wa Uganda ni haki ya kila mwananchi na wala si upendeleo unaosimikwa na uongozi wowote. Hakuna uongozi au serikali inayoruhusiwa kuwaua watu au kuwapiga kwenye vizuizi barabarani. Tunawaambia wanajeshi wetu kwamba wakiwanyanyasa wananchi watapata adhabu kali itakayo toa fundisho. Na kuhusu mauaji, mwanajeshi akiua mtu naye atauwa”(uk 71) tafsiri ni yangu; ni nukuu ya maneno ya Museveni, kutoka kwenye kitabu chake cha “ What is Africa’s Problem?”
Mwandishi anatoa mifano mingi ya kuonyesha jinsi sasa hivi wanajeshi wa Uganda wanavyowanyanyasa watu na kuendesha mauaji bila kuchukuliwa hatua yoyote ile.
Pili, ni wazi kwamba mwandishi amefanikiwa kutimiza lengo lake la kutupatia upande mwingine wa Yoweri Museveni. Kama alivyosema Profesa J. Okola-Onyango, kwenye dibaji, hiki ni kitabu pekee kinachomwandika Museveni, kwa kuangalia sehemu zote mbili, tofauti na vitabu vilivyozoeleka vya kuimba sifa za Museveni.
Tatu, mwandishi anatufumbua macho kuona ukweli wa kile ambacho siku zote tunakiita “ Harakati za ukombozi”. Je, zinakuwa harakati za ukombozi wa wananchi, au ukombozi wa watu binafsi? Kwa upande wa Uganda, mwandishi anatuonyesha wazi kwamba, harakati za ukombozi zilikuwa za watu binafsi. Wakati wa Obote na Amin, hakukuwa na uchaguzi; leo hii kuna uchaguzi, lakini swali ni je ni nani anapita? Kuna tofauti gani na kutokuwa na uchaguzi kama anayeshinda ni yule yule tena bila kupitishwa na wananchi.
Tano, ni kutuonyesha wazi utata wa Museveni, alipoingia madarakani alisema anataka watu wote wavae viatu; aliwalaumu viongozi waliomtangulia ambao walikuwa wakienda Ulaya kwa kutumia ndege binafsi ya Rais, wakati watu wanaishi kwenye umasikini. Leo hii yeye Museveni ana ndege ya kisasa na ndege hiyo ilimbeba binti yake kwenda kujifungua kwenye hospitali ya Ujerumani. Wachambuzi wa mambo wanasema gharama zilizotumika kwenye safari hiyo zingewasaidia mamia ya wanawake wa Uganda; na kwa vile Uganda ina Hospitali nzuri, huyo binti wa Rais Museveni angejifungua salama.
Yeye Museveni anasema si swala la kuwa na hospitali nzuri bali usalama wa familia yake. Anaweka wazi kwenye kitabu hiki kwamba kwenye swala la usalama wa familia yake, hana suluhu na anaweza kutumia njia zote kuhakikisha usalama wa familia yake.
Pia kwamba kwa kipindi cha miaka ishirini iliyopita hajatibiwa Uganda; akitibiwa ndani ya nchi ni lazima ufanyike mpango maalumu wa kulinda usalama wake, lakini mara nyingi anatibiwa nje ya nchi. Si kwamba hospitali za Uganda si nzuri, bali ni kuhofia usalama wake. Kiongozi anayelipenda taifa lake, ambaye yuko tayari kufa akilitetea, anawaogopa watu wake! Hili ni fundisho kubwa tunalolipata kwenye kitabu hiki na linatufumbua macho pia kwa viongozi wetu wanaopenda kutibiwa nje ya nchi. Wanaogopa usalama wa maisha yao. Kama mtu anawahudumia watu wake vizuri, kwa ini aogope usalama wa maisha yake?
Sita, Kobusingye, amefanikiwa kutushawishi kwamba yeye ni mwandishi mzuri. Kwenye kitabu anaonyesha ukweli kwamba mdogo wake Saasi, aliteswa na kufa akiwa ameshikiliwa na serikali, ndugu zake wengine wameikimbia Uganda na kuishi nje ya nchi kwa kukimbia mkono mrefu wa Museveni. Kaka yake Dr. Besigye, ameteswa na bado anaendelea kupata misukosuko kutoka kwa Museveni, lakini Kobusingye, anaandika kwa utulivu mkubwa na kufafanua matukio yote bila hasira na chuki. Mfano, yale yanayoandikwa juu ya Museveni, hayatofautiani sana na yale tuliyokuwa tukisikia wakati wa utawala wa Idi Amin, lakini uandishi wa Kobusigye, umejipambanua na uandishi wa enzi zile za Idi Amin.
VI. Hitimisho
Kwa kuhitimisha, nawaomba watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Ni muhimu sana kwetu, maana tunapoingia kwenye Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, ni vyema kuwafahamu marais wetu wa nchi hizi zinazotengeneza umoja huu wa nchi zetu. Lakini pia ni vyema kuvisoma vitabu vya Museveni kwanza, ili kulinganisha kama Kobusingye, amemtendea haki Museveni.
Sisi, hapa Tanzania, ukimwondoa Baba wa Taifa, marais wetu hawaandiki. Ni vigumu sana kuyafahamu mawazo yao na kuwapima pale wanapoteleza. Yoweri Museveni, ameandika na ni mzunguzaji mzuri tangia enzi zile akisoma Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, aliposikika akiusifiwa Ujamaa, kwamba siasa ya Ujamaa na kujigemea ndo njia pekee ya kumkomboa Mwafrika kutoka katika hali yake ya umasikini. Tangia awe Rais wa Uganda, hajasikika tena akiusifia Ujamaa au yeye kuendeleza kule Uganda. Kumbe tabia ya kutenda kinyume na imani yake, ni kitu cha siku nyingi.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment